JE! NI KWELI KWAMBA, MKRISTO ANATAKIWA KUTII KILA AMRI YA MWENYE MAMLAKA?

Na Abel Suleiman Shiriwa.

Nimelazimika kuandika somo kutokana na upotoshwaji unaofanywa kwa makusudi au pengine kwa kutokuja, kutoka na andiko hili la Mtume Paulo, katika Waraka wake kwa Warumi.
Warumi 13: 1Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.
2 Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.
3 Kwa maana watawalao hawatishi watu kwa sababu ya matendo mema, bali kwa sababu ya matendo mabaya. Basi, wataka usimwogope mwenye mamlaka? Fanya mema, nawe utapata sifa kwake;
4 kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga bure; kwa kuwa ni mtumishi wa Mungu, amlipizaye kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5 Kwa hiyo ni lazima kutii, si kwa sababu ya ile ghadhabu tu, ila na kwa sababu ya dhamiri.
6 Kwa sababu hiyo tena mwalipa kodi; kwa kuwa wao ni wahudumu wa Mungu, wakidumu katika kazi iyo hiyo.
Hapa ndipo ambapo watu wengi huchanganyikiwa, na kushindwa kuelewa kusudi la Paulo katika maneno hayo: wao hudhani kila kiamriwacho na mwenye mamlaka basi kitiiwe tu, kwa mtu ambae anasoma kwa uongozi wa Roho Mtakatifu, hapo hawezi kupata tabu, maana maandiko yamejieleza vizuri kabisa, Paulo anazungumza juu ya Mamlaka yenye kuongoza vema, kuwa Serikali zimewekwa kwa ajili ya kuwafanya watu waishi vema, mfano sheria ya mauaji, kuwa, hautakiwi kuua, ukiua, Mwenye mamlaka atakushughulikia, sasa wataka asikushughulikie? Tenda mema ambayo Mungu amekutaka uyatende, hapo hutoona mwenye mamlaka akikusumbua wewe.
Sheria nyingi za Nchi, zimekataza kuiba, kutumia madawa ya kulevya, sasa kama wewe utajiepusha na hayo, maana yake utakuwa umeepukana na ghadhabu ya mwenye mamlaka, Mwisho Paulo akasema, Mwalipa Kodi, kodi ni mpango wa Mungu, kwa ajili ya Kuendesha Nchi, mtu anae kwepa kulipa kodi, huyu anakuwa ni muhalifu hata kwa Mungu, maana hata Yesu, mwenyewe jambo hilo la kutoa Kodi, alikubaliana nalo.
Luka 20:20 Wakamvizia-vizia, wakatuma wapelelezi waliojifanya kuwa watu wa haki, ili wamnase katika maneno yake, wapate kumtia katika enzi na mamlaka ya liwali.
21 Wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, twajua ya kwamba wasema na kufundisha yaliyo ya haki, wala hujali cheo cha mtu, bali unafundisha njia ya Mungu kwa kweli.
22 Je! Ni halali tumpe Kaisari kodi, au sivyo?
23 Lakini yeye alitambua hila yao, akawaambia,
24 Nionyesheni dinari. Ina sura na anwani ya nani? Wakamjibu, Ya Kaisari.
25 Akawaambia, Basi, vya Kaisari mpeni Kaisari, na vya Mungu mpeni Mungu.
26 Wala hawakuweza kumshitaki kwa maneno yake mbele ya watu; wakastaajabia majibu yake, wakanyamaa.
Watu walitafuta kila njia ya kutaka kumshitaki Yesu, wakakosa, wakaonelea, wamtege Yesu kuhusu mamalaka ya Kaisari, ya kulipa Kodi, ili akisema kuwa siyo halali, basi wapate kumfungulia Mashitaka, ila kwa sababu kodi ni jambo zuri, Yesu akasema, Ya Kiasari apewe Kaisari,na ya Mungu apewe Mungu, kwa hivyo ukimpa Kaisari yaliyo yake, (Kodi) Hutojipatia hatia mbele za Mungu, maana ni jambo njema.
Sasa kuna amri zingine ambazo hazitakiwi kufuatwa na Wakristo, hata kama zimetolewa na mwenye mamlaka, maana Petro alitambua kuwa, wapo watu ambao watakuja kupotosha habari za Paulo kuhusu kutii kila mamlaka, kama alivyotoa Tahadhari kwa Wakristo.
2 Petro 3:15 Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;
16 vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe.
17 Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu.
18 Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele.
Petro ametuweka wazi kuwa, Paulo katika uandishi wake, kuna hekima kubwa sana ambayo aliyoitumia katika kuandika kwake, hekima ambayo, alipewa na Mungu, ambayo ni vigumu kuelewa nayo, sasa watu ambao hawana elimu, huzichukua kama zilivyo na kisha kuzifundisha kwa kuzipotosha, kwa hivyo tukaambiwa kuwa, watu kama hao tujiepushe nao, Petro akafafanua kuhusiana na utii wa Mamlaka, ni yepi hayo? Petro anasema:
1 Petro 2:13 Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa;
14 ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema.
Tunatakiwa kutii kila kinacho amriwa na mwenye mamalaka kwa kile ambacho kipo katika riadhaa ya Bwana, yaani kile ambacho hakitaenda kinyume na Mungu, yaani ambacho hakipingani na sheria ambazo Mungu ameziweka kwa watu waishi kwazo, sasa kama ikiwa ni kutii kila mamlaka, na usipotii unakuwa umekosea Mungu kama ambavyo wengi wanafundisha:
Nchi nyingi zinataka kupitisha sheria ya kuruhusu Ndoa za Jinsia moja, mfano mzuri, Ireland. Ambayo tayari imeshakuwa ni NCHI ya ushoga na usagaji, mwenye mamlaka akiamuru wanaume muoane, wewe ukaolewa, au ukamuoa mwanume mwenzio, au wewe mwanamke ukamuoa mwanamke mwenzio, kwa sababu imetolewa na mwenye mamlaka, Je! hutojipatia Hatia mbele za Mungu? Maandiko yanasemaje? Ukiamriwa ufungishe ndoa hiyo madhabahuni, Mungu hatokuhesabia hatia kwa sababu umetii amri ya Mwenye mamlaka?
1 Korintho 6:9 Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,
10 wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi.
Kama maandiko yamesema wafiraji na Walawiti mbinguni hawaendi, na mwenye mamlaka amesema, ufanye hivyo, na wewe unakomaa kuwa, usipomtii mwenye mamlaka umepingana na Mungu, ukifanya hayo Mungu atakuwa na ridhaa nawe? Ndugu yangu, si kila kiamariwacho, kinatakiwa kufuatwa,
Paulo mwenyewe kuna mambo mangapi ambayo alipingana na wenye mamlaka? Alikamatwa na kuwekwa gerezani, akiamriwa aache kutoa mapepo,
Matendo 16:16 Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua.
17 Akamfuata Paulo na sisi akipiga kelele, akisema, Watu hawa ni watumishi wa Mungu aliye juu, wenye kuwahubiria njia ya wokovu.
18 Akafanya hayo siku nyingi. Lakini Paulo akasikitika, akageuka akamwambia yule pepo, Nakuamuru kwa jina la Yesu Kristo, mtoke huyu. Akamtoka saa ile ile.
19 Basi bwana zake walipoona ya kuwa tumaini la faida yao limewapotea, wakawakamata Paulo na Sila, wakawakokota mpaka sokoni mbele ya wakuu wa mji;
20 wakawachukua kwa makadhi, wakasema, Watu hawa wanachafua sana mji wetu, nao ni Wayahudi;
21 tena wanatangaza habari ya desturi zisizokuwa halali kwetu kuzipokea wala kuzifuata, kwa kuwa sisi tu Warumi.
22 Makutano wote wakaondoka wakawaendea, makadhi wakawavua nguo zao kwa nguvu, wakatoa amri wapigwe kwa bakora.
23 Na walipokwisha kuwapiga mapigo mengi, wakawatupa gerezani, wakamwamuru mlinzi wa gereza awalinde sana.
Hapo wamekamatwa na kupigwa kwa sababu ya kumtoa pepo wa uaguzi, wenye mamlaka hawakutaka iwe hivyo nataka mniambie, Je Paulo aliacha kutoa Pepo kwa sababu wenye mamlaka walikataa, alipotoka Gerezani hakuendelea na kazi yake aliyopewa na Yesu?
Matendo 19:11 Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;
12 hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.

Paulo angekuwa na maana hiyo ambayo wengi huifikiri, angeendelea na kazi ya Mungu wakati ameshakatazwa na wenye mamlaka?
Mwangalie Yesu nae alichokijibu kwa mwenye mamlaka alipotaka kumzuia kwa habari ya Kazi yake ya Kiungu.
Luka 13:31 Saa ile ile Mafarisayo kadha wa kadha walimwendea, wakamwambia, Toka hapa, uende mahali pengine, kwa sababu Herode anataka kukuua.
32 Akawaambia, Nendeni, mkamwambie yule mbweha, Tazama, leo na kesho natoa pepo na kuponya wagonjwa, siku ya tatu nakamilika.
33 Pamoja na hayo imenipasa kushika njia yangu leo na kesho na kesho kutwa; kwa kuwa haimkini nabii aangamie nje ya Yerusalemu.
Ingekuwa ni kutii kila kiamriwacho na wenye mamlaka, Yesu alivyoambiwa aondoke ili asije kuuawa, asingeondoka? Petro nae vile vile msikilize alicho wajibu wenye mamalaka ambao walipingana agizo la Mungu la kuhubiri Injili kwa jina la Yesu,
Matendo 5:22 Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa habari,
23 wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango; lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani.
24 Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo.
25 Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu.
26 Ndipo yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu wasije wakawapiga kwa mawe.
27 Walipowaleta, wakawaweka katika baraza. Kuhani Mkuu akawauliza,
28 akisema, Je! Hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu.
29 Petro na mitume wakajibu, wakisema, Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu.
Ingekuwa ni kutii kila kinacho amriwa na wenye mamlaka, Petro na wenzie, wangeendelea Kuhubiri kwa Jina la Yesu mara baada ya kutolewa gerezani na Malaika, wakati walishaamuriwa wasihubiri kwa jina la Yesu? Pengine waweza kujiuliza ni wapi ambako walizuiwa wasilitaje Jina la Yesu? Ni hapa
Matendo 4:16 wakisema, Tuwafanyie nini watu hawa? Maana ni dhahiri kwa watu wote wakaao Yerusalemu ya kwamba ishara mashuhuri imefanywa nao, wala hatuwezi kuikana.
17 Lakini neno hili lisije likaenea katika watu, na tuwatishe wasiseme tena na mtu awaye yote kwa jina hili.
18 Wakawaita, wakawaamuru wasiseme kabisa wala kufundisha kwa jina la Yesu.
19 Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia, Kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe;
20 maana sisi hatuwezi kuacha kuyanena mambo tuliyoyaona na kuyasikia.
21 Nao walipokwisha kuwatisha tena wakawafungua, wasione njia ya kuwaadhibu, kwa sababu ya watu; kwa kuwa watu wote walikuwa wakimtukuza Mungu kwa hayo yaliyotendeka;
Sasa kaa utafakari, ikiwa tunatakiwa kutii kila mwenye mamlaka, Hao walioacha kutii ni wenye hatia? Petro atahukumiwa kwa sababu hakutii alipoamriwa asilitumie jina la Yesu? Paulo nae ataingia hatia kwa sababu nae alizuiwa na wenye mamlaka, kutoa mapepo, na akaendelea kutoa mapepo? Yesu nae ataingia hatiani kwa sababu nae hakutii agizo la Mtawala Herode la kuondoka asiwaponye wagonjwa, kuwafanya vipofu kuona, na viziwi kusikia? Wapo wengi tu, kama Shedrack Meshack na Abedinego, ambao nao hawakutii amri ya Mfalme Nebukadreza ya kusujudia sanamu aliyoifanya, hata kutupwa motoni ili waangamie, (Daniel 3:1-30) Je hawa nao tuseme wana hatia mbele za Mungu kwa sababu hawakumtii mwenye mamlaka?
Yupo Daniel, ambae nae katika Ufalme wa Dario, nae alitakiwa kutokuomba dua kwa Mungu wake wa mbinguni, kwa muda usipongua siku 30, isipokuwa, aombe kwa mfalme Dario hiyo dua, yaani Mfalme asimame kama Mungu, lakini Daniel alikataa, na hatimae kutupwa katika shimo ambalo lina simba, (Daniel 6:1-28) Je huyu nae ana hatia mbele za Mungu kwa sababu tu hakutii amri ya mwenye mamlaka, kwa sababu kila mamlaka imetoka kwa Mungu? Na kila amwasie mwenye mamlaka apingana na Mungu, hebu nisaidie katika hili jama, ninyi ambao mnasema, ni lazima kutii kila mamlaka.

Comments