KAMA MLIVYOMPOKEA YESU, ENENDENI HIVYO HIVYO KATIKA YEYE.




BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze neno la MUNGU.
Leo nasema hivi; Kama Mlivyompokea YESU, Enendeni Hivyo Hivyo Katika Yeye

Wakolosai 2:6-10 '' Basi kama mlivyompokea KRISTO YESU, BWANA, enendeni vivyo hivyo katika yeye; wenye shina na wenye kujengwa katika yeye; mmefanywa imara kwa imani, kama mlivyofundishwa; mkizidi kutoa shukrani.  Angalieni mtu asiwafanye mateka kwa elimu yake ya bure na madanganyo matupu, kwa jinsi ya mapokeo ya wanadamu, kwa jinsi ya mafundisho ya awali ya ulimwengu, wala si kwa jinsi ya KRISTO. Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa MUNGU, kwa jinsi ya kimwili. Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka. ''.

-Kumbe kama ulivyompokea BWANA YESU unatakiwa uenende hivyo hivyo katika yeye maana yake hutakiwi kumwacha wala hutakiwi kuliacha fundisho lake maana ukifanya hivyo utaangukia kwenye mapokeo ya wanadamu na kuliacha neno la MUNGU.

 -Kuna wakristo leo kwa sababu hawana shina katika KRISTO hufanywa mateka na baadhi ya watu kwa mafunshisho ya uongo.
-Katika KRISTO ndipo ukamalilifu wote wa MUNGU kwa jinsi ya mwili unakaa. Kama hutadumu au hutakaa katika KRISTO YESU kama ulivyompokea unaweza kukutana na hatari ya kurudi nyuma baada ya kupotoshwa na wapinga wokovu. 
siku zote shetani anatamani kukurudisha duniani ili uendelee kumtumikia yeye. 
ndugu kama umepata neema ya kuokolewa na BWANA YESU nakuomba shikilia wokovu wako ulio wa dhamani sana.

 Warumi 6:23 '' Kwa maana mshahara wa dhambi ni mauti; bali karama ya MUNGU ni uzima wa milele katika KRISTO YESU BWANA wetu.'' 

- Ndugu Yangu, Ni Nani Anabadilisha Maamuzi Yako Hata Unataka Kumwacha YESU?. 
-Ni Nani Anakuambia Usiendelee Na Wokovu? 
-Ni Nani Anakushauri Kumwacha YESU?.
-Ni Nani Anakushauri Vibaya Hata Unataka Kuliacha Tumaini La Uzima Wa Milele?.
 Biblia Inakuambia Neno Muhimu Sana Kwamba Kama Ulivyompokea YESU Endelea Hivyo Hivyo Katika Yeye. 

 Yoshua 23:7-8 ''  Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao; bali shikamaneni na BWANA, MUNGU wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo. ''

-Ndugu, kama kuna mtu atataka kukuondoa kwa YESU na wewe ukakubali basi tambua kwamba huyo anakupeleka motoni.
-Hao Wanaokushauri Vibaya Kuhusu YESU Hakuna Hata Mmoja Anayeweza Kukupa Uzima, Hakuna Hata Mmoja Anayejua Kesho Yako, Lakini KRISTO Anajua Ndio Maana Neno Lake Ninakushauri Kwamba Usije Ukamwacha Maana Hakuna Uzima Wa Milele Kwingine Nje Na KRISTO. 

Yoshua 24:14 '' Basi sasa mcheni BWANA, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye BWANA.''

-Kila mtu kabla hajampokea YESU kuna vitu vibaya alikuwa anajihusisha navyo, vitu hivyo ni dhambi. inawezekana kabisa ulikuwa unateswa na dhambi hata dhambi hiyo ikawa kama miungu kwako. lakini sasa umempokea BWANA wa utukufu YESU KRISTO maana yake umeingia katika kundi la  waenda uzima wa milele. 

Yohana 3:36 '' Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya MUNGU inamkalia.'' 

MUNGU wa kweli ni mmoja tu na anapatikana katika KRISTO YESU pekee. ukiondoka kwa YESU maana yake unaliondoa jina lako mwenyewe kwenye kitabu cha uzima. ndugu yangu, kama ulivyompokea BWANA YESU enenda hivyo hivyo katika yeye.
Enende katika KRISTO bila kugeuka geuka wala  kurudi nyuma.  Dunia na mambo yake yote yatapita, anasa zote zitapita lakini BWANA atadumu milele na uzima wa BWANA utadumu milele.

2 Kor 5:17 '' Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya KRISTO amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.''

-Ndugu Endelea Hivyo Hivyo Kama Ulivyompokea YESU. Usimwache YESU ndugu Yangu Hata Jina Lako Likaondolewa Kwenye Kitabu Cha Uzima. 
-Ndugu Usilegee Wala Usiangalie Pembeni, Bali Mwangalie KRISTO Aliyekuokoa. 
-Wanadamu Ni Akina Nani Hata Wakuamulie Maisha Yako?
- Ndugu Mfuate Na Mwangalie YESU KRISTO Tu Aliyekuokoa. BWANA YESU Yuaja Ili Kumlipa Kila Mtu Kama Kazi Yake Ilivyo.
BWANA YESU anasema
 '' Tazama, naja upesi, na ujira wangu u pamoja nami, kumlipa kila mtu kama kazi yake ilivyo. Mimi ni Alfa na Omega, mwanzo na mwisho, wa kwanza na wa mwisho.-Ufunuo 22:12-13''

 -Ndugu Uliyempokea YESU KRISTO Kama BWANA Na Mwokozi Wako Ni Lazima Uendelee Kukua Kiroho. Ni Lazima Ufikie Mahali Ujiamini Na Kujiongoza Chini Ya Neno La MUNGU Maana Upo Upande Wenye Nguvu. 
-Upande Wa YESU Ndio Upande Wenye Nguvu Maana Ndio Upande Wa Uzima Wa Milele. 
-Ndugu Usikubali Kuongozwa Na Tamaa Tena Usikubali Kuongozwa Na Wanadamu Bali Ongozwa Na Neno La MUNGU.
BWANA anasema
 '' Mbingu na nchi zitapita; lakini maneno yangu hayatapita kamwe.-Mathayo 24:35'' 

 Ndugu, Kama kweli uko katika wokovu wa BWANA YESU hakika wewe  ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. Kama siku zilizopita  ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments