WAMWACHAO BWANA YESU WATATEKETEZWA.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze neno la MUNGU la uzima wa roho zetu.


Isaya 1:28 ‘’ Lakini kuharibika kwao wakosao nao wenye dhambi kutatokea wakati mmoja, nao wamwachao BWANA watateketezwa.   ‘’


=Wakosaji watateketezwa siku ya mwisho kama hawatatubu wangali hai leo.

Wakosaji ni wale wanaomkataa YESU na kukataa kuishi kwa kulifuata Neno la MUNGU, Hawataki utakatifu, hata kama wanakwenda kanisani lakini kama ni wakosaji kwa MUNGU hao wanatakiwa watubu maana wasipotubu kuna jehanamu mbeleni.

=Wenye dhambi watateketezwa kama wasipotubu wangali hai.

Wenye dhambi karibia wote wanajifahamu na wanajua kabisa kwamba dhambi hizo zitawafikisha jehanamu ya milele lakini wameshupaza shingo zao, hawataki kutubu.

=Wamwachao BWANA watateketezwa kama hawatatubu wakati wakiwa hai duniani.

Wamwachao BWANA ni wengi sana.

-Kuna ambao wanamwacha BWANA YESU baada ya kupokea kile walichohitaji kutoka kwake.

Kuna watu wamepona magonjwa ya ajabu baada ya maombezi, watu hao waliapa mbele ya kanisa na mbele za MUNGU kwamba wao hawawezi kumuacha BWANA YESU maana amewatendea makuu sana. Ni kweli ni makuu lakini huwezi amini kuna baadhi ya watu wa jinsi hiyo hata mwezi hauishi wanaacha wokovu na kurudi duniani. Kuna watu walipotendewa muujiza na MUNGU waliahidi huku wakitoa machozi mengi kwamba wao na YESU milele lakini hata miezi miwili haipiti wanarudi tena duniani. Hawamkomeshi mchungaji wala yeyote bali ni kwa uangamivu wao wenyewe. Wakienda jehanamu MUNGU hana hasara na kama wakirudi na kutubu kisha wakaenda mbinguni ni kwa faida yao wenyewe na sio MUNGU. Lakini je! Unamwacha MUNGU ili iweje?


Kumbu 32:15 ‘’ Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha MUNGU aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake.   ‘’

-Waisraeli walimwacha BWANA baada ya BWANA  kuwapa amani na furaha, walikuwa tu wanasikia kwamba kuna mataifa ni wakimbizi.

Hata leo akina Yeshuruni wapo wengi sana.

Kuna mtu alikuwa mtumishi mzuri wa MUNGU lakini baada tu ya kubarikiwa kwa gari kwa sasa safari zake sio za kanisani tena kama zamani bali kila siku yuko safarini kwenda kwenye starehe.

Ndugu yangu, hata kama BWANA atakubariki utajiri usije ukamwacha.

-Hata kama umebarikiwa kwa kufunga ndoa takatifu lakini isiwe hiyo ndiyo chanzo cha kumwacha Mwamba wa wokovu wako.

Kuna watu walikuwa hawana kazi kwa miaka mingi, waliomba sana , walilia sana lakini hawakupata maana adui alikuwa anawakamata kwa sababu walikuwa upande wake, watu hao wakaokoka na kuingia katika ufalme wa Mwana wa pendo la MUNGU, BWANA YESU akawabariki kazi. Lakini wamekuwa waaminifu mwezi wa kwanza tu lakini baada ya hapo hata mchungaji akiwapigia simu hawapokei au wanapokea na kusema wako busy kazini kumbe hata hawako kazini. Ndugu kama unafanya hivyo hiyo ni kwa uangamivu wako mwenyewe.

Kuna watu baada ya MUNGU kuwabariki hata Kiswahili wamebadili. Zamani walikuwa wanyenyekevu sana kwa MUNGU lakini sasa watumishi wakiwatafuta kwenye simu  majibu yao ni haya ‘’ I will call you later au  wait a minute kisha hiyo minute inageuka mwezi mmoja na nusu, au anajibu  I am busy today kumbe wala hakuna busy wala nini’’, Watu hawa wakati wanaombewa walikuwa wapole sana na hata hawajawahi kuchanganya lugha lakini baada ya Baraka kufika hawamhitaji tena Mwamba wa Wokovu wao. Ndugu unayefanya hayo tambua kwamba ni kwa uangamivu wako mwenyewe.

Kuna watumishi wamewahi kufunga siku 5 au zaidi ili kuwaombea tu watu Fulani wapate kazi nzuri lakini baada ya MUNGU kuwapa Baraka ya kazi watu hao wamegeuka na kuanza hata kuwasema vibaya hao hao ambao walilia mbele za MUNGU kwa ajili yao kwa ajili ya kazi. Ndugu unayefanya hayo tambua kwamba hiyo ni kwa uangamivu wako mwenyewe.

-Kuna watu huokoka ili wafanikiwe kisha wakishafanikiwa wanamwacha BWANA YESU aliyewaokoa.


Wagalatia 1:6-7 ‘’ Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya KRISTO, na kugeukia injili ya namna nyingine. Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya KRISTO. ‘’


-Nastaajabu unamwacha YESU upesi kiasi hiki.

Umeokoka baada ya kukaa miaka zaidi ya 35 bila kuolewa maana ulikuwa na laana ya kutokuolewa, lakini BWANA amekuondolea laana hiyo na umeolewa lakini kwanini unamwacha BWANA upesi namna hii.

-Umeokoka baada ya kutangaziwa na wachawi kwamba humalizi mwaka huu, BWANA amekuzingira pande zote maana wewe sasa ni mtoto wake, lakini je kwanini unataka kumwacha upesi namna hii?

BWANA YESU hana hasara, ukimwacha wewe ni kwa kujiangamiza wewe mwenyewe.

Wakati wa matatizo kila mtu anamtaka YESU amsaidie.

Wakati wa matatizo kila mtu ni mnyenyekevu sana kwa MUNGU lakini akipokea Baraka yake anakuwa tofauti, anaweza hata akawatukana watumishi wa MUNGU wale wale waliomwombea.

Ndugu zangu kuna madhara kama ukimwacha BWANA YESU aliyekuokoa na kukuponya na mabaya.


Mithali 4:6 ‘’ Usimwache, naye atakuhifadhi; Umpende, naye atakulinda. ‘’


-Ndugu, usimwache BWANA hata siku moja.

-Kaa katika wokovu wake siku zote naye atakulinda.

Kuna watu wanamwacha BWANA hata kama wako makanisani maana dhambi zao ndizo zinawatenga na MUNGU .

Kuna  watumishi wamemwacha BWANA hata kama wako makanisani, ukiacha agizo la MUNGU maana yake umemwacha MUNGU.

Mafalisayo walikuwa wanafanya kazi ya MUNGU lakini walikuwa wamechagua tu ya kuyafuata huku wameacha utakatifu na hawakuwa wanakemea dhambi tena


Luka 11:42 ‘’ Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa MUNGU; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.  ‘’


-YESU hakuwakataza kutoa zaka alitaka watoe zaka ila sio kutoa zaka tu bali walitakiwa kumtii MUNGU katika yote.

Hata leo yawezekana kuna watumishi ambao hawajawahi kukemea dhambi, hawawezi kusisitiza utakatifu kwa waumini lakini kila siku jambo la kusisitiza ni zaka tu, sio vibaya kusisitiza zaka maana mteule lazima atoe zaka lakini MUNGU anataka yote kwa pamoja. Usikemee  tu uchawi wakati wazinzi unawafahamu na haujawahi kuwakemea, BWANA hataki hivyo.

-Hao ambao huwakemei wamemwacha BWANA hata kama wanahudhuria ibada. MUNGU anataka uwakemee waovu ili wageuke na kuacha uovu wao. Mitume walikemea dhambi na imani yetu imesimama katika misingi ya mitume na manabii, mbona hatufuati kile mitume walichofanya? Ndugu mtumishi wa BWANA YESU nakuomba kemea kwa ujasiri. Wambie watu waikatae dhambi, waikimbie dhambi, waiogope dhambi na wasifanye dhambi.

Kama hawajaacha dhambi hao wememwacha BWANA hata kama wanakuja kanisani kila ibada ikifika.


Yeremia 2:17 ‘’ Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha BWANA, MUNGU wako, alipokuongoza njiani?  ‘’


-Ndugu unayemwacha BWANA YESU baada ya kubarikiwa unaweza wakati mwingine ukapata mabaya hapa hapa duniani lakini pia mabaya zaidi ni kama utaondoka bila kurudi kwa BWANA YESU maana hapo utapata mabaya zaidi yaani jehanamu.

Yeye MUNGU huwa hamwachi mtu yeyote lakini sisi ndio tunaomwacha, matendo mabaya ndiyo yanawatenga watu na MUNGU muumbaji wao.


Waebrania 13:5-9 ‘’  Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa. Hata twathubutu kusema, BWANA ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?  Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la MUNGU; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.  YESU KRISTO ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida. ‘’

-Usimwache BWANA YESU siku zote za maisha yako.

 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako
Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments