KIJANA UNAYETAKA KUOA AU KUOLEWA HAKIKISHA UNAYAJUA HAYA.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
2 Timotheo 2:22 '' Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao BWANA kwa moyo safi.'' 
-Kila mwanadamu anatakiwa azikimbie tamaa za ujanani.
-Hata kama umefikia muda wa kuolewa na kuoa hakikisha unamuomba MUNGU maana ukienda kichwa kichwa unaweza kuoa au kuolewa na mtu ambaye bado hajazikimbia tamaa za ujanani hata kama ana miaka 60.
-Tamaa za ujanani ni kuwaza ngono, ni kuwaza kuwaharibia maisha wengine, ni kuwaza kuwaambukiza magonjwa watu wengine, Tamaa za ujanani ni dhambi ya uasherati.
Kuna watu walioolewa na watu ambao hawajakimbia tamaa za ujanani ndio maana kwa sasa kila siku wanasalitiwa na wenzi wao maana ''jini tamaa za ujanani hajatoka moyoni''
Ndiyo maana Biblia inakataa kufungwa nira moja na watu ambao hawajaokolewa na BWANA YESU.
2 Kor 6:14-18 ''  Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya KRISTO na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la MUNGU na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la MUNGU aliye hai; kama MUNGU alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa MUNGU wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike, ''
-Yaliyosemwa katika maandiko haya yanatakiwa kueleweka vizuri kwa kila kijana mcha MUNGU, Maana unaweza kuwa kijana mcha MUNGU lakini usipokuwa makini utaingia katika ndoa na mpagani na kukupelekea uanze kusuasua katika Wokovu ambao ni wa thamani sana.
-Kijana kabla ya kuwaza ndoa au mahusiano anatakiwa kwanza awaze uzima wa milele.
-Kuwaza uzima wa milele ni pamoja na kuwaza kuwa na mtu katika ndoa ambaye atakusaidia katika safari yako ya mbinguni, usikubali kuja kuingia katika uchumba na mtu ambaye anakusaidia kwenda jehanamu na sio mbinguni. 
Mithali 19:14 '' Nyumba na mali ni urithi apatao mtu kwa babaye; Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na BWANA. ''

Kuingia kwenye ndoa ni jambo linalohitaji umakini mkubwa sana.
 - Umoja Katika Imani Ni Msingi Na Dhamana Ya Umoja Katika Ndoa. 
Kijana Aliyempokea YESU Akitaka Kuoa/Kuolewa anatakiwa ajiulize  Maswali kama haya; 
=Je, huyu ndugu ameokoka kweli na ana nia ya KRISTO ndani yake?
=Huyu Ndugu Je Ni Mkristo Anayemcha MUNGU?. 
=Je Ningependa Kusali Pamoja Naye?.
Mr and Mrs Peter M Mabula
=Je Ana Dalili Za Kunivumilia Hata Kwenye Nyakati Ngumu?.
=Je Anasali Akitarajia Mbinguni Au Anasali Tu Ili Kuwalidhisha Watu? 
= Je Atanisaidia Na Kunishauri Kiroho Ili Wote Tumpendeze MUNGU Siku Zote?. 
 Kama Kaka Au Dada Huyo Anaendana Na Majibu Sahihi Ya Hapo Juu, Huyo Anafaa Kuwa Mke/Mme Mwema. 
 Mithali 1:7 '' Kumcha BWANA ni chanzo cha maarifa, Bali wapumbavu hudharau hekima na adabu. ''
-Kumcha BWANA ndio chanzo cha maarifa mazuri.
-Maarifa ni elimu iliyo katika matendo.
-Matendo mema yanatakiwa yaonekane sio kwa mtu kujisifu yeye bali yaonekane kwa wengine.
-Kumbuka kwamba kama unataka kuingia katika uchumba na mtu asiye mcha BWANA YESU basi una hasara.
-Kama mtu hamchi BWANA basi huyo lazima tu atakuwa anamcha shetani. 
Yakobo 4:7 '' Basi mtiini MUNGU. Mpingeni Shetani, naye atawakimbia ''
-Kama huyo ndugu ambaye wewe unataka uingie katika uhusiano nae wa uchumba ili baadae kidogo mtafunga ndoa, hakikisha anamtii MUNGU.
Maana iko wazi kabisa mtu kama hamtii MUNGU maana yake anamtii shetani. anayetaka mfanye mapenzi kabla ya ndoa huyo anamtii shetani na ni wa kumuepuka.
Ndugu, Uhusiano Wako Na MUNGU Ni Muhimu Zaidi Kuliko Hata Mme Au Mke.  Kama mchumba wako anataka mfanye mapenzi sasa basi tambua huyo hakufai maana wengi wa wasaliti kwenye ndoa zao ndio wale ambao hata kabla ya kuoa au kuolewa walikuwa waasherati.
Biblia inakataa uzinzi na uasherati, Biblia inasema
Kutoka 20:14 ''Usizini''

Kuna watu walikataa kufuata utaratibu wa kibiblia na kujikuta wakitaabika baada ya kuingia katika ndoa.
-Kuna Watu Walikuwa Na Huduma Nzuri Lakini Walipoingia Kwenye Ndoa Tu Utumishi Ulikoma, Tatizo Ni Ndoa Na Sio Vinginevyo. 
-Ushauri Mbaya Wa Mwenzi Wako Wa Ndoa Unaweza Ukakuharibia. 
-Kuna Wakaka Walikuwa Watoaji Wa Sadaka Na Zaka Kanisani Lakini Baada Ya Kuingia Kwenye Ndoa Ameacha Kumtii MUNGU Kwa Sababu Ameoana Na Asiye Na Hofu Ya MUNGU Ndio Maana Nimesema Mwanzo Kwamba "umoja Katika Imani Ni Msingi Na Dhamana Ya Umoja Katika Ndoa".

Moja ya mambo yanayowakosesha wavulana na mabinti wengi ni kufanya mapenzi kabla ya ndoa.
-Shetani amewapotosha wanadamu na kuhakikisha siku zote wanamkosea MUNGU muumba wao. Hata kuwa na girlfriend na boyfriend sio mpango wa Biblia, ni machukizo anayoyapanda shetani ili kuwaharibia vijana.

KIJANA/MSICHANA OMBA UPATE UBAVU WAKO SAHIHI USIJE UKAPATA UBAVU ULIOPINDA NA BAADAYE NDOA YENU IKAWA NDOANA

Na hata kama kwa bahati mbaya ulijikuta umeingia katika uhusiano na kuharibu hakikisha unatubu na kurejea.
Kama uko kwenye ndoa ambayo ilianza vibaya basi hakikisha mnatubu na kuanza kumtii MUNGU. Kumbuka kukiri kwako udhaifu kila siku kumesababisha uwe hivyo ulivyo {mithali 18:21}
-Kama umeshasamehewa hakikisha unabaki kwenye msamaha wako.

  -Kama Kuna Jambo Linaumiza Vijana Wengi, Ni Kuvunjika Kwa Mahusiano Ya Uchumba Kabla Ya Ndoa. Mara Nyingi Chanzo Kikuu Cha Kuvunjika Uhusiano Huo Ni Uasherati. 

-Ndugu Yangu, Mkitaka MUNGU Aondoe Ulinzi Wa Uchumba Wenu Basi Fanyeni Uasherati. 
MUNGU Ni Utakatifu, Ataulinda Uchumba Huo Kama Tu Ni Uchumba Katika Utakatifu. 
-Wengi Wanaishi Kwa Maumivu Makubwa Leo Kwa Sababu Ya Kuachwa, Wanawalaumu Waliowaacha Kumbe Wamesahau Kwamba Chanzo Ni Dhambi Waliyoiruhusu.
- Kuna Wengine Baada Ya Uchumba Kuvunjika Baada Ya Dhambi Hujikuta Hata Kuoa/Kuolewa Tena Inakuwa Tatizo. Ni Kama Dhambi Ile Ya Kwanza Imegeuka Gundu Kubwa Waliyojipaka Mwili Mzima. Baada Ya Hapo Kuna Watu Wamejikuta Wakidandia Magari Yasiyo Yao Ya Wakiolewa/kuoa na Wasio Sahihi.
 Ndugu Yangu, MUNGU Anataka Utakatifu, Ukiukataa Utakatifu Wakati Wa Uchumba Ujue Unakaribishwa Hatari Mbeleni Kama Hutageuka.  ''Maana mtu anayetaka kuyaokoa maisha yake mwenyewe, atayapoteza, lakini mtu atakayepoteza maisha yake kwa ajili yangu na kwa ajili ya injili, atayaokoa.-Marko 8:35''

