HATIMAYE SIKU YA MWISHO ITAFIKA.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno hai la MUNGU Mwenyezi.

Hatimaye siku ya mwisho itafika.

Siku hiyo wababe wote wa dunia watakuwa wapole kama kondoo.

Wanaokataa Wokovu wa BWANA YESU leo siku hiyo watakuwa wapole sana.

Isaya 1:31 ‘’ Na mtu hodari atakuwa kama makumbi, na kazi yake kama cheche ya moto; nao watawaka pamoja, wala hapana atakayewazima. ‘’

-Watu hodari siku hiyo watakuwa wapole.

-Wale hodari kwa kufanya dhambi watawaka moto wala hapana wa kuwazima.

-Wanaomkataa YESU leo siku hiyo watamjua yeye ni nani.

-Siku hiyo BWANA pekee ndiye atakayetukuzwa..

Isaya 2:11-12 ‘’ Macho ya mwanadamu yaliyoinuka yatashushwa chini, na kiburi cha mwanadamu kitainamishwa, naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Kwa maana kutakuwa siku ya BWANA  wa majeshi juu ya watu wote wenye kiburi na majivuno, na juu ya yote yaliyoinuka; nayo yatashushwa chini.   ‘’.

-Wanaojivuna leo kwa sababu ya umaarufu wao wa dhambi, siku hiyo watakuwa wapole sana.

-Wanaotesa wanadamu wenzao leo, siku hiyo watawaka moto milele.

-Watenda dhambi wasiotubu leo, siku hiyo watalia na kusaga meno hadi meno yataisha nab ado hata asilimia 1% ya kulia watakuwa hawajaimaliza.

Maonyo hayo ni makali lakini muda wa kugeuka na kutubu ni leo kabla ya kifo kufika.

Muda wa Kuokoka na kuanza kuliishi neno la MUNGU ni leo wala sio kesho.Usikubali kumkataa YESU.

Ni muda wa kuacha dhambi maana ukiendelea na dhambi  maisha yako yote basi tambua kwamba kuna ziwa la moto mbeleni. Ni ziwa la moto ambalo watakaoingia humo watazama na kuteseka milele. Hakutakuwa tena na kifo wakati huo, kifo kitazuiliwa na yatakuwa mateso makali sana maana ndivyo Biblia isemavyo. BWANA YESU ni muhimu kwako leo kuliko yote uyawazayo wala uyatendayo. Mpokee na jina lako litaandikwa kwenye kitabu cha uzima.

Ukishindwa kumtii KRISTO basi hakika unamtii shetani.

Kumbuka shetani hatakuwa na wa kumcheka siku hiyo maana hata yeye na nabii wa uongo wake watatupwa kwenye ziwa la moto tena hata kabla ya wanadamu kuhukumiwa.

Siku hiyo inakuja, ndugu yangu, ni bora Kuokoka leo.

Viburi nya duniani havitamsaidia mtu yeyote.

Siku hiyo atatukuzwa BWANA pekee.

Isaya 2:17-20 ‘’ Na majivuno ya mwanadamu yatainamishwa, na kiburi cha watu kitashushwa; naye BWANA, yeye peke yake, atatukuzwa siku hiyo. Nazo sanamu zitatoweka kabisa. Na watu wataingia ndani ya pango za majabali, na ndani ya mashimo ya nchi, mbele za utisho wa BWANA  na utukufu wa enzi yake, atakapoondoka ili aitetemeshe mno dunia. Siku hiyo kila mtu atazitupilia mbali sanamu zake za fedha, na sanamu zake za dhahabu, walizojifanyia ili kuziabudu, kwa fuko na popo;  ‘’

-Siku hiyo hakutakuwa na mtu maarufu na Yule ambaye hakuwa maarufu duniani.

Siku hiyo hakutakuwa na raisi wala mbunge, hakutakuwa na diwani wala meneja, hakutakuwa na machinga wala mamantilie, wote watakuwa sawa wakihukumiwa kila mmoja sawasawa na dhambi Na matendo yake.

Hakuna umaarufu  wa sasa wa mtu utakaomsaidia siku hiyo.

Ndugu yangu, Leo yako ndio inayoamua kesho yako itakavyokuwa. Mwamini YESU leo na mpokee ili kesho yako iwe mbinguni na sio motoni.

Mpokee YESU KRISTO leo,  ishi maisha matakatifu, jitenge na dhambi na jitenge na kila machukizo.



Wanaomdharau YESU leo siku hiyo watapiga magoti mbele yake bila mafanikio.

Wanaomdharau BWANA YESU leo siku hiyo watamkiri sana ila watakuwa wamechelewa.

Wafilipi 2:9-11 ‘’ Kwa hiyo tena MUNGU alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;  ili kwa jina la YESU kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI BWANA, kwa utukufu wa MUNGU BABA.  ‘’

-Kumkataa YESU ni kuukataa uzima wa milele.

Ndugu yangu uliyesoma ujumbe, nakuomba kama hujampokea BWANA YESU basi mpokee leo maana hujachelewa. Kama umeshaokoka tayari basi shikilia sana ungamo lako.

MUNGU wa mbinguni aleta neema yake kuu ya Wokovu Kwa kila ndugu atakayesoma ujumbe huu.

Waefeso 1:17-23 ‘’ MUNGU wa BWANA wetu YESU KRISTO, BABA wa utukufu, awape ninyi roho ya hekima na ya ufunuo katika kumjua yeye;  macho ya mioyo yenu yatiwe nuru, mjue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo; na utajiri wa utukufu wa urithi wake katika watakatifu jinsi ulivyo;  na ubora wa ukuu wa uweza wake ndani yetu tuaminio jinsi ulivyo; kwa kadiri ya utendaji wa nguvu za uweza wake; aliotenda katika KRISTO alipomfufua katika wafu, akamweka mkono wake wa kuume katika ulimwengu wa roho;  juu sana kuliko ufalme wote, na mamlaka, na nguvu, na usultani, na kila jina litajwalo, wala si ulimwenguni humu tu, bali katika ule ujao pia; akavitia vitu vyote chini ya miguu yake, akamweka awe kichwa juu ya vitu vyote kwa ajili ya kanisa; ambalo ndilo mwili wake, ukamilifu wake anayekamilika kwa vyote katika vyote. ‘’

-BWANA YESU ana mamlaka kuu san asana.

Siku ya Mwisho BWANA YESU atakuja kuhukumu wanadamu wote.

Ukimkimbia leo na Wokovu wake basi siku hiyo utakuwa na hasara.

Ndugu Mkimbilie BWANA YESU leo. Yeye BWANA YESU anasema

Ufunuo 22:12-13 ‘’ Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.   ‘’
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments