FAIDA ZA KUMSIFU MUNGU BABA.

Scholar Mabula pamoja na praise team wenzake wa Kawe Pentecostal Church.

i).Kufunguliwa na kuachiliwa huru.


Wakati ule Paulo na Sila walipokuwa wakihubiri INjili kwa nguvu sehemu nyingi na kufanya miujiza ya pekee hasa walipomfungua Yule kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo la utambuzi, walikamatwa kwa kuteswa na kufungiwa gerezani na wale walinzi wakaamriwa wawalinde sana.Lakini panapo usiku wa manane Paulo na Sila wakakumbuka siri iliyomo katika kufanya ibada hususani katika eneo la kusifu, wakawa wakimwomba Mungu na kumwimbia nyimbo za kusifu, na mara tetemeko kuu la nchi likatokea, Gereza nalo likatikisika wakati huo vifungo vya wote vikalegezwa na milango ikafunguka.Matendo ya mitume 16:16-35.Huu ni ukweli usiopingika, nakumbuka kuna wakati ambapo tulikuwa tunaomba kwa ajili ya watu watatu ambao walikuwa wamefungwa na nguvu za giza kwa namna mbalimbali ndipo Mungu akaniambia niache kuomba nianze kusifu.Nilipoanza kusifu nilijishangaa kuona kwamba nikiimba nyimbo hata ambazo sijawahi kuzisikia mithili ya mtu anenaye kwa lugha, nikazidi kupata bubujiko ndipo wale watu wakaanza kufunguliwa kwa namna ya ajabu sana isivyotegemewa.Kuna wakati mwingine unakuwa na vifungo mbalimbali katika maisha yako, unaona akili ni nzito na huwezi kutatua matatizo au magonjwa mbalimbali labda watoto wako hawafanyi vizuri katika masomo yao na umekata tamaa.Nakusihi hebu ingia kumsifu Mungu na utaona maajabu ambayo haukutegemea.


ii).Kuta za Yeriko zinaondoka katika maisha yako.

Katika mfululizo au hatua ya kumiliki kwa wana Israeli nchi ambayo walikuwa wamepewa na BWANA kuna wakati wakiendelea na safari Mungu aliwaonesha mji wa Yeriko na kuwapa.Lakini haikuwa rahisi kama unavyoweza kufikiria kwani ule mji ulikuwa umefungwa kabisa na kuzungushiwa ukuta mkubwa na imara.

Mungu akasema na Yoshua na kumwambia, “……………………Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita mkizunguka mji mara moja, fanyeni hivi siku sita…………………..kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini palepale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kuukabili………………………”.Yoshua 6:1-20.
Sasa anaposema wapige kelele kwa sauti kuu sio kwamba sauti yenye maneno yasiyo na maana ila watoe sifa kwa nguvu sana kushangilia ushindi.Mahali pengine Biblia inasema, Msifuni Mungu kwa kelele za shangwe.KELELE ni sauti isiyo na mpangilio mzuri lakini maneno yatokayo kwenye hiyo sauti yanakuwa na maana halisi.
Mara nyingi unapewa maono mbalimbali ya vitu ambavyo umepewa na Mungu lakini ukitazama huvioni ila unaona ukuta uliovizunguka.Pengine kuna kizuizi cha aina nyingine kinachokufanya usipite na kuyakabili hayo maono.Ninakwambia, “ PIGA KELELE KWA SAUTI KUU” Umsifu Mungu,Lazima huo ukuta utaanguka tu na hicho kizuizi kitatoka tu maana Mungu wetu ni Mungu ambaye anafanya njia pale pasipokuwa na njia.Kama aliwavusha Israeli kwenye Bahari ya Shamu uwe na uhakika hata katika mapito yako utavuka tu.Usimwache Shetani achukue nafasi kwa kukudanganya na kukukatisha tamaa katika mawazo yako kuwa Mungu hawezi.Yeye ni Alfa na Omega maana yake jinsi alivyofanya jana ndivyo atakavyofanya leo na hata milele yote.Haleluya!!!


iii).Unajazwa kila kitu unachokihitaji.

