PASAKA NI BUBUJIKO LA UZIMA.




BWANA YESU atukuzwe ndugu.
Karibu tujifunze habari za Pasaka.
Pasaka ni ukombozi lakini ukombozi huu unamtegemea sana huyo anayekombolewa.

 1 Kor 5:7 ''Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, KRISTO; ''
-Pasaka wetu ni KRISTO.


Jukumu la kila mmoja anayetaka kumpokea Pasaka wetu kujua majukumu ya kufanya yanayompendeza MUNGU.
Katika  kusherekea Pasaka hakikisha unabaki kwenye kumtii MUNGU.

         1. Jisafisheni.
Pasaka wetu amekwisha kutolewa sadaka lakini ili tushiriki upendo huo wa ukombozi ni lazima siku zote za maisha yetu tuzingatie kuwa safi katika matendo na katika maneno yetu. Ndio maana Biblia imesema Jisafisheni. BWANA Mungu anasema
Isaya 1:16-17 ''  Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane.  ''

-Usafi huu ni wa mwili na roho yako.
-Sio usafi wa siku moja bali siku zote.
-Kuna watu wengine huwa watakatifu sana wakiwa kanisani kwenye ibada lakini wakitoka utakatifu wanauacha kanisani na wao wanaondoka waitenda ubaya wa kila namna.

1 Timotheo 6:11-12 ''Bali wewe, mtu wa MUNGU, uyakimbie mambo hayo; ukafuate haki, utauwa, imani, upendo, saburi, upole.Piga vita vile vizuri vya imani; shika uzima ule wa milele ulioitiwa, ukaungama maungamo mazuri mbele ya mashahidi wengi. ''

-Wakati huu wa sikukuu usikubali kuwa na utakatifu wa kwenye ibada tu ya pasaka lakini ukitoka nje unaenda kutekeleza ahadi mlizoahidiana na yule mzinzi unayemjua.
Ndugu, Ni heri usingeenda kabisa kanisani na ikajulikana kabisa wewe ni mtu wa shetani kuliko kwenda kanisani na kunyenyekea ukiwa kanisani lakini ukitoka unaenda kutekeleza dhambi. mimi nakuonya maana ni hatari kwako.
Maovu mengi sana hutendeka wakati wa sikukuu.
Hata kwenda tu kwenye Disko au matamasha ya nyimbo za kidunia ni dhambi kuu.
Pasaka haihusiki na uovu wako ila uovu huo utakuletea madhara wewe mwenyewe maana MUNGU hataki dhambi na anataka utende matendo mema tu kama andiko hapo juu.

           2.  Mkatoe chachu ya Kale.
Pasaka wetu amekwishatolewa sadaku kuwa upatanisha wetu kwa MUNGU.
Lakini hatusherekei tu Pasaka au ukumbusho  kuja kwa ukombozi wetu ulioletwa na BWANA YESU aliye pasaka wetu bali lazima tutimize utakatifu wa MUNGU.
Lazima tutoe Chachu ya kale yaani tuachana na matendo ya zamani kipindi hatujaokolewa na BWANA YESU.
Waefeso 2:1-6 '' Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu; ambazo mliziendea zamani kwa kuifuata kawaida ya ulimwengu huu, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi; ambao zamani, sisi sote nasi tulienenda kati yao, katika tamaa za miili yetu, tulipoyatimiza mapenzi ya mwili na ya nia, tukawa kwa tabia yetu watoto wa hasira kama na hao wengine. Lakini MUNGU, kwa kuwa ni mwingi wa rehema, kwa mapenzi yake makuu aliyotupenda;hata wakati ule tulipokuwa wafu kwa sababu ya makosa yetu; alituhuisha pamoja na KRISTO; yaani, tumeokolewa kwa neema. Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika KRISTO YESU.  ''
-Matendo ya kale ndiyo hiyo chachu  ambayo hakuna mwenda mbinguni anayetakiwa kuyatenda.
-Wakati wa sikukuu ndio ahadi nyingi za kukutana na marafiki hutokea lakini ahadi zingine huwa ni pando la shetani.
-Yawezekana uliwahi kuwa mlevi sana lakini kwa Neema ya BWANA YESU ukaokoka na sasa uko vizuri kwa YESU lakini unapata mwaliko wa kukutana na rafiki zako ambao bado wako kabisa kwa shetani, usipochunga unaweza kujikuta unakunywa na wewe pombe hizo na kuwa machukizo makuu.

Pasaka ni bubujiko la uzima.
Pasaka ni kukumbuka kuja kwa ukombozi duniani.
Sherekea katika BWANA YESU. Mtii MUNGU katika njia zako zote.
Kataa mialiko ya dhambi na hakikisha uhusiano wako na MUNGU unaimalika zaidi kuanzia sasa sio uhusiano wako na MUNGU uanze kuharibika wakati wa Pasaka.
Zamani kabla hatujampokea YESU kama BWANA na mkombozi wetu, wakati huo tulikuwa watumwa wa dhambi lakini sasa tumekuwa wana wa MUNGU.
Yohana 1:12-13 ''Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake; waliozaliwa, si kwa damu, wala si kwa mapenzi ya mwili, wala si kwa mapenzi ya mtu, bali kwa MUNGU.   ''
Mimi Peter M Mabula nakutakia Pasaka njema ila utakatifu wa wakati wa Pasaka ufanye kuwa wa siku zote za maisha yako.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments