JE UMEVAA VAZI AU BADO UKO UCHI?



 
BWANA YESU asifiwe.

Karibu tujifunze ujumbe maalum kwa ajili ya kila Mwanadamu.

Adamu na Eva walipokubali kuzidiwa ujanja na shetani. waliogopa na kujificha kwa sababu walijiona wa tofauti sana.

Hawakuwa kama walivyokuwa zamani.

Uwepo wa MUNGU uliondoka.

Walishindwa kujiamini tena, walikuwa na hofu kubwa.

Walikuwa uchi.
Mwanzo 3:21 '' BWANA MUNGU akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. ''

-Ndivyo leo watenda dhambi walivyo.

-Watenda dhambi wako uchi tena uchi wa mnyama maana Vazi lao hawana.

-Ndio kazi ya shetani kuwavua nguo wanadamu ili wabaki uchi siku zote.

Aliye uchi hana haki, huwezi kuwa uchi harafu ukaanza kuhubiri, hata kama una upako kiasi gani lakini ukiwa uchi lazima tu ushindwe kwenda katika uzuri autakao MUNGU.

-Mchungaji kuwa uchi harafu unawahubiria waumini wako waliovaa nguo.

-Hata kama una hotuba nzuri kiasi gani Mweshimiwa, huwezi kuwahutubia raia wako ukiwa uchi.
Baada ya Adamu na Eva kutenda dhambi, MUNGU aliwavika mavazi kwa neema yake, hayo mavazi yana maana sana na ndio maana hata mbinguni unaweza kuwakuta kwa sababu ya kile kitu kizuri ambacho MUNGU alikifanya kwao.

Ndugu zangu kuna vazi na vazi hilo anatakiwa alivae mwanadamu, mwenye dhambi akilivaa anaitwa mtakatifu. Na mtakatifu aliyevaa vazi hilo anatakiwa aishi kama vazi hilo litakavyo lasivyo vazi hilo linaweza kujiondoa kwake au likachafuka na akakosa sifa za uzima wa milele. Vazi hilo tunavikwa na MUNGU pekee kwa neema yake ambayo tunatakiwa tuitumie vizuri. BWANA anazungumza katika Isaya 61:10 juu ya vazi ambalo yeye MUNGU ndiye atatuvika wanadamu wanyenyekevu  kwake na waaminifu kwake.
Isaya 61:10 '' Nitafurahi sana katika BWANA, nafsi yangu itashangilia katika MUNGU wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua, na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo BWANA MUNGU atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote. ''
=Kupitia andiko hilo tunapata kujua kwamba.
-MUNGU huvika wanadamu vazi la Wokovu.
-Vazi la Wokovu ni vazi la haki na atalipata mwenye haki tu.
-Kupitia vazi hili la Wokovu, MUNGU huotesha haki kwa kila mtu kutoka kila taifa ambaye atalivaa vazi hilo. Ni haki ya kumshinda shetani, ni haki ya kuingia uzima wa milele, ni haki ya baraka na ushindi.
 
Isaya 51:6-7 '' Inueni macho yenu mbinguni, mkaitazame nchi chini; maana mbingu zitatoweka kama moshi, na nchi itachakaa kama vazi, nao wakaao ndani yake watakufa kadhalika; bali wokovu wangu utakuwa wa milele, na haki yangu haitatanguka. Nisikilizeni, ninyi mjuao haki, watu ambao mioyoni mwenu mna sheria yangu; msiogope matukano ya watu, wala msifadhaike kwa sababu ya dhihaka zao.'' 
-Wokovu wa BWANA YESU ni wa milele.
-Walioukataa Wokovu wake wataangamia.
-Wateule wanaofuata sheria ya MUNGU yaani kulitii neno la MUNGU wanatakiwa wasikate tamaa wala kufadhaika kwa sababu ya matukano ya watu ambao hawako katika Wokovu.

Katika Luka sura ya pili kuanzia mstari wa 25 hadi 31 kuna habari za mtu mmoja Simeoni mcha MUNGU ambaye ROHO MTAKATIFU alikuwa amemwahidi kwamba hatakufa hadi amuone BWANA YESU ambaye ndiye Wokovu wetu, huyu ndugu alikuwa ni mzee sana lakini bado ahadi ya MUNGU ilikuwa ni kwamba hatakufa hadi auone Wokovu uliokuja duniani, Wokovu huo Ni BWANA YESU. Huyu Simeoni baada ya kumuona BWANA YESU alisema neno hili. 
''Sasa, BWANA, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote;-Luka 2:29-31 '' 
-Aliuona Wokovu kwa macho yake ambao wokovu huo ni kwa ajili ya watu wote watakaoamua kuchagua wokovu.
-Kumuona YESU ni kuuona Wokovu, na Wokovu ni njia ya uzima. Kuukubali Wokovu maana yake ni kumkubali YESU, Na kumkataa YESU ni kuukataa Wokovu. kumkataa YESU ni kuukataa uzima wa milele, kumkataa YESU ni kujipeleka jehanamu huku unajiona. 
-Ni wakati wa kuvaa vazi jipya kutoka kwa MUNGU, Vazi hilo ndilo tiketi yako ya uzima sasa na uzima wa milele.

Halipatikani kwingine vazi hilo ila kwa BWANA YESU.

Matendo 4:12 ''Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo ''
-Ndugu zangu hakuna Wokovu kupitia mwingine awaye yeyote ila wokovu uko katika BWANA YESU pekee.

-Wokovu  ndilo vazi la kuvaa kila mwanadmu.

-Wengi leo hawajalivaa vazi hilo la WOKOVU.

-Ukiwa huna vazi la Wokovu maana yake uko uchi.

-Ukiwa huna vazi la wokovu utakuwa tu upande wa shetani lazima.



-Na wewe ambaye uliokoka na kurudi nyuma hakikisha unageuka na kutubu.

Wewe mwenda mbinguni hakikisha vazi lako ni safi.

Ufunuo 22:14-15 '' Heri wazifuao nguo zao, wawe na amri kuuendea huo mti wa uzima, na kuingia mjini kwa milango yake.
Huko nje wako mbwa, na wachawi, na wazinzi, na wauaji, na hao waabuduo sanamu, na kila mtu apendaye uongo na kuufanya.''
-Biblia inasema heri wale wafuao mavazi yao ili wapate kuuendea mti wa uzima ambao ni BWANA YESU ili wapate uzima wa milele.
-Nje, yaani jehanamu kutakuwa na watu waliomkataa BWANA YESU na kuendekeza dhambi zao. nje kutakuwa na wazinzi, wachawi, waabudu sanamu na watenda dhambi wote ambao katika maisha yao ya duniani hawakutubu na kumpokea BWANA YESU.



-Leo  kuna watu kujikaza, na kufanya majukumu yao mbele  za watu huku wakiwa uchi, huwapendezesha wanadamu lakini MUNGU je?

-Ni vizuri kila Mwanadamu kufanya kazi yake kwa lengo moja tu la kumpendeza MUNGU.

-Wengi leo wanafanya mambo ambayo huwabariki wanadamu lakini mambo hayo hayo ni machukizo makuu kwa MUNGU.

Mfano leo kila kijana anawaza kuwa msanii wa miziki ya kidunia. Hata mimi zamani nilikuwa na mawazo hayo hayo  na nilikuwa mtunzi mzuri wa nyimbo hizo za kidunia lakini MUNGU hakutaka maana kila nilipokuwa natunga nyimbo na kujaza daftari, daftari hiyo ilipotea katika mazingira ambayo nilikuwa najua kwamba naonywa. 
-Kuwaza ndoto za kuwa mwimbaji mahiri wa nyimbo za kidunia ni kuwaza kufurahi kidogo duniani kisha ukateseke jehanamu.

-Kuwaza kuwa msanii wa nyimbo za kidunia ni kuwaza jehanamu.

Hata wale ambao leo wanafanya miziki hiyo ya kidunia, wahurumie na sio kuwashangilia.

Kwa jinsi ya rohoni wako uchi kabisa tena macho yao yamepofuka na masikio yao yamezibwa kwa pamba za kuzimu. wanahitaji neema kuu kutoka kwa BWANA YESU.
Mbinguni wanaingia walio na vazi la Wokovu tu.
Ufunuo 7:9 ''Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao;'' 
-Hawa wako mbinguni na wamevaa mavazi meupe yasiyo na uchafu.

MUNGU ametoa vazi zuri ambalo kila mwanadamu anatakiwa alivae.

Ni vazi la Wokovu, Ni vazi la bi harusi wa kwenda uzima wa milele.
Hakikisha BWANA anakuwa Wokovu wako.
Zaburi 27:1 ''  BWANA ni nuru yangu na wokovu wangu, Nimwogope nani? BWANA ni ngome ya uzima wangu, Nimhofu nani? ''

.

Ndugu yangu hakikisha unavaa vazi hili na usikubali kuwa uchi tena.
Usikubali kumwacha YESU.
Usikubali kuukosa uzima wa milele kwa sababu tu ya kushawishiwa na watu kwamba umuache YESU.
-Usikubali kuukosa uzima wa milele kwa sababu tu ya kushawishiwa na wanadamu kwamba usiache dini ya wazazi wako na kumpokea YESU.
Hakuna Mwanadamu ambaye atakupeleka uzima wa milele bali anayepeleka watu uzima wa milele ni BWANA YESU pekee. Mpokee na jina lako litandikwa kwenye kitabu cha uzima mbinguni.
Usikubali jina lako likaandikwa tu kwenye daftari la kura au la sensa huku jina hilo kwenye kitabu cha uzima mbinguni halimo.
Kumbuka mbinguni watakatifu wanavaa mavazi safi meupe na sio mavazi machafu.
Ufunuo 7:13-17  '' Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Na wametoka wapi? Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha MUNGU, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na MUNGU atayafuta machozi yote katika macho yao '' 
-Kuwa na YESU ni raha sana.
-BWANA YESU  atupe kufika mbinguni wote.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. ROHO MTAKATIFU aliyenipa ujumbe huu ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili. MUNGU Akubariki.

Comments