MAMBO KUMI YANAYOWEZA KUWACHELEWESHA WACHUMBA KUFUNGA NDOA

BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu upate maarifa ya kukusaidia katika hatua zako za maisha.
Zaburi 119:9 '' Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako. ''
-Kijana ili aifanikishe njia yake lazima amtii MUNGU huku ulikifuata Neno la MUNGU.
Ili uifikie ndoa njema ni lazima utengeneze njia yako ukimtii MUNGU na kulifuata neno la MUNGU.
-Kila njia ya mafanikio au ya baraka unayoiendea lazima umtii MUNGU na kulifuata neno la MUNGU.

Kwa vijana kudharau neno la MUNGU na kutomtii MUNGU huwagharimu sana na kuwaletea matatizo makubwa maana usipomtii MUNGU lazima tu utakuwa unamtii shetani, na ukimtii shetani hata hufiki mbali.

Kuna sababu kadhaa nimeziandaa ambazo ni chanzo cha vijana wengi wachumba kutokufikia hatua ya ndoa au kucfika kwa kuchelewa sana.
  Wagalatia 5:16 ''Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.''

      1.    Dhambi ya uasherati.
dhambi ya uasherati ni chanzo kikuu cha wachumba wengi kutokufikia hatua ya ndoa na kuacha machungu na hasira nyingi.
-Kujirahisi kwa binti humfanya kijana awe kama ameoa kabisa maana kila anachotaka cha kindoa anapata.
-Binti anayeruhusu uasherati ana hatari kubwa sana ya kuachwa na huyo mchumba wake na huleta majuto makubwa baadae.
-Kijana ambaye kama ni ngono anapata na kwa hilo tu hawezi kukuoa maana kila kitu ambacho angekipata kwenye ndoa tu anakipata sasa maana binti hajitambui.
shetani hupanda magugu  na kuleta matengano.
Hata kama mnapendana lazima tu vikwazo viwe vingi maana shetani amewavamia. 
 “Lakini zikimbie tama za ujanani; ukafuate  haki. na imani. na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi. 2 Timotheo 2: 22

       2.  Kumfanya mchumba kama mme kabla ya ndoa.
Mfano una mfulia nguo, unamuoshea vyombo, unampikia chakula na out mnatoka kila siku, matokeo ya hapo ni hakuna ndoa ila  kucheezeana. Ni hatari sana kwa binti maana unamfanya mwanaume akujue udhaifu wako na udhaifu kidogo tu unaweza kuwaachanisha na kukuacha wewe ukilia, kumbe tatizo ni kumfanya huyo kijana kama ndio mmeshaoana.  na kwa sababu ya kutoenda kitakatifu shetani lazima awadandie tu na ka udhaifu kidogo tu kanaweza kuwaachanisha au kuwachelewesha kuoana mapema.
  -Ushauri wangu ndugu,  usikubali kukaa kwenye Mazingira hatarishi.
Mhubiri 12:14 ''Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya.   ''


       3.  Wazazi kumuuza binti{Mahari kubwa sana}
Mahari leo imekuwa ni mradi wa wazazi wa mabinti kutoka kiuchumi.
Miaka kadhaa nyuma kipindi nasoma shule ya msingi, kuna mzee mmoja alikuwa hana ng'ombe hata mmoja, lakini wakati binti zake 3 walikuwa katika harakati za kumaliza shule ya msingi, yule mzee alitengeneza zizi la ng'ombe  na tukawa tunashangaa sana. zizi bila ng'ombe kumbe lengo lake ni binti zake ndio wataleta mali hizi mpya katika familia. Baada tu ya wale binti zake kumaliza darasa la saba walioolewa hata kabla ya matokeo kutoka ya darasa la saba  hata kama wote walifeli mitihani.
Binti wa kwanza aliolewa kwa ng'ombe 7 hivyo yule mzee akaanza kuwa mfugaji kwa staili hiyo, baadae wale mabinti wengine 2 walileta kila mtu ng'ombe 5 na hivyo yule mzee ndani ya miezi 5 akawa mfugaji mwenye ng'ombe zaidi ya 15. huo ni mfano tu wa mabinti wengi ambao leo wamekuwa mradi wa wazazi wao kutoka kiuchumi.
Hapo nilijifunza kabisa kwamba wakati mwingine binti anaweza akajifelisha ili tu kuolewa na kutimiza lengo la mzazi.
Jiulize ng'ombe 7 kila ng'ombe ni Tsh ngapi?
Je ni vijana wote wanaweza kutoa mahali ng'ombe 7?
Kukosekana kwa pesa ya mahari kubwa namna hii unaweza kuvunja uchumba hata kama mlipendana vipi, mahari kubwa kama hii au zaidi sio vijana wote wanaiweza hivyo uchumba unaweza kufa kabisa.

    4.  Kujirahisisha kwa Binti.
Mfano mchumba  wa kiume akifanya mapenzi na binti ambaye ni mchumba wake atajisemea moyoni
 ''mbona imekuwa rahisi hivyo kwa mchumba wangu kukubali kulala na mimi, huyo nahakika hata kwa wengine anaweza kuwa rahisi hivihivi na wanaweza kumpata kiurahisi kama vile mimi nilivyompata kiurahisi hata haogopi kuzini''

-huo ni mfano lakini ni dhahiri kwa walio wengi.
-kumbuka mkizini shetani lazima apande magugu yake na magugu hayo sio rahisi kuyang'oa.
-Kujirahisisha kwingine ni kama kila muda unamtembelea hadi umekuwa kero hata kama hajakuambia, hata kumtembelea tu ukiwa peke yako haitakiwi na ni makosa.
1 Kor 6:18 '' Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. ''

     5.  Sababu nyingine inayoweza kuchelewesha ndoa au kufuta kabisa uchumba ni  mahitaji yasiyo na mipaka na makubwa.
Mfano  kabla hata ya ndoa utakuta binti kila siku anataka hela ya saluni 30,000, mara 20,000 ya lotion na mengine mengi ambayo yanaweza kumfanya kijana aghairi au mchelewe kufunga ndoa.
Kipato kinaweza kuyumba au kuisha kabisa hata kabla ya kufika kwenye ndoa na kusababisha uchumba kufa au kuchelewa sana kuoana.

       6.  Kutokuwepo kwa utakatifu na maombi kunaweza kuharibu uchumba wenu hata kama hamjafanya dhambi, maombi ni maisha na tambua kwamba ukijitenga tu na MUNGU basi shetani yuko upande wako na hivyo lazima tu alete tatizo ambalo linaweza kuvunja uchumba au kuwachelesha kufika kwenye ndoa takatifu.
Hata uchumba lazima ukabidhiwe mikononi mwa MUNGU ndipo mtafanikiwa, lakini ikiwa wachumba wanafanya uasherarti kila siku mtaukabidhije kwa MUNGU?

      7.  Mchumba kuchaguliwa na wazazi na sio muoaji/muolewaji.
-haiwezekani baba yako au mama akalazimisha uoe binti fulani harafu ukafanya mipango haraka wakati hata humpendi.

     8.  Tamaa za kutaka koloni la zamani.
Binti mmoja aliniambia kwamba ana mchumba na wako katika hatua za kuoana ila hampendi mchumba wake kama yule kijana wa zamani ambaye waliachana, anasema kwamba anaendelea na mipango ya ndoa hivyo nimuombee lakini ikitokea yule wa zamani atarudi au hata atamtumia mesage nzuri ataghairi kwa huyu wa sasa. niliwaza na kushangaa na hakika sikuomba maana hapo hapahitaji maombi ila maamuzi. anampenda wa zamani ila ana wa sasa ambaye anataka waoane. hapo mipango ya kuelekea ndoa lazima iyumbe maana upande mmoja bado haujaamua hata kama hauonyeshi hadharani kwamba haujaamua.
Kumb 5:21 '' Wala usimtamani mke wa jirani yako; wala usiitamani nyumba ya jirani yako, wala shamba lake, wala mtumwa wake, wala mjakazi wake, wala ng'ombe wake, wala punda wake, wala kitu cho chote alicho nacho jirani yako.   ''

    9.   Taratibu ngumu kwa baadhi ya makanisa inaweza  kuwa tatizo pia. 
-Kuna baadhi ya viongozi wa makanisa huwa ni wasumbufu sana. maana hata tu tangazo la uchumba unatakiwa uandike barua na barua hiyo inaweza kujibiwa miezi 7 ijayo maana anasubiriwa mchungaji ambaye yuko masomoni. 
-Kuna wakati wachungaji wakichelewesha wanakua sahihi kabisa maana ni kwa kumsaidia kijana wao asije akalaumu baadae.
 Na haiwezekani binti ana mimba na wewe unataka uchumba utangazwe, haipo hiyo na haitatokea.
Kama kuna tatizo mahali lazima wachungaji wacheleweshe ili kukusaidia. lakinini nachozungumzia mimi ni kwamba kwa wachumba hakuna tatizo hata moja lakini bado wanachelewesha bila sababu maalumu hadi wanachelewa kufunga ndoa au kuhatarisha kabisa uchumba huo kuendelea hasa ikiwa kijana na binti wanaabudu madhehebu tofauti.
Uchumba unacheleweshwa givyo, je tangazo la ndoa itakuwaje?

     10. Tabia za asili pia zinaweza kuhatarisha uchumba au hata kuchelewesha hatua ya kufikia ndoa.
Mfano kijana ana tuhuma za wizi, au binti ana tuhuma za uongo au uchawi kwenye familia yao.
Mmoja wao atataka kuchunguza kwanza tuhuma hizo ambapo uchunguzi huo unaweza kuwa wa muda mrefu wakati mwingine.
Mathayo 5:27-32 '' Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.
 Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini. ''


Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments