IPO SIKU MAMBO YAKO YOTE YA SIRI YATAKUWA PEUPE.



BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.

Karibu tujifunze Neno la MUNGU.

Siku ya mwisho mambo yote yatakuwa peupe.

  Mathayo 13:49-51 ''Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. YESU aliwauliza, Mmeyafahamu hayo yote? Wakamwambia, Naam.'' 
-Siku hiyo wauvu na uovu wao utakuwa dhahiri. Hukumu ya MUNGU sio kama hukumu za kibinadamu, hukumu ya MUNGU ni halisi maana kila kitu kitakuwa wazi siku hiyo.

-Mambo ya siri uliyoyafanya yote yatakuwa peupe.

-Wewe mama uliyekuwa unaisaliti ndoa yako kwa siri kubwa siku hiyo itajulikana hadhararni kwamba wewe ulikuwa msaliti.

-Wewe baba ambaye una nyumba ndogo siku hiyo itajulikana wazi dhambi yako hiyo.

-Kila aina ya dhambi aliyokuwa anaifanya mwanadamu siku hiyo itakuwa dhahiri.

Ayubu 8:3 '' Je! MUNGU hupotosha hukumu? Au, huyo Mwenyezi hupotosha yaliyo ya haki?''
-Hukumu ya MUNGU haina upendeleo. 
Kila mtu matendo yake ya ndio yatakayomfuata. Kila alichokipanda mtu hicho ndicho atavuna. Kama ulipanda moto hakika utavuna jehanamu na kama ulipanda uzima wa milele hakika utavuna uzima wa milele.
Kama ulimuona YESU wa kawaida kawaida tu wakati wa uhai wako hata hukutaka kumpokea na kuliishi neno lake, na wewe siku hiyo BWANA YESU atakuona wa kawaida kawaida kama hutampokea na kutubu ungali duniani.
Ukweli mmoja wa kufahamu ni huu ''Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA  wetu.-Warumi 6:23''

Ndugu zangu huu sio wakati wa kujifurahisha katika dhambi bali ni wakati wa kutubu na kuacha dhambi.
Huu sio wakati wa kushanglia dhambi bali ni wakati wa kumrudia BWANA YESU na kutubu kisha kuanza kuishi maisha matakatifu.

Mhuburi 12:14 '' Kwa maana MUNGU ataleta hukumuni kila kazi, pamoja na kila neno la siri, likiwa jema au likiwa baya. '' 
-Ndugu, hakuna kukwepa siku hiyo.
-Ni siku ya mambo yote peupe.

-Wewe mfanyakazi wa serikali unayeiba pesa siku hiyo wizi wako utajulikana.

-Wewe mchawi unayeroga watu kwa siri huku ukienda kanisani kama kujificha uovu wako huo watu wasijue siku hiyo dhambi yako hiyo itajulikana.

-Wewe unayetapeli watu siku hiyo mambo yako yote yatakuwa peupe.

-Wewe changudoa siku ya mwisho mambo yako yote yatakuwa peupe.

-Wewe ambaye huwa unafanya uovu kwa kumuogopa tu mchungaji, mchungaji akiwa karibu wewe ni mwema sana lakini mchungjai akiwa mbali unafanya dhambi, ndugu siku hiyo mambo yake yote yatakuwa peupe.

-Wewe uliye na utajiri wa kishetani siku hiyo ya mwisho itajulikana.

-Wewe unayetembea na hirizi siku hiyo mambo yako yote yatakuwa peupe na dhambi yako hiyo itakuwa dhahili.

Hakuna mwanadamu ambaye atasema ameonewa maana hukumu ya MUNGU iko wazi sana maana hata matendo yako mabaya yatazungumza.
Yohana 12:31 '' Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.''
-Shetani ndiye mkuu wa ulimwengu huu, anawadanganya wengi lakini siku hiyo hata yeye atatupwa katika ziwa la moto.
Kuna maelfu ya watu leo wanampokea shetani na mawakala wake na kuanza kumtumikia, ndugu., siku hiyo hata huyo shetani unayemuona ana nguvu leo siku hiyo atatupwa jehanamu.
Ndugu jiulize, kama umemtegemea shetani katika maisha yako, umepata utajiri wa kishetani, umepata umaarufu wa kishetani, umepata madaraka kwa nguvu za shetani. je siku hiyo utakuwa wapi?
Itakufaidi nini kujiburudisha katika uovu huo kwa miaka michache tu kisha ukaondoka na kwenda matesoni?
Warumi 2:16 ''  katika siku ile MUNGU atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa KRISTO YESU.''
-Hukumu ipo ni i karibu. Yaliyotabiriwa yote yameshatimia, tunao muda mchache ndugu zangu wa kutengeneza kesho yetu kama tutataka hiyi kesho iwe uzima wa milele na sio jehanamu.
Kila mmoja atasimama mbele za BWANA YESU na kuhukumiwa.
Wanaomkataa YESU leo siku hiyo watamuona wa thamani kuliko vyote.
Wanadamu waliokuwa na juhudi sana katika kufuata dini zao zilizokinyume na Wokovu wa BWANA YESU siku hiyo watajikuta wako nje, matendo yao mema hayatahesabiwa maana kumkataa YESU KRISTO ni kuukataa uzima wa milele.
Siku hiyo ni siku ya mambo peupe.
Kama ulikuwa unaabudu shetani huku ukidhani ni MUNGU baada ya kudanganywa na dini yako inayokataa Wokovu wa KRISTO siku hiyo utakuwa nje na uzima wa milele.
MUNGU analeta neno lake kama hili ili tu kukusaidia usiende jehanamu.
Dini yako wala haina uwezo wa kukupeleka uzima wa milele maana anayepeleka uzima wa milele ni BWANA YESU pekee. Na Biblia iko wazi kabisa kwamba '' kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka.-Warumi 10:13 ''
-Wakati wa kuliitia jina la BWANA YESU ni leo. kuokoka ni lazima kwa yule mwanadamu anayeutaka uzima wa milele. Kuukataa WOKOVU ni kuukataa uzima wa milele.
-Siku ya mambo peupe ni heri itukute katika kweli ya KRISTO.
 Maana Biblia iko wazi sana ikisema kwamba
''Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha KRISTO, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya-2 Kor 5:10''


KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.
''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments