BWANA YESU KRISTO NDIYE PASAKA WETU.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze kuhusu Pasaka
Jina la "PASAKA" limetokana na Neno ''pasakh''  kwa lugha ya Kiyahudi. Ni sherehe kubwa sana kwa kanisa la MUNGU.
Kwa Waisraeli kusherekea Pasaka ilikuwa ni agizo kutoka kwa BWANA MUNGU.

Kumb 16:1-2 ''Utunze mwezi wa Abibu, ukamfanyie pasaka BWANA, Mungu wako, kwa kuwa ilikuwa ni mwezi wa Abibu alipokutoa Misri usiku BWANA; Mungu wako. Nawe umchinjie pasaka BWANA, Mungu wako, katika kundi la kondoo na la ng'ombe, mahali atakapochagua BWANA apakalishe jina lake. ''
-Maana ya kwanza ya Pasaka ni Kondoo kuchinjwa kwa ajili ya kusudi maalumu.
-Pasaka ya kwanza ilifanyika katika Bustani ya Edeni. Baada ya Adamu na mkewe kufanya dhambi walijificha kwa sababu ya dhambi waliyoifanya maana walijiona uchi.
 MUNGU kwa upendo wake alichinja kondoo na kuwavika mavazi mazuri Adamu na mkewe. Vazi Kibiblia  lina maana kubwa sana na ndio maana hata Wokovu Wetu unaitwa vazi (Isaya 61:10, Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika MUNGU wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, ...... )
Na BWANA YESU anaendelea kuwaonya wateule wake waendelee kufua mavazi yao 
(Ufunuo 22:14, Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake. )
-Vazi walilovikwa akina Adamu sio vazi kama vazi tu ila lina maana  sana kiroho. Hiyo ilikuwa Pasaka ya kwanza.
-Ibrahimu alimchinja kondoo badala ya Isaka mwanae, hiyo nayo ina maana kubwa sana.
-Waisraeli hapo juu tumeona waliamriwa kabisa na BWANA kwamba wawe wanasherekea Pasaka.
Na yule ndugu aliyeniuliza kwamba kwanini BWANA YESU alisherekea Pasaka na wanafunzi wake huku sisi tukisherekea Pasaka nyingine ambayo ni ukombozi kupitia YESU naomba ajue kwamba BWANA YESU alipokuja duniani alipitia Israeli na Biblia iko wazi kabisa kwamba YESU alizaliwa chini ya sheria za kiyahudi na alizifuata ili kuzileta katika ukamilifu wake.
Wagalatia 4:4 '' Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, MUNGU alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,   ''
  Alizifuata sheria katika kuwapeleka wanadamu katika Ukweli sahihi wa sheria hizo.
na kwa ujio wake YES kulimaanisha mwanzo mpya. Kivuli ambacho ni Torati kimefika mwisho  maana mwili halisi ambao ni KRISTO sasa unaonekana
Waebrania 10:1 ''  Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao  ''
-Neno Pasaka kwa kiingeleza lina maana ya Passover yaani ni ile hali ya kupita kutoka sehemu moja na kuhamia sehemu nyingine  kwa makusudi  maalumu.
Kondoo alihusika sana Kama ishara ya Pasaka au ishara ya kuyafuata mabadiliko mengine.
Leo Pasaka wetu yupo, ni kondoo asiye na hila.
YESU KRISTO ndio Pasaka wetu yaani kwa kupitia yeye sisi sasa ni watu wapya. Tumefanyika wateule wa MUNGU na warithi sawasawa na ahadi za MUNGU.
Kupitia YESU KRISTO ambaye ndiye Pasaka wetu, Biblia inasema hivi

1 Kor 5:7 ''Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO;  '' 
-Pasaka wetu YESU KRISTO amekwisha kutolewa sadaka kwa ajili ya sisi kupata ondoleo la dhambi.
-Waisraeli walisherekea Pasaka kama tukio la kukumbuka kutoka utumwani Misri na kwenda katika nchi ya ahadi yaani kaanani.
-Walitoka Misri ya kimwili  na kuelekea kaanani ya kimwili vile vile . Lakini Wateule wa BWANA YESU leo hawasherekei kutoka Misri ya kimwili bali wanasherekea Kutoka Misri ya Kiroho yaani kwa shetani na sasa wako safarini wakielekea Kaanani yao yaani Uzima wa milele.
-Hatutakiwi kurudi Misri bali ni kuelekea Kaanani tukiwa watakatifu na wakamilifu waliookoka baada ya kumpokea BWANA YESU na kuanza kuishi kama neno la MUNGU litakavyo.

Kumpokea Pasaka wetu ambaye ni BWANA YESU lazima kuje mabadiliko katika maisha yetu.
Wakolosai 3:1-3 ''Basi mkiwa mmefufuliwa pamoja na KRISTO, yatafuteni yaliyo juu KRISTO aliko, ameketi mkono wa kuume wa MUNGU. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na KRISTO katika MUNGU.''
-Ndugu yangu, hakikisha kuna badiliko ndani yako, hakikisha mwili wako umekufa kwa habari ya dhambi na tamaa, na ukifa kufa matendo ya dhambi basi hakikisha unafufuka na KRISTO ukiwa mteule usiye na mawaa.
-Tunapokumbuka kufufuka kwa BWANA YESU lazima pia tuzingatie kile alichokuja kukifanya BWANA YESU. 
BWANA alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichokuwa kimepotea ambacho ni mimi na wewe. 
 Luka 19:10 '' Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea. ''
-Hili ndilo lengo kuu la kuja kwa BWANA YESU, Kututafuta na kutuokoa sisi tuliokuwa tumepotea.

Hivyo ni muhimu na wajibu wetu kuishi matendo yampendezayo BWANA YESU aliye Pasaka wetu.  
Warumi 6:2-4 '' Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi? Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika KRISTO YESU tulibatizwa katika mauti yake? Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama KRISTO alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa BABA, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.''
-Ndugu yangu, hakikisha utakatifu wa wakati wa pasaka unauendeleza siku zote za maisha yako.
Hakuna uzima nje na YESU KRISTO.
Hakuna mwanadamu atakayeenda uzima wa milele huku hamtaki YESU.

Luka 24:1-8 ''Hata siku ya kwanza ya juma, ilipoanza kupambazuka, walikwenda kaburini, wakiyaleta manukato waliyoweka tayari. Wakalikuta lile jiwe limevingirishwa mbali na kaburi,  Wakaingia, wasiuone mwili wa BWANA YESU.  Ikawa walipokuwa wakifadhaika kwa ajili ya neno hilo, tazama, watu wawili walisimama karibu nao, wamevaa nguo za kumeta-meta; nao walipoingiwa na hofu na kuinama kifudifudi hata nchi, hao waliwaambia, Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu? Hayupo hapa, amefufuka. Kumbukeni alivyosema nanyi alipokuwa akaliko Galilaya,  akisema, Imempasa Mwana wa Adamu kutiwa mikononi mwa wenye dhambi, na kusulibiwa, na kufufuka siku ya tatu. Wakayakumbuka maneno yake. '' 
-Nalipenda neno la Malaika kwamba ''Kwa nini mnamtafuta aliye hai katika wafu?''
-Hakika BWANA YESU yu hai milele na hukumu yote iko na yeye. 
Nakutakia pasaka njema, fufuka na BWANA YESU.
Ndoa yako ifufuke tena na BWANA YESU.
Omba maombi ya kufufua uchumi wako na biashara yako.
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.


Comments