UTAFANYAJE BAADA YA KUTAMKIWA MANENO MABAYA?





BWANA YESU asifiwe.
Karibu tujifunze na kuomba na  ili kufuta laana  au maneno mabaya tuliyotamkiwa au kujitamkia sisi wenyewe.

Hebu naomba tuone kazi 5 za maneno unayotamka au kutamkiwa.

     1.   Ndugu yangu, Ulimi unaumba haijalishi ni ulimi wa mtu mzuri au mtu mbaya. haijalishi ni ulimi wako au ni ulimi wa mtu mwingine( Mithali 18:20-21,  Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake.Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake. )
-Ndugu, unayojitamkiwa wewe mwenywe yanaweza kuja kutokea baadae. Kama unajilaani kwa maneno yako tarajia kuishi katika laana hiyo uliyojitamkia.
-Mauti na uzima viko katika uwezo wa ulimi kupitia kutamka.
-Je ukitamkiwa mauti na watu utafanyaje?
Jifunze somo lote utapata majibu ya ushindi kwako.

     2.    Maneno mabaya au mazuri yana uwezo wa kumkamata mtu(Mithali 6:2,Basi umetegwa kwa maneno ya kinywa chako, Umekamatwa kwa maneno ya kinywa chako, ).
-Ndugu ulijinenea nini? au umenenewa nini?
je ulisema kwamba mimi kufaulu haiwezekani?
je ulisema kwamba mimi kufunga ndoa ni labda tu maana ukoo wetu hakuna hata mmoja aliyefunga ndoa kanisani?
Kama uliwahi kujinenea lolote baya ndilo hilo linaloweza kutokea wakati huu au wakati ujao.
Umetegwa na maneno ya kinywa chako.
Umekamatwa na maneno ya kinywa chako.
-Je ukitamkiwa mabaya na watu utafanyaje?

      3.    Kwa Maneno unayotamka unaweza ukapewa haki yako nzuri(Warumi 10:10,   Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu.)
-Matumizi mazuri zaidi ya kila kinywa cha mwanadamu yanatakiwa yahusike na msitari huu wa Biblia. Kwa kumkiri BWANA YESU kwa kinywa chako na kuamini moyoni mwako kwamba alikufa na kufufuka kwa ajili ya dhambi zako unaokoka.
-Kwa kinywa unaweza kukiri hata kupata Wokovu.
Kinywa kina nguvu sana hivyo jichunge sana usijitamkie mabaya bali mema .

     4.    Kwa maneno yako mabaya unayojinenea au kunenewa unaweza kujikwaa(Yakobo 3:2,  Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu. )
-Kama wewe hutajikwaa kwa maneno yako wewe ni mkamilifu.
-Kwa kinywa mtu anaweza akasema uongo, huko ni kujikwaa.
-Kwa kinywa mtu anaweza kugombanisha ndugu, huko ni kujikwaa.
-Ni heri kuwa mkamilifu


     5.   Maneno huzaa mabaya au mazuri(Mithali 12:14,  Mtu atashiba mema kwa matunda ya kinywa chake; Na atarudishiwa matendo ya mikono yake. )
-Matunda huzaliwa na mti ambaye ni wewe.
-Mtu atashiba mema ya kinywa chake. ndugu ulishawahi kujiuliza inakuwaje kwa mtu ambaye amejitamkia mabaya kwa kinywa chake?
Na yeye atashiba mabaya ya kinywa chake.

