Askofu Gwajima amtaka Rais Kikwete kuvikemea vyombo vya Dola vinavyomfuatafuata

Askofu Mkuu  Dr Josephat Gwajima.

Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuvikemea vyombo vya dola vinavyomfuatafuata vikihoji mambo binafsi na kwamba akishindwa kufanya hivyo itakuwa wazi kwamba yeye ndiye anawatuma.


Akihubiri mamia ya waumini wa kanisa hilo jana, Gwajima alisema amekuwa akifuatwafuatwa na vyombo vya Serikali utadhani yeye si raia wakati ni Mtanzania halisi.

“Rais Kikwete tafadhali namuomba awakemee watu hawa... asipowakemea, basi kanisa langu litajua kwamba yeye ndiye anayewatuma,” alisema Gwajima huku akishangiliwa na waumini waliokuwa wakimsikiliza.

Huku wakinyeshewa na mvua, waumini hao walikuwa wakimsikiliza Askofu Gwajima, siku tatu baada ya kiongozi huyo kuhojiwa kwa mara ya pili na polisi na kutakiwa awasilishe mambo 10 yanayohusiana na usajili wa kanisa, uongozi na mali zake.

Uraia wake
“Mimi ni Mtanzania halisi acheni nifanye kazi ya Mungu, kama mnadhani mimi si Mtanzania, basi mmepotoka kwani kwa hilo mtashindwa,” alisema.

Alisema makundi ya jamii yamekuwa yakitoa kauli mbalimbali lakini hayabughudhiwi anavyofanyiwa.

“Madaktari, wanasiasa, wafanyabiashara wamekuwa wakitoa misimamo yao lakini hawabughudhiwi iweje Gwajima tu? Nitaendelea kuwapa vidonge vyenu kila mtakapopotoka, nafanya kazi ya BWANA,” alisema.

Kuhusu utajiri wake
Gwajima alisema amekuwa akishangazwa na vyombo vya Serikali vinavyohoji utajiri alionao bila kujua anaongoza idadi gani ya waumini. Alisema anaongoza kanisa lenye waumini zaidi ya 70,000 ambao ni kama watoto wake na kwamba yeye ni baba yao wa kiroho.

“Waumini hawa mimi ni baba yao wa kiroho, nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 tu nitakuwa na Sh70 milioni, halafu mnahoji utajiri ninaupata wapi?” alisema na kisha kuwauliza waumini hao... “Hivi baba yenu nikiwaomba kila mmoja anipe Sh1,000 mtanipa au mtaninyima?”

Alijibiwa, “Tutakupaaaa!” Baada ya majibu hayo waumini hao walianza kupeleka fedha katika jukwaa kuu huku wakiimba nyimbo za kumtukuza Mungu.



Waumini hao, wengi wao wakiwa wameshikilia noti za Sh10,000 na Sh5,000 walianza kusonga mbele na kutumbukiza kwenye maboksi.

Mchango huo ulichukua dakika 25 kuanzia saa 6.30 hadi saa 6.55 mchana na ulisimama pale Askofu Gwajima kuwaambia... “Basi basi naomba muache kuleta fedha, zinatosha, kaeni msikilize mahubiri, tukiendelea kupokea fedha hapa tutakesha. 



Watu wa idara ya fedha kusanyeni maboksi yenye fedha na pelekeni kunakohusika, hizi ni fedha za kanisa ambazo zitatumika katika mambo mbalimbali ikiwamo kununua mafuta ya kuendesha jenereta la kuzalisha umeme.”

Gwajima alisema kutokana na idadi ya waumini wake kama kila mmoja atampa Sh10,000 basi atakuwa na Sh700 milioni.

“Wakinipa Sh100,000 kila mmoja ina maana nitakuwa na Sh7 bilioni, nawashangaa wanaohoji kuwa huu ni utajiri, watu hawalali usingizi wanajiuliza Gwajima anapata wapi utajiri huu, nawaambia mimi siyo tajiri hizi ni fedha za kanisa,” alisema.


Idadi ya waumini
Askofu huyo alisema mbali na utajiri, watu wanahoji anapata wapi waumini wengi namna hiyo.

“Shida si kumkashifu Askofu Pengo, bali sasa wanahoji waumini wengi wanafuata nini hapa,” alisema na kuongeza,” nao wakija kunisikiliza watafahamu nini mnachokifuata kwani nao watabaki hapahapa hawatatoka.”

Alisema baada ya kuandamwa na vyombo vya Serikali, maaskofu walitaka kutoa tamko lakini aliwakataza kwa sababu aliona anafanyiwa hivyo kwa sababu binafsi. Alisema katika kipindi ambacho amekuwa akiandamwa na polisi, waumini wameongezeka kanisani kwake.

“Walokole wakiwa katika tabu, ndiyo kwanza wanashikamana, ukitaka kuwasambaratisha wape neema utafanikiwa. Wakipata nyumba nzuri, gari zuri, kazi nzuri na safari katika nchi mbalimbali wanaacha kuja kanisani lakini wakiwa katika matatizo wanashikamana, hamuwezi kuwasambaratisha,” alisema.

Ilivyokuwa awali
Gwajima amehojiwa mara mbili na polisi kutokana na matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, lakini mara ya pili mwelekeo wa mahojiano ulibadilika ukalenga zaidi kanisa na mali zake.

Mara ya kwanza kuhojiwa ilikuwa Machi 27, siku ambayo alizimia na kupelekwa katika Hospitali ya TMJ alikolazwa kwa siku nne huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa baada kuhojiwa mambo yake binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.

Baada ya kutoka Polisi, Gwajima amekuwa akitembea kwa kutumia kiti cha magurudumu mawili hadi Aprili 6, Siku ya Pasaka baada ya kuombewa na wachungaji kutoka Japan.

Alhamisi iliyopita, alihojiwa kwa mara ya pili na kutakiwa kurudi tena Polisi Aprili 16 akiwa na mambo 10 yakiwamo hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini, idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa, muundo wa uongozi wa kanisa, waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa na nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari.



Source:Mwananchi

Comments