JITENGE NA WALIOJIINGIZA KWA SIRI ILI KUIBADILI INJILI YA KRISTO.





BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la kutusaidia kutambua na kuchukua maamuzi mazuri.

Yuda 1:4 ‘’ Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya MUNGU wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na BWANA wetu YESU KRISTO. ‘’

-Mara nyingi shetani hutaka kuweka la kwake katika kila jambo jema. Japokuwa vitu orginal vipo lakini shetani  hupenda kuweka vitu feki mahali pa vitu orginal ili wanadamu wakikaa vibaya wanaweza kujikuta hata vitu orginal hawatavijua tena kama ni orginal na watajikuta wakidhani kwamba vile orginal ndio feki na vile feki ndio orginal.
-Shetani ni wa vitu feki tu.
Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU ambao pekee unapatikana katika KRISTO YESU. Injili ya KRISTO ni  gari ya kuwabeba watu tayari wa kuwapeleka uzima wa milele. Lakini shetani ana injili yake feki ambayo lengo lake ni kuwapotosha wanadamu na hadi kuna wanadamu hudhani kwamba injili feki ndio mpango wa MUNGU wakati si kweli. Biblia iko wazi kabisa kwamba  kuna watu  wanaotumika vibaya, hawa wako upande wa shetani hata kama wataitwa wahubiri, ni mawakala wa shetani maana wana mikataba na shetani,  ni makafiri waibadilio kweli ya MUNGU kuwa ufisadi.

Wagalatia 2:4-5 ‘’ Bali kwa ajili ya ndugu za uongo walioingizwa kwa siri; ambao waliingia kwa siri ili kuupeleleza uhuru wetu tulio nao katika KRISTO YESU, ili watutie utumwani;  ambao hata saa moja hatukujitia chini yao, ili kwamba kweli ya Injili ikae pamoja nanyi. ‘’

-Kwa sababu ya kuingia kwao kwa siri katika injili wamepelekea baadhi ya  watu kutokuwatambua. Wameweka baadhi ya miongozo yao na kuwalazimisha wanadamu  waifuate hiyo badala ya kufuata Biblia takatifu. Wabaya hawa wamewahamisha watu kutoka kuitegemea Biblia  na sasa wanategemea tu sheria za kanisa.

Warumi 15:18 ‘’ Maana sitathubutu kutaja neno asilolitenda KRISTO kwa kazi yangu, Mataifa wapate kutii, kwa neno au kwa tendo,  ‘’

Kazi ya watu hawawaongo  kulingana na Yuda 1:4 ni;

       1.   WANAIBADILI NEEMA YA MUNGU KUWA UFISADI.

-Wanaondoa watu kwenye kusudi la MUNGU la uzima wa milele.
-Hawaihubiri injili ya kweli.
-Wanaunganisha ukweli na uongo pamoja na kuwakosesha maelfu ya waumini.
-Wanahubiri kwa kulaghai ili wapate pesa.
-Wanahalalisha yaliyo machukizo kwa MUNGU.

=Baadhi ya waongo hawa waliojiingiza kwa siri katika injili ni hawa;

  a.  Wanaruhusu ushoga na kufungisha ndoa hizo za mashoga katika makanisa yao.
  b.   Wanaabudu sanamu badala ya Kumwabudu MUNGU wa mbinguni.
 c.   Wanadanganya watu kwa kufundisha kwamba hakuna jehanamu.
 d.  Wanafundisha watu kwamba pombe ni halali tu.
 e. Wanamkataa ROHO MTAKATIFU wala hawamhitaji katika makanisa au huduma zao.
 f. Wanakataa wokovu na wanakataza watu kuokoka.
 g.  Wanaibadili Biblia kwa lengo la kunufaisha uongo wao walioingia mkataba na shetani.
 h. Wanairekebisha Biblia ili Biblia iwafuate wao badala ya wao kuifuata Biblia.

