KUFUFUKA KWA YESU

Na Askofu Zakaria Kakobe.
Kwa muda mrefu sasa, tumekuwa tukijifunza Kitabu cha MATHAYO.  Leo, tunajifunza sura ya mwisho ya Kitabu cha MATHAYO.  Katika MATHAYO 28:1-20, pamoja na mambo mengine, tunajifunza kwa mapana na marfu juu ya “KUFUFUKA KWA YESU”.  Tutayagawa mafundisho tunayoyapata katika mistari hii katika vipengele vinne:-
(1)            KUFUFUKA KWA YESU (MST. 1-15);
(2)            KUFANYA MAAGIZO YA YESU KWA GHARAMA YOYOTE (MST. 16-17);
(3)            MAMLAKA ALIYOPEWA YESU (MST. 18);
(4)            AGIZO KUU (MST. 19-20).
(1)      KUFUFUKA KWA YESU (MST. 1-15)
Tukichambua msitari mmoja mmoja katika mistari hii, tunajifunza mengi mno katika ripoti hii ya kufufuka kwa Yesu:-
  1. KUFUFUKA KWA YESU SIKU YA KWANZA YA JUMA – (MST. 1) – Siku ya tatu, Mariamu Magdalene na Mariamu yule wa pili (huyu siye mama yake Yesu, bali ni Mariamu wa Klopa, mamaye Yakobo mdogo – (YOHANA 19:25; MARKO 15:40; MATHAYO 27:56), walikwenda kulitazama kaburi.  Waliamini maneno ya Yesu na ahadi yake kwamba atafufuka siku ya tatu.  Heri wanaosadiki maneno ya Yesu bila kungojea kuona (YOHANA 20: 27-29).  Tuwe kama wanawake hawa, tusiwe kama Tomaso.  Kungojea kuamini baada ya kuona, ni jambo linaloweza kutugharimu kukosa uzima wa milele.  Alifufuka siku ya tatu kutimiliza unabii (HOSEA 6:2).  Siku ya sita ya juma ndipo alipoimaliza kazi msalabani aliposema “IMEKWISHA”.  Hakufufuka siku ya sabato, bali sabato ilizikwa pamoja naye na akafufuka siku ya kwanza ya juma, JUMAPILI.  Siku ya kwanza kabisa ya juma ndipo Mungu alipoamuru nuru iangaze na kuitenga giza (MWANZO 1:1-4).  Yesu kama Nuru ya Ulimwengu alifufuka siku ile na kutengwa mbali na giza la kaburi.  Jumapili ni siku ya Bwana, Siku ya Nuru ya Ulimwengu uliojaa giza, ndiyo maana tunakuja ibadani siku hii kuifurahia Nuru hii iliyotutoa giza, ndiyo maana tunakuja ibadani siku hii kuifurahia Nuru hii iliyotutoa gizani!  SSabato ilikuwa ni ishara ya pumziko la Mungu baada ya kuumbwa kwa mbingu na nchi (KUTOKA 31:16-17).  Hata hivyo, kazi aliyoifanya iliharibiwa na dhambi ya Adamu, ikawa si njema tena.  Yesu siku alipofufuka, alifanya YOTE kuwa mapya tena na mwanamke aliyekuwa wa kwanza kuliasi Neno la Mungu kutokana nma kwenda kwa kuona, ndiye aliyekuwa wa kwanza kufika kaburini kwa kuliamini na kulitii Neno la Mungu kwa imani bila kuona.  Ndiyo maana leo tunaikumbuka Jumapili ambayo ni siku ya kuyafanya yote kuwa mapya.

  1. TETEMEKO KUBWA LA NCHI WAKATI WA KUFUFUKA  (MST. 2)
Tetemeko hili lilikuwa lazima kuwepo kabla ya “vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote” kuja kwetu.  Siku hii pia, ilikuwa ni siku ya kujaza tena nyumba yetu utukufu uliopungua kwetu kwa kutuokoa au kutupa awokovu wa kutamaniwa (HAGAI 2:6-7; WARUMI 3:23).  Tetemeko pia hapa, lilikuwa ishara ya ushindi wa Yesu wakti mifupa yake iliposogeleana tena, akafufuka (EZEKIELI 37:7).
  1. MALAIKA WA BWANA ALISHUKA – (MST. 2) – Wakati wa kuzaliwa kwa Yesu, malaika walikuwepo (LUKA 2:12-14) vivyo hivyo wakti wa kujaribiwa kwake nyikani (MATHAYO 4:11), wakati wa mateso yake (LUKA 22:43) na wakati wa kufufuka kwake.  Hawakuwepo tu wakati alipokuwa msalabani.  Hapa alizichukua dhambi zetu.  Kila mmoja wetu binafsi na Kanisa kwa ujumla, tutaona malaika wakituhudumia tutakapoichukia dhambi wakati wote.
  2. ALILIVINGILISHA JIWE AKALIKALIA – (MST.2) – Nyakati za Biblia, watu walilivingirisha jiwe kubwa kama ishara ya kukiri kufanya makosa (1 SAMWELI 14:32-33).  Pasipo kujua, walinzi na wanadamu wengine wenye dhambi tulilivingilisha jiwe na kuliweka kwenye mlango wa kaburi la Yesu.  Huku kulikuwa ni kukubali kuwa sisi ni wakosaji.  Malaika alikuja tena hapa akalivingirisha na kuliondoa, kuonyesha msamaha wa dhambi unaokuwepo kwa kila anayekiri kukosa kwa kumaanisha kuacha dhambi (MITHALI 28:13).  Alilikalia kama ishara ya ushindi katikati ya maadui waliodhani Yesu hatafufuka.  Hata kama adui ametuweka katika kaburi la mateso kiasi gani na kutuwekea jiwe na muhuri ili tusitoke, iko siku inakuja ya ushindi kwetu na maadui watapigwa butwaa.
  3. KUTETEMEKA KWA WALINZI  – (MST.3–4) – Askari ambao tungetegemea wasingekuwa na hofu mbele za Mungu hapa, tunaona wakiogopa na kutetemeka na kuwa kama wafu.  Hakuna yeyote aliye na ujasiri mbele za Mungu anapotokea katika utukufu wake.  Majeshi yote ya Shetani yanatetemeka kwa hofu kama wafu, tunapoliitia Jina la Yesu.
  4. KUTOKUOGOPA TUNAPOMTAFUTA YESU – (MST. 4) – Ikiwa tunamtafuta Yesu kwa kuacha madhehebu yetu na kuitafuta kweli, maana kweli ni Yesu, hatuna haja ya kuogopa.  Watakuja wengi kututisha na kusema “Mkiacha kusali hapa hatutawazika, au tutawatenga, au hatutawapa msaada tena, au tutawalaani, au mtapata hiki au kile kibaya n.k.”.  Maneno yaja ni upuuzi.  Hatuna haja ya kuogopa tunapomtafuta Yesu aliyesulibiwa.  Yeye atakuwa pamoja nasi.
  5. AMEFUFUKA KAMA ALIVYOSEMA – (MST. 6) – Malaika au mjumbe yeyote wa Mungu husema kama Yesu alivyosema.  Yesu ndiye Neno (UFUNUO 19:13), hivyo mjumbe yeyote wa Mungu hata awe malaika atasema sawasawa na Neno la Mungu, au sivyo, siyo mjumbe wa Mungu (YOHANA 3:34; WAGALATIA 1:8-9).
  6. AGIZO LA KWENDA UPESI – (MST. 7-9) – Mungu wetu anataka maagizo yake yote tuyafanye kwa upesi ndipo tunapomfurahisha (ZABURI 119:32,60).  Kazi ya Mungu yote kwa ujumla inataka wepesi.  Kila jambo ni lazima tulifanye harakaharaka mbiombio maana kazi ya Mungu ni ya Mfalme wetu, inataka haraka (1 SAMWELI 21:8).  Kuja Kanisani, lazima iwe mbiombio na kuhakikisha hatuchelewi; na kila tunalolifanya lazima tulifanye kwa haraka.  Anayefanya kazi ya Mungu kwa ulegevu na kufanya kazi za dunia kwa haraka, amelaaniwa (YEREMIA 48:10).  Ni muhimu pia kwenda upesi kupeleka habari njema za kufufuka kwa Yesu yaani Injili kwa kila mtu.  Tuwe kama wanawake hawa akina Mariamu.  Hofu iliambatana na furaha nyingi.  Mwili hauamini upesi miujiza, ni kama maono au ndoto hivyo huleta hofu lakini yenye furaha nyingi (MATENDO 12:9).  Kufufuka kwa Yesu kulikuwa muujiza mkubwa.
  7. KUTHIBITISHWA KWA NENO LA MJUMBE WA MUNGU – (MST. 9-10) – Yesu alisema “Salamu!” Neno hili maana yake “Salama iwe kwenu au kwako” au “Amani iwe kwako au kwenu” (YOHANA 20:19).  Yesu alisema neno lilelile alilosema malaika wake (MST. 10).  Ni muhimu kufahamu kwamba akisema Mtumishi wa Mungu neno lolote kwetu, ni Mungu amesema nasi.  Yeye hulithibitisha neno la watumishi wake (ISAYA 44:26; 1 WATHESALONIKE 2:13).  Yesu anawaita watu waliookoka “Ndugu zake”, Sisi ni ndugu zake hivyo hawezi kutuacha au kutusahau Yeye aliye kaka yetu!
  8. KUIKATAA KWELI KWA SABABU YA FEDHA  – (MST. 11-15) – Kupewa fedha au vyeo na wakuu wa makuhani, au viongozi wa dini, kumewafanya watu wengi kushindwa kuacha madhehebu yao yaliyojaa kila namna ya uongo na kuifuata kweli.  Vyeo au fedha itatusaidia nini tukipata hasara ya nafsi zetu?  (MARKO 8:36).  Kulala kwa walinzi na mtu akatoroka, au kutoroshwa wakti wa ulinzi wao, hukumu kwa walinzi hao ilikuwa kifo (MATENDO 12:18-19).  Hapa wanatunga uongo wa dhahiri bila aibu na kutumia fedha.  Liwali akisikia walilala, angewaua, hivyo wanasema watasema naye!  Yote haya ni aibu!  Yesu alifufuka!  Walijuaje ni wanafunzi wamemwiba wakati walikuwa wamelala usingizi?  Waliwaona kwa macho?  Ni uongo wa waziwazi!
(2)      KUFANYA MAAGIZO YA YESU KWA GHARAMA YOYOTE (MST. 16-17)
Galilaya, ilikuwa karibu maili 100 kutoka Yerusalemu.  Wanafunzi wa Yesu walikubali kwenda maili zote hizo kutii agizo la Yesu.  Hii ndiyo gharama ya uanafunzi wa Yesu.  Ni lazima tuwe tayari kukubali gharama yoyote kutii maagizo ya Yesu, ndipo tutakapofanikiwa.  Tukikwepa gharma, tutaabika (ZABURI 119:6).  Vilevile tuwe tayari kwenda hata maili zaidi ya 100 kuitafuta kweli.  Tusiridhike kusali karibu tu!  (MATHAYO 12:42).
(3)      MAMLAKA ALIYOPEWA YESU (MST.18)
Yesu kama Mungu, alikuwa na mamlaka hiyo wakati awote, lakini hapa kama Mwana wa Adamu alirudishiwa kwa niaba yetu, mamlaka atuliyonyang’anywa na Shetani pale Adamu wa kwanza alipofanya dhambi, na kupoteza utawala wake aliokuwa nao; na kumfanya Shetani atawale (MWANZO 1:26-28).  Yule unayemtii, ni mtawala wako.  Adamu alimtii Shetani akawa mtawala wake.  Sasa utawala huo tumerudishiwa wote tuliookoka.  Shetani yuko chini ya miguu yetu (LUKA 10:18-19).
(4)      AGIZO KUU (MST. 19-29)
Yesu hakutuagiza kufanya mikutano ya Injili tu na kufurahia kuona wengi wakinyosha mikono kukata shauri kuokoka, na kuishia hapo.  Agizo ni kuwafuatilia mpaka wamekuwa wanafunzi wa Yesu wakiwa wamebatizwa na baadaye kuwafundisha kuyashika yote aliyotuamuru.  Tukifanya hivyo ndipo tutakapouona mkono wake kwetu, atakuwa pamoja nasi hadi ukamilifu wa dahari, yaani mpaka tutakapomwona tena.  Kanisa halioni miujiza mingi kwa kukosa kulitekeleza Agizo hili Kuu wa utimilifu (YOHANA 15:16).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe.

Kwa Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe  Fungua      

Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

Comments