MAANA TATU(3) ZA UTAKASO.

BWANA YESU atukuzwe ndugu zangu.
Karibu sana tujifunze Neno la MUNGU.
Leo nazungumzia utakaso.
2 Samweli 22:25-33 ''Basi BWANA amenilipa sawasawa na haki yangu; Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.Kwa mtu mwenye fadhili utakuwa mwenye fadhili Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu; Kwake ajitakasaye utajionyesha kuwa mtakatifu; Na kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi. Na watu wanaoonewa wewe utawaokoa; Ila macho yako ni juu ya wenye kiburi, uwadhili. Kwa kuwa wewe u taa yangu, Ee BWANA; Na BWANA ataniangazia giza langu. Maana kwa msaada wako nafuatia jeshi; Kwa msaada wa MUNGU wangu naruka ukuta. MUNGU njia yake ni kamilifu; Ahadi ya BWANA imehakikishwa; Yeye ndiye ngao yao Wote wanaomkimbilia. Maana ni nani aliye MUNGU, ila BWANA? Ni nani aliye mwamba, ila MUNGU wetu? MUNGU ndiye ngome yangu yenye nguvu; Naye huwaongoza wakamilifu katika njia yake.''
-Utakaso ni jambo la muhimu kwa kila mkristo.
-Utakaso wa kweli unaanzia na juhudi yako kama mtoto wa MUNGU kuamua kuishi maisha yale ayatakayo MUNGU.
-Utakaso ni zao la kuokoka.
Katika maandiko hapo juu tunaweza kujifunza kwamba 
-MUNGU atakulipa sawasawa na haki yako. hiyo haki inasimamia mambo mengi ikiwemo na toba ya kweli.
-Aliyetakaswa maana yake ni msafi japokuwa zamani hakuwa msafi.
-Wakaidi MUNGU hawahitaji.
Ndugu yangu, Kuokoka maana yake ni kupokea mambo matatu ikiwemo utakaso.
Yakobo 4:8-10 '' Mkaribieni MUNGU, naye atawakaribia ninyi. Itakaseni mikono yenu, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili. Huzunikeni na kuomboleza na kulia. Kucheka kwenu na kugeuzwe kuwa kuomboleza, na furaha yenu kuwa hamu. Jidhilini mbele za BWANA, naye atawakuza. '' 
- Ndugu, Je! umempokea YESU hata ukapata utakaso wa dhambi zako?
-Uzima wa milele wataingia walio safi maana yake waliokombolewa na kutakaswa kwa damu ya YESU KRISTO.
 
Maana 3 Za Utakaso Ni Hizi; 

{A} Utakaso Ni Kusafishwa Dhambi.
 1 Thesalonike 4:3-5 ''Maana haya ndiyo mapenzi ya MUNGU, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua MUNGU.''
-Ndugu shika utakaso uliotakaswa kwa damu ya thamani sana ya BWANA YESU KRISTO.
 
Waebrania 9:27-28 ''
Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu; kadhalika KRISTO naye, akiisha kutolewa sadaka mara moja azichukue dhambi za watu wengi; atatokea mara ya pili, pasipo dhambi, kwa hao wamtazamiao kwa wokovu. ''
 
 {B} Kutakaswa Ni Kutengana Na Dhambi. 
2 Kor 6:17-18 '' Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema BWANA, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa BABA kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,''
-Ndugu, baada ya kutubu toba ya kweli hakikisha unajitenga na maovu yote, jitenge na marafiki wabaya, jitenge na mazingira mabaya ya dhambi, jitenge na anasa za dunia.
Luka 15:7 '' Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. '' 
-Ukiona hakuna umuhimu wa kutubu hiyo ni kwa uangamivu wako mwenyewe.
-Ukiona kujitakasa sio kitu kwako basi endelea lakini ni kwa hasara yako.
-Kutubu ni kumruhusu MUNGU awe upande wako tena.
Zaburi 32:1-2 ''  Heri aliyesamehewa dhambi, Na kusitiriwa makosa yake. Heri BWANA asiyemhesabia upotovu, Ambaye rohoni mwake hamna hila. ''

 {C} Kutakaswa Ni Kuwekwa Wakfu Kwa MUNGU. 
 Hesabu 8"17-18 '' Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama; siku hiyo niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu mwenyewe. Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli.''
-Hakuna kitu kizuri kama MUNGU kukuweka wakfu, wapo watu wengi tu waliowekwa wakfu na MUNGU.
-Kama umeokoka na unaishi maisha matakatifu na njina lako liko katika kitabu cha uzima mbinguni wewe umewekwa wakfu kwa ajili ya uzima wa milele.
Zaburi 19:12-14 ''Ni nani awezaye kuyatambua makosa yake? Unitakase na mambo ya siri. Umzuie mtumishi wako asitende mambo ya kiburi, Yasinitawale mimi. Ndipo nitakapokuwa kamili, Nami nitakuwa safi, sina kosa lililo kubwa. Maneno ya kinywa changu, Na mawazo ya moyo wangu, Yapate kibali mbele zako, Ee BWANA, Mwamba wangu, na mwokozi wangu.'' 

Je Mwenzangu Wewe Umetakaswa Kwa Utakaso Gani Katika Utakaso Huo Wa Aina 3? 

 2 Nyakati 29:15-17 ''Wakawakusanya ndugu zao, wakajitakasa, wakaingia, kama alivyoamuru mfalme kwa maneno ya BWANA, ili waisafishe nyumba ya BWANA. Nao makuhani wakaingia nyumbani mwa BWANA, katika mahali pa ndani, ili waisafishe, wakatoa uchafu wote waliouona hekaluni mwa BWANA, wakautupa nje uani mwa nyumba ya BWANA. Walawi wakautwaa, ili wauchukue nje mpaka kijito cha Kidroni. Basi wakaanza kutakasa siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza, hata siku ya nane ya mwezi wakafika katika ukumbi wa BWANA; wakaitakasa nyumba ya BWANA katika muda wa siku nane; wakamaliza siku ya kumi na sita ya mwezi wa kwanza.''
-Ndugu, kutubu ni muhimu sana kwako, sio ile toba isiyo ya kweli yaani unatubu na baadae kidogo unarudia dhambi ile ile.
Sio ile toba ya sekunde kadhaa tu huku ukiendelea na uovu. maandiko hapo juu yanaonysha toba ya kweli na ni toba endelevu maana haikufanyika kwa masihara tu ya sekunde chache.
MUNGU akupe kuifikia toba ya kweli. 
Dhambi zinawatenga wanadamu na MUNGU muumba wao.
Dhambi ni barabara ndefu ya kwenda jehanamu hivyo kutubu ni kubadilisha njia, badala ya kwenda kuzimu sasa kupitia YESU KRISTO unaanza kuelekea mbinguni kwenye uzima wa milele. 
'' Mimi, naam, mimi, ndimi niyafutaye makosa yako kwa ajili yangu mwenyewe, wala sitazikumbuka dhambi zako.-Isaya 43:25''
 Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana.
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments