SIFA ZA MWALIMU WA NENO LA MUNGU

Na Askofu Zakaria Kakobe.
Leo, tunajifunza Biblia kutoka katika MATHAYO 22:1-46.  Ingawa kichwa cha somo letu ni  “SIFA ZA MWALIMU WA NENO LA MUNGU“, kuna mafundisho mengi ya kujifunza katika sura hii nzima.  Tutayagwa mafundisho tunayoyapata katika sura hii, katika vipengele sita:-
(1)              MFANO WA KARAMU YA ARUSI (MST. 1-14);
(2)            SIFA ZA MWALIMU WA NENO LA MUNGU (MST. 15-16);
(3)            KUMLIPA KAISARI YALIYO YA KAISARI (MST. 17-22);
(4)              HAKUNA KUOA AU KUOLEWA MBINGUNI (MST. 23-33);
(5)            AMRI MBILI KUU ZA AGANO JIPYA (MST. 34-40);
(6)            KRISTO, MKUU KULIKO DAUDI (MST. 41-46).

(1)      MFANO WA KARAMU YA ARUSI (MST. 1-14)
Baada ya Wakuu wa makuhani na Mafarisayo, kutafuta kumkamata (MATHAYO 21:46).  Yesu alitambua mipango waliyokuwa nayo mawazoni mwao, na ndipo akawaambia kwa mithali, akitumia mfano huu.  Katika mfano huu, mfalme mmoja, ni Mungu mwenyewe, MFALME WA WAFALME.  Mfalme huyu, anamfanyia arusi mwanawe Yesu Kristo ambaye ni Bwana Arusi (YOHANA 3:28-29).  Habari njema za wokovu, au Injili, ni Habari ya mema, ya vinono; na inafananishwa na mwaliko wa arusi, ambao watu wanaoalikwa, wanakuja kula mema wasiyoyagharimia (ISAYA 25:6).  Habari ya mema au Injili hii, kwanza walipelekewa Wayahudi.  Walipopata mwaliko huu wa arusi, walikataa kuja (YOHANA 1:11) na wakawakamata watumwa wa Mungu, manabii, waliowapa mwaliko huo, na kuwatenda jeuri na kuwaua (LUKA 11:49-51; 13:34).  Baada ya matukio haya, mfalme alighadhibika akapeleka majeshi yake na kuwaangamiza wauaji hao na kuuteketeza mji huo.  Jambo hili lilitokea kwa dhahiri, mnamo mwaka wa 70 B.K.  Majeshi ya Warumi, yaliuteketeza mji wa Yerusalemu na kufanya mauaji makubwa kwa Wayahudi, na kuharibu kila kilichowatia kiburi, pamoja na Hekalu la Sulemani.  Baada ya Wayahudi kukataa kuja kwa Yesu, watumwa wa Mungu walitumwa kwa WOTE WALIOWAONA (Mataifa), na wengi wakauitikia mwito wa Injili (MATENDO 14:27).  Hata hivyo, wengine wanaouitikia mwito wa Injili, ingawa wanaonekana Kanisani kila siku na kuonekana kama wameokoka, ni WANAFIKI, hawana vazi la Arusi, VAZI LA WOKOVU.  Vazi la wokovu, ndiyo mapambo ya dhahabu kwa mtu aliyeokoka (ISAYA 61:10).  Wanafiki hawa kwa sasa, wanaweza wasijulikane Kanisani, lakini mfalme atakuja kuwatazama na kuwafichua, na atawatenga mbali na ngano au samaki na kuwatupa katika Jehanum ya moto (MATHAYO 13:28-30, 40-43, 47-50).

(2)      SIFA ZA MWALIMU WA NENO LA MUNGU (MST. 15-16)
Biblia inaweka waziwazi sifa za Mwalimu yeyote wa Neno la Mungu.  Ni muhimu kwa yeyote anayejiita mwalimu wa Neno la Mungu, kujipima na kujithibitisha kama kweli ni mwalimu wa Neno, anayempendeza Mungu, kwa kuangalia kama ana sifa tano (5) zifuatazo:-

(1)              Awe amekwisha kuhesabiwa haki na Mungu, kwa kuzaliwa mara ya pili, au kuokolewa (ZABURI 50:16);
(2)              Ayafahamu asemayo kwa UTHABITI.  Ni vigumu mtu kuwa mwalimu, bila yeye mwenyewe kuwa tayari kuwa mwanafunzi KWANZA ( 1 TIMOTHEO 1:7).  Inampasa mwalimu kuwa mtu wa KWELI yaani mtu wa NENO, aliyejaa Neno la Mungu maana Neno lake ndiyo kweli (MST. 16; YOHANA 17:17);
(3)              Aifundishe njia ya Mungu katika KWELI (MST. 16), maana yake, aifundishe njia ya Mungu ya kufanya kila jambo, kwa kutumia NENO au BIBLIA na siyo mawazo yake tu au maneno  tu ya kibinadamu;
(4)              Awe hajali cheo cha mtu awaye yote, wala kutazama sura za watu (MST. 16).  Kila mmoja amfundishe kweli bila kujali ni tajiri, afisa mkubwa, au maskini hata kwa gharama ya kusababisha maadui (2 WAKORINTHO 13:8; WAGALATIA 1:10, 2:5-6);
(5)              Afanye anayoyafundisha, KABLA ya kuwafundisha wengine (MATENDO 1:1; WARUMI 2:21-24).  Watu wengi wanaopenda kuwa Waalimu wa neno la Mungu, bila kuwa na sifa hizi, wanajitafutia HUKUMU KUBWA ZAIDI kuliko hukumu ya wenye dhambi wengine, maana hawa, wanashiriki kuwadanganya na kuwapoteza wengi (YAKOBO 3:1).
(3)      KUMLIPA KAISARI YALIYO YA KAISARI (MST. 17-22)
Yesu Kristo hapa, hakuwa na fedha kabisa mfukoni mwake.  Aliwaambia, “Nionyesheni fedha ya kodi”.  Nao wakamletea dinari.  Watumishi wa Mungu, inatupasa kutafuta uhusiano na Mungu kwanza, KABLA ya kutafuta fedha za Injili na vipaza sauti.  Tukiwa na Roho Mtakatifu wakati wote, na nguvu zake kuwa pamoja nasi, na tukafanya mapenzi yote ya Mungu na kuifundisha njia ya Mungu katika kweli, VYOTE hivyo vitafuata (MATENDO 3:6).  Hapa pia, wanafiki hawa walimtegea Yesu aseme kwamba yeye ni Mfalme, ili wapate njia ya kumshtaki; hawakujua kwamba yeye hakuwa mfalme wa dunia hii.  Kwa sheria, yule ambaye picha yake au sanamu yake ilionekana kwenye fedha ndiye aliyekuwa mfalme, na ilieleza waziwazi kwamba fedha zote za nchi hiyo ziko chini yake.  Yesu aliwaeleza hapa na pia anatufundisha kulipa kodi za Serikali kwa sababu wafalme ni watumishi wa Mungu kwetu kwa ajili ya kutupa mema kama barabara nzuri, na huduma nyinginezo za jamii (WARUMI 13:4).  Kwa kulipa kodi, tunamrudishia Kaisari yaliyo yake.  Hata hivyo, inatupasa kumlipa Mungu yaliyo ya Mungu.  Yaliyo ya Mungu, ni mioyo yetu na roho zetu.  Hivi ni mali yake.  Kama tunavyolipa kodi ya Serikali kama wajibu wa kisheria, inatupasa kumpa Mungu mioyo na roho zetu azitawale.  Hivi siyo vya Serikali.  Tusiwape wafalme mioyo yetu na kujikuta tunachukuliwa na mambo ya dunia hii kuliko ya Mungu (MITHALI 23:26; EZEKIELI 18:4).  Wanafiki hawa, pamoja na maelezo haya mazuri, bado walimshtaki Yesu kwamba walimwona  Yesu anawazuia watu wasimpe Kaisari kodi, akisema yeye ni mfalme.  Hata tukimjibu vizuri mwenye nia mbaya, nia ile itakuwa dhahiri (LUKA 23:1-2).

(4)      HAKUNA KUOA AU KUOLEWA MBINGUNI (MST. 23-33)
Mungu wetu, siyo Mungu wa wafu au miili hii itakayokufa na kubaki kaburini.  Ni muhimu tuangalie zaidi mambo yasiyoonekana kuliko yanayoonekana, maana mambo ya mwili huu ni ya muda tu, bali ya rohoni ni ya milele (2WAKORINTHO 4:18).  Ni hatari kubwa kumfuata mume au mke anayetuzuia kuokolewa, vilevile, ni hatari kubwa kuacha wokovu kwa sababu ya mateso ya mume au maudhi ya mke.  Kuliko kubaki na mume na kuacha wokovu, ni heri kwa mbali mno, kubaki na Wokovu na kuachwa na mume au mke.  Mume au mke hatutaenda naye mbinguni.  Kule, tutaishi kama malaika, bila kuoa au kuolewa.  Vivyo hiyo, hatupaswi KULAZIMISHA kurudiana na mume, aliyetuacha, ambaye hajaokoka.  Tukae hivyo hivyo bila kuolewa, na kumwomba Mungu ili amwokoe au ambadilishe kwanza mume wetu, ili kurudiana kwetu kusiwe mwisho wa imani yetu ya wokovu kwa kuzuiwa na mume huyo.  Pale tunapoona kurudiana kwetu hakujakamilika, Mungu ana makusudi ya kumtengeneza KWANZA yule mume kwa faida yetu.  Wakati huo wa subira, tuangalie ya mbinguni kusikokuwa na kuoa au kuolewa.  Vivyo hivyo, tunapochelewa kuolewa au kuoa, kamwe tusiache wokovu na kuoa au kuolewa na mataifa watakaotuzuia kwenda mbinguni, ni heri kukaa hivyohivyo.  Itatufaidia nini tukiupata ulimwengu wote na kupata hasara ya nafsi zetu (MARKO 8:36).

(5)      AMRI MBILI KUU ZA AGANO JIPYA (MST. 34-40)
Leo hatuko chini ya amri kuu KUMI.  Tuko chini ya amri kuu mbili tu, na nyingine nyingi zilizopo zinaingizwa katika hizo.  Ukimpenda Mungu kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote, huwezi kuwa na miungu mingine ila yeye, utahubiri wokovu wake na kumtumikia na kufanya yote aliyoamuru.  Ukimpenda jirani yako, yaani kila mtu mwingine kama nafsi yako, huwezi kuzini na mke wake, kumwambia uongo, kumwua, kumsengenya, kumwibia, n.k; maana usingependa wewe pia kufanyiwa hayo (WARUMI 13:8-10).

(6)      KRISTO, MKUU KULIKO DAUDI (MST. 41-46)
Mafarisayo, walifahamu kwamba Yesu ni Mwana wa Daudi kutokana na ZABURI  89:35-36; ISAYA 9:6-7 na ISAYA 11:1.  Kama Yesu angekuwa ni Mwana wa Daudi tu, hapo ingemaanisha kwamba Yesu alikuwa mwanadamu tu kama Daudi, hakuna la zaidi.  Sasa hapa, anawakumbusha juu ya ZABURI 110, ambaye waliifahamu sana kwamba ilimzungumzia Yesu.  Katika Zaburi hiyo Daudi kwa Roho Mtakatifu, anamtaja Yesu kuwa ni BWANA (YEHOVA) au Mungu wa Daudi (ZABURI 110:1), tena ni Kuhani kwa mfano wa Melkizedeki, hana baba, hana mama, hana mwanzo wa siku zake wala mwisho wa uhai wake (ZABURI 110:4; WABRANIA 7:1-3) na Mfalme mwenye enzi juu ya adui zake (ZABURI 110:2), aliyeketi mkono wa kuume wa Bwana.  Kristo kama MUNGU, alikuwa BWANA wa Daudi.  Yesu Kristo alikuwa Imanueli, Mungu pamoja nasi (MATHAYO 1:23).
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Ili kupata Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe  Fungua     
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA

Comments