ENENDENI KWA HEKIMA MBELE YA WALIO NJE HUKU MKIUKOMBOA WAKATI.


Wakolosai 4:5 '' Enendeni kwa hekima mbele yao walio nje, mkiukomboa wakati. ''
BWANA YESU asifiwe.
Kupitia andiko hilo tunajifunza mambo 7.

        1. Wanaoelezwa hayo  yote kwenye andiko hilo ni Wateule wa MUNGU ambao tayari walishampokea YESU KRISTO na wanaishi maisha matakatifu.
2 Kor 5:17 ''Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO  amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''
-Je wewe unayesoma ujumbe huu ni mmoja wao? na kama sio mmoja wao unadhani ni kwanini? majibu yote najua unayo wewe ila mimi Peter NAKUSHAURI TU KWAMBA UAMUE VYEMA.

       2. ''Enendeni kwa hekima '' Wateule wanaambiwa waenende maana yake hawana siku ya kupumzika kuenenda maana ni maisha yao yote waenende kwa hekima
2 Kor 8:21 ''  tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za BWANA tu, ila na mbele ya wanadamu.  '' .
- Kuenenda huku ni mfumo mzima wa maisha yao hawa wateule, na hawatakiwi kuenenda tu bali ni kuenenda kwa hekima, Je wewe ni mteule? kama sio mteule unasubiri nini kuwa mteule? Kama ni mteule unaenenda kwa hekima? na hekima ipi unayoenenda nayo? majibu yote unayo wewe mwenyewe ila mimi nakushauri uamue vyema.

       3.  ''Hekima''. Hekima ni elimu iliyo na akili nzuri ndani yake na akili hiyo imechanganya na maarifa. Maarifa ni elimu iliyo katika matendo. 

Kuna hekima za 3. 
-Hekima ya Ki-MUNGU ambayo ndio unayotakiwa kuenenda nayo na hekima hii inasimamiwa na ROHO MTAKATIFU
Mithali 2:6 '' Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu;  ''.
-kuna hekima ya kibinadamu ambayo huendeshwa na nafsi ya mtu na wakati mwingine hekima hii inaweza kuwa na hila ndani yake, Mteule wa MUNGU hatakiwi kuitegemea hekima hii. 

-Hekima ya tatu ni hekima ya kishetani. Kama umewahi kumwombea mtu mwenye mapepo unaweza kabisa kuona hekima ya kipepo ambayo pepo kupitia mtu linaweza kuongea. Kuna pepo moja kupitia mtu mmoja aliyekuwa anaombea, pepo hilo lianza kusema kwamba kuna wachungaji ni watu wa shetani na wametumwa na shetani, watu waliokuwa wanaombea walikodoa macho yote na kuanza kusikiliza jini likiwataja watumishi hao, kumbe ni uongo na mbinu ya majini hayo kuitana ili yaongezeke ndani ya mtu na mshindwe kuyatoa maana wakati yakiwasimulia uongo mtashindwa hata kukemea. ilikuwa ni hekima ya uongo ya kupotosha na kuhakikisha watu wanachanganyikiwa kabisa hata kama wakiwa kwenye imani ya Kweli. Hekima ya mapepo inaweza hata ikasema kwamba Mungu Hatawahukumu wanadamu maaana anawapeda sana kumbe uongo. Pepo linaweza kuongea kupitia mtu kwamba YESU amesharudi na yuko nchi fulani. ni hekima ila ni hekima ya kishetani. BWANA YESU hakuwa anawaruhusu sana mapepo kuongea maana mapepo ni watoto wa shetani na watoto wa shetani ni waongo kama baba yao shetani alivyo muongo daima. Je ndugu, wewe ni mteule wa MUNGU? Kama hujaokoka je unasubiri nini? Na kama ni mteule je unahekima gani au unatumia hekima gani ndani yako? Majibu yote unayo wewe mimi Peter Nakushauri tu uamue vyema.

     4. ''Walio nje''. Kumbe kuna walio nje Wokovu wa BWANA YESU. Kama watabaki kuwa nje sasa na hata siku ile wanaweza kujikuta wako nje ya Uzima wa milele.
Ufunuo 22:15 '' Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.  ''.
-nje ni kubaya sana na haitakiwi mtu awe huko nje. Je ndugu uko nje? na kama uko nje unapanga kuingia ndani lini? Majibu yote unayo wewe lakini nakushauri uamue kuingia ndani yaani kwenye wokovu wa BWANA YESU.

5 ''Mkiukomboa wakati.''. Kazi mojawapo ya wateule wa MUNGU ni kuukomboa wakati, maana yake kuishi kama wapitaji hapa duniani maana siku yoyote isiyofahamika kuna kuondoka.
1 Petro 2:11 ''  Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.   ''.
 -Wakati huu sio wa kuchekelea dhambi wala kulala. Ni wakati wa toba ya kweli na maombi. Ni wakati wa kuwaombea ndugu zako na familia yako ili wasiende jehanamu. Ni wakati wa kuishi kama wapitaji maana duniani sisi sio wakaaji bali wapitaji, tungekuwa wakaaji basi tungekuwa kama Bahari  ambayo ipo tangu mwanzo wa uumbaji wa MUNGU. Je wewe ni mteule wa BWANA YESU? Kama sio mteule wa MUNGU unapanga kuwa mteule lini? na kama ni mteule je unaukomboa wakati? Majibu yote unayo wewe ila mimi nakushauru tu uamue vyema.

6. ''Walio ndani'' Walio ndani ni watakatifu wa MUNGU, Walio ndani ni wateule wa MUNGU. Walio ndani ni wale waliompokea YESU kama BWANA na MWOKOZI wa maisha yao na kuendelea kuishi maisha matakatifu.
Luka 13:24 ''  Jitahidini kuingia katika mlango ulio mwembamba, kwa maana nawaambia ya kwamba wengi watataka kuingia, wasiweze. ''.
-Kuna mlango wa kuingia ndani huko.
Je wewe ni  uko ndani ya wokovu wa BWANA YESU? Kama hauko ndani je unapanga kuingia ndani lini?
Kumbuka ndani  ya wokovu ndiko kuna uzima wako wa milele kama ukiamua uhusike na uzima huo.

7. Nini kinawafanya watu wawe ndani na wengine wawe nje.
Kumkataa YESU na Dhambi ndivyo vitu viwili Vinawafanya watu wawe nje ya Wokovu wa BWANA YESU  na kuwa nje ya Uzima wa milele.
Yohana 3:17-21 '' Maana MUNGU hakumtuma Mwana ulimwenguni ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi; asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa MUNGU.Na hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru; kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika MUNGU.  ''
-Kinachowafanya watu wawe ndani ni Kuokoka na kuishi maisha matakatifu.
 Je wewe uko nadni au nje? wewe ndiye mwenye majibu yote, mimi kazi yangu ni kukushauri tu.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments