USHIRIKA NA SANAMU NI KUIABUDU SANAMU.





BWANA YESU apewe sifa ndugu yangu.
Karibu tujifunze jambo la kutuvusha kutoka kwenye  giza.
1 Kor 10:14 ‘’ Kwa ajili ya hayo, wapenzi wangu, ikimbieni ibada ya sanamu.   ‘

Haya ni machukizo kwa MUNGU.
Ujumbe wa MUNGU unakuonya kwamba uikimbie ibada ya sanamu maana yake ondoka kwenye Kanisa au dini wanaoabudu sanamu na Biblia inakushauri vizuri kwamba ingia katika Nuru ya ajabu ya BWANA YESU.
1 Petro 2:9-10  Biblia inasema ‘’ Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya MUNGU, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika NURU YAKE YA AJABU;  ninyi mliokuwa kwanza si taifa, bali sasa ni taifa la MUNGU; mliokuwa hamkupata rehema, bali sasa mmepata rehema.  ‘’
-Watu hawa walioingia kwenye nuru ya MUNGU ya ajabu ni watu wa kitofauti sana, hawafuata tu taratibu kisa taratibu hizo zilikuwepo kwa miaka mingi.
-Wakristo hawa wametengwa mbali na dunia.
-Wanajitambua na wako mbali kabisa na machukizo, -wanamtii MUNGU katika utakatifu wake.
Ndugu zangu, Kama unataka kumpendeza MUNGU hakikisha unamtii MUNGU.

Yako mambo mengi sana ya kumtii MUNGU lakini leo nazungumzia ubaya wa sanamu. 1 Thesalonike 1:9 ‘’ Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia MUNGU mkaziacha sanamu, ili kumtumikia MUNGU aliye hai, wa kweli;   ‘’
-Ndugu, kumbe MUNGU wa kweli haabudiwi kwa kuchanganya na sanamu.
Hii ni dhambi.
Ndugu zangu vitu vingi ambavyo tunadhani ni vitu vizuri na vitakatifu kwa macho yetu, hivyo ni vibaya sana na ukikaa rohoni unaweza kugundua jambo hilo, Mwaka 2012 nilipita  mtaa Fulani na kukutana na kijana mmoja anayeuza yale makaratasi makubwa magumu yenye ujumbe wa MUNGU na picha kubwa za Yule wanaodhani wanadamu kwamba ni YESU na Mariamu, sikuipenda picha ile ila nilipenda andiko ambalo lilikuwa limeandikwa kwenye karatasi hiyo, nilinunua na kwenda kubandika chumbani kwangu, ilikuwa ni picha kubwa sana ikiwa na andiko ambalo ndilo hasa mimi nililipenda. Baada ya muda nilianza kuona ugumu Fulani katika maombi, sikujua kwamba tatizo lilikuwa ni nini, usiku niliona katika maono kwamba lile karatasi ni antenna ya kuzimu ili kuona kila ninalofanya. Nilishtuka sana na kuomba kwa juhudi, kesho yake nililitoa lile karatasi lenye picha ya sanamu na tangu siku hiyo nikajifunza jambo jipya. Ndugu zangu haina maana kila karatasi yenye picha ya Mariamu au Yusufu  ni mbaya ila kumbuka shetani hutaka kujipenyeza kwenye kila eneo ili tu akupate wewe mteule wa MUNGU.
Kuisujudia sanamu na kuitumikia ni kujiunganisha nayo, Hosea 4:17 -19‘’ Efraimu amejiungamanisha na sanamu; mwache.  Kileo chao kimegeuka kuwa uchungu; huzini daima; wakuu wake hupenda aibu. Upepo umemfunikiza kwa mbawa zake; nao watatahayarika kwa sababu ya dhabihu zao.  ‘’.
Ndugu Efraimu wa leo ni wewe mwabudu sanamu na unayesujudia sanamu, ni machukizo na kuna adhabu usipotubia na kubadilika.

