ASKOFU? SIFA 16 ZA ASKOFU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze.
Leo namzungumzia Askofu, kazi ambayo Biblia inasema ni kazi njema sana.
Askofu ana sifa zilezile za mchungaji na askofu hutokana na wachungaji.
Askofu ni mwangalizi.
1 Timotheo 3:1-7 '' Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema.Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;(yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la MUNGU?) Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi. ''

 
SIFA 16 ZA ASKOFU NI.


1.Askofu lazima awe asiyelaumiwa kwa sababu ya uovu wowote. ila uwe uovu wa kweli sio udaku wa magazetini ambao ni mkakati wa shetani kuzuia injili ya BWANA YESU ili isiwafikie maelfu ya watu maana wataanza kudanganyana kwa kutumia gazeti lenye uhusiano na shetani.

2. Askofu lazima awe katika ndoa ya mke mmoja. mwenye wake wawili au mwenye masuria huyo sio askofu maana hana sifa njema ya askofu.

3. Askofu lazima awe na kiasi. sio kwa sababu wewe ni askofu basi ndiye kila kitu katika huduma, hapana haiko hivyo.

4. Askofu lazima awe na busara za ki-MUNGU. kuna busara za ki-MUNGU, Kuna busara za kibinadamu na kuna busara za kishetani. Askofu lazima awe na busara za ki-MUNGU kwa kuongozwa na ROHO MTAKATIFU. Askofu lazima akemee upotovu maana ana busara ya ki-MUNGU. Mwenye busara za ki-MUNGU lazima tu awe na msimamo na hawezi kufanya jambo kwa lengo la kumpendelea mtu. Ndio ya askofu ni ndio na sio ya askofu ni sio. sio askofu ambaye ni ndiyo sio. akiwa na wenzake ni ndio na akiwa pekeyake ni sio. huyo hafai.

5.Askofu lazima awe mtu wa utaratibu mzuri. utaratibu mzuri ni pamoja na kuwa na maono mazuri na mikakati mizuri ya kuhakikisha watu wote wanaokolewa na BWANA YESU.

6.Askofu lazima awe mkaribishaji. sio askofu kumuona lazima utume barua ya maombi na ichukue miezi 4 ndipo umuone, hapana. wakati mwingine huduma inaweza kuwa kubwa na askofu hawezi kuonana na kila mtu mmoja mmoja hivyo askofu lazima awe na wasaidizi au watenda kazi wenzake ambao watawasaidia watu kiroho. 

7. Askofu lazima awe anajua kufundisha neno la MUNGU kwa ufasaha. askofu lazima ajua kwamba mbinguni wataingia watakatifu tu hvyo ahakikishe anawafundisha watu utakatifu, kumtegemea MUNGU, Kumtii ROHO MTAKATIFU, Kuenenda kwa imani na kuhubiri injili ya KRISTO inayookoa. askofu akiipoozesha injili ya BWANA YESU inayookoa huyo hafai.

8. Askofu hatakiwi kuwa mlevi. kama askofu atakuwa mnywa pombe basi hakika atawafundisha waumini wake kunywa pombe na kujikuta mna kanisa la walevi. Biblia inasema ''Tena msilewe kwa mvinyo, ambamo mna ufisadi; bali mjazwe ROHO;- Waefeso 5:18 ''

9.Askofu hatakiwi kuwa mpiga watu. asiwapige watu kwa vyovyote hata kama ni kwa maneno ya laana hatakiwi kuwalaani bila sababu za kimbinguni.

10. Askofu anatakiwa awe mpole. upole ambao uko kwa jinsi ya KRISTO. Upole ambao sio wa kuacha kukemea wala sio upole wa kuacha kuonya na kukaripia kwa yule anayeipindisha sheria ya BWANA YESU. Upole wa kuvumilia na upole wa kuwahurumia wanadamu ili wasiende jehanamu hivyo anawaonya.

11. Askofu hatakiwi kuwa mtu wa kujadiliana katika mambo ambayo hayambariki MUNGU. Askofu hatakiwi kuwa mfano kwenye ubishi wa kubishania mpira au siasa.

12. Askofu hatakiwi kuwa mpenda fedha. asiwe mpenda fedha za aibu ,1 Timotheo 6:9-11 '' Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu. Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi. Bali wewe, mtu wa MUNGU, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole. ''
-Sio kwamba Askofu hatakiwi kuwa tajiri bali anatakiwa kuwa tajiri lakini utajiri wa haki, sio tamaa ambazo husababisha kudanganywa na hata unaweza ukauza kanisa kwa tamaa tu.


13.Askofu lazima awe anajua kuisimamia nyumba yake vyema. sio watoto wa askofu wanakuwa ndio chanzo cha huduma kuyumba, sio mabinti wa askofu ndio huvaa kikahaba kabisa, kwa staili hiyo hata kanisa litaiga maana Askofu hamkemei binti yake. haiwezekani mtoto wa askofu ndio mtaalamu wa kutoa mimba, hiyo haifai maana kanisa litaiga ujinga huo. Sio askofu kila siku yeye na mkewe ni ngumi, sasa ikiwa hivyo je waumini itakuwaje?

14. Askofu lazima ajue kutiisha watoto wake ili wawe na adabu nzuri. sio mtoto wa askofu hajawahi kufunga tangu miaka 4 iliyopita, ni mbaya. sio mtoto wa askofu ndio mtalaamu wa kutukana , ni mbaya hiyo. askofu lazima awakemee.

15. Askofu hatakiwi kuwa mtu aliyeokoka juzijuzi tu maana anaweza akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.

16. Askofu lazima ashuhudiwe mema na watu wote. sio mara askofu jana ailikuwa bar maana tulimuona saa 8 usiku, mara askofu kazaa na mke wa fulani, haitakiwi kuwa hivyo ila hao wanaomshuhudia lazima washuhudie ukweli maana maelfu ya watu siku hizi hupotoshwa na magazeti ambayo shetani ndiye mmiliki wake yaliyo mengi. hatushuhudii kwa habari za mitandaoni wala magazeti ya udaku bali tunashuhudia kile ambacho ni halisi kabisa.
Tito 1:7-11 ''Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno ,kwa kuwa ni wakili wa MUNGU;asiwe mtu wa kujipendeza nafsi yake,asiwe mwepesi wa hasira,asiwe mlevi wala mgomvi,asiwe mpenda mapato ya aibu.bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake;akilishika lile neno la imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.Kwa maana kuna wengi wasiotii, wenye maneno yasiyo na maana, wadanganyaji, na hasa wale wa tohara, ambao yapasa wazibwe vinywa vyao. Hao wanapindua watu wa nyumba nzima, wakifundisha yasiyowapasa kwa ajili ya mapato ya aibu. ''
Kazi ya uaskofu ni kazi njema sana ila inahitaji umakini mkubwa sana.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
mabula1986@gmail.com
+255714252292.
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments