AFANYEJE MTU ILI AURITHI UZIMA WA MILELE?

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze habari njema za ufalme wa MUNGU.
Ujumbe huu MUNGU ameutunza ndani yangu kwa muda mrefu  na ni ujumbe ambao ROHO MTAKATIFU alinifundisha nikiwa kazini.
Afanyeje mtu ili aurithi uzima wa milele?
Mtu mmoja tajiri aliuliza swahi hili kwa BWANA YESU.
Marko 10:17 ''  Hata alipokuwa akitoka kwenda njiani, mtu mmoja akaja mbio, akampigia magoti, akamwuliza, Mwalimu mwema, nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele? '' 
Hata leo watu wengi wana swali hili mioyoni mwao.
Yawezekana hata wewe umewahi kujiuliza swali hili muhimu. Biblia ina majibu yote ya swali hili na hatua zote za mpaka kumkamilisha mwanadamu hata akaurithi uzima wa milele.

Kuna hatua saba(7)  ambazo mtu  akizitii zote lazima ataurithi uzima wa milele.

       1. KUOKOKA:
-Kuokoka pekee ni sifa ya kumfanya mtu aurithi uzima wa milele lakini kwa sababu maisha yanaendelea ni muhimu sana hatua hizi 6 zingine kuzifuata. Kuna watu huokoka lakini baadae hurudi nyuma na kukosa sifa za kuingia uzima wa milele.
-Kuokoka ni kumpokea BWANA YESU.
Matendo 16:30-31 ''  kisha akawaleta nje akasema, Bwana zangu, yanipasa nifanye nini nipate kuokoka? Wakamwambia, Mwamini BWANA YESU, nawe utaokoka pamoja na nyumba yako'' .
-Kuokoka ni kumpokea YESU, kumkiri na kutubu na ukitimiza hayo jina lako linaandikwa katika kitabu cha uzima mbinguni.
Warumi 10:9-11,13 '' Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu. Kwa maana andiko lanena, Kila amwaminiye hatatahayarika. kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.''

        2. KUJITENGA NA SHETANI:
Kujitenga na shetani ni kujitenga na dhambi zote. 
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia. ''
-Hata kama kuna dhambi ya aina gani inakutesa lakini kama unautaka uzima wa milele ni lazima uachane nayo.
Luka 15:7 '' Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.''
-Wanaoutaka uzima wa milele ni lazima waache dhambi maana dhambi zina madhara makubwa.
Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA  wetu. ''
-Waenda uzima wa milele ni lazima wajitenge na dhambi yaani wakae mbali na dhambi siku zote.

        3. ALITAFAKARI, KUJIFUNZA NA KULIISHI NENO LA MUNGU: 
-Waenda mbinguni lazima walitafakari na kulitendea kazi Neno la MUNGU.Neno la MUNGU ni Biblia
Zaburi 4:4 '' Mwe na hofu wala msitende dhambi, Tafakarini vitandani mwenu na kutulia.'' 
-Waenda mbinguni ni lazima wajifunze neno la MUNGU na kulitendea kazi.
Wakolosai 3:16 '' Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. ''
-Waenda mbinguni ni lazima waliishi neno la MUNGU yaani waishi kwa kulitii Neno la MUNGU lile walalojifunza kanisani au kwenye mikutano ya injili au semina mbalimbali za kiroho.
Luka 7:24 ''  Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;''
-Ndugu hakikisha unatendea kazi lile neno la MUNGU ulilofundishwa, usitendee kazi neno la mtu ila tendea kazi neno la MUNGU.
Yakobo 1:22-24 ''  Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. ''

      4.ASIIPENDE DUNIA: 
-Kuipenda dunia ni kupenda anasa zake.
- kuipenda dunia ni kupenda vitu vya kidunia ambavyo ni machukizo kwa MUNGU. 
1 Yohana 2:15-17 '' Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda BABA hakumo ndani yake. Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na BABA, bali vyatokana na dunia. Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya MUNGU adumu hata milele ''
-Kuipenda dunia ni kufanya mambo ya kidunia ambapo mengi katika hayo yana undugu na kuzimu.
-Kuipenda dunia ni kupenda dhambi za duniani na kuzitenda.
1 Kor 2:12 '' Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali ROHO atokaye kwa MUNGU, makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na MUNGU. ''

     5. AVUMILIE KUJARIBIWA KWA IMANI YAKE: 
Imani ya KRISTO ni ya dhamani sana maana ndio imani ya uzima wa milele hivyo lazima ipingwe. ipo moja tu imani ya kweli ambayo kwayo utauoata uzima wa milele. Imani ya kweli chanzo chake ni kulisikia Neno la KRISTO.
Warumi 10-17 ''  Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.''
-Wakati mwingine huja majaribu lakini nena la BWANA YESU ni kwamba uvumilie hadi mwisho.
Marko 14:38 '' Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. ''
-Maombi ni lazima kwa mwenda mbinguni lakini pia ni lazima kuvumilia majaribu.
1 Kor 10:13 ''  Jaribu halikuwapata ninyi, isipokuwa lililo kawaida ya wanadamu; ila MUNGU ni mwaminifu; ambaye hatawaacha mjaribiwe kupita mwezavyo; lakini pamoja na lile jaribu atafanya na mlango wa kutokea, ili mweze kustahimili.''
-Mwenda mbinguni huyashinda majaribu.
Yakobo 1:2,3,12 '' Ndugu zangu, hesabuni ya kuwa ni furaha tupu, mkiangukia katika majaribu mbalimbali; mkifahamu ya kuwa kujaribiwa kwa imani yenu huleta saburi. Heri mtu astahimiliye majaribu; kwa sababu akiisha kukubaliwa ataipokea taji ya uzima, BWANA aliyowaahidia wampendao.''

   6.  KUENENDA  NA KUONGOZWA NA ROHO MTAKATIFU: 
- ROHO MTAKATIFU ni muhimu sana kwa maisha ya wateule, -ROHO MTAKATIFU atakuwa na wateule milele. Kama huna -ROHO MTAKATIFU ni vugumu sana kushinda dhambi. 
Warumi 8:9 '' Lakini ikiwa ROHO wa MUNGU anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na ROHO  wa KRISTO, huyo si wake.''
-Kama huna ROHO MATAKTIFU ni vigumu sana kukwepa hila za shetani. ROHO MTAKATIFU ndiye huushuhudia uzima wa milele ndani yetu.
Warumi 8:14,16 '' Kwa kuwa wote wanaoongozwa na ROHO wa MUNGU, hao ndio wana wa MUNGU.  ROHO mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa MUNGU; ''

    7. YAFIKIRI YALIYO JUU SIO YALIYO CHINI
-Kufikiri yaliyo juu kutakufanya ujitahidi sana ili usije ukaukosa uzima wa milele. 
 Wakolosai 3:1-3 ''  Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na KRISTO, yatafuteni yaliyo juu KRISTO aliko, ameketi mkono wa kuume wa MUNGU. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU.''
-Kama mtu unawaza kwamba miaka michache ijayo utaenda mbinguni kuishi milele na unajua kabisa kutenda dhambi yeyote kunaweza kukufanya usitimize lengo la uzima wa milele, naamini kabisa utajitahidi sana ili usiikose mbingu ndio maana Biblia inatushauri kuyatafakari yaliyo juu.
-Kutafakari yaliyo juu ni pamoja na kumtafakari MUNGU na upendo wake kwako.
-Kutafakari yaliyo juu ni pamoja na kufakari uzima wa milele.


Wafilipi 3:20 '' Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, BWANA YESU KRISTO;''

Naamini umejifunza kitu na kama mtu akikuuliza njia za kumfanya mtu aurithi uzima wa milele utamueleza zote na kumsihi azifuate zote maana zamani hizi ni za uovu na pia watenda dhambi hawataurithi ufalme wa MUNGU wakiwa na dhambi zao, ila kama wanautaka uzima wa milele basi watubu sasa na kumpokea BWANA YESU.
1 Yohana 5:11-12 '' Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba MUNGU alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe. Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa MUNGU hana huo uzima. ''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments