AINA 12 ZA WATU WASUMBUFU KATIKA JAMII! WATU AINA YA SPONJI

Na Mchungaji Peter Mitimingi, Huduma ya The Voice of hope Ministry.

Katika orodha ya watu wasumbufu unaopaswa kuwajua tunaingia kwa mtu wa pili. Mtu huyu anaitwa Sponji. Je unaifahamu sponji? Tunayo magodoro yaliyotengenezwa na sponji. Ukichukua kipande cha sponji ukakiingiza kwenye bakuli lililojaa maji ni nini kitatokea? Maji yote yaliyojaa kwenye bakuli yatahamia kwenye sponji. Lile sponji lenyewe lilikuwa halina hata tone wala chanzo chochote cha maji lilikuwa kavu. Lakini ukilishika baada ya hapo limeshakuwa zito limejaa maji. Kwa hiyo kila ukiliingiza hilo sponji kwenye bakuli lililojaa maji litafyonza maji yote yaliyomo kwenye bakuli na kuyaingiza ndani yake.
Sponji ni Mtu wa Kupokea tu kamwe Hatoi Kitu
Je umeanza kupata picha ya watu wa aina hiyo wenye tabia ya sponji? Hao watu wanaoitwa sponji hakuna siku watatoa walichonacho. Wao ni wafyonzaji tu. Wao hula vya wengine tu. Hakuna siku watalisha, hakuna siku watatoa vya kwao. Kila siku watasema, “Jamani naomba, jamani nisaidieni. Jamani nimeshachukua hii, nimeshachukua na hii.” Wewe ni lini utatoa? Sponji ni aina ya watu ambao hawana tabia ya kutoa ila wana tabia ya kuchukua. Wana tabia ya kupenda kupewa tu, hawawezi kutoa. Na hao watu wapo sana katika makanisa. Huyu ni mtu ambaye wakati wote yeye ni mhitaji. Wanatumia vitu na mali za watu wengine kwa manufaa yao binafsi. Anataka yeye tu ndiye apewe, na asipopewa anakuwa mkali kama pilipili!
Mtu huyu hatoi sadaka, wala fungu la kumi, wala michango. Inapotokea amefiwa na mwili wa ndugu yake ndio unatakiwa usafirishwe, ikahitajika achangiwe, atadai michango kama vile alikopesha! Usipomsaidia inakuwa ni kesi kubwa kuliko kesi nyingine zote. Kwa sababu ni mtu amejihesabia haki ya kupewa, haki ya kupokea. Na kamwe hatoi. Tunasoma katika Biblia mstari ambao ni muhimu sana.
Matendo 20:35
Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea Hii ni dondoo tu lakini ujumbe kamili unapatikana katika kitabu kifuatacho, kitafute na utapata maarifa makubwa . Wasiliana na Mchungaji Peter Mitimingi.

.

Comments