BAADHI YA KWELI AMBAZO NI MSAADA KATIKA MAISHA YA WOKOVU, Sehemu ya tatu!

Na Nickson Mabena
Nakusalimu katika JIna la Yesu, karibu tuendelee na somo letu, ambalo nililianza mwanzoni mwa wiki hii, Bado namwamini Mungu kwamba baada ya kuusoma ujumbe huu, kuna kitu Roho Mtakatifu ataachilia kwenye Moyo wako!
Tumeshaziangalia kweli nne, lao nakuletea ya tano.
Karibu tuendelee....
5.KUKIRI USHINDI NI USHINDI, BALI KUSHINDWA NI KUSHINDWA
Kwenye kweli hii tunatakiwa kujua nguvu iliyomo katika maneno!, kuna ushindi mkubwa sana kwenye kutamka…!!
Hata wokovu hupatikana kwa kukiri,
ona “Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata WOKOVU”. RUMI 10:10
Kwa kuwa Wokovu ni kitu kikubwa sana na cha thamani, lakini cha patikana kwa KUKIRI, basi tunaweza kukiri mambo mengine kwenye maisha yetu na Ushindi ukapatikana lakini mtaji wetu mkubwa ukiwa ni WOKOVU wa Bwana Yesu!.
Kwenye magumu unayopitia Kiri ushindi, ipo nguvu nakwambia kwenye Kutamka, maana
“Tumbo la Mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake. Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake.” MITHALI 18:20-21
Wewe huwa unakiri nini ukutanapo na changamoto!?
Ndiyo maana Mzazi hutakiwi kumtamkia Mtoto maneno magumu, hata kama ni mchanga hasikii, au pengine yupo mbali sana na wewe, siku zote kumbuka kwamba waweza kuharibu ‘future’ ya mtoto wako, maana maandiko ya Mungu yanasema;-
“Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako,” MITHALI 6:2
Si umeshaanza kuona kwamba kwa kinywa tu unaweza ukategwa!?,
basi usijtamkie laana, usijikatae, usijisemee maneno magumu, usijisemee maneno ya kushindwa, kiri ushindi hata kama huoni njia.
Pia ukigundua kwamba kuna mahali ulikwama kwa sababu ulitamkiwa maneno mabaya pengine na wazazi wako, au mababu zako (kama ulishawahi kutamkiwa maneno kwenye ibada za mizimu ya ukoo),
Basi Unaweza kuingia kwenye maombi na kuyatangua hayo maneno maana Mungu anasema;-
“Mimi nayaumba matunda ya midomo; Amani, amani, kwake yeye aliye mbali, na kwake yeye aliye karibu; asema BWANA; nami nitamponya.” MITHALI 57:19

BWANA ameahidi kukuponya ila kama utaamua kuingia kwenye maombi kutangua vilivyotamkwa pia na kutamka vipya!
Ngoja nikuonyeshe madhara ya kutamka tamka maneno Magumu, au maneno ya Ovyo.
HESABU 14:28, “Waambieni, kama niishivyo, asema BWANA, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanya ninyi”.
Ukiyasoma vizuri hayo maandiko utagundua kwamba Mungu alikuwa anazungumza akiwa amekasirika sana, anawaambia kama walivyonena ndivyo atakavyowafanya. Je! Aliwafanya nini!?,
tuendelee kusoma
29.Mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu , kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung’unikia,
30.hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

Sijui wewe umetamka nini kwenye masomo, ndoa, au kwenye familia yako ulipokutana na changamoto nyingi,
wana Wa-Israeli walikiri kufa jangwani,
ona mstari wa pili wa sura hii ya 14 wa kitabu cha hesabu , imeandikwa hivi “Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, ingekuwa heri kama tungalikufa kwenye nchi ya Misri ,au, ingekuwa heri kama tungalikufa KATIKA JANGWA HILI.” HESABU 14:2
Na kweli kama tulivyo tangulia kuona jinsi walivyokula matunda ya midomo yao!!, Je! Umeliona hilo kwa uzito wake sasa!?.
Maisha yako yametamkiwa maneno gani!?, au umemtamkia nini Mtoto wako!?.
Utawasikia wengine wanasema “Yule, hawezi kufaulu tena”, au “hawezi kuokoka na hata akiokoka lazima arudi nyuma”.
Katika Jina la Yesu, hebu tafuta mda wa Kuombea Jambo hilo. Na Roho Mtakatifu atakusaidia kuomba jinsi ikupasavyo kuomba!! (Rumi 8:26)
Yesu alikufa kwa ajili yako, acha kuridhika kirahisi kiasi hicho….. Acha kunung’unika mwangaliye Yesu Msalabani, Damu yake ya thamani ilimwagika kwa Ajili yako, hebu chukua hatua ya Imani na mimi, Ingia kwenye Maombi, nguvu Za Mungu zipo na zinatenda kazi hata leo!.
Mwambie Yesu, kiri Ushindi Usikubali kushindwa, wala usikubali kurudishwa nyuma, Inawezekana inawezekana nasema tena, Inawezekana kuwa mshindi!!.. Pamoja na Kristo tutatenda mambo makuu!!
........Somo litaendelea......
Kama una swali, maoni, ushauri au Una Shida yoyote, niandikie kwenye
email yangu: mabenanickson@gmail.com

Au Simu namba 0769323490!!.
Na Mungu wa Mbinguni Akubariki sana!!...

Comments