BWANA NITOE KATIKA MAWINDO YAO

Na Mchungaji Bryson Lema , Ufufuo na uzima Morogoro.

Utangulizi: Ukumbuke kuwa shetani  ni mwindaji, anafanya jitihada kuwakamata watumishi wa Mungu  na kuwawinda. Shetani hafanyi hii kazi peke yake, bali hushirikiana na wachawi, waganga wa kienyeji, wasoma nyota na mawakala wengineo watumiao nguvu za giza. Leo tunamfuata mwindaji popote alipo. Unapoina ndoa yako au biashara yako au  kazi yako  n.k. haviendi vizuri ujue  hakika kuwa kuna mwindaji keshaishughulikia.

1SAMWELI 23:25…[Basi Sauli na watu wake wakaenda kumtafuta. Watu wakamwambia Daudi; basi kwa hiyo akashuka mpaka mwambani, akakaa nyikani pa Maoni. Naye Sauli alipopata habari, alimwinda Daudi nyikani pa Maoni.]…. Kama wewe ungekutana na Daudi akikimbilia huko nyikani ungejiuliza maswali  ni kwa nini anakimbilia huko nyikani, asitulie? Bila shaka Daudi angekujibu kuwa kuna mwindaji anauyetaka uhai wake.  Ni baada tu ya Daudi kupakwa mafuta ya kuwa mfalme, ndipo Sauli akaanza kumwinda Daudi. Lengo la Sauli ni kuzuia mpango wa Mungu kwa Daudi. Hata kazini kwako,  kwenye ndoa, kwenye biashara n.k wapo watu wenye wivu wanaowinda hivyo ulivyo navyo. Katika vita, mtu hatari sana ni mwindaji,  kwani katika Biblia wanajulikana kama watu mashuhuri. Hawa hujifanya marafiki  lakini kumbe sivyo walivyo. Hata wewe ulivyo okoka tayari ulianza safari ya kuelekea kwenye ufalme wako. Shetani naye aliaanza papo hapo mipango yake ya kukuwinda, kwa kila unachokifanya. Usipomwangamiza mwindaji huwezi kufanikiwa. Elewa kuwa mwindaji ni makini, kwa sababu hataki agundulike kuwa anakuwinda na pia anajua kuwa mtego alioutega waweza pia kumnasa yeye mwenyewe. Ndiyo maana mwindaji huwa karibu na wewe ili aifahamu mipango yako.
Sisi kama kanisa lazima kwanza tushinde rohoni. Kumbuka mfalme yule (Balaki) ambaye aliwaona Waisraeli  wakija na akasema hawa watu  si rahisi kuwashinda mwilini,  lakini endapo  mtu wa kuwalaani atatokezea, basi kuwashinda itawezekana tu.  Mtu akikulaani rohoni unakuwa umelaaniwa kweli kweli. Ilimfanya Mungu amlazimishe punda aongee na Balaam kumwambia asithubutu kuwalaani wana wa Israeli, kwani angewalaani tu hiyo laana igetokea.
Maisha yako hayajaanza pale  ulipozaliwa.  Maisha yako  yalianza tokea ulipotungwa mimba. Hebu jiulize swali, wale mamajusi waliokuwa wakiifuatilia nyota ya Yesu wakitokea mashariki je, safari yao waliinza lini hadi wakafika Jerusalemu? Kumbuka nchi walizotoka ni mbali sana. Hili swali ni muhimu kwa sababu enzi hizo ndege wala meli za kutumia mafuta zilikuwa hazipo. Hii inamaana kuwa, safari yao waliianza hata kabla Mariamu hajajua kuwa atapata ujauzito  kwa njia ya Roho Mtakatifu.
Kinachonipa nifanikiwe siyo elimu  yangu, wala kusoma sana, bali ni  kwa sababu yumo anayekaa ndani yangu aliye msaada wangu. Huyu ni Yesu Kristo, ambaye alikuwa name wakati wa vita. Shujaa mimi bado nipo hai, ingawa walijitokeza wawindaji wengi toka kuzaliwa kwangu, lakini Yesu alinipigania na kuvunisha. Tena ninao uwezo wa  kumfuatilia Yule aliyetesa maisha yangu. Ewe adui uliyekaa katika maisha yangu, ukawa unayapindisha,leo nakufuatilia kwa Jina la Yesu. Sijazaa siyo kwa sababu sitaki kuzaaa, bali ni kwa sababu yupo aliyekaa kama mwindaji maishani mwangu. Sijasoma siyo kwa sababu sitaki kusoma, bali ni kwa sababu yupo aliyekaa kama mwindaji maishani mwangu. Kuna jinsi navyotaka kuvaa, lakini yupo aliyekaa kama mwindaji maishani mwangu.
Imeandikwa ‘Mimi  ni rungu la Bwana na silaha za Bwana  za vita”. Hii ni saa yangu kuanza kuwapiga wote waliokaa ili  kuniwinda. Mimi siyo kama wale uliowawinda. Vita vinaendelea,kwa sababu bado napumua,  na kupitia pumzi hii, nitaimaliza kazi aliyonipa ya kukomesha wawindaji wa maisha yangu. Namwambia Bwana kwa kuwa uliniweka hapa duniani kama silaha, basi niwezeshe nipambane na hao maadui waliojipanga kinyume na maisha yangu kwa Jina la Yesu.  Maisha yako hayawezi kuwa sawa kama Yule mwindaji hujamwondoa. Lazima usimame kinyume naye. Hapa nilipo siyo sawa na hatima ambayo Bwana alitaka niwe. Leo lazima mwindaji huyu aangamie kwa Jina la Yesu.

MIKA 7:2…[Mtu amchaye Mungu ametoweka, asionekane katika nchi, wala hapana mtu mwenye adili katika wanadamu; wote huotea ili kumwaga damu; kila mtu humwinda ndugu yake kwa wavu.]…. Kumbe wanaowinda wengine ili kuwaangamiza wanawawinda hata ndugu zao. Hata makanisani watu wa aina hii wapo.                                                                                                                
HOSEA 9:8…[Efraimu alikuwa mlinzi pamoja na Mungu wangu; na huyo nabii, mtego wa mwinda ndege u katika njia zake zote; katika nyumba ya Mungu wake umo uadui.]…. Bado  mpendwa au mchungaji waliopo nyumbani mwa Bwana wanawawinda watu. Wapo wachungaji na waazee wa makanisa waliojificha makanisani, wakiwa na ngozi za kondoo lakini ndani ni mbwa - mwitu. Ndiyo maana si vyema kujidaganya eti huyu mpendwa tunasali naye mchana. Hawa ni wale huenda kanisani siyo kwa miniajili ya kusali,  bali ni kwa ajili ya kujua afya yako inaendelea je, hasa baada ya kukupitia usiku wake ulipokuwa umelala. Ni sawa, mnakuwa wote kanisani mchana, lakini je, usiku unajua anachokifanya? Ndiyo maana tunasema wapo maadui hata makanisani.

Si ajabu kwa Tanzania kuwaona wachungaji wakiwasifia waganga wa kienyeji. Siyo ajabu kusikia kuwa kuna mchungaji ameenda kupata nguvu kwa waganga wa kienyeji. Si ajabu kuona vibao vya wagamga wa kienyeji ni vingi kuliko vibao vya makanisa.
HESBAU 23:22….[Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati.]… Huyu ndiye Mungu tunayemtumikia, nanguvu zake ni kama za nyati. Kama ulifikiri Mungu wangu ni yule anayekaa msalabani hapo umekosea. Kama ulidhani Mungu  wangu ni yule aliye mikononi mwa Mariamu ujue umekosea sana. Mungu wa maisha yangu aliyeniweka hai mpaka sasa anaongea na mimi sasa. Hii ni saa ya kuwafuatilia wale waliojikusanya kupambana na wewe kwa Jina la Yesu. mungu hakupanga niwe kama nilivyo. Nilazima nirudi kama ambavyoBwana alivyotaka niwe. Ewe adui uliyepambana nami katika ujana wangu sikubaliani  na wewe. Leo tunalifuatilia jeshi la mwindaji wanaowinda maisha yangu, na lazima apigwe kwa Jina la Yesu.
Vipo  vitu viwili tu: Aidha unaokoka au  unakufa kwa Jina la Yesu. Biblia inasema “na alaaniwe mtu yule asiyutumia upanga wake kumwaga damu”. Mimi ni nani nisiue kama nabii mkuu kama Eliya aliwakata vichwa manabii wa Baali 450 (mia nne hamsini)? Sitaki kujua mwindaji ni nani. Pale nitakapopata taarifa ya msiba, uwe wa kazini au biasharani kwangu, nitafahamu tu ni kuwa huyu ni yuleyule aliyekuwa anawinda maisha yangu. Wapo wawindaji wengine wanaowinda huduma zetu. Hawa hufanya juhudi ili watu wasifike kanisani au kusababisha mtu akose nauli ya kuja kanisani. Kama ni elimu, uliipindisha. Kama ni ndoa yangu, ni kweli uliiharibu. Cha muhimu siyo kile nilichopoteza, bali ni kinachofuata baada ya hapa.  Ni saa ya mimi kuongelea yule Mungu mkuu kuliko  miungu yote.

Kinachofuata sasa: Endapo hujaokoka, sirahisi kuwashinda wawindaji wa maisha yako.  Ni vyema leo kufanya maamuzi ya kuokoka ili uwe na uwezo wa kupokea nguvu kutoka kwa Yesu Kristo kupigana na wawindaji wa maisha yako.
 
WIKI HII NI MFUNGO RASMI WA KUMSHUGHULIKIA KILA ALIYEWINDA

MAISHA YETU. NI OPERESHENI “FUATILIA MWINDAJI”
UKIRI:
Kwa Jina la Yesu, mimi ni  rungu la Bwana,  na silaha  za Bwana za vita, leo ninataka kuwakomesha walioniwinda kwa Jina la Yesu. Bwana Yesu kwa kuwa mimi ni silaha nigeuze niwe moto ili niwateketeze walioniwinda kwa Jina la Yesu.
Amen

Comments