Mtu mmoja anaswa akiwa na bastola yenye risasi nane kanisani


 Hofu imewakumba waumini wa Kanisa Katoliki la Mtakatifu Stephano, Kisarawe mkoani Pwani katika ibada ya Ijumaa Kuu baada mtu mmoja kukamatwa katikati ya ibada ya Ijumaa Kuu akiwa na bastola yenye risasi nane.
Kwa mujibu wa habari zilizopatikana kutoka kwa waumini na kuthibitishwa na polisi, mwanaume huyo ambaye si muumini wa kanisa hilo anadaiwa kutaka kufanya uhalifu kanisani hapo na alikamatwa baada ya waumini kushtukia mienendo yake isiyo kuwa ya kawaida.

Tukio hili limetokea katika kipindi ambacho kuna tishio la uhalifu unaohusishwa na ugaidi katika maeneo mbalimbali nchini, ambapo kuna uporaji wa silaha unaofanywa na watu wasiojulikana baada ya kuwaua polisi.

Miongoni mwa matukio hayo, mawili yametokea mkoani Pwani na la hivi karibuni la Kongowe, limetokea mpakani mwa Dar es Salaam na Pwani.

Vilevile tukio hili limetokea wakati waumini hao hawajasahau mauaji ya kutisha nchini Kenya ambako magaidi wamevamia Chuo Kikuu cha Garissa na kuua wanafunzi 147.

Kutokana na hofu ya kiusalama, makanisa mbalimbali katika kipindi hiki cha sikukuu yameongeza ulinzi na katika baadhi ya makanisa ni marufuku kuingia mikoba au vifaa vingine visivyoeleweka.

Ilivyokuwa
Kwa mujibu wa waumini wa kanisa hilo, tangu alipoingia kanisa na ibada ilipokuwa inaendelea yeye, alikuwa anaonekana kufanya mawasiliano ya simu mara kwa mara, kinyume na kanuni za ibada kanisani humo.

Waumini hao walisema mtu huyo aliwahi kabla ya muda wa ibada na kuketi katika viti vya nyuma, lakini baadaye alikuwa anahamahama na wakati mwingine alitoka nje kufanya mawasiliano.

“Unajua sisi Wakristo tunajuana na kama mgeni pia ataonekana mgeni kikanisa, lakini siyo kinidhamu, maana nidhamu ya ibada inalingana katika makanisa yote. Lakini huyu jamaa alikuwa na pilika nyingi, mara atoke nje, anaongea na simu, mara atume ujumbe wa simu, kweli alionekana tofauti kabisa,” kilisema chanzo chetu.

“Tukiwa katikati ya ibada, mtuhumiwa alimwomba muumini mmoja wa kike aliyekuwa jirani naye amwonyeshe choo kilipo, akatoka nje lakini kwa kuwa waumini walikuwa wanamwona tofauti, walimfuatilia na kukuta hajaelekea chooni alikoelekezwa, bali alijibanza ukutani na kuongea na simu huku akiingiza mkono ndani ya koti,” aliongeza muumini huyo.

Wakati mtu huyo akiwa nje, ilitolewa taarifa Kituo cha Polisi kilichopo karibu na askari walifika kanisani hapo na kumkamata.

Paroko wa Parokia hiyo, Padri Nicholas Kirimo alisema mtu huyo anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 40 alikamatwa baada ya waumini kumtilia shaka kutokana na kukosa utulivu wakati wa ibada.

Alisema baada ya mtu huyo kuingia kanisani alikuwa akihama kutoka kiti kimoja hadi kingine huku akitoka mara kwa mara nje kwenda kuongea na simu, ndipo viongozi wa kanisa walipomtilia shaka na kuwapa taarifa polisi waliokuwamo kanisani.

“Ni mara ya kwanza kutokea kwa tukio kama hili na hatujajua alikuwa na lengo gani,” alisema Padri Kirimo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Ulrich Matei alisema mtuhumiwa huyo alipopekuliwa alikutwa na bastola aina ya browing na risasi nane na anashikiliwa kwa mahojiano zaidi.

Kamanda Matei alisema katika mahojiano ya awali, mtuhumiwa alisema ni mkazi wa mkazi wa Mburahati, Dar es Salaam na mara nyingine akadai ni mkazi wa Mkuranga.

Alisema pia kuwa mtuhumiwa huyo amewaeleza polisi kuwa ni mkandarasi, anafanya kazi ya kujenga bandari kavu katika eneo la Kazimzumbwi wilayani Kisarawe na ndiyo maana aliona vyema akasali jirani katika kanisa hilo.

Hata hivyo, Matei alisisitiza kuwa anashikiliwa kwa mahojiano zaidi ili polisi wajiridhishe na maelezo na uhalali wa kumiliki silaha na risasi hizo.

Matei aliwataka waumini wa makanisa mbalimbali kuendelea na misa kama kawaida kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa pindi wakibaini watu wanaowatilia shaka.

Matukio ya uhalifu kanisani
Mchungaji wa Kanisa la Apostolic lililoko mji mdogo wa Shirati wilayani Rorya, Mkoa wa Mara, Owiti Ariri, aliuawa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi kwa kupigwa risasi usiku muda mfupi baada ya kukabidhiwa sanduku la fedha za kikundi chao cha kuweka na kukopa alichokuwa akikifanyia kama mweka hazina.

Huko Mombasa nchini Kenya watu wenye silaha wasiofahamika walimfyatulia risasi na kumuuwa mchungaji mmoja wakati wa ibada kanisani siku ya Jumapili. Mauaji hayo yalitokea ndani ya mlango mkuu wa kuingilia kwenye kanisa la Maximum Revival Centre katika mtaa wa majengo.

Pia, Bukoba mkoani Kagera watu wasiojulikana walimuua muumini wa Kanisa la Pentecostal Asemblies of God (PAG), Mwalimu Dionizi Ng’wandu alipokuwa kwenye mkesha wa ibada.

Huko Bangui, Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR), watu wenye silaha walimteka Waziri wa Michezo na Vijana wa nchi hiyo, Armel Ningatoloum Sayo, wakati akitoka kanisani kuhudhuria ibada ya Jumapili.

Jeshi la Polisi mkoani Tanga walikawamata watu saba kwa tuhuma za kuhusika kuweka mabomu yaliyokuwa yameandaliwa tayari kulipuka kwenye nyumba mbili tofauti za ibada.

Source: Mwananchi

Comments