  -Dhambi Ni Mbaya.
Kijana epuka uasherati wakati wa uchumba.
Dhambi Ya Uzinzi Na Uasherati Ni Kama Chatu Anavyotaka Kumkamata Mbuzi Na Kisha Kummeza. 
Watenda Dhambi Ni Mfano Wa Mbuzi, Hukaa Katika Eneo Huku Hawajui Kwamba Chatu Yuko Jirani, Chatu Husogea Bila Mbuzi Kujua, Chatu Akiona Amekaribia Alipo Mbuzi Bila Kushtukiwa Humpiga Ngwala Mbuzi Na Kumkamata, Baada Ya Hapo Humzonga Na Kumvunja Mbavu Na Kumumaliza Nguvu, Baada Ya Hapo Anaweza Akamwacha Kidogo Maana Anajua Hawezi Kumkimbia, Kisha Anaweza Kumlamba Na Kisha Kumumeza Kabisa. Leo Kuna Watu Dhambi(chatu) Inawafuata Na Kuwaotea Ila Wao Hawaoni Na Wanadhani Ni Kwema Tu. Wachumba kila siku wako pamoja gizani wakiwa wawili tu kumbe chatu naye anawamendea. Chatu Husogea Na Kuwakamata Maana Yake Dhambi Imewakamata, Wakati Huu Mchungaji Akikushauri Na Kukuonya Unaweza Kusema "haka Kazee Kamekosa Kazi Maana Kananifuatilia Mimi Tu". Chatu Atakuzonga Na Kukumaliza Nguvu Kisha Anakumeza. Akikumeza Chatu Huyu Usipoangalia Anaweza Kukutapika Jehanamu. Leo Kuna Watu Dhambi ya uzinzi na uasherati Inawanyemelea.
Wengine hawana Nguvu Za Kiroho tena baada ya dhambi hiyo.
Wengine chatu  anawalamba Na Wengine amewameza kabisa . Kutubu Ni Leo Ndugu wachumba mnaozini, kutubu ni leo nyie mnaojiita boyfriend na boyfriend, kutubu ni leo wanandoa mnaosaliti ndoa zenu.
Matendo 3:19 '' Tubuni basi, mrejee, ili dhambi zenu zifutwe, zipate kuja nyakati za kuburudishwa kwa kuwako kwake BWANA; ''
- wengi walikuwepo sasa hivi wako wapi? ndugu tukimbilie kwa YESU KRISTO maana hakuna ajuaye kesho itakavyokuwa unaweza ukasema nitatubu kesho harafu na hiyo kesho usifike chukua hatua leo kisha kataa tena kumkosea MUNGU. Huyo mchumba ni wako tu vumilia hadi mfunge ndoa takatifu. usiipangie sana kesho kwa ajili ya kutubu bali kutubu ni leo.  "ndugu, tunamhitaji MUNGU BABA ili tuwe hai kesho"


-Kufanya wema machoni pa watu ili kupata sifa ni mbaya pia. unakuta binti hata hataki kuingia dhambini lakini kwa kutaka kumridhisha mchumba wake anakubali na kutenda dhambi kubwa.
Fanya wema kwa watu katika MUNGU na sio wema katika shetani. Fanya wema kwa BWANA YESU kwa kutii neno lake.
Yesu alitoa maonyo makali kwa wafuasi wake wajiepushe na unafiki kwa kutamani kufanya wema wa aina yoyote kwa nia ya kujitafutia umaarufu au kusifiwa,
'' Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe na wao; kwa maana mkifanya hivyo, hampati thawabu kwa BABA yenu aliye mbinguni.-Mathayo.6:1''
-Kama hutapata thawabu basi utapata adhabu maana umewatii wanadamu na kumkosea MUNGU.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments