BAADHI YA KWELI AMBAZO NI MSAADA KATIKA MAISHA YA WOKOVU Sehemu ya Pili

Na Nickson Mabena
Bwana Yesu asifiwe ndugu yangu, natumia nafasi hii kukukaribisha kwenye madhabahu hii kwa ajili ya Kujifunza maneno ya Mungu!
Somo letu lina kichwa kinasema:

Sehemu ya Kwanza tuliziangalia kweli mbili, leo nakuletea ya tatu na ya nne!
3.MTI WENYE MATUNDA, NDIO UNAOPIGWA MAWE.
Huu ni msemo wa Kiswahili, ila una maana kuwa sana, na umethibitishwa Kibibila kabisa. Hebu tusome kidogo.
YOHANA 15:18-19 “ulimwengu Iwapo ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi. Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia”.
Maneno hayo Yesu aliwaambia wanafunzi wake, Akasema watachukiwa na ulimwengu, kwa sababu tu wamechaguliwa na Yesu!!. Watu wengi wanashindwa kuelewa kwa nini alipofanya tu Uamuzi wa Kuokoka, ndipo watu, tena wa karibu huinuka na kuanza kumpiga vita, wengine kuchukiwa bila sababu.
Yesu ameshasema “ulimwengu Iwapo ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi”. Ujue Mtu aliyeokoka amembeba Yesu ndani yake, kwa hiyo ni tishio kwenye ulimwengu war oho, ndiyo maana lazima apigwe vita sana, mengine tunayopitia ni kwa sababu tumembeba Yesu ndani yetu!.
Soma tena hapa 2TIMOTHEO 3:12
“Naam, na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa katika Kristo Yesu wataudhiwa”.
Umelieewa hilo andiko!?, yaani wote wanaotaka kuishi maisha matakatifu na ya kumpendeza huyu Yesu, watapata maudhi, watapata machukizo, watasingiziwa!!.

Unajua kwa nini!?, Kwa sababu Wamembeba YESU!. Kwa wewe hujasikia kuna dini zingine ni heri uwe jambazi au changudoa lakini UKIMPOKEA YESU TU, Wanataka kukuua!!?
Ndiyo maana wapo wanafunzi mashuleni wanatamani sana wampokee Yesu kama Bwana na Mwokozi wa Maisha yao, lakini wanawaogopa wazazi wao wasije wakakataa kuwalipia Ada!!.
Kwa wewe ambaye unatamani sana maisha ya wokovu lakini unamwogopa Mzazi, au mke au mme, rafiki n.k. nikwambie tu Usiogope!,

na wewe unayepitia manyanyaso kwa sababu ya wokovu pia nikwambia Usiogope ,
hebu ona alichokisema Mungu hapa. ISAYA 43:4 “Kwa kuwa ulikuwa wa thamani machoni pangu, na mwenye kuheshimiwa, nami nimekupenda; kwa sababu hiyo nitatoa watu kwa ajili yako; na kabila za watu kwa ajili ya maisha yako”.
Usihofu, Mungu anazo njia nyingi kwa ajili yako, Pia ana watu wengi amewaandaa kwa ajili yako.
UNAPIGWA MAWE<KWA SABABU UNA MATUNDA!!.

4.UMOJA NI NGUVU, UTENGANO NI UDHAIFU.
Ndugu yangu moja ya vitu muhimu sana katika kuleta mafaniko katika jambo lolote ni UMOJA, na hii ni kwa sababu binadamu tunategemeana!!.
Ndiyo maana Yesu aliamua kuingia kwenye maombi na kuliombea kanisa Umoja, ona;
“Wala si hao tu ninaowaombea; lakini na wale watakaoniamini kwa sababu ya neon lao. Wote wawe na Umoja; kama wewe, Baba, ulivyo ndani yangu nami ndani yako; hao nao wawe ndani yetu; ili ulimwengu upate kusadiki kwamba wewe ndiwe uliye nituma.” YOHANA 17:20-21

Umeyaona maombi ya Yesu!?, Ametuombea Umoja!, kwa hiyo tunapaswa kujua kwamba umoja ni kitu muhimu sana. Kabla sijakupa mfano hebu tuyasome maneno yafuatayo;
‘’Afadhali kuwa wawili kuliko mmoja; Maana wapata ijara njema kwa kazi yao. Kwa maana wakianguka, mmoja wao atamwinua mwenzake; lakini ole wake aliye peke yake aangukapo, wala hana mwingine wa kumwinua! Tena, wawili wakilala pamoja, hapo watapata moto; lakini mmoja aliye peke yake tu awezaje kuona moto? Hata ikiwa mtu aweza kumshinda Yule aliye peke yake, wawili watampinga; wala kamba ya nyuzi tatu haikatiki upesi.” MHUBIRI 4:9-12
Bwana Yesu asifiweee…. Ukiyatafakari vizuri hayo maandiko hapo juu, utaona jinsi ambavyo Mungu alikuwa anasisitiza suala la Umoja!, Tukiwa na umoja Mbele Za Mungu inapendeza sana kwani imeandikwa; “Tazama, jinsi ilivyo vema, na kupendeza, Ndugu wakae pamoja, kwa umoja.” ZAB 133:1
Tunatakiwa kuwa na umoja kwenye kila jambo, kwenye maisha ya kawaida na katika huduma!. Umoja ni muhimu sana hasa kwenye huduma, tunajua kwamba hakuna Mtu ameitwa kwenye huduma ili atumike peke yake, hata kama ana upako kiasi gani bado anahitaji msaada wa wengine kwenye huduma.
Kwani kila mtu na sehemu yake kwenye Mwili wa Kristo, ndiyo maana ni hatari sana mtu kutaka kutumika kama flani, pia ni hatari mtu kuacha kutumika tena ni hatari zaidi mtu asiijue nafasi yake ya kutumika!!.
Hebu tuone 1Kor 12
“12.Maana kama vile mwili ni mmoja nao una viungo vingi, na viungo vyote vya mwili ule, navyo ni vingi ni mwili mmoja; vivyo hivyo na Kristo. …………………….
14.Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.
15. Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?
16.Na sikio likisema, kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?
17.Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?
18.Bali Mungu amevitia viungo katika mwili kama alivyotaka.
19.Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?
20.Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni Mmoja.
21.Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi. Bali zaidi sana vile viungo vya mwili vidhaniwavyo kuwa vinyonge zaidi vyahitajiwa zaidi.”

Unaweza kuendelea kusoma hadi mstari wa 27, Biblia imeendelea kusisitia umuhimu wa umoja kwenye Mwili wa Kristo, ndiyo maana nilikwambia kila mmoja ana nafasi yake!.
Ndiyo maana hutakiwi kujikweza, na kujiona bora kuliko wengine kwenye huduma!, bado unamuhitaji mwingine ili uweze kusonga Mbele.
Hata kwenye maombi tunahitaji kushirikiana, kwani Maombi ya wengi huwa na matokeo ya haraka zaidi. Si unajua Moto wa kuni nyingi huwa Mkali zaidi, na ndio unaoivisha kwa haraka sana kuliko moto wa kuni moja!!.
Unajua kwa nini udhihirisho wa nguvu za Mungu kwenye ibada za ndani huwa chache kuliko kwenye mikutano ya nje!?,
Hii ni kwa sababu wanaoombea ibada za ndani huwa ni wachache kuliko wanaombea Mikutano ya nje!. Mungu yapo tayari kutenda matendo makubwa sana tu, ila anawasubiri waombaji waamue ajidhihirishe kwa kiwango gani (SOMA, EFESO 3:20).
Na siri ya kuwa mwombaji lazima uwe tayari kuomba, na huwezi kujua kuomba isipokuwa unaomba. Kama kuna kikundi cha maombi kanisani kwako, jiunge na wewe utamuona Mungu akikutia nguvu,
UMOJA NI NGUVU…..!!
>>>MATONE MENGI YA MAJI HULOWESHA NCHI, BALI TONE MOJA HUPOTEA TU<<<<<<<
TUSHIRIKIANE!

Kama umebarikiwa na Mafundisho haya, usiache kumshirikisha na Mwingine!!.
NB: Kama unataka kumpa Yesu maisha yako, au kwa Maombi na Ushauri tutafutane, na Mungu atakubariki kwa Jina la Yesu!!.
Ubarikiwe ndugu kwa kuusoma ujumbe huu!!.
.....Subiri Sehemu ya Tatu!.......
By Nickson Mabena

Comments