Na Frank Philip Seth. |
Nimesoma tena habari za Ayubu nikaona jambo. Kuzimia roho maana yake ni kukata tamaa au kuishiwa nguvu za kuendelea na msimamamo au jambo unalofanya. Ayubu alifika mahali pa kuzimia roho wakati anapita kwenye JARIBU ambalo lengo lake ni KUPIMA kile ambacho Mungu aliona ndani yake, yaani “mkamilifu, mwelekevu, mcha Mungu na aliyejiepusha na uovu” (Ayubu 1:1). Kwa sababu ya UBORA wa Ayubu, Mungu akajisifu juu ya Ayubu lakini Ibilisi aliona kwamba Ayubu alikuwa na SABABU nyingine ya kuishi hicho kiwango bora cha maisha na wala sio kwa sababu ya kumcha Mungu tu. Angalia hapa, “Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi” (Ayubu 1:9, 10).
Kuna tofauti ya kumcha BWANA kwa sababu ya sheria, watu wanaokuzunguka, hofu ya matokeo ya uovu wako kwa jamii, hofu ya mume au mkeo, hofu ya kupoteza kazi, hofu ya kupata aibu, hofu ya magonjwa, hofu ya kufa, nk. na kumcha Mungu kwa sababu UNAMHESHIMU na KUMPENDA tu. Iko tofauti kubwa, na hii sababu ya kumcha Mungu kwa sababu umeamua kumheshimu na kumpenda, ni jambo ambalo ni bora na la kumvutia Mungu sana. Angalia, Mungu anasema “hakuna aliye kama Ayubu duniani” (Ayubu 1:8), inamaana Mungu aliangalia na kuona viwango tofauti ndani ya “watakatifu walioko duniani” kisha akaona “ni yupi anampendeza zaidi”. Safari hii, BWANA aliamua kusema habari za Ayubu kwa maana viwango vyake vilikuwa vya juu kuliko wenzake wote juu ya nchi.
Angalia tena jambo hili, akili za kawaida za mke wa Ayubu hazikujua kwamba hata walio wakamilifu na wacha Mungu hupatwa na mambo magumu! Ona tena hapa Ayubu anamjibu mkewe, “Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake” (Ayubu:2:10). Angalia tena, kama jambo halikufikishi mahali pa kutenda dhambi hilo sio jaribu. Ayubu hakutenda dhambi hata kwa hatua hii ambayo mkewe alimfikisha, yaani hata kumwazia Mungu vibaya licha ya kufanya dhambi kwa matendo yake.
Angalia jambo hili tena, wakati Ayubu anajua na kutarajia kutiwa moyo, kufarijiwa na kupata bega la kuegemea wakati wa shida yake, hakupata sio kwa mkewe wala marafiki zake! Ndipo akasema, “Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi”. Ndipo nikajua, kumbe! Watu wengi wanakata tamaa, kuchoka au hata kumtenda Mungu dhambi, eti, hawajatiwa moyo! Au kuna mtu amewakatisha tamaa au kuwavuruga? Na sasa WAMEAMUA kufanya dhambi tu! Je! Umeona kiwango hiki cha kumcha Mungu? Yaani mtu anamcha Mungu kwa sababu “ametendewa mema”, akitendewa asivyotarajia “anaacha kumcha Mungu”! Basi nikajifunza jambo hili. Katika shida zangu na majaribu yangu, wapo watu ambao kazi yao itakuwa kuondoa tegemeo langu kwao, au kunikatisha tamaa, au kuweka vikwazo zaidi, au kuja na namna mbali mbali za kunisukuma ili kuniangusha. Ole wake ambaye nguvu zake ziko katika “wema wa wanadamu” na kusaidiwa nao! Maana kama Ayubu naye angekuwa hivyo, jina lake lisingetajwa kamwe japo alifanya mengi mazuri huko nyuma, ila jaribu hili asingevuka kwa sababu “rafiki na watu wake hawakumtendea wema”.
Angalia jambo hili la rafiki wataabishaji wa Ayubu, “Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi? Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.” (Ayubu 4:7,8). Mawazo yao ni kama ya wale wasiojua njia za Mungu. Wanajaribu kumwambia Ayubu kwamba anapata mabaya kwa sababu ametenda dhambi, kumbe! Ni kinyume chake. Ayubu anapata majaribu kwa sababu ya ubora wake sio kwa sababu ya uovu wake! Naye Ayubu akajibu na kusema, “Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa. Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini kuhoji kwenu, je! Kumeonya nini? (Ayubu 6:24,25). Kila ayubu akiangalia na kujitathimini haoni jambo, ndipo anasema jamani, niambieni nimekosa nini sio kunisomesha tu maneno, niambieni mimi nijue maana kuhoji kwenu hakunisaidii kitu, niambieni nimekosea wapi?
Angalia tabia ya ayubu. Sio tu kwamba alikuwa hatendi dhambi ila “alijiepusha na uovu” kwa kiwango kwamba hata alitoa sadaka na toba kwa watoto wake ili isije ikawa wanatenda dhambi au kumkufuru Mungu wakati yeye hajui! (Ayubu 1:5). Ayubu alifika kiwango cha kufanya toba hata kwa dhambi ya kudhaniwa achilia mbali aijuayo, leo anaambiwa “mabaya haya ni kwa sababu umetenda dhambi”! jambo hili likamsumbua Ayubu. Hata leo, mbona wanadamu wanazidi kuwaza namna hii? Yaani mmoja wetu akipatwa na mabaya akili zinakimbilia kufikiri ni kwa sababu ya uovu wake, na sasa analipwa sawa na matendo yake! Kwanini tusijifunze kwa Ayubu?
Katika mambo yote, yaani yalikuwa mengi, Ayubu hakutenda dhambi. Mara nyingi Jaribu linakuwa moja ila linakuwa na awamu zake nyingi. Kwa mfano, mtu anaweza asizini, ila katika mchakato wa kuepuka zinaa, kashatukana, tamani, laani, pigana, kusema uongo, nk. umeona hapo? Je! Huyo naye kashinda jaribu? Kwanini kuruka majivu na kukanyaga moto? Sasa angalia tena kwa Ayubu, haya ndio majaribu ya Ayubu, alipewa majaribu mawili, kwanza kuguswa mali zake na pili, kuguswa mwili wake, lakini ukiangalia utaona wanakuja watu hapo, mkewe na rafiki zake ili Ayubu akosee na kutenda dhambi NYINGINE. Lengo la Ibilisi ni utende dhambi, na usimche Mungu, haijalishi ni dhambi ipi au humchi Mungu kwa mtindo gani. Katika mambo yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa matendo, kinywa wala mawazo.
Jifunze kujua na kutambua majaribu yako. Jifunze kujua jinsi ya kushinda kwa halali, na jifunze kusimama peke yako bila kumlaumu mwingine kwa kushindwa kwako kwa maana hatukuitwa kwa makundi bali mmoja mmoja. Jifunze kujua mchakato na vipengele vya muhimu kujilinda ujaribiwapo ili upate ushindi kamili. Nguvu zako zinatoka wapi wakati wa Majaribu?
Heri mtu yule ambaye anamcha Mungu kwa sababu AMEAMUA kumcha bila kujali kupungukiwa, kuwa na vingi wala kufanyiwa mema au mabaya na mtu awaye yote. Huyo ni kivutio kikubwa cha Mungu Baba.
Frank Philip Seth.
Comments