JE NI SAWA KWA MUIMBAJI WA NYIMBO ZA INJILI KUMUIMBIA MWANASIASA ?

Na Mchungaji Gasper Madumla.


Bwana Yesu asifiwe…
Walaka huu wa wazi ni kwa watu wote haswa watumishi wa Mungu wenye kusimamia makanisa,na wale wenye kuhudumu mezani pa Bwana. Nimesukumwa kuandika haya pale nilipoona watu wengi wakizungumzia suala hili,hasa katika mitandao ya kijamii kama vile facebook. Walaka huu umetoka na swali linaloulizwa mara kwa mara sehemu tofauti tofauti. Swali hili limetokana na waimbaji wetu wa nyimbo za injili kuonekana katika majukwaa ya siasa wakihudumu kwa kuwaimbia wanasiasa.
Kila mtu mwamini katika Kristo Yesu amefanyika chombo cha kazi yake Bwana Mungu. Nasema watu wote waamini ni vyombo vya Bwana kwa utukufu wa jina lake Mungu. Mfano mitume,manabii,wainjilisti,wachungaji na walimu~hawa wote ni vyombo vitakatifu kwa ajili ya kuukamilisha mwili wa Kristo ( Waefeso 4:11-12 )
▪ Watumishi wote wa namna hii wamewekwa katika kazi moja tu,ambayo ni kuwakamilisha watakatifu kusudi kazi ya huduma itendeke.
~Ikiwa ndio hivyo basi,hakuna mtumishi wa Mungu yeyote anayepaswa kufanya kinyume na hapo. Sasa tuwaangalie kundi la wainjilisti ambalo ndilo sababisho kubwa la ujumbe huu kwa watu wote.
Wana injili ni wale wote wenye karama ya kupeperusha injili ya Kristo Yesu kwa watu wote. Kitu kinachopeperusha injili,au jambo la k-Mungu huitwa chombo. Hivyo yeye mwenye karama ya kupeleka injili kwa watu yeye ni chombo kiteule cha Mungu Baba mwenyewe. Chombo hiki kimeundwa kwa kazi moja tu,kazi ya injili kwa utukufu wa Mungu.
▪ Wana injili ni pamoja na waimbaji wa nyimbo za injili. Hivyo basi mwimbaji wa nyimbo za injili ni mwinjilisti sawa sawa na wainjilisti wengine kwa sababu kazi yao ni moja,kazi yao ni injili kwa watu wote.
Chombo cha sifa za Bwana kikitumika kinyume na hapo,basi ni dhahili kabisa kimeenda kinyume na neno la Bwana ( Waefeso 4:11-12 ). Kazi moja kubwa ya chombo cha sifa ni kumtukuza na kumsifu MUNGU peke yake. Maana hakuna anayestahili kusifiwa isipokuwa MUNGU pekee ( Zab.135:1-2).
Jambo la ajabu siku hizi:
Chombo cha sifa kinaonekana katika majukwaa ya kisiasa kikiimba sifa za mwanasiasa ambaye ni mwanadamu kama yeye,tena mwanasiasa ambaye ni muongo maana anachokieleza kwa wananchi hawezi kukutekeleza na wala hana mpango wa kukitekeleza. Chombo cha sifa kimetoka katika misingi yake ya kumtukuza MUNGU aliyekifanya na kumgeukia mwanadamu mdhambi kisha na kumfanyia ibada.
Sababu nyimbo ni sehemu ya ibada. Sikia; nyimbo zozote ni sehemu ya ibada fulani hata kama ni nyimbo za kidunia nazo ni sehemu ya ibada za kidunia. Nyimbo za Mungu nazo ni sehemu ya ibada ya Mungu,ndio maana popote uendapo penye madhabahu ni lazima nyimbo ziimbwe kwa sababu nazo ni sehemu ya ibada. Ukienda kwa mganga wa kienyeji  naye huimba ili kuikamilisha ibada yake na mizimu yake,alikadhalika kwetu sisi wapendwa huimba ili kuikamilisha ibada kwake MUNGU.
Sasa mwimbaji anapoimba sifa za mwanasiasa,naye hufanya ibada akimtukuza na kumuinua mwanasiasa huyo,na hapo mwimbaji huyo atakuwa anamuabudu mwanadamu wala si Mungu tena maana mwenye kusifiwa ni Bwana tu.
Chombo hiki cha sifa kimechukuliwa huko kanisani,kisha kikawekwa katika jukwaa ili kitumike katika matakwa ya kuwasifu wanasiasa na sio Mungu. Hapo MUNGU anakishangaa,kwamba mbona alikifanya kisimame na kupeperusha injili lakini kimesimama na kupeperusha habari za kibinadamu, tatizo ni nini? Au ni pesa? Au tamaa za kujulikana?
Kwani Yeye aliyekifanya chombo hiki Yeye ni mjinga? Hajui mahitaji ya chombo chake? Umeonaa!!
▪ Ikiwa chombo cha sifa,mwimbaji wa injili au mwinjilisti wa nyimbo akialikwa katika jukwaa la wanasiasa basi ni bora aende kisha akifika huko na kupewa muda,na aimbe nyimbo za injili maana ndivyo alivyo na ndivyo anavyojulikana. Wenye kushangaa washangae lakini ujumbe wa Yesu ufike kwa sababu kama walikuwa hawataki injili kwa nini wamemuita? Kama hawataki si waende kuwaita waimbaji wa kidunia,wapo huko tena wengi,wawaite wao. Lakini kama watamuita yeye chombo cha sifa ni lazima kiimbe sifa za Bwana tu.
Mimi ninashangaa sana kuona chombo cha sifa kinatumika katika matumizi mengine. Mfano mwimbaji wa injili analikwa katika jukwaa la siasa,kisha anakuja na kuimba nyimbo za sifa za mwanasiasa tena na ametunga kabisa wimbo kwa ajili ya mwanasiasa, huu ni upuuzi!!! Ni kumfanyia Bwana dhihaka.
Baada ya kuliangalia jambo hili naligundua mambo yafuatayo;
▪ Wapo wanamziki wa nyimbo za injili,pia  wapo wasanii wa nyimbo za injili. Waimbaji wa nyimbo za injili ni vile vyombo vyenye karama ya uinjilisti kwa njia ya uimbaji. Lakini wasanii wa nyimbo za injili ni wale wenye kuimba nyimbo za injili pasipo KARAMA ndani yao,hivyo uimba kwa kutafuta mkate,yaani pesa. Wasanii ni watu wabunifu hubadilika badilika kulingana na nyakati kulingana na pesa ipo wapi. Hivyo yeye asiyekuwa chombo cha sifa,anaweza kutumika kumtangaza mwanadamu na kumuacha Mungu kwa sababu yeye ni msanii.
WITO WANGU KWAKO KIONGOZI WA KANISA.
~ Usikubali kabisa vyombo vya Mungu ulivyopewa kwa dhamana kubwa vitumike nje katika matakwa ya mwanadamu awaye yote hata kama ni rais. Kama watawaihitaji (Vyombo vy Mungu) basi na viende kumsifu Mungu na si vinginevyo.
~ Ni afadhali sana chombo kikae sehemu moja katika matumizi sahihi kuliko kiangaishwe katika matuzi yasiyofaa. Maana kitachakaa na kukosa uthamani wake,na hatimaye kitatupwa huko na huko kutakuwako kilio na kusaga meno.
Ikumbukwe kuwa;
Siasa ni muhimu kuisikiliza,maana kupitia hiyo ndio tunaweza kumchagua mtu mmoja atakaye ongoza taifa letu kama raisi wa nchi. Lakini kisichotakiwa kufanyika ni chombo cha ibada kutumika kumsifu mwanasiasa kwa nyimbo na mapambio kana kwamba yeye ni Mungu.Bali chombo hiki kinapokuwa siasani kiendelee kutumika kueleza sifa za Bwana kwa hao wanasiasa na watu wote.
Sasa unisikilize sana wewe usomaye walaka huu;
~ Wanasiasa wengi kama si wote,wamejawa na uongo mkubwa sana. Wengi uhaidi mambo ambayo wao wenyewe hawawezi kuyatekeleza kabisa,na wanaahidi wakijua kwamba ni mambo ya uongo mtupu. Hivyo mtu yeyote asemaye uongo na hali akijua alitendalo,mtu wa namna hii ni machukizo mbele za Bwana. Sasa,mwimbaji wa injili naye akijua ya kwamba huyu ninaye muimbia ni muongo na yote haya ni machukizo huku akiendelea kumuinua mwanasiasa kwa nyimbo na kumtukuza,mwimbaji huyu pia amekuwa ni machukizo mbele za Bwana Mungu.
Ni afadhali angeliimbia jina la Bwana Mungu kwa muongo huyo ili yamkini atubiye uongo wake kisha aokoke aje kwa Bwana na usiasa wake. Kuliko kumsapoti uongo nawe ukafanyika muongo,sasa ikiwa wote ni wa dhambi thamani ya wokovu ya huyu mwimbaji ipo wapi? Atawezaje kumrejesha huyu asemaye uongo ? maana wapo pamoja!!!
▪ Ifike wakati sasa,tusikubali tukatumia karama zetu kumtukuza mwanadamu bali Mungu. Sisemi kwamba usiende siasani,nenda lakini kamtukuze Mungu huko huko siasani ili kuwepo na tofauti kati yako wewe uliyeokoka na yule asiyeokoka.
UBARIKIWE.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,usisite kunipigia kwa namba yangu hii 0655111149.
Mch.Gasper Madumla.
Beroya bible fellowship church ( Kimara,Dar Tanzania )
UBARIKIWE.

Comments