Duniani hapa wanadamu wote ni wahitaji kwa namna moja au nyingine.Uhitaji ni hali ya kupungukiwa kitu Fulani ambacho ni muhimu sana kwako.Inaweza ikawa ada ya shule, fedha ya matumizi, usafiri, nyumba nzuri, chakula, nafasi ya kazi na mengineyo.Watu wengi wameshindwa kupata vitu wanavyovihitaji kwa kukosea kitu hiki; wanashindwa kusifu kikamilifu kwa vile wanakumbuka uhitaji wao badala ya kumsifu Mungu bila kujali una uhitaji wa namna gani ili Mungu akujaze.Nilikwambia usijaribu kutafakari ukubwa wa tatizo ulivyo wakati unasifu bali tafakari ukubwa wa uweza wa Mungu juu ya hilo tatizo au uhitaji.
“Wanasimba hutindikiwa, huona njaa, bali wamtafutao BWANA hawahitaji kitu chochote kilicho chema”.Zaburi 34:10.Hii haimaanishi kuwa hawatatumia vitu vyema.Maana yake hapa ni kuwa hata kama watapungukiwa chochote wana sehemu ya kufanya viongezeke, kwenye kumcha BWANA(katika sifa).
Kuna tofauti kubwa kwa mtu Yule ambaye ameishiwa fedha ya matumizi na anayo ya leo tu na ya kesho hajui ataipata wapi yaani anasubiri muujiza na yule ambaye ingawa ameishiwa leo lakini benki katika akaunti anayo fedha ya kutosha mwaka mzima.Lazima huyu wa pili hawezi kuhangaika au kupoteza muda wake kuanza kuombaomba kwa majirani.Wakristo wengi wamegeuka kuwa ombaomba kwa watu hata wasiomjua Mungu(wapagani) kwa sababu wameshindwa kutulia na kumsifu Mungu ili awajaze kile wanachokihitaji.Matokeo yake wameingia kwenye gharama ya kupokea vitu kimikataba au kimaagano ambayo ni ya shetani au pengine kupokea vitu ambavyo vimetolewa sadaka kwa miungu, mizimu au kafara.Hebu acha kuwa ombaomba na kumwaibisha Mungu,Mpendwa wa BWANA!! Kumbuka Mungu anacho kila unachohitaji hivyo jukumu lako ni kugeuka na kuanza kumsifu na kumshuhudia Mungu kwa mambo makuu anayoyatenda na hakika atakupa unachokihitaji.Hata kama unasumbuliwa na ugonjwa Fulani hebu uambie kwa imani tulia kimya niweze kumsifu Mungu halafu anza kumsifu Mungu kwa moyo wako wote hakika Mungu atatenda.


iv)Unapewa kushinda na zaidi ya kushinda.

Sifa inatumika pia kama moja ya silaha kuu ya kiroho.Kumbuka vita vyetu kama watu tuliookoka ni vya rohoni kwa sababu maadui tunaopambana nao wapo katika mfumo wa roho katika ulimwengu wa roho maana yake silaha tunazopaswa kuwa nazo ni za rohoni(2wakorintho 10:3-5).Mara nyingi Mungu alipokuwa anawatuma watu wake kwenda kupigana vita silaha kuu aliyowaambia kuitumia ni sifa.Ndivyo ilivyokuwa hata kwa wana wa Israeli kabila la Yuda wakati wanaongozwa na mfalme Yehoshafati. “naye alipokwisha kufanya shauri na watu, akawaweka wale watakaomwimbia BWANA na kusifu katika uzuri wa utakatifu, wakitoka mbele ya jeshi na kusema,Mshukuruni BWANA; kwa maana fadhili zake ni za milele.Nao walipoanza kuimba na kusifu, BWANA akawaweka waviziao juu ya wana wa Amoni na Moabu, na wa mlima Seiri, waliokuja juu ya Yuda; nao wakapigwa”.2Mambo ya nyakati 20:21-22.
Na ukisoma sura yote utaona kuwa ilifikia maadui wakaanza kuuana wenyewe kwa wenyewe lakini sababu yake ni sifa.

Ndugu yangu usione maadui wanakuja mbele yako halafu ukaanza kupiga mahesabu ya kujisalimisha hebu piga kelele sema, “NAMSHUKURU BWANA KWA MAANA FADHILI ZAKE NI ZA MILELE”.Nakuambia iwe wachawi, mizimu, mapepo, majini, waganga wa kienyeji au aina yoyote ile ya mateso hata ya kimwili njaa, magonjwa, ukame, na adui yoyote Yule, usiogope.Maana Mungu wetu hataki kuaibika na unapomsifu juu ya ukuu wake mbele za adui ndipo anataka ajioneshe kwa adui uhalisia wa kile kinachotamkwa na wewe kupitia sifa zako, atakupigania nawe utanyamaza kimya.
“Lakini katika mambo hayo yote tunashinda, na zaidi ya kushinda, kwa yeye aliyetupenda”.Warumi 8:37.Ushindi wako hautakuwa wa kawaida utakapochukua hatua ya kumsifu Mungu sawasawa.Tamka mafanikio katika BWANA hata kabla ya kuona mafanikio.Tamka lolote jema ambalo unaamini lipo mbele yako hata kabla hujaliona Mungu akupendaye atakapoiangalia hiyo sifa yako lazima atakujibu tu.

Comments