Kinywa kina mamlaka sana ndio maana MUNGU aliwaambia watumishi wake kwamba barikini wala msilaani(Warumi 12:14 'Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani., )
-Matumizi mazuri zaidi ya kinywa chako naomba iwe kubariki watu na sio kuwalaani. Laana ni jambo kubwa mno hata kama wanadamu wengi siku hizi wanawatishia wengine kuwalaani bila hata kosa. Mbona wewe hukulaaniwa na MUNGU baada ya kutenda dhambi kila siku?. Ni mara chache sana MUNGU alipotamka laana kwa mwanadamu. Hata Adamu na Eva licha kufanya kosa kubwa ambalo limetughalimu wanadamu wote lakini MUNGU hakuwalaani ila aliilaani ardhi badala ya Adamu lakini wanadamu leo kutamka laana imekuwa kama silaha, yaani mtu akikukosea kidogo unasema ''Nakulaani sasa hivi''. Hiyo  ni mbaya na pia laana isiyo na sababu haimpigi mtu(Mithali 26:2b). Ndugu tusipende kulaana watu wa MUNGU na hata Musa na Haruni waliambiwa wawabariki wana wa israeli wala wasiwalaani.Hesabu 6:22-27 '' Kisha BWANA akanena na Musa, na kumwambia, Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia; BWANA akubarikie, na kukulinda;BWANA akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;BWANA akuinulie uso wake, na kukupa amani.Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.  ''
-MUNGU BABA anawafundisha watumishi wake kubariki lakini katika dunia ya leo laana imekuwa silaha, ni mbaya ndugu zangu.
Watumishi wengi hutamkiwa maneno mabaya leo lakin hayawapati kwa sababu ni waombaji na wanajua msaada u wapi wa kuyaruka maneno ya watu wabaya. kumbuka hata wachawi huroga kwa kufanya vitu vyao lakini lazima na kutamka kuwepo ndani.
Watu wengi wamenenewa kwa waganga wa kienyeji, kinachofanyika huko ni mtu kutoa kuku au mbuzi na manuizo yanafanyika yakiambatana na maneno mabaya juu yako. damu ile huwa haifi hivyo maneno hayo yalioyamkwa kuhusu wewe mfano kwamba uugue ugonjwa wa ajabu yatabaki na kusaidiwa na damu ile na majini ndio hutumika katika kufanikisha kusudi la mganga na yule mwenda kwa mganga, wote hao ni mawakala wa shetani na hakikisha unajitenga na uganga.
Hebu tuonne watumishi wawili walionenewa mabaya na watu wabaya.
Nabii Yeremia alipigwa kwa maneno. kumbe maneno yana uwezo wa kupiga lakini MUNGU alimshindia kupitia yeye mwenyewe Yeremia kutamka kinyume chao wale watu wabaya.
Yeremia 18:18-23 ''   ''Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.Niangalie, Ee BWANA, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami.Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate. Kwa sababu hiyo, uwatoe watoto wao waone njaa, uwatoe nguvu za upanga ziwapate; wake zao wafiwe na watoto wao, na kufiwa na waume zao; wanaume wao wauawe, na vijana wao wapigwe kwa upanga vitani.Kilio na kisikiwe kitokacho katika nyumba zao, hapo utakapoleta kikosi juu yao kwa ghafula; kwa maana wamenichimbia shimo waninase, nao wameifichia miguu yangu mitego.Lakini wewe, BWANA, unajua mashauri yao yote juu yangu, ya kuniua; usiwasamehe uovu wao, wala usifute dhambi yao mbele za macho yako; bali wakwazwe mbele zako; uwatende mambo wakati wa hasira yako. ''
-Watu hawa walimpiga kwa maneno yao, walimchimbia shimo kwa maneno yao. Yeremia alikata rufaa kwenye mahakama ya Mwisho yaani kwa MUNGU. Ndugu, je umetamkiwa nini?
Kata rufaa kwa BWANA YESU, huko ndiko kuliko na msaada pekee.
Kama wanakutesa kupitia vinywa vyao na wewe watese kwa kuyapeleka maneno yao yote Golgotha kisha yaache huko huku ulirudi ukiwa huru, kisha Mwambie MUNGU ashughilike nao. BWANA ana mbinu nyingi za kukushindia wewe uliyemtegemea. inawezekana kabisa ugonjwa walioutamka kwako ukawapata wao waliokunenea. Omba katika MUNGU kupitia YESU KRISTO ukibatilisha maneno yao. Walitumia vinywa na wewe tamka ushindi ukitumia kinywa chako. Sema ''kwa jina la YESU KRISTO sitakufa bali nitaishi ili niyasimulie matendo makuu ya MUNGU kwangu.''

Daudi naye alinenewa lakini alimtegemea MUNGU akashinda.

Zaburi 64;3-9 '' Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu, Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi. Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona?Hutunga maovu; husema, Tumefanya shauri kamili; Na mawazo ya ndani ya kila mmoja wao, Na moyo wake, huwa siri kabisa. Kwa hiyo MUNGU atawapiga shabaha, Kwa mshale mara watapigwa.
Ndivyo watakavyokwazwa, Ulimi wao wenyewe ukishindana nao. Wote wawaonao watatikisa kichwa.Na watu wote wataogopa, Wataitangaza kazi ya MUNGU, Na kuyafahamu matendo yake.  ''

-Kumbe ulimi ni kama upanga, unauwezo wa kukata kwa njia ya kutamka.
-Walitunga maovu kwa mtu wa MUNGU.
MUNGU akamshindia Daudi hata baada ya kutamkiwa mabaya. Daudi aliomba na kupokea.
Ndugu yangu. Najua kuna maneno mengi umetamkiwa lakini BWANA YESU nasema tukiomba lolote kupitia jina lake MUNGU anatupa(Yohana 14:14,  Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya. )
Kama wewe ni muombaji hakika hakuna neno la adui zako litakalokukamata na kukutesa.

=Kama wewe mwenyewe ulijinenea mabaya  ili yasikutese omba toba kwa ajili ya maneno yako mwenyewe. MUNGU atakusamehe na hayatakuwa na nguvu tena juu yako.
=Tubu kwa ajili ya maneno uliyonenewa na watu. Kutubu ni kumruhusu MUNGU ashughurike na wewe.

''Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji. -Waebrania 4:16''

                                    Maombi. 
BABA katika jina la YESU KRISTO nakuabudu na nakushukuru kwa kunilinda. BABA tazama kuna maneno mabaya ambayo nilitamkiwa na mengine mabaya nimejitamkia mwenyewe ambayo yamenikamata. BWANA ninatubu kwa ajili ya kila neno baya nililojinenea na natubu kwa ajili ya kila neno baya nililonenewa. Natubu kwako BWANA YESU ili damu yako inihesabie haki tena. BWANA nashukuru kwa kunisamehe. Kwa sasa niko kinyume na kila kusudi la shetani, kwa jina la YESU KRISTO. Ninafuta kila neno baya ambalo nilitamkiwa au nilijitamkia mwenywe, ninafuta yote hayo kwa damu ya YESU na kwa  jina la YESU KRISTO. Waliosema sitasoma, Kwa jina la YESU KRISTO nitasoma, Waliosema sitaolewa/kuoa natangaza ushindi katika mipango yangu yote. Kila ajenda ya siri iliyopangwa juu yangu naifuta kwa damu ya YESU KRISTO.
Kila mtu anayenitamkia mabaya najitenga na maneno yake mabaya kwa jina la YESU KRISTO. Hakuna neno baya nitakalonenewa na likanipata, damu ya YESU inifunike na nitakaa salama siku zote. Kama kuna mtu aliniendea kwa mganga wa kienyeji ili kuniharibia maisha yangu, ninaharibu, nangamiza, navunja na kuangamiza mipango hiyo ya kipepo kwa jina la YESU KRISTO. Kama kuna damu ya mnyama na inanena mabaya juu yangu natumia damu ya YESU KRISTO kufuta damu zote za wanyama ambazo zinanena mabaya juu yangu, nazifuta kwa damu ya YESU KRISTO na kwa jina la YESU KRISTO.
BWANA YESU nakushukuru maana kwako uko uzima na ushindi daima. asante BABA wa mbinguni maana upendo wako umenifunika, nakushukuru maana wewe ndio una ushindi wangu na ushindi huo umenipa leo. Nakushukuru BWANA na yote haya nimeomba  na kupokea katika jina la YESU KRISTO.
Amen. 

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments