PALE JUU - FUVU LA KICHWA!

Na Frank Philip Seth

Niinuapo macho ya nafsi yangu, huku nikiwa nimefumba macho yangu, ndipo niuonapo MSALABA...na machozi yangu humwagika kama mito...
Hapo ndipo BWANA wangu alipoaidharau AIBU, akiwa mtu mzima, angali UCHI, aliangikwa hadharani kungali mchana, naam, ndiye nimjuaye kama Mfalme wa wafalme na BWANA wa mabwana.
Hapo ndipo nipatapo nguvu zangu, naam, mimi, hupata nguvu zangu na kusimama hata nisipoweza tena. Kwa KAZI ya msalaba, umasikini wangu ulichuliwa, magonjwa yalipata dawa, uzima nilipokea, laana ilikoma na ushindi wa kudumu tulipewa bure, si kwa fedha wala kwa dhahabu ila kwa ile DAMU ya thamani iliyomwagika pale msalabani.
Nautazama sana msalaba, bado nauona hata sasa japo haupo tena kwa jinsi ya mwili, naiona Damu japo haipo kwa jinsi ya mwili, namwona BWANA japo macho ya mwili hayamwoni, nauona ushindi japo vidole vyangu haviwezi kupapasa, ASANTE BWANA kwa MSALABA, ASANTE kwa KUNICHAGUA, sina maneno ya kusema bali chukua shukurani zangu toka moyoni mwangu kwa maana unaziona... asante BABA kwa kumleta MWANAO.
Bado najitazama, naona udhaifu na ubinadamu tu, je! mimi si mavumbi tu na humo nitarudi? Kiburi changu ki wapi? Je! Elimu na mali ni kitu gani hata nimwonee YEYE aibu mimi niliye mavumbi tu? Kani fahari ya mwandamu ni nini zaidi ya upepo na moshi upitao haraka? Basi nitazidi kukaa hapo chini ya msalaba, najua hakuna KIVULI wala kukingwa mvua, wala pa kujificha, bali mimi nitaketi hapo maana ndimo nguvu zangu zilipo.
Asane Roho wa Ufufuo uliyemwinua BWANA kutoka kulala, naam, wewe Roho wa Uzima unipaye uzima. Mwalimu wangu na Kiongozi, wewe unikumbushaye na kunifunulia SIRI za BABA kwa maana wewe naye mu wamoja! Asante Roho wa Uzima maana hata WAJINGA hunena na watu wakawasikiliza, naam mimi nisiyejua kitu hunipa cha kusema, nami nitafumbua kinywa kwa kuwa Upo uliyepo.
Siandiki haya kwa sababu ni msimu wa Pasaka, BWANA wangu hana msimu ila WOKOVU wake na USHINDI wake wa Calvary (Fuvu la kichwa) upo haupungui majira yote. Nani aliyemchagua akaaibika? Nani aliyemfuata akapata hasara?
Frank Philip Seth

Comments