Maaskofu wamjibu Rais Kikwete


Siku tano baada ya Rais Jakaya Kikwete kusema kuwa tamko la Jukwaa la Wakristo (TCF) kuwataka waumini wao kupigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa lilikuwa la hasira, viongozi hao wamejitokeza tena na kusisitiza kwamba msimamo wao huo utabaki kama ulivyo.
Katika tamko pamoja walilolitoa jana baada ya kukutana juzi mjini Dodoma, viongozi hao wamemtahadharisha Rais Kikwete kuwa kuendelea kupigia debe Katiba Inayopendekezwa na kuruhusu Mahakama ya Kadhi, kunaweza kulitumbukiza Taifa katika machafuko na hali ikiwa hivyo Serikali ndiyo itakayolaumiwa.

Tamko hilo limesainiwa na viongozi walewale waliosaini lile la awali la Machi 12, mwaka huu ambao ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk Alex Malasusa, Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa Katoliki Tanzania (TEC), Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa na Mwenyekiti wa Kanisa la Pentekoste Tanzania (CPCT), Askofu Daniel Awet.

Tamko hilo la maneno 921, limeendelea kuwataka waumini wao kujitokeza kwa wingi kujiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, kuisoma Katiba Inayopendekezwa na kujitokeza kuikataa kwa kupiga kura ya ‘hapana,’ msimamo ambao tayari umeibua msuguano baina yao na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo aliyesema viongozi wa dini hawana mamlaka ya kuwaamulia waumini wao aina ya kura wanayostahili kupiga.

Pia, Jukwaa hilo limewataka viongozi wakuu wa Serikali –Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Rais Kikwete wasifurahi kwamba ujumbe wao umewafikia viongozi wa dini waliozungumza nao hivi karibuni, kwa kuwa watu waliokutana nao si wawakilishi rasmi na hawana uwezo wa kutoa uamuzi au kukubaliana juu ya jambo la kitaifa.

“Maaskofu tuliokutana hapa (mjini Dodoma) hatuna hasira na wala hatuongozwi na hasira wala mihemko katika kufikia maamuzi tunayofanya kama ambavyo wengine wanavyotutafsiri, tunafikia maamuzi yetu baada ya maombi na sala na tunasukumwa na upendo kwa wananchi ili kujenga Taifa lenye umoja, amani, utulivu na maelewano,” lilisema tamko hilo likihitimishwa kwa maneno ya Biblia kutoka Mithali 29: 1, “Aonywaye mara nyingi akishupaza shingo, atavunjika ghafla, wala hapati dawa.”

Jumamosi iliyopita, Rais Kikwete akifungua mkutano wa Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam iliyoshirikisha wajumbe kutoka mikoa mbalimbali ikijumuisha viongozi wa dini za Kiislamu na Kikristo, alisema msimamo wa TCF kuhusu kuipigia kura ya ‘hapana’ Katiba Inayopendekezwa ni wa hasira na usiokuwa na tija kwa maendeleo ya Taifa.

“Nimeyasoma matamko hayo yote kwa umakini, imenishangaza, imenisikitisha na kunihuzunisha. Siamini kwa nini wamefikia huko kwa kuunga au kutokuunga mkono,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete alisema: “Waacheni waumini waamue Katiba wanayoitaka wao... hayo matamko niliyoyasoma yamejaa hasira kwa Serikali kupeleka bungeni Muswada wa Mahakama ya Kadhi.”

Maaskofu hao walikuwa Dodoma kufuatilia kwa kina Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali ya mwaka 2014 unaopendekeza, pamoja na mambo mengine, marekebisho ya Sheria ya Tamko la Sheria za Kiislamu la mwaka 1964 unaotambua Mahakama ya Kadhi.

“Muswada huu unapendekeza kuanzishwa Mahakama ya Kadhi ambao utawasilishwa bungeni leo kwa hati ya dharura na hivyo kuufanya umma wa Watanzania kutokujua maudhui yaliyomo katika muswada huo wakati bado hoja zetu za msingi tulizopeleka kwenye Kamati ya Katiba na Sheria ya Bunge na kwa Waziri Mkuu hazijajibiwa,” Ilieleza taarifa hiyo.

“Tunamtaka Rais aagize muswada huu uondolewe bungeni na usijadiliwe tena kwa kuwa utafiti wa Tume ya kurekebisha sheria ulishaonyesha madhara ya uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi. Vinginevyo, kuendelea kujadiliwa kwa muswada huu maana yake ni kwamba Serikali inajihusisha na itagharimia mahakama hiyo.”

Walisema; “Yalijitokeza kwenye semina kwa wabunge mwishoni mwa wiki ni ishara ndogo ya kile kitakachotokea maeneo yote ya nchi yetu. Hapa tunajiuliza, endapo maneno ya Rais ni kweli, mbona Bunge linaendelea kujadili kitu ambacho Serikali haitajihusisha wala kukigharamia?”

Tamko hilo lilionya: “Tunamtaka Rais (Kikwete) aiepushe nchi yetu na kuingizwa kwenye mapigano ya kidini ambayo kuyadhibiti itakuwa vigumu. Pia tunamwomba Rais Kikwete akumbuke na kutafakari kile kilichotokea na kinachotokea nchi ya Afrika ya Kati, kati ya kundi la Seleka na kundi la Anti Balaka.


Bunge laondoa Muswada wa Mahakama ya Kadhi
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana bungeni jana na kuthibitishwa kwa nyakati tofauti na Naibu Spika, Job Ndugai na Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashillilah zilisema kuwa muswada huo hautajadiliwa katika mkutano wa 19 wa Bunge unaomalizika leo, badala yake utapangiwa siku nyingine.

“Suala la Mahakama ya Kadhi halitawasilishwa bungeni tena mpaka hapo litakapopangiwa siku nyingine. Hata Waziri Mkuu (Mizengo) Pinda wakati akizungumza katika semina ya wabunge aliliweka sawa suala hili. Kwa kauli alizozitoa hakuna haja tena ya kuhoji kama suala hili litakwenda bungeni au la,” alisema Kashillilah.

Ndugai alisema ni vigumu kwa suala hilo kuwasilishwa bungeni na kwamba litajadiliwa katika vikao vijavyo vya Bunge.

Mikutano ya viongozi
Maaskofu katika tamko lao, walisema wameshangazwa na tabia ya viongozi wa Serikali ya kuitisha na kuendesha mikutano wanayodai ni ya viongozi wa dini lakini isiyo rasmi.

“Machi 03, 2015 Waziri Mkuu (Pinda) aliitisha mkutano kupitia mchungaji mmoja ambapo hakuna hata kiongozi mmoja wa taasisi au kanisa aliyeshiriki. Jambo la kushangaza ni kile kilichotokea Machi 28, 2015 ambapo Rais Kikwete alishiriki kikao cha kikundi ambacho siyo rasmi, yaani Kamati ya Amani ya Mkoa wa Dar es Salaam.

“Mikutano ya jinsi hii kati ya Serikali na wale ambao imewaona kuwa ndiyo viongozi wa dini siyo sahihi kwani viongozi wa dini wana taratibu zao za kualikwa au kuwakilishwa katika mikutano na viongozi wa Serikali au wa dini au madhehebu mengine.

“Kwa mantiki hiyo tunawashauri viongozi wa Serikali waache kabisa kutumia vikundi visivyo rasmi kualika mikutano wanayodhani kuwa itakubalika na waumini wa dini hizo. Mikutano yote ya jinsi hiyo itakayoitishwa ni batili na maamuzi yake hatuyatambui na hatutayatambua.”

Chanzo:Mwananchi

Comments