Mawakili wa Gwajima wamwandikia Kova barua

Askofu Josephat Gwajima.

WAKILI wa Askofu Mkuu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima, Peter Kibatala, ameliandikia barua Jeshi la Polisi nchini akiomba vifungu vya sheria vilivyotumika kuomba nyaraka za umiliki wa vitu mbalimbali vya Askofu huyo.

Pamoja na hilo, Kibatala aliomba mteja wake huyo kuambiwa kwa maandishi juu ya vitu vinavyotakiwa kuwasilishwa kwa Jeshi hilo.
Barua hiyo ambayo Kibatala ameielekeza kwa Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, pia nakala yake ameituma kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Ernest Mangu na kwa mteja wake huyo.
“Kwa barua hii tunaomba Jeshi la Polisi kwa niaba ya mteja wetu kumwandikia rasmi kwa maandishi mteja wetu mkiainisha nyaraka mnazohitaji na vifungu vya sheria vinavyotumika na Jeshi la Polisi kutaka nyaraka hizo.
“Tutashukuru kupata hati hiyo, ambayo bado hatujaipa jina, kwani tunategemea jeshi hilo litafahamu jina la kisheria la nyaraka husika inayotumika kutaka mteja wetu alete nyaraka tajwa na mara tu mteja wetu akipata maandishi tuliyoomba atatimiza wito au kuchukua hatua stahiki za kisheria,” ilisomeka sehemu ya barua hiyo.
Juzi wakili mwingine wa Gwajima, John Mallya, alilalamikia hatua ya polisi akisema mahojiano yalichukua mambo binafsi badala ya kile alichoitiwa na kutakiwa kuwasilisha vitu 10.
Wakili huyo alitaja mambo yanayotakiwa kuwasilishwa polisi kuwa ni hati ya usajili wa kanisa, namba ya usajili, majina ya Baraza la Wadhamini (Baraza la Kiroho), idadi ya makanisa (matawi) anayohudumia, nyaraka za helikopta ya kanisa na muundo wa uongozi wa kanisa
Vitu vingine ni waraka wa maaskofu uliosomwa makanisa yote, nyaraka za nyumba na mali za kanisa, nyaraka kuonyesha taarifa za hesabu kutoka kwa Msajili wa Vyama vya Hiari na kuambatana na mtu anayepiga picha za video kanisani hapo.
Hata hivyo, katika barua ya wakili huyo wa Gwajima, Kibatala, ilieleza kwa mshangao kwamba Askofu huyo, ambaye anatuhumiwa au anapelelezwa kuhusiana na tuhuma za kutoa lugha ya matusi wakati wa mahojiano, hakutaarifiwa kama tuhuma hizo ziko chini ya kifungu gani cha sheria.
Gwajima alitakiwa kurejea katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam Aprili 16, mwaka huu, akiwa na vitu hivyo 10, hatua ambayo imekuja kinyume na matarajio ya wengi kuwa kiongozi huyo angekuwa anahojiwa tu kuhusu matamshi yake ya kashfa dhidi ya Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo.
Kutokana na matamshi hayo yaliyosambaa kwa kasi kwenye mitandao ya kijamii kwa njia ya video na sauti, Gwajima alitakiwa kuripoti polisi kuhojiwa Machi 27, mwaka huu, ambapo kabla ya kukamilika kwa mahojiano aliishiwa nguvu na kupelekwa hospitalini alikolazwa kwa siku nne, huku taarifa zikieleza kuwa alishtushwa na kuhojiwa taarifa binafsi badala ya tuhuma alizoitiwa polisi.
Baada ya kutoka hospitalini, Gwajima aliendelea kutembea akiwa kwenye kiti chenye magurudumu, alichotumia hadi Aprili 6, alipohubiri katika Ibada ya Pasaka ambako alionekana kusimama kutokana na kudai kuombewa na wachungaji wageni waliofika kanisani hapo kutoka Japan.
Kamishina Kova hakupatikana kuzungumzia kupokea barua hiyo kutokana na simu yake kuita bila majibu.

Source:Mwananchi

Comments