2 Petro 2:1-3 ‘’ Lakini kuliondokea manabii wa uongo katika wale watu, kama vile kwenu kutakavyokuwako waalimu wa uongo, watakaoingiza kwa werevu uzushi wa kupoteza, wakimkana hata BWANA aliyewanunua, wakijiletea uharibifu usiokawia. Na wengi watafuata ufisadi wao; na kwa hao njia ya kweli itatukanwa. Na katika kutamani watajipatia faida kwenu kwa maneno yaliyotungwa; ambao hukumu yao tangu zamani haikawii, wala uvunjifu wao hausinzii.   ‘’

    2.  HUMKANA MUNGU BABA NA BWANA YESU.

-Wanamkataa YESU KRISTO japokuwa wanaitwa wakristo maana wameingia mkataba na shetani ili kupeleka watu jehanamu.
-Wanamkata MUNGU kwa sababu ya kufundisha kwao uongo.
-Hawahubiri toba bali mambo ya dunia tu.
-Wanamkana MUNGU kwa sababu wanaipenda dunia na anasa zake kuliko kumpenda BWANA MUNGU.
-Wanamkana JEHOVAH MUNGU wa kweli kwa wao kuvaa mavazi ya kikahaba na kufuata elements za majini.
-Wanamkana MUNGU kwa wao kukataa kuwa chini yake MUNGU muumbaji wao.
-Wanamkana MUNGU kwa wao kujipa vyeo vya KRISTO jambo ambalo ni baya sana maana kuna wengine hata hudai kwamba wao ndio Kristo wa pili waliotumwa na MUNGU kukamilisha kazi ya ukombozi maana BWANA YESU KRISTO alishindwa kuimaliza kumbe ni uongo tu wa shetani ili kuhakikisha wanadamu hawafiki uzima wa milele.
-Wanamkana MUNGU BABA kwa wao kuabudu wafu.
-Wanamkana BWANA mbele za ulimwengu.
-Wanamkana BWANA YESU kwa wao kukataa kazi yake.
-Wanamkana MUNGU kwa wao kusema wametumwa na yeye kumbe ni uongo wao tu wa kutaka kupeleka wanadamu jehanamu.
-Husema kwamba MUNGU ni wa huruma sana hivyo hawezi kuwaangamiza wanadamu. Ndugu zangu, hatuwezi kumzidi MUNGU huruma ambaye ndiye aliyeleta ukombozi wetu kupitia YESU KRISTO, Haitakuwepo huruma kwa mwanadamu atakayemkataa YESU na bila kutubu hadi kifo chake maana ndivyo maandiko yasemavyo. MUNGU ana huruma sana lakini sodoma na gomora waliangamia wote maana walikataa maonyo ya MUNGU, Wakati wa Nuhu MUNGU aliangamiza ulimwengu wote kwa sababu ya wanadamu kujitenga na MUNGU muumba wao. Na hata sasa mwisho ukifika ataangamiza waasi wote maana wameikataa kweli yake ambayo ni KRISTO.
-Wanamkana MUNGU kwa wao kuwabebesha wanadamu mizigo mizito ambayo mizigo hiyo wala haitokani na MUNGU wala Neno lake.

1 Yohana 2:22-23 ‘’ Ni nani aliye mwongo ila yeye akanaye ya kuwa YESU ni KRISTO? Huyo ndiye mpinga Kristo, yeye amkanaye BABA na MWANA.  Kila amkanaye MWANA, hanaye BABA; amkiriye MWANA anaye BABA pia.   ‘’

Ndugu yangu, jitenge na hao haijalilishi wapo tangu miaka 1800 iliyopita, jitenge na waongo hao haijalishi wapo tangu miaka 200 iliyopita.
-Ukiona injili yeyote inamkataa BWANA YESU kama Mwokozi pekee wa wanadamu wote tambua kwamba injili hiyo haikutoka kwa MUNGU mbinguni.
-Ukiona kanisa au dhehebu wanaoukataa uungu wa BWANA YESU hao jitenge nao.
-Ukiona dhehebu au kanisa ambalo mwanzilishi wake wanampa heshima ya KRISTO hao jitenge nao.
-Ukiona kanisa wanaabudu wafu hao tambua kabisa wanahitaji kusaidiwa wao, jitenge nao.
-Ukiona kanisa wana Biblia yao peke yao hao wakimbie tena ni matapeli maana wameirekebisha Biblia ili Biblia iwafuate wao  badala ya wao kuifuata Biblia. Kuna waongo hata Biblia kwao hawaiti Biblia bali wanaita ‘’kitabu cha Bwana’’ kumbe huyo Bwana anayeitwa kwamba kitabu cha Bwana ndiye mwanzilishi wa dhehebu hilo na si BWANA yaani MUNGU.
-Kuna madhehebu hawataki kusikia uungu wa YESU japokuwa ukweli ni kwamba  kuna maandiko mengi sana ambayo yanamtambua YESU kama ni MUNGU lakini wao wameyabadili maandiko hayo katika Biblia zao. Mfano kuna makanisa andiko la Yohana 1:1  ambalo linamtaja BWANA YESU kama MUNGU mkuu, wao badala ya kuaandika ‘’Mungu’’ Kama ilivyo katika Biblia zote wao kwenye Biblia yao wameandika ‘’mungu’’ ambayo kibiblia mungu maana yake ni shetani. Inawasumbua kuandika kwamba YESU KRISTO ni MUNGU na wao wanaandika katika Biblia yao hiyo ya kipekeyao kwamba YESU ni mungu, hii ni matokeo ya mwanzilishi wa dhehebu hilo kuwa wakala wa shetani. Hao ni wa kuwakimbia.  Katika Biblia takatifu ukiona Neno ‘’mungu’’ ya kuanza na herufi ya kwanza ndogo hiyo inamaanisha shetani mfano

2 Kor 4:3-4 ‘’ Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;  ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. ‘’
-Kupitia andiko hilo tunamuona kwamba shetani ni mungu ikianza na herufi ndogo lakini pia andiko hilo hilo linamtaja MUNGU BABA wa mbinguni, hivyo hawa kitendo chao cha Yohana 1:1 kuibadili ni taarifa tu kwako kwamba wao ni mawakala wa shetani.

Ukiwauliza kwanini YESU kwenye andiko hilo wamemwita mungu badala ya Mungu wanakosa jibu. Hawa ni wapinga KRISTO waliojipenyeza kanisani na kupotosha maelfu ya watu ndio maana hadi Biblia wameibadili.
BWANA YESU mwenyewe anawataja waongo hawa.

Mathayo 24:11 ‘’ Na manabii wengi wa uongo watatokea, na kudanganya wengi. ‘’

Ndugu yangu, usijitenge na uzima wa milele kwa kushika na kufuata mafundisho yaliyo kinyume na Biblia ya kweli.
-Ndugu achana na mafundisho ya mashetani ya wapinga Kristo.
-Ndugu yangu achana na mafundisho yanayotokana na roho zidanganyazo.

1 Timotheo 4:1-2 ‘’ Basi ROHO anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani;  kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe;   ‘’

-Waongo hawa hufundisha kwamba dhehebu lao tu ndio watakaoingia uzima wa milele maana yake ukiwa nje ya dhehebu hilo huendi uzima wa milele kitu ambacho ni uongo mkubwa. Watu hawaingii mbinguni kwa tiketi ya dhehebu bali wokovu uliotimia katika utakatifu.
Ndugu yangu injili ya kweli ipo na inahubiriwa, ifuate hiyo katika makanisa ya kweli ya kiroho.
-injili ya kweli humhubiri KRISTO anayeokoa.

Kumb 13:4 ‘’  Tembeeni kwa kumfuata BWANA, MUNGU wenu; mcheni na kushika maagizo yake na kuisikia sauti yake, nanyi mtumikieni na kushikamana naye. ‘’

-Ndugu naomba uutendee kazi ujumbe huu.
Namshukuru ROHO MTAKATIFU kwa kunipa ujumbe huu leo kwa ajili ya ndugu zangu wote watakaosoma na kuutendea kazi.

Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine.na kama hujampokea BWANA YESU muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
0714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili. MUNGU Akubariki.

N.B. (Kwa wale wanaobadilisha masomo yangu sehemu za mwisho na kujiandika wao na kuweka namba zao za simu na kuomba pesa za kukuza huduma zao kupitia ujumbe wangu,hiyo ni mbaya. share somo, weka katika blog yako ila usibadilishe chochote na pia fundisha watu kupitia ujumbe huu, print na usambaze kokote kwa njia yeyote maana hapo utakuwa unahubiri injili. mmepewa bure toeni bure. binafsi sijawahi kuandika masomo ili nipate pesa hata kama nina uhitaji wa pesa. ubarikiwe)

Comments