JUKWAA la
Wakristo Tanzania (TCF), limeendelea kushikilia msimamo wake wa
kuwashinikiza waumini kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa.
![]() |
Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa |
![]() |
Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania |
Limesema Katiba Inayopendekezwa imefika hapo ilipo kwa njia ya ubabe na kukosa uadilifu.
Tamko la umoja
huo lililotolewa jana na kusainiwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo
Tanzania (CCT), Askofu Dk. Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la
Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na
Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kipentekoste Tanzania (CPCT), Askofu
Daniel Awet, limesema wao hawana hasira kama ambavyo watu wengine
wamekuwa wakitafsiri.
Kauli hiyo
inaonyesha kujibu kauli ya Rais Jakaya Kikwete aliyoitoa Machi 28, mwaka
huu alipokutana na viongozi dini wanaounda Kamati ya Amani ya Mkoa wa
Dar es Salaam.
Akizungumza na
viongozi hao, Rais Kikwete alisema msimamo wa TCF wa kuwataka waumini
wao kuipigia kura ya hapana Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira, pia
usiokuwa na tija kwa maendeleo ya taifa.
Rais Kikwete
alikuwa akizungumzia tamko la TCF la Machi 12, mwaka huu lililowataka
waumini wake kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu
la Wapigakura na kuipigia kura ya hapana Katiba hiyo.
Jukwaa hilo
lilitaja sababu za uamuzi wake huo ni Muswada wa Mahakama ya Kadhi
kukiuka misingi ya taifa kuwa na Serikali isiyo na dini, na kura ya
maoni ya Katiba Inayopendekezwa kuweza kusababisha mgawanyiko.
Katika tamko
lake la jana, maaskofu hao wamesema kwa kuwa utafiti wa Tume ya
Kurekebisha Sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya
Kadhi ni vema Serikali ikaacha kujadili.
“Sisi maaskofu
wa Jukwaa la Wakristo Tanzania tunatamka kwamba matamshi ya Rais Kikwete
wakati akihutubia watu aliowaita viongozi wa dini Machi 28, kuwa
Mahakama ya Kadhi ni ya Waislamu wenyewe na Serikali haitajihusisha wala
kugharamia, yanakinzana na kile kinachoendelea bungeni na nje ya
Bunge.
“Hapa
tunajiuliza, endapo maneno ya rais ni ya kweli, mbona Bunge linaendelea
kujadili kitu ambacho Serikali yake haitajihusisha wala kukigharimia?
“Kwa mantiki
hiyo, tunamtaka rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na usijadiliwe
tena kwa kuwa utafiti wa Tume ya Kurekebisha Sheria ulishaonyesha
madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, vinginevyo kuendelea
kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha na
itagharimia.
“Maaskofu
tuliokutana hapa hatuna hasira na wala hatuongozwi na mihemko katika
kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri.
“Tunafikia
maamuzi yetu baada ya maombi na sala, na tunasukumwa na upendo kwa
wananchi ili kujenga taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano,”
ilisema sehemu ya tamko hilo.
Maaskofu hao
wamesema wako mjini Dodoma kufuatilia kwa kina muswada wa marekebisho ya
sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza pamoja na mambo mengine,
marekebisho ya sheria ya tamko la sheria za Kiislamu la mwaka 1964.
Wamesema
muswada huo unaopendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi utawasilishwa
bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania
kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo, wakati bado hoja zao za
msingi walizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa
Waziri Mkuu hazijajibiwa.
“Tangu
tulipokutana Machi 10, mwaka huu tukatoa tamko letu kuhusiana na
Mahakama ya Kadhi na Katiba Inayopendekezwa, tumekuwa tukiendelea
kutafakari juu ya yale tuliyokuwa tumesema katika matamko yetu
mbalimbali na jinsi amani na utulivu wa nchi yetu vinavyoendelea
kumomonyoka siku zinavyokwenda.
“Kwanza
tumeshangazwa na tabia ya viongozi wa Serikali ya kuitisha na kuendesha
mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini, lakini isiyo rasmi.
“Machi 3,
mwaka huu Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliitisha mkutano kupitia mchungaji
mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au kanisa
aliyeshiriki.
“Jambo la
kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, ambapo rais alishiriki kikao
cha kikundi ambacho si rasmi, yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es
Salaam. “Tunasema kamati hiyo siyo rasmi kwa sababu haina baraka za
viongozi wa ngazi za juu wa kidini wa mkoa huo na haina mwongozo wa kazi
zake.
“Mikutano ya
jinsi hii, kati ya Serikali na wale ambao imewaona kuwa ndio viongozi wa
dini si sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za kualikwa au
kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa Serikali au wa dini au
madhehebu mengine.
“Tunawashauri
wanaohutubia na wanaoshiriki mikutano hii wajue washiriki hawana uwezo
wa kuamua au kukubaliana na jambo lolote kwa niaba ya viongozi wao wa
juu, na pia viongozi husika wa Serikali wasifurahi kwamba ujumbe wao
umewafikia viongozi wa dini, kwani hao washiriki si wawakilishi rasmi na
hawana uwezo wa kutoa maamuzi au kukubaliana juu ya jambo fulani la
kitaifa,” imesema sehemu ya tamko hilo.
Pamoja na mambo
mengine, tamko hilo linasema kuhusu muswada wa Mahakama ya Kadhi
imebainika walichokuwa wakikisema awali kitatokea kimeaanza kutokea
bayana kutokana na yale yaliyotokea kwenye semina kuhusu mahakama hiyo
ambapo baadhi ya wabunge walitofautiana na kutaka kupigana.
Hata hivyo,
maaskofu hao wamesema endapo wabunge wa dini za Kikristo na Kiislamu
watapigana na kisha baadaye wananchi nao wakafanya hivyo katika maeneo
yao, Serikali itakuwa ndiyo chanzo cha mapigano hayo.
Maaskofu hao
walioweka kambi mjini Dodoma, wamewataka viongozi wa Serikali kuacha
kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano wanayodhani itakubalika
na waumini wa dini hizo.
Wamesema mikutano yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na uamuzi wowote utakaofikiwa hautatambulika kwao.
Muswada
Mahakama ya Kadhi waota ‘mbawa’ Wakati huohuo, Mwandishi Wetu Fredy
Azzah anaripoti kutoka Dodoma kuwa muswada wa sheria ya uanzishwaji wa
Mahakama ya Kadhi iliyotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo, imeahirishwa.
Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilila, aliwaambia waandishi wa habari
mjini Dodoma jana kuwa uwasilishwaji wa sheria hiyo umesitishwa hadi
itakapopangwa tena.
“Sheria hii
haitawasilishwa tena, shughuli nyingine zitaendelea na kuna miswada
mingi tu imeahirishwa ambayo kutokana na muda haitawasilishwa kwenye
kikao hiki ikiwamo ya habari,” alisema Dk. Kashilila. Alisema mkutano wa
20 wa Bunge hilo unaotarajiwa kuanza Mei, ni mahususi kwa bajeti,
lakini wabunge wakiona inafaa wanaweza kubadili kanuni wakajadili
miswada watakayoona inafaa.
Chanzo:Mtanzania
Comments