SOMO: WATU WASIOFAA

Na Mchungaji Bryson Lema, Ufufuo na uzima Morogoro.

Utangulizi: Andiko muhimu sana la thamani  kwako siku  ya leo lipo katika 2NYAKATI 13:7… [Wakamkusanyikia watu mabaradhuli, wasiofaa kitu, waliojitia nguvu juu ya Rehoboamu mwana wa Sulemani, Rehoboamu alipokuwa kijana na wa moyo mwororo, asiweze kuwazuia.]…Biblia inasema waliosimama ni ‘watu’, na ‘siyo shetani wala pepo’. Biblia inawaita hao watu ni ‘mabaradhuli’. Kwa sababu Yeroboamu hakuwa mtu wa vita, watu hawa walimshinda. Watu wanaosimama mbele yako na kukuzuia, ni ‘watu wasiofaa’. Unapoona mambo yako hayaendi kama unavyotarajia, na pengine yanarudi nyuma ujue wapo watu wasiofaa waliojikusanya ili kukuzuia. Kumbuka kuwa, mwanadamu amejaa wivu. Ubinafsi wa kusema ‘mimi’ umemjaa mwanadamu.  Unapoishi vizuri,  mwanadamu  huinuka na kuuliza, “kwa nini wewe?” mwishowe mwanadamu wa aina hii  huwaendea wachawi na waganga wa kenyeji ili  kuhakikisha kuwa kile ulicho nacho, na asichotaka uwe nacho unakipoteza.

Kile kitu unachokitafuta kipo, na Mungu alishakupatia hata kabla ya kuwekwa kwa misingi ya ulimwengu. Binti au kijana unayetafuta mwenza, au wewe unayetafuta mtaji wa biashara, au wewe unayetafuta matibabu ya ugonjwa wako, ni baadhi ya vitu ambavyo tayari  ulishapatiwa na Mungu ingawa hujavipokea kwa sababu ya uwepo  wa wazuiaji (watu wasiofaa).
Mfano wa Kibiblia:  1 WAFALME 21:1-10, imeandikwa hivi…[Ikawa baada ya hayo, Nabothi Myezreeli alikuwa na shamba la mizabibu katika Yezreeli, karibu na nyumba ya kifalme ya Ahabu mfalme wa Samaria. 2 Ahabu akasema na Nabothi, akamwambia, Nipe shamba lako la mizabibu nilifanye shamba la mboga, maana ni karibu na nyumba yangu; nami nitakupa badala yake shamba la mizabibu lililo zuri zaidi; au ukipenda, nitakupa fedha sawasawa na thamani yake. 3 Nabothi akamwambia Ahabu, Bwana apishe mbali nikupe wewe urithi wa baba zangu. 4 Basi Ahabu akaenda nyumbani kwake, ana moyo mzito, tena amekasirika, kwa sababu ya neno lile aliloambiwa na Nabothi Myezreeli, akisema, Sitakupa urithi wa baba zangu. Akajilaza kitandani pake, akageuza uso wake, akakataa kula.  5 Lakini Yezebeli mkewe akamwendea, akamwambia, Kwa nini roho yako ina huzuni hata usile chakula? 6 Akamwambia, Kwa sababu nimesema na Nabothi Myezreeli, nikamwambia, Unipe shamba lako la mizabibu kwa fedha, au, ukipenda, nitakupa shamba la mizabibu lingine badala yake. Akajibu, Sitakupa shamba langu la mizabibu. 7 Yezebeli mkewe akamwambia, Je! Sasa wewe unaumiliki ufalme wa Israeli? Ondoka, ule chakula, moyo wako ufurahi; mimi nitakupa shamba la mizabibu la Nabothi Myezreeli. 8 Basi, akaandika nyaraka kwa jina la Ahabu, akazitia muhuri yake, akazipeleka zile nyaraka kwa wazee, na kwa watu wenye nguvu waliokuwa katika mji wake, waliokaa pamoja na Nabothi.9 Akaandika katika zile nyaraka, akasema, Pigeni mbiu ya watu kufunga, mkamweke Nabothi juu mbele ya watu, 10 mkainue watu wawili, watu wasiofaa, ili wamshitaki, na kumshuhudia, kunena, Umemtukana Mungu na mfalme. Kisha mchukueni nje, mkampige kwa mawe, ili afe.]…Hivi ndivyo wanadamu  walivyo: wanapoangalia mafanikio ya watu wengine (shamba la mizabibu), hujadiliana ama waibe hayo mafanikio  unayomiliki au wakuue. Kinachowahangaisha ni hicho  kitu ulicho nacho. Wapo watu hawalali usiku kwa sababu tu wameona kiti chako ofisini  mwako, au wameona watoto wako wanasoma shule nzuri, au wameona ndoa yako ilivyo na amani n.k. na matokeo yake wanakereka kwa wivu.
Kikao cha ‘watu wasiofaa’ wanamtumia shetani kama mwenyekiti wao. Mimi ninaye mwenyekiti wa kikao cha kuwazuia ‘watu wasiofaa’, ambaye ni Mungu mkuu kuliko miungu yote. Huyu Mungu wangu huweka kikao na watu  wake ili kuwazuia ‘watu wasiofaa’, kwa sababu Mungu wangu anaona vile vya sirini. Mchana wa leo tunawafuatilia wabaya wote waliokaa vikao na shetani na kuwaharibia mipango yao kwa Jina la Yesu.
Wapo watu wasiofaa kwenye maisha. Hawa hawafanyi kazi, ila hukaa vikao kutafuta namna gani wataiba mashamba  (mafanikio) ya wengine. Ni  hao ambao wakiona ndoa za watu ni nzuri huvizia na kuanza kutaka kuzivuruga hizo ndoa kwa wivu wao. Watu hawa wanasahau msemo  wa Kiswahili usemao, ‘Ukiona vyaelea vimeundwa’. Jina lako linaweza kujadiliwa kwenye  vikao  vya wachawi,  na wakafikia  maazimio ya kukuharibia, kuanzia kazini, nyumbani,  kwenye biashara zako n.k.
Mungu humpa mwanadamu ushindi wa maisha yake tokea pale mwanadamu anapozaliwa, lakini wengine wasiofaa wanapoona hayo maisha huyatamani, kama ambavyo Ahabu alilitamani  shamba la Nabothi. Yeremia alijulikana hata kabla ya kuzaliwa kwake. Mungu alishaandaa mazingira yote ya mwanadamu kabla ya kutungwa mimba, na ndiyo  maana Mungu  humpa mtu  hatima yake hata kabla ya kuwepo duniani.
Siyo mpango wa Mungu mwanadamu aishi kwa taabu. Maandiko  yanasema ‘Adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake’. Ni wale watu anaoongea nao kila siku. Ni wale mnaokutana nao  kila siku, na ndiyo maana Biblia inawaita ‘ni watu  wasiofaa’.  Mganga wa Kienyeji na Wachawi ni watu wasiofaa katika  jamii kwa sababu wao ndio wanaokaa vikao hivi na kujadili majina ya wengine ili wale wanaojadiliwa waishi  maisha ya taabu. Mungu ameniambia, ‘Atanibariki niingiapo na nitakapo’, sasa iwe je leo hizi Baraka sizioni? Ni kwa sababu wapo watu waliovuruga mipango yangu.
Katika Mhubiri imeandikwa ‘kuna majira na saa kwa kila jambo’. Saa ya kupita katika ugumu  imefika mwisho. Ni saa ya  Bwana kutenda. Uliniambia nisubiri nikiwa na miaka 20, hivi  sasa imetimia miaka 40, lazima nipate  hicho kitu sasa, siyo wakati wa kusubiri tena. Lazima aliyezuia hatima yangu aachie kwa Jina la Yesu. Wewe uliyekaa kwenye njia zangu, jua kuwa naachia mishale ya moto nao ina macho ya kupiga sawasawa. Imeandikwa ‘Amelaaniwa yeye azuiaye upanga wake kumwaga damu’ na mimi leo naachilia upanga wangu kumwaga damu ya wewe unayenizuia kufikia hatima yangu katika Jina la Yesu.
Katika Biblia tunaona kuwa ‘kila mfalme mtata hukumbana na Nabii mtata’. Akiinuka Ahabu, Mungu humuinua Eliya ili kumdhibiti swasawa na ujeuri wake. Angetokea Nabii Yeremia, asingeweza kumshughulikia Ahabu kwa sababu Yeremia angelia lia tu. Lakini mfalme Ahabu kwa ujeuri wake alikumbana na Nabii Eliya, jeuri mwenzake aliyezuia mvua kunyesha kwa miaka mitatu na nusu. Gideoni alipokumbana na yule Jemedari, hakumkimbia bali alimuuliza, ‘je wewe upo upande wetu au upo upande wa adui zetu’.  Maana yake ni kuwa, endapo huyu  jemedari angemwambia yupo upande wa adui, Gideoni angemmaliza pale pale.
Kuna wakati Mungu alichungulia jeshi la Wamisri ili awaangamaize. KUTOKA 14:24-25…[Ikawa katika zamu ya alfajiri, Bwana akalichungulia jeshi la Wamisri katika ile nguzo ya moto na ya wingu, akalifadhaisha jeshi la Wamisri. 25 Akayaondoa magurudumu ya magari yao, hata yakaenda kwa uzito; na Wamisri wakasema, Na tukimbie mbele ya Israeli; kwa kuwa Bwana anawapigania, kinyume cha Wamisri.]….  Kitendo hiki cha Mungu kuchungulia hili jeshi, lilisababisha matairi/magurudumu ya magari ya Wamisri kuachia, na matokeo yake wakaangamizwa. Ni maombi yetu siku ya leo, kila anayekuonea katika maisha yako, Mungu amchungulie na kumshughulikia kwa Jina la Yesu.
Kama wewe hujaokoka, kwa kumpa Yesu maisha yako, ni siku nzuri kufanya hivyo ili Mungu aweze kukupigania kinyume na hao wanavuruga maisha yako.

Comments