Dada mmoja alishuhudia kwamba kasanamu ka mariamu kalikokuwa nyumbani kwao alikuwa anakaona usiku kakigeuka nyoka na kuanza kutembea, kasanamu hako walikatoa kanisani, ndugu, MUNGU anapokataza sanamu ni kwa kukusaidia wewe maana macho yako ya kibinadamu hayaoni. Dada mmoja aliota ndoto akiwa anapiga picha na majoka, aliumia sana na akanishirikisha ili ajue maana ya ndoto hiyo, nilipata ufunuo katika hilo, kumbe kila wakipiga picha huwa wanazi-edit kwa picha zao kuweka ndani ya picha nyingine ambazo zimetengeneza huko Ulaya,  picha ile   nzuri kumbe wala sio picha ya kawaida ni majini. Sasa Yule dada alipoona anapiga picha na majoka na kuogopa kumbe ni kwa picha yake kuunganisha na picha mbaya ambao wemeitoa kwenye internet. Hata wateule wengine mimi binafsi huwa nawashangaa sana, utakuta mtu kaweka picha anayodai ni ya YESU na kukulazimisha uandike amen ili ubarikiwe. Hakuna Baraka za hivyo ndugu yangu, na usiamnini kila picha zingine zimetengeneza na kuzimu kabisa hata kama zinavutia kiasi gani. Hii mifano yote ni picha tu na visanamu vidogo lakini vina madhara makubwa sasa sanamu ni zaidi.

Watu wa zamani waliangushwa sana na kujihisisha na sanamu lakini kanisa la leo hata hatujifunzi kwako.
Waisraeli waliabudu sanamu ya ndama jangwani na ndio maana wengi sana MUNGU aliwaangamiza huko huko jangwani, hata hatujifunzi kwao.

MUNGU anasema kwamba heshima yake wala sifa zake hatawapa sanamu.
Isaya 42:8 ‘’ Mimi ni BWANA; ndilo jina langu; na utukufu wangu sitampa mwingine, wala sitawapa sanamu sifa zangu. ‘’
Machukizo madhabahuni.
Ndugu zangu, jambo la muhimu naomba mtambue kwamba MUNGU hana mwakilishi katika vitu vyote duniani. MUNGU hutumia neno lake kama mwakilishi wa matakwa yake. Neno la MUNGU husomwa na kufafanuliwa na wanadamu waaminifu wakielekezwa na ROHO MTAKATIFU. Hakuna zaidi ya hapo. Sanamu haimwakilishi MUNGU kwa vyovyote vile.
-MUNGU hatawapa sanamu heshima yake.
-BWANA hatawapa sanamu sifa zake.
-MUNGU wa kweli haambatani na sanamu kwa namna yeyote ile.
-Sanamu ni mungu wa kutengeneza na wanadamu, wala sanamu hazihusiki na MUNGU aliye hai.
-Ukitumia sanamu katika mazingira yeyote ya ibada unamkosea MUNGU aliye hai.
Kuna watu hutumia sanamu za Bikra Mariamu na watakatifu wengine wa zamani kwa kuzibusu kwa heshima na kuomba kwa kutumia hizo, Ndugu yangu unayefanya hivyo tambua neno hili ya kwamba unafanya machukizo makuu.
-Kuna watu husujudia sanamu, ni makosa makubwa sana.
Kusujudia sanamu ni kumsujudia shetani(Ufunuo 13:12 ‘’  Naye atumia uwezo wote wa mnyama yule wa kwanza mbele yake. Naye aifanya dunia na wote wakaao ndani yake wamsujudie mnyama wa kwanza, ambaye jeraha lake la mauti lilipona. ‘’)

Mtume Yohana kwa hofu alitaka kumsujudia Malaika, Malaika alimkataza na kumwambia Yohana kwamba wa kusujudiwa ni MUNGU pekee(Ufunuo 22:8-9), MUNGU wa pekee ni MUNGU katika utatu mtakatifu ndio maana BWANA YESU katika maandiko mengi alisujudiwa na hata mbinguni malaika wote humsujudia(Ufunuo 5:8-14, Ufunuo 7:9-12).
-Ndugu yangu, MUNGU BABA amekataza kusujudia sanamu wala kuitumikia, Kumb 5:8-9 ‘’ Usijifanyie sanamu ya kuchonga, mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, au kilicho chini duniani, au kilicho majini chini ya nchi.  Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi BWANA, MUNGU wako, ni MUNGU mwenye wivu, nawapatiliza wana uovu wa baba zao; hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,  ‘’

Kutokana na neno la MUNGU hapo kuna mambo 3 kuhusu sanamu ambayo mwanadamu hatakiwi kuyafanya.

           1.    Usitengeneze sanamu ya mfano wa kitu chochote kiwe mbinguni, duniani wala kuzimu.
-Hivyo wanaotengeneza sanamu na wewe unaitumia wote wawili mmepotoka.
-Yawezekana wewe hujatengeneza lakini hata kutumia tu katika Ibada ni dhambi.

       2.  Usisujudie sanamu.
-Wengi wanasujudia sanamu, ni dhambi.
-Wengi wanajishughilisha na sanamu, ni makosa.
-Wengi hudhani kuna uwepo wa MUNGU wakiwa karibu na Sanamu, kumbe kuna uwepo wa shetani, ni dhambi ndugu.


 3.  Usiitumikie sanamu.
-Maelfu ya watu wanazitumikia sanamu, ni dhambi.
-Watu wengi hutumia sanamu katika ibada zao, ni dhambi.
-Hata kuweka masanamu kanisani kutawasababisha kanisa lenu liwe la kimwili badala ya kuwa la kiroho.
-Kanisa lenu likijaa masanamu, huo ni mlango wa shetani kuwa sehemu ya ibada yenu, ni dhambi.

Makampuni mengi yanatengeneza sanamu za wale ambao  majina yao yamo ndani ya Biblia ili tu kuwakosesha watu wengi ambao huzitumi asanamu hizo katika ibada.

MUNGU hataki wewe ndugu uhusike na sanamu katika mazingira yako yoyote ya kiteule. Unadhani kwanini sanamu zimejaaa zaidi makanisani? Ni kwa sababu shetani anawatafuta zaidi watu wa kanisa maana hao wakipata akili ya kuzichoma sanamu hizo watakuwa ni kama wamechoma macho yake ya kuwaona watu wa kanisani. Sanamu zile ni mpango wa shetani kuhakikisha mwanadamu hafiki uzima wa milele.
-Kuna watu ukikemea sanamu wanadhani unaanza kuwavuta watu wahame kanisa lao, lakini ndugu kama kanisa lako lina masanamu hakika ni heri kuhama maana nyie kunena kwa Lugha mtakuwa tu mnakusoma kweli Biblia nyie hakuwahusu.
-Kuombea mtu mapepo yakamtoka mtakuwa tu mnaona kwenye TV na kudhani kwamba hao mnaowaona wanatumia nguvu za giza kumbe ni mamlaka ya MUNGU aliye hai.
-Mkiwa na masanamu kanisani kwenu, Nguvu za MUNGU aliye hai mtakuwa tu mnazisikia redioni.
-Mkiwa na masanamu kanisani Karama za ROHO MTAKATIFU  mtakuwa tu mnaziona kwenye TV.

MUNGU anachukizwa na sanamu. Na kibaya zaidi ambacho MUNGU hataki ni  kanisa lenu kufuata ratiba ya kanisa la Ulaya, hivyi kanisa la Ulaya likianguka dhambini na nyie lazima tu mtaanguka maana mnawafuata wao, kanisa la Marekani wakitekwa na shetani na kuchapicha kitu kibaya na nyie tu kitawanajisi maana nyie mnawafuata hao kwa kila kitu. Ndio maana Biblia inasema Tuongozwe na ROHO MTAKATIFU na sio kanisa Fulani. Wagalatia 5:18-21 ‘’ Lakini mkiongozwa na ROHO, hampo chini ya sheria.  Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,  husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa MUNGU.    ‘’
Biblia inatutaka tusijiunganishe na sanamu, tena tujilinde na sanamu,  yaani tuziepuke sanamu ,1 Yohana 5:21 ‘’  Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.   ‘’
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
0714252292
mabula1986@gmail.com

MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments