IMANI YA UZIMA IPO MOJA TU, ISHINDANIE.



BWANA YESU asifiwe.
Ni siku nyingine aliyoifanya MUNGU mwenyezi ili tuiishi.
Namshukuru sana BWANA YESU maana agizo lake ninalifanya, Karibia mwaka wa 3 sasa tangu nianze kupost Neno lake mtandaoni na amenipa masomo zaidi ya 250 na sasa kazi inaendelea, Namshukuru MUNGU kwa wale waliobadilika, kutiwa moyo, kurekebisha, kuongezewa imani na kumpokea YESU kupitia Masomo yangu. Wengi wamenijulisha kwamba masomo hayo yamewasaidia hakika ni jambo jema sana na utukufu Wote kama ulivyo tunampa BWANA YESU KRISTO Mwenye kuianzisha na kuitimiza Wokovu wetu

(Waebrania 12:2, tukimtazama YESU, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha MUNGU.)
Leo nazungumzia kuishindania Imani ya uzima ambayo ipo moja tu.
-Imani Ya Uzima Hushindaniwa.
- Imani Ya Uzima Ipo Moja Tu Yaani Wokovu Wa YESU KRISTO, Biblia inasema

Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.''
-Ni jina la YESU KRISTO pekee, hiyo ndio imani ya pekee ya uzima, na imani hii ya uzima lazima tuishindanie.
Imani hiyo ya uzima ni moja tu na chanzo chake ni kulisikia neno la KRISTO na kumpokea kama BWANA na MWOKOZI wako na baada ya hapo unatakiwa ujiunge na wana kanisa wengine katika kuukulia wokovu na kuomba.
''Basi imani, chanzo chake ni kusikia; na kusikia huja kwa neno la KRISTO.-Warumi 10:17''

-Hiyo ndio imani ya kweli ambayo unaipokea baada ya kulisikia Neno la KRISTO YESU na sio vinginevyo.
Ndugu, shika yote yanayoelekezwa katika Imani ya KRISTO kupitia Biblia maana yaliyo nje na KRISTO ni dhambi.

''Na kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi.Warumi 14:23b''
Imani Haishindaniwi Kwa Mapigano Bali Kwa Matendo Mema Ya Kumpendeza MUNGU tukiwa ndani ya imani hii ya uzima.
Hatutakiwi kuitwa tu wakristo bali tunatakiwa kuitwa wakristo walio na KRISTO ndani yao. Ni imani ya ndani kabisa ya moyo wa mtu, ni uhusiano wa ndani kabisa kati ya mwanadamu na muumba wake.

Ukiipokea imani hii ya uzima , Biblia inasema hivi
''Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.-2 Kor 5:17''
Kwanini Tunatakiwa Tuishindanie Imani Ya KRISTO?
= Ni Kwa Sababu Ndio Imani Pekee moja tu Ya Uzima Wa Milele
Yuda 1:3 ''Wapenzi, nilipokuwa nikifanya bidii sana kuwaandikia habari ya wokovu ambao ni wetu sisi sote, naliona imenilazimu kuwaandikia, ili niwaonye kwamba mwishindanie imani waliyokabidhiwa watakatifu mara moja tu. ''
=Ni kwa sababu kuna wakati mwingine kuna kupita kwenye nyakati ngumu na kupingwa.
Wafilipi 1:27-29 '' Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya KRISTO, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili; wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa MUNGU. Maana mmepewa kwa ajili ya KRISTO, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake; ''
-Katika Imani Yetu Ya Uzima Tunatakiwa Kujitahidi Sana Katika Yale Yanayompendeza MUNGU.
2 Petro 1:5-11 ''Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua BWANA wetu YESU KRISTO. Maana yeye asiyekuwa na hayo ni kipofu, hawezi kuona vitu vilivyo mbali, amesahau kule kutakaswa dhambi zake za zamani. Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe. Maana hivi mtaruzukiwa kwa ukarimu kuingia katika ufalme wa milele wa BWANA wetu, Mwokozi wetu YESU KRISTO.''.
-Tunaposema Tunaishindania Imani Maana Yake Tunafanya Yale Tu Yanayokubalika Na Imani Hiyo Ya Uzima.
-Kwenye Imani Ya Uzima Lazima Tujue Kwamba Tunashindana Na Maadui Ambao Wanataka Kututoa Kwenye Imani Hiyo Pekee Ya Uzima

Maadui Hao Ni
-Shetani Na Majeshi Yake,
-Dunia Na Anasa Zake
-Pamoja Na Mwili Na Matakwa Yake.

Hivyo Tukijua Tuko Kwenye Mashindano Na Tuvumilie Maana Tumepewa Imani Sio Kuamini Tu, Bali Na Kuishindania Na Kuteswa Pia Kwa Ajili Ya Imani
Wafilipi 1:29 ''Maana mmepewa kwa ajili ya KRISTO, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;.''
-Katika Imani Lazima Tuzae Matunda Na Kumpendeza MUNGU.
Wakolosai 1:10 ''mwenende kama ulivyo wajibu wenu kwa BWANA, mkimpendeza kabisa; mkizaa matunda kwa kila kazi njema, na kuzidi katika maarifa ya MUNGU; ''.
-Katika Imani Lazima Kusaidiana Kiroho.
Wafilipi 4:3-6 '' Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima. Furahini katika BWANA sikuzote; tena nasema, Furahini. Upole wenu na ujulikane na watu wote. BWANA yu karibu. Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na MUNGU. ''
Shika Imani Ya Uzima Daima siku zote wala usisitesite.
MUNGU anasema.

''Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.- Waebrania 10:38''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili. MUNGU Akubariki.

Comments