TUNZA UHUSIANO WAKO BINAFSI NA MUNGU KULIVYO VYOTE UNAVYOTUNZA.

BWANA YESU atukuzwe.
Karibu tujifunze mambo ya uzima wa roho zetu.
Usikubali mtu yeyote akaingilia uhusiano wako binafsi na MUNGU.
Uhusiano wako na MUNGU ni uhusiano wa kipekee wa maisha yako ya sasa na yajayo. 

1 Samweli  12:24-25 ''Mcheni BWANA tu, mkamtumikie kwa kweli kwa mioyo yenu yote; maana, kumbukeni jinsi alivyowatendea mambo makuu. Lakini kama mkiendelea kutenda mabaya, mtaangamia, ninyi na mfalme wenu pia.''

Ndugu, ili uhusiano wako na MUNGU uwe safi na hai ni lazima 
-Umche MUNGU.
-Umtumikie BWANA kwa moyo wako wote.
-Kumbuka matendo makuu ya MUNGU kwako na hadi sasa anaendela kukutunza na kukulisha. mpe heshima yake anayostahili.
Ukitenda mabaya utaangamia.
Uhusiano wako na MUNGU ni muhimu sana.
-Kuna waume wanaharibu uhusiano wao na MUNGU muumbaji wao kwa sababu tu ya wake zao, ni hatari sana.
-Kuna wamama wanaharibu uhusiano wao na BWANA YESU kwa sababu tu ya wanaume zao.
-Kuna vijana hata wanaacha Wokovu kwa sababu tu ya maneno ya watu.
-Kuna wadada wanamwacha YESU kwa sababu tu ya kupata wachumba wapagani.
Ndugu, usikubali uhusiano wako na MUNGU muumbaji wako ukaathiriwa na mwanadamu awaye yyote. Kumbuka mwanadamu hana mbinguni ya kukupeleka na wala mwanadamu hana msaada kwako kama ukiwa hujiwezi.

Zaburi 34:8-9 ''Onjeni mwone ya kuwa BWANA yu mwema; Heri mtu yule anayemtumaini. Mcheni BWANA, enyi watakatifu wake, Yaani, wamchao hawahitaji kitu.   ''

Tunza uhusiano wako binafsi na MUNGU. 
Kwa sababu 
Isaya 45:18-24 ''Maana BWANA, aliyeziumba mbingu, asema hivi; Yeye ni MUNGU; ndiye aliyeiumba dunia na kuifanya; ndiye aliyeifanya imara; hakuiumba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu; Mimi ni BWANA, wala hapana mwingine. Sikusema kwa siri, katika mahali pa nchi ya giza; sikuwaambia wazao wa Yakobo; Nitafuteni bure; Mimi, BWANA, nasema haki; nanena mambo ya adili. Jikusanyeni mje; na kukaribia pamoja, ninyi wa mataifa mliookoka; hawana maarifa wale wachukuao mti wa sanamu yao ya kuchonga; wamwombao mungu asiyeweza kuokoa. Hubirini, toeni habari; naam, na wafanye mashauri pamoja; ni nani aliyeonyesha haya tangu zamani za kale? Ni nani aliyeyahubiri hapo zamani? Si mimi, BWANA? Wala hapana MUNGU zaidi ya mimi; MUNGU mwenye haki, mwokozi; hapana mwingine zaidi ya mimi. Niangalieni mimi, mkaokolewe, enyi ncha zote za dunia; maana mimi ni MUNGU; hapana mwingine. Kwa nafsi yangu nimeapa, neno hili limetoka kinywani mwangu katika haki, wala halitarudi, ya kwamba mbele zangu kila goti litapigwa, kila ulimi utaapa. Mmoja ataniambia, Kwa BWANA, peke yake, iko haki na nguvu; naam, watu watamwendea yeye, na wote waliomkasirikia watatahayarika. ''
Maandiko haya tu hapo juu yanaonyesha MUNGU  anataka nini kwako. 
-BWANA ni muumbaji wako.
-MUNGU ndiye aliyetaka uishi na hata sasa unaishi.
-BWANA ndie aliyeandaa mpango mzuri wa maisha yako yajayo kama tu ukimtii.
-MUNGU ndiye pekee anayeijua kesho yako.

Hakuna yeyote unayetakiwa kuwa na uhusiano nae mzuri kama MUNGU BABA.

MUNGU ni zaidi na baba yako au  mama yako.

MUNGU ni zaidi ya mke wako au mme wako.
MUNGU ni zaidi ya mtoto wako wala rafiki yako.

MUNGU anatakiwa apewe kipaumbele katika mambo yako yote.

Wanadamu wengi katika midomo yao huonyesha kwamba MUNGU ni namba moja kwako lakini katika matendo na maisha yao huonyesha kabisa kwamba MUNGU ni ziada tu kwao. BWANA anasema  '' Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami. Nao waniabudu bure, Wakifundisha mafundisho Yaliyo maagizo ya wanadamu.   -Mathayo 15:8-9''
-Ndugu, je unamheshimu MUNGU kwa mdomo tu huku moyo wako ko mbali naye? je utapata faida gani kwa kuacha kumheshimu MUNGU kwa mdomo na matendo yako yote? Hakuna faida ndugu zaidi ya jehanamu.

Kama unataka uhusiano wako na MUNGU uwe mzuri na imara ni lazima umtii MUNGU siku zote na katika yote anatakayo.

Unajua MUNGU Siku zote anataka nini?

       1.   MUNGU anataka uokoke na ubaki kwenye wokovu wake.
Yohana 3:16-18 '' Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU. '' 

       2.   MUNGU anataka uishi maisha matakatifu siku zote.
1 Petro 1:15-17 '' bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote; kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu. Na ikiwa mnamwita BABA, yeye ahukumuye kila mtu pasipo upendeleo, kwa kadiri ya kazi yake, enendeni kwa hofu katika wakati wenu wa kukaa hapa kama wageni. ''
 
       3.    MUNGU anataka  uishi kwa matendo mema.
Waefeso 2:10 ''  Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika KRISTO YESU, tutende matendo mema, ambayo tokea awali MUNGU aliyatengeneza ili tuenende nayo. ''
 
      4.    MUNGU anataka usiipende dunia na machukizo yake. 
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele. ''
      5.    MUNGU anataka Tuongozwe na ROHO wake na kuongozwa na ROHO wake.
-Kuongozwa na ROHO MTAKATIFU.
Warumi 8:14 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.''
 -Kuenenda kwa ROHO MTAKATIFU.
Wagalatia 5:16 ''Basi nasema, Enendeni kwa ROHO, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili.   '' 

      6.   MUNGU anataka usitende dhambi maana dhambi ina madhara makubwa.
1 Kor 6:9-11 '' Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la BWANA YESU KRISTO, na katika ROHO wa MUNGU wetu. '' 

       7.   MUNGU anataka umpe heshima yake siku zote maana ni  BABA Mzazi wa roho yako. 
Zaburi 29:1-2  ''Mpeni BWANA, enyi wana wa MUNGU, Mpeni BWANA utukufu na nguvu; Mpeni BWANA utukufu wa jina lake; Mwabuduni BWANA  kwa uzuri wa utakatifu.'' 
Tumpe MUNGU utukufu wake hata baada ya kutendewa muujiza na yeye.
Luka 17:17-19  '' YESU akajibu, akanena, Hawakutakaswa wote kumi? Wale kenda wa wapi? Je! Hawakuonekana waliorudi kumpa MUNGU utukufu ila mgeni huyu? Akamwambia, Inuka, enenda zako, imani yako imekuokoa. ''

Ndugu yangu, naamini kabisa baada ya kusoma ujumbe huu umeona ni wapi hutendi vyema. pale ambapo hutendi vyema rekebisha ndugu.
-Pale ambapo unachukuwa wewe heshima ya MUNGU, hakikisha unairudisha heshima hiyo kwa MUNGU.
-Kama umepishana na mpango wa MUNGU wa wokovu kwa sababu ya matendo yako, basi badilika na nenda katika KRISTO kwenye wokovu.
Warumi 10:9-11 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. ''
 
-Kama maisha yako umemwazima shetani ili ayatumie, hakikisha unamnyang'anya maisha yako na usikubali kumwazima tema milele, bali kimbili kwenye mpango wa MUNGU yaani kimbili kwa YESU KRISTO ili uokolewe.
Yakobo 4:7-8 ''Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili.   ''
=Tengeneza uhusiano wako na MUNGU kwa kuanza kumtii na kulitii Neno lake.
=Tunza uhusiano wako na MUNGU maana ukimkosea MUNGU hakuna msaada tena kwako maana hakuna mwenye nguvu na uwezo kama BWANA MUNGU.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments