YEHOVA NI MUNGU WA KARIBU WALA SIO MUNGU WA MBALI.

Na Mtumishi wa MUNGU, Peter M Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Kuna watu wakianza kuomba kuweka akili zao kwamba MUNGU yuko mbali sana hivyo watumie njia mbadala ndipo atawasikia.
-Kuna watu huomba huku wameshikilia vitu fulani vya kuvaa shingoni na kudhani kupitia vitu hivyo MUNGU atawasikia kumbe ndio wanamkasirisha MUNGU.
-Kuna watu huegamia kasanamu na kuomba kwa MUNGU kwa staili ya kuomba ka sanamu kumbe ndio kabisa wanatenda dhambi.
-Kuna watu huomba huku wameweka mikono mifukoni wakijua MUNGU yuko mbali hivyo kwa neema tu atasikia kumbe hawa wamekosa heshima, maana kama wangejua kwamba MUNGU yuko karibu nao na anawaona wangeomba kwa utii na unyenyekevu.
Yeremia 23:23 inathibitisha kwamba MUNGU sio MUNGU wa mbali ni MUNGU wa karibu.

Yeremia 23:23 '' Mimi ni MUNGU aliye karibu, asema BWANA, mimi si MUNGU aliye mbali.''
-BWANA ni MUNGU aliye karibu sana.

Je wale watu ambao huongea uongo kanisani wanajua kwamba MUNGU ni MUNGU wa karibu sana?
Je wale watu ambao huenda kuroga katika mikutano ya injili wanajua kwamba MUNGU yuko karibu sana?
Kuna watu wamewahi kutaka kuroga kwenye mikutano ya injili wakageuka wagonjwa wao au vilema maana BWANA aliwapiga kwa nguvu zake.
Yeremia 23:24 ''Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema BWANA. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema BWANA. ''
-Hakuna pahali utakuwa harafu useme kwamba MUNGU hakuoni.
Leo nazungumzia zaidi waomba na wale ambao hufanya masihara kanisani huku wakidhani MUNGU hawaoni kumbe MUNGU anawaona.
-Kuna watu hata sadaka zao ni majanga yaani anaweza akatoa pesa ambayo hata haitumiki, huyu hajui alitendalo na BWANA amemuona.
-Kuna watu huwasema vibaya wachungaji wao tena wakiwa madhabahuni, hawa wanahitaji neema.
-Kuna watu wanaweza hata kuchat na kutumiana picha za ngono wakiwa kanisani, hawa wanahitaji neema maana BWANA amewaona.
-Kwenye maombi watu pia hufanya masihara sana.
-Walio wengi wanadhani MUNGU yuko mbali kumbe yeye ni MUNGU wa karibu.
Ndugu zangu ni muhimu sana kuwa na nidhamu katika maombi.
Tunatakiwa tumwombe BABA wa mbinguni bila kutumia sanamu wala mikufu.
Tunatakiwa tumuombe BWANA MUNGU kwa unyenyekevu na nidhamu maana yeye anaona na yuko hapo hapo tulipo tukiomba.
Zaburi 11:4-7 '' BWANA yu katika hekalu lake takatifu. BWANA ambaye kiti chake kiko mbinguni, Macho yake yanaangalia; Kope zake zinawajaribu wanadamu.BWANA humjaribu mwenye haki; Bali nafsi yake humchukia asiye haki, Na mwenye kupenda udhalimu.Awanyeshee wasio haki mitego, Moto na kiberiti na upepo wa hari, Na viwe fungu la kikombe chao.Kwa kuwa BWANA ndiye mwenye haki, Apenda matendo ya haki, Wanyofu wa moyo watamwona uso wake. ''
-BWANA yuko katika hekalu lake. je wanaoleta masihara hekaluni hao wanafanya nini?
-MUNGU yuko mbinguni lakini anaona pote, hatutakiwi kuwa na masihara mbele zake. hatutakiwi tuwe na utani mbele zake. hatutakiwi katika maombi tukidhani kwamba MUNGU hatuoni.
Zaburi 139:7 '' Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? ''
-Ni vizuri kuwa na nidhamu katika maombi.
Kuna watu huomba huku mawazo yako kwingine.
Kuna watu tukisema tuombee taifa au kanisa hutawasikia wakiomba na watakuwa wazito lakini kama kiongozi wa maombi ukisema kwamba ''sasa tunavunja laana zote zilizomkamata yeyote aliyeko mahali hapa'' utaona kila mtu anaamka na kuanza kuomba kwa juhudi sana. wakati huo hutamuona mtu akiomba huku mikono mifukoni. kila mtu atavunja na kuvunja, kubaribu na kubomoa hakika.


Ndugu zangu maombi ambayo yanajibiwa ni haya.


1.Kuomba sawasawa na mapenzi ya MUNGU.
''Na huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. -1Yohana 5:14-15''
-Kuomba sawasawa na mapenzi ya MUNGU maana yake hatumlazimishi MUNGU kutujibu ila kwa neema yake tunabaki katika kusudi lake ambalo ameshalipanga tayari kutupa.


2. Kuomba katika ROHO MATAKTIFU.
''Kadhalika ROHO naye hutusaidia udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo, lakini ROHO mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Na yeye aichunguzaye mioyo aijua nia ya ROHO ilivyo, kwa kuwa huwaombea watakatifu kama apendavyo MUNGU. - Warumi 8:26,27''

3.Kuomba kwa imani kile kilicho mapenzi ya MUNGU.
''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu. -Marko 11:24''

Maombi yote password yake ili yajibiwe ni jina la YESU KRISTO.
Lazima maombi tuombe kwa jina la YESU KRISTO na katika jina la YESU KRISTO.
Yohana 14:12-14 '' Nanyi mkiomba lo lote kwa jina langu, hilo nitalifanya, ili BABA atukuzwe ndani ya Mwana.Mkiniomba neno lo lote kwa jina langu, nitalifanya.''

Licha ya kuyajua hayo yote lazima tutambue kwamba maombi yanahitaji nidhamu ya hali ya juu. wengine hawaombi ila wanapeleka majungu tu ambayo hata hayawezi kujibiwa.
Lazima tuwe na nidhamu katika maombi.
-Omba kwa imani.
-Omba katika ROHO MTAKATIFU.
-Tumia mamlaka ya KRISTO iliyo ndani yako
lakini nidhamu bado inabaki pale pale kwamba ni muhimu kwa na nidhamu. huku ukijua kwamba MUNGU sio MUNGU wa mbali ila ni MUNGU wa karibu.
Waebrania 4:13 '' Wala hakuna kiumbe kisichokuwa wazi mbele zake, lakini vitu vyote vi utupu na kufunuliwa machoni pake yeye aliye na mambo yetu. ''
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
Maisha ya Ushindi Ministry.
mabula1986@gmail.com
+255714252292.
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili

Comments