KWA NINI NIMEAMUA KUMTUMIKIA MUNGU NINGALI KIJANA?


Na Abel Shiriwa.
Wapo watu wengi sana ambao wamekuwa wakinishangaa kwa nini nimeamua kumtumikia Mungu ningali kijana? Kwa nini nisile kwanza ujana, maana maisha yenyewe mafupi, wengine wakinitaka kwenda kujirusha kwenye kumbi za starehe, na kufanya kila aina za anasa, ambazo ndizo hasa zinatafsiriwa kama chakula cha ujana:
Jawabu langu me ni hili
1 Timotheo 4:12 Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi.
Sitaki mtu awaye yote audharau ujana wangu, kwani nahitaji kila mtu auheshimu ujana wangu, maana nikila ujana, sitokuwa na heshima, maana mademu wengi watauona mwili wangu ulivyo kupitia kufanya uzinzi nao, sasa heshima yangu itakuwa wapi? Nikila ujana,nitavaa mlegezo, matako yangu yatakuwa nje, na mchirizi wa sehemu ya haja kubwa, utaonekana, sasa heshima yangu itakuwa wapi? Nikila ujana, nitavuta bangi, nitatumia madawa ya kulevya, nitakuwa mlevi na kuwa mtukanaji, mlopokaji, sasa heshima yangu itakuwa wapi? Nikila ujana, nitakuwa mwizi, kibaka, na hatimae kwenda Jela, heshima yangu itakuwa wapi? Nani atakae uheshimu ujana wangu? Lakini nikipelekwa Jela, kwa sababu ya kumuhubiri Kristo, heshima yangu itapotea katika ujana wangu? La hasa, heshima yangu haitopotea, kwa hivyo, Ili heshima yangu isipotee ni lazima niyafanye haya:
2 Timotheo 2:22 Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, pamoja na wale wamwitao Bwana kwa moyo safi.
23 Walakini uyakatae maswali ya upumbavu yasiyo na elimu, ukijua ya kuwa huzaa magomvi.
Pengine unaweza kujiuliza, ni kwa nini nimeambiwa nizikimbie tamaa za ujanani na siyo za Uzeeni? Ni kwa sababu mawazo ya kufanya uovu kwa mtu huanza pale awapo kijana.
Mwanzo 8:21 BWANA akasikia harufu ya kumridhisha; BWANA akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya.
Kwa hivyo siwezi kuyaruhusu hayo mawazo mabaya yautawale moyo wangu ningali kijana, wewe tembelea magerezani, vijiweni, wengi ni vijana, maana ndiyo ambao wanaongoza kwa kufanya maasi, maana wanazo nguvu za kufanya hivyo, kwani si rahisi mzee kufanya ujambazi, kwa sababu ya udhaifu, bali mimi nitazitumia nguvu za ujana wangu kumtumikia Mungu wangu,
1 Yohana 2:14……. Nimewaandikia ninyi, vijana, kwa sababu mna nguvu, na neno la Mungu linakaa ndani yenu, nanyi mmemshinda yule mwovu.
Kwa sababu mimi kijana nina nguvu na pia neno la Mungu limo ndani mwangu, yanipasa kuutumia vema ujana wangu, ili niepukane na hukumu ya Mungu.
Muhubiri 11:9 Wewe kijana, uufurahie ujana wako, na moyo wako ukuchangamshe siku za ujana wako, ukaziendee njia za moyo wako, na katika maono ya macho yako, lakini ujue wewe ya kwamba kwa ajili ya hayo yote Mungu atakuleta hukumuni.
NJIA kubwa, ya kuniepusha na hukumu ya Mungu, juu ya ujana wangu, ni kumbuka Mungu siku zote za ujana wangu,
Muhubiri 12:1 Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo.
Kwa hivyo siwezi kusubiri eti, mpaka niwe mzee ndiyo nije kumkumbuka Mungu, maana sijui kama uzee wenyewenitaja kuuona, kwa kuwa bado ningali kijana nguvu uwezo ni nano wa kumtumikia Mungu, sina budi kufanya hivyo, nijapokuwa mzee sitoweza kabisa kuijongoza kama nilivyo kijana:
Yohana 21:18 Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako, na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka.
Kwa hivyo Sitoacha kumtumikia Mungu ningali kijana, njia yangu katika ujana, nitaisafisha na kuliweka neno la Mungu moyoni mwangu, na kuwa mtii kwa kazi ambayo Mungu ameitaka niifanye
Zaburi 119:9 Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako.
Nikishayafanya hayo, ni wazi kuwa hata nikiwa mzee, sitoweza kuiacha Njia ya BWANA
Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.
Kwa hivyo uzee wangu utakuwa bora, hata mvi zangu zitaheshimika sana, kwa sababu tangu utoto na ujana wangu, niliishi katika Njia nzuri yenye kumpendeza Mungu.
Mithali 16:31 Kichwa chenye mvi ni taji ya utukufu, Kama kikionekana katika njia ya haki.
Lakini nikila ujana nikitegemea eti nitakuja kumtumikiaMungu katika uzee, hapo nitakuwa najidanganya kabisa, hata kama nitakuwa mzee mwenye cheo, na mwenye hela nyingi, maana nitakuwa mzee mpumbavu kabisa, ambae nazidiwa hekima na kijana masikini.
Muhubiri 4:13 Heri kijana masikini mwenye hekima, kuliko mzee mfalme Mpumbavu, ambae hawezi kupokea maonyo.
Kwa hivyo mimi nimeamua kumtumikia Mungu ningali kijana bado, sihitaji kula ujana, bali nitakula neno la Mungu kila iitwapo leo, maana ndiyo chakula bora kuliko vyakula vyote Ulimwengu, Ukila Neno la Mungu, hutokuwa na haja ya kula vyakula vya Ujana, yaani
UZINZI
UASHERATI
WIVI
UJAMBAZI
KUVAA MLEGEZO
UTOAJI MIMBA
KUJIRUSHA NA MADEMU
UTUMIAJI WA MIHADARATI
KUFANYA UKAHABA
UTUKANAJI

Kwa hivyo nakusihi kwa moyo wa dhati kabisa, wewe rafiki yangu ambae unae usoma ujumbe huu, ambae akili yako imegubikwa na falsa ya kula ujana, kwa sababu maisha ni mafupi, daily upo clubn unajirusha na mademu, umekuwa kama popo, (hulali) hebu badili mwenendo wako huo, uutumie vema Ujana wako kumtumikia Mungu, maana ghadhabu yangu yaja, ambayo hutoweza kuepeukana nayo, kwani maisha haya ambayo unaishi kwayo, yanapita, ujana ukiula ni mtamu tu mdomoni, ila ukishaingia tumboni ni kama acid, utauyeyusha utumbo wako, na kukuacha na maumivu, ambayo hayana tiba kabisa, kinga ni bora kuliko tiba.

Comments