KIBALI


Na Mchungaji Bryson Lema
Utangulizi: Ili mtu akusaidie au  uweze kuongea nae  lazima upate kibali machoni pake. Imeandikwa katika MWANZO 39:21…[ Lakini Bwana akawa pamoja na Yusufu, akamfadhili, akampa kibali machoni pa mkuu wa gereza.]…. Umuhimu wa kibali upo palepale.  Ili maisha yangu yakae vizuri na sawa, lazima nipate kibali mahali fulani. Hata kama ninafanya biashara mahali fulani, kama watu  hawapati kibali cha kuja kwenye biashara yangu,  hakuna nitakachoweza kukifanya kikafanikiwa. Kwanza jiulize, Umepata kibali wapi  ili ufanye nini? Umepata kibali wapi ili ufanye biashara wapi? Shetani anao uwezo wa kuibadilisha sura yako ya nje kiasi kwamba mtu wa pembeni akikuangalia anakuona ukiwa mtu wa ajabu ajabu tu. Wewe binafsi huwezi kushtukia hilo, ila mtu mwingine anachokiona ndani ya ufahamu wake anakuona tofauti. Mathalani, endapo unajiona uko safi, lakini mwenzako anakuona u mchafu, hata kama ungejitetea vipi haitasaidia,  kwa sababu mtazamo wa ndani ya ufahamu wake mtu huyo ni tofauti na wewe. Waswahili husema ‘Uzuri wa mtu upo kwenye macho ya watu wengine siyo  wewe binafsi’. Vivyo hivyo Uzuri wa bidhaa upo kwenye macho ya mnunuaji wala siyo muuzaji.

Adui  anaweza kuibadilisha sura yako au hata usemi wako.  Maana yake, unapoongea tu inaweza kutafsiriwa tofauti na yule anayesikia usemi wako. Shetani anafahamu kuwa umeokoka, na hivyo hawezi kukugussa wewe  lakini badala yake atamvuruga mtu  yule unayetaka kukutana naye ili akunganishe na hatima yako. Kumbuka ujenzi wa mnara wa Babeli jinsi ambavyo Mungu mwenyewe alikiri kuwa kwa namna ile ya kusikilizana kwa wanadamu,  asingekuwepo wa kuwazuia mpango wa hawa wanadamu walivyokuwa katika umoja na sauti moja. Ilimpasa Mungu achafue usemi wa hawa wanadamu ili kwamba kila anachokiongea kila  mmoja wao kieleweke tofauti na mwenzake. Ndicho anachokifanya shetani hata sasa katika maisha ya wanadamu. Pengine ni neno dogo tu linazungumzwa kataka maisha yenu ya ndoa lakini kwa neno hilo ndoa inavunjika. Hii ni kwa sababu shetani anachezea usemi wao ili kupoteza kile kibali cha ndoa,  kwa kuwachafulia semi zao ndani ya ndoa.

Unapoona kazini kwako unafukuzwa ujue ni  kibali chako kimechezewa. Unapoona kwenye ndoa yako mambo hayaendi vizuri ujue ni  kibali kimechezewa. Unapoona kazini watu wanakusema sema ovyo au kudharauliwa unapoongea jambo lolote ofisini mwako ujue ni kibali kimechezewa. Ni lazima leo tuvifuate vibali vyetu kule viliposhikiliwa na adui zetu kwa Jina la Yesu.  Lazima kila nikiongea watu waseme huyu ni Bwana. Kama wazo langu halishindi maana yake hata mimi mwenyewe nimeshindwa. Ili kazini  kwangu niweze kusifiwa kwa kile ninanachokifanya lazima nipate kibali. Ukiona mtu asiye na kibali ujue kwa lugha nyepesi huyo  mtu amelaaniwa. Biblia inasema “kibali cha mtu  humketisha na wakuu”. Shetani ana uwezo wa kuchezea kibali cha mtu na kukishikilia mahali, na kila atakachokifanya mtu wa aina hii kinakuwa kigumu na kisichompendeza mtu  yeyote. Kibali kinapokamatwa ujue maisha nayo yanakuwa yamekamatwa.

KUTOKA 33:12…[Musa akamwambia Bwana, Angalia, wewe waniambia, Wachukue watu hawa; nawe hukunijulisha ni nani utakayemtuma pamoja nami. Walakini umesema, Nakujua jina lako, nawe umepata neema mbele zangu.]…. Musa alianza kujiuliza maswali kujua ni kwa mamlaka gani atawapeleka Israeli Kanaani. Ni rahisi sana  kusema neno “neema” bila kujua maana yake. Katika Agano Jipya,  Paulo anasema aliwekewa  miiba na adui, na baada ya kuomba mara nyingi iondoke, Bwana akamwambia “Neema yangu yakutosha”. Katika MWANZO 6:8 imeandikwa…[Lakini Nuhu akapata neema machoni pa Bwana.].... Kilichomuokoa Nuhu asiangamie na ile gharika ni neema (yaani Upendeleo wa Kimungu).  Neema ya Mungu ndiyo kibali.  Ni kwa sababu kupitia neema hii unapata kibali kisichobishaniwa. Ndiyo maana hata katika Nyaraka za Paulo katika Agano Jipya, Paulo anamalizia hizi nyaraka kwa kusema ‘Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae nanyi”, akijua kuwa Neema ya Yesu Kristo ndiyo kibali.

YOHANA 1:14…[Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli.]… Yesu Kristo alitupa neema isiyobishaniwa. Leo ni siku ya kulivaa vazi  la neema, ili  kila nitakapokaa, nipate kibali machoni pa wengine. Ipo neema ya kuingia popote unapotaka kuingia. Haijalishi umefanyiwa uchawi wa aina gani, ninachokijua lipo vazi la neema ya Yesu Kristo nitakapolivaa hayupo wa kunipinga wala kunizuia. Vazi hili alilivaa Musa nyakati zile  kiasi kwamba watu wakamwita yeye ni Mungu katikati ya wanadamu. Kilichompa Musa kibali ni  ile neema.

 KUTOKA 33:13-16…[Basi, sasa nakuomba, ikiwa nimepata neema mbele zako, unionyeshe njia zako, nipate kukujua, ili nipate neema mbele zako; ukakumbuke ya kuwa taifa hilo ndilo watu wako. 14 Akasema, Uso wangu utakwenda pamoja nawe, nami nitakupa raha. 15 Naye akamwambia, Uso wako usipokwenda pamoja nami, usituchukue kutoka hapa. 16 Kwa maana itajulikanaje kuwa nimepata neema mbele zako, mimi na watu wako? Siyo kwa sababu unakwenda pamoja nasi, hata mimi na watu wako tutengwe na watu wote walio juu ya uso wa nchi?]… Kama alivyosema Musa,  hata sisi inabidi tuseme hivyo hivyo. Inakuwaje leo maombi yangu hayapati  kibali machoni pa Bwana? Kuna vazi (la rohoni) ambalo ukilivaa, afya yako  inakuwa tofauti. Kila ulivaapo vazi hilo, milango  yote iliyokuwa haifunguki itafunguka kwa ajili yako. Tunaihitaji neema ya Mungu ili kanisa liinuke. Tunahitaji neema ya Mungu  ili kuiharibu  misingi ya shetani katika taifa hili. Ni  saa ya Bwana kunivalisha vazi la neema ili nikipita popote, milango ikafunguke yenyewe, siyo kwa sababu ya elimu yangu bali ni  kwa sababu ya neema ya wokovu ndani mwangu. Hilo vazi la aibu ulilo nalo, vazi la kuitwa “msengenyaji”,  au “asiyeolewa” n.k. leo ulivue kwa Jina la Yesu.  Ukilivaa hilo vazi la utukufu hata waliokudharau watakushangaa. Soma habari za Esta, kilichomfanya  apate kibali kwa mfalme siyo sura yake,  bali ni kwa sababu alikuwa na vazi la neema ya Bwana.
Musa alimwambia Mungu siwezi kuongea vizuri, lakini tazama mtu huyo huyo ndiye ambaye Mungu alimtuma aende kwa Farao, ni kwa sababu kinachomfanya Musa aongee siyo elimu yake wala akili au  nguvu zake, bali  kwa sababu anayo neema itokayo kwa Baba wa Mbinguni.
ZABURI 68:7-10…[Mungu huwakalisha wapweke nyumbani; Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa; Bali wakaidi hukaa katika nchi kavu.7 Ee Mungu, ulipotoka mbele ya watu wako, Ulipopita nyikani, 8 Nchi ilitetemeka Naam, mbingu zilidondoka usoni pa Mungu; Hata Sinai usoni pa Mungu; Mungu wa Israeli. 9 Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema; Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu. 10 Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.]… Daudi anaonesha kuwa wana wa Israeli na safari yao kutoka Misri hadi Kanaani, haikuwa kwa sababu wanajua sana kutembea, bali ni kwa sababu  ya neema tu. Mungu  ndiye aliwavisha Adamu na Eva mavazi yaliyotokana na ngozi ya mnyama. Wao wenyewe walijisitiri kwa majani, wakasahau kuwa baada ya muda,  jua litayanyausha hayo  majani nao watarudia kuwa uchi tena‼!
Katika Biblia, Stefano  aliwashinda maadui  zake kwa neno, alipoweza kuisoma (kwa ufupi) Biblia yote kuanzia Mwanzo hadi Ufunuo ndani ya ukurasa mmoja. Hajawahi kuwepo mtu aliyemtumaini Bwana katika Biblia yote ‘Mwanzo hadi Ufunnuo’ mtu huyo akakosa neema. Kinachowapa watu mafanikio siyo elimu  zao bali ni neema. Usikate tamaa wewe ambaye watu wanakusema vibaya, bali waambie baada ya muda mfupi tu watasema ‘hakika wewe ni Mwana wa Mungu’. Hata askari yulee aliyemchoma Yesu mkuki, mwishowe ilimpasa kukiri ya kuwa ‘hakika huyu alikuwa  mwana wa Mungu
Imeandikwa KUTOKA 33:17 … [Bwana akamwambia Musa, Nitafanya na neno hili ulilolinena, kwa maana umepