Ufufuo na uzima Morogoro katika ibada. |
Utangulizi: Hili ni swali ambalo leo napenda kukuuliza, kwa sababu hata mimi niliwahi kujiuluza swali hili. Hivi kwa nini mimi ninaumwa? Sina shaka kusema majaribu huletwa na adui. Huyu adui hupenda kuniwekea mazingira ya kunifanya nikate tamaa. Kumbe sasa hiyo shida imesababishwa na mtu mmoja ambaye aliamua kunirushia hii shida. Je, lakini kama ni adui ameniletea hii shida, kwa nini Mungu ambaye ni msaada wangu, kimbilio langu hakuzuia hili jaribu lisinitokee wakati mimi nimeokoka? Kwa nini sasa Mungu amewaachia hawa watu wakakaa vikao vya uharibifu, hata wakafanikiwa kuniletea hili jaribu?
Wakati mwingine nawaona wale wasiomtii Mungu wanazidi kufanikiwa na kuinuliwa. Wapo wezi wanaiba,
wanafanikiwa na maisha yao yanazidi kunawiri. Wapo wengine wasiomtii Mungu
wakikosa kazini hawachukuliwi hatua yoyote, lakini mimi ninayemcha Bwana ikitokea
nimekosa kazini hata mara moja nitapewa onyo kali au barua ya kujieleza eti kwa nini nisifukuzwe
kazi!!!.
WAAMUZI
3:1-2…[Basi haya ndiyo mataifa ambao Bwana aliwaacha, ili awajaribu
Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya
Kanaani; 2 ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha
vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule;]… Hili andiko linataja mataifa ambayo Mungu
alimwambia Joshua asiwaondoe kabisa,bali awaache. Siyo kwa sababu hawa ni watu
wake, au kwamba wanafaa sana. La hasha‼!. Wameachwa kwa sababu ya kazi maalumu. Hata katika maisha yako, wapo watu walioachwa
siyo kwa sababu wewe ufe bali ni kufanya wewe ujue jinsi ya kupigana vita. Kumbe haja ya Mungu ni
kuniona mimi nakuwa mpiganaji wa hii vita.
Hili tatizo ulilo nalo Mungu ameliacha ili ujue jinsi ya kupigana vita.
Adui yako hajaachwa ili kwamba
akuangamize, bali kupitia huyo adui amefanyika kama chuo cha mafunzo ya vita yako. Huyo adui ni kiwanda cha
Bwana cha kukutengeneza. Maana bila Penina,hakuna Samweli. Kumbuka Hanna alikuwa
akistarehe na mumewe, lakini alipokuja
Penina, ikamfanya Hanna amtafute Eli.
Ndiposa Eli akamwabia Hanna kuwa,”Bwana
na akutane na haja ya moyo wako”.
Bila Penina, Hanna asingekubali mwanae
Samweli akae hekaluni. Hilo jaribu lako siyo la kukuangamiza, bali la kukufanya
uinuliwe. Bwana huruhusu adui aje kwako kwa njia moja lakini humtawanya kwa njia saba. Uonapo jaribu furahia, kwa
sababu lipo kwa ajili ya kukuvusha ng’ambo ya pili.
ZABURI
119:67…[Kabla sijateswa mimi nalipotea, Lakini sasa nimelitii neno lako]… Mateso yalimfanya Daudi ajue jinsi ya kumtafuta
Bwana. Hiyo shida yako si bure,
ila kuna kitu kimo ndani yako
ambacho maadui wanakiwinda ili kukipata.
Usimchukie aliyeinuka ili kufanya vita
nawe, ila kwa kupitia hilo tatizo alilotengeneza
utakuwa mtu wa tofauti.
ZABURI
119:71…[Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, Nipate kujifunza amri zako.]…. Wakati
mwingine unaweza kudhani Mungu hakupendi,
ila ujue kuwa Mungu anataka ujue
Yeye ni nani. Mungu hupenda kutufundisha,na huyo adui yako yupo ili
ujifunze jinsi ya kukaa kwake. Nyuma ya kila jaribu kuna ushindi. Yule aliyeshikilia
vitu vyako kukuzuia wewe usipate Baraka
zako, lazima umfyeke kwanza ili uweze kuvuka ng’ambo ya pili. Kabla ya tatizo,
nilikuwa mtu wa kawaida, lakini baada ya tatizo nimehitimu chuo cha vita. Sikuzuii
kunipinga ila ninaachojua ni kuwa
nitakusagasaga, kwa sababu imeandikwa “mimi ni rungu la Bwana na silaha za Bwana za vita”.
Kila kizazi kina mfalme na nabii wake. Mungu huangalia, pale anapoinuka
Ahabu na Eliya lazima ainuke. Ahabu
haogopi machozi ya akina Yeremia.
Anapaswa kuinuka Eliya ili aizuie mvua
kwa miaka mitatu na nusu. Eliya hana majadiliano. Hata kwa sasa lazima liwepo kanisa ambalo halina majadiliano, Kanisa ambalo
linalosema , "kabla ya kuzika huyu mtu, ‘maombi
kwanza". Sisi hatusemi ‘Bwana ametoa na Bwana ametwaa’ hapana‼! Kwa sababu hata wanadamu wapo
wanaotwaa‼! Shetani hapaswi kubembelezwa. Siyo muda wa kukaa na kusema
‘tumshukuru Bwana kwa kila jambo’ siyo muda wa kufarijiwa kwa maneno matupu.
Shetani ni wa kupigwa siyo wa kuombolezewa. Biblia
inasema MATHAYO 2:18…“Sauti
ilisikiwa Rama, Kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake,
Asikubali kufarijiwa, kwa kuwa hawako.”. Inakuwa je wewe unakubali kirahisi tu kusimama na kumsubiri Bwana, badala ya kudai
kilicho chako? Ili hilo tatizo lako liondoke, pigana‼
Usikatishwe tamaa na tatizo lililopo maishani mwako, kwa sababu upo mlango wa kutoka kwa hilo tatizo. Limekuwepo
ili wewe ujue jinsi ya kupigana. Biblia
inasema ”Kila pando asilolipanda Baba litang’olewa”. Pando la magonjwa, pando la
umaskini, pando la kukosa kazi n.k lazima
yang’oke kwa Jina la Yesu. Cha muhimu kwako ni kupigana. Waliokueweka
gerezani ili usage ngano kama Samsoni, wajue kwamba
hiyo ni njia ya kufanya misuli yako iongezeke. Na pale nywele za kichwa chako
zitakapoota tena kama za Samsoni, wale utakaowaua baada ya kusaga ngano gerezani
watakuwa ni wengi zaidi ya wale ulioua kabla
ya tatizo lako. Tatizo la kanisa la leo ni kuwa watu wamezoea
kufarijiwa. Huyu shetani tuliye naye amezoea kuona unafarijiwa. Zipo aina mbili
za sura ya mdai anapokwenda kwa mdaiwa
wake. Sura ya kwanza ya anayedai ni ile ambayo humwendea mdaiwa huku akitabasamu, na kwa upande wa mdaiwa
huwa haogopi chochote jinsi ya kulipa hilo deni la mtu kama huyu. Lakini mdai anapokuja na sura
ya ghadhabu, mdaiwa hufanya juhudi zote
ili kulipa salio lote la hilo deni husika. Leo
ni siku ya kudai kilicho chetu, kwa kuvaa sura ya ukali kwa wale waliotuonea.
Bila kuwa na Yesu maishani mwetu si rahisi kudai kilicho chetu kutoka kwa
shetani. Wewe ambaye hujaokoka ni wasaa
wako sasa kuamini na kumpa Yesu Krsito maisha
yako kwa kuokoka.
© Information
Ministry (Ufufuo Na Uzima - Morogoro)
Mtaa wa Nguvu Kazi,
(Minara Mitatu), Mkundi-Morogoro.
/or
Contact our Senior
Pastor:
Dr. Godson Issa Zacharia
(Ufufuo Na Uzima – Morogoro)
Cellphone: (+255) 757 550878 / +255 719798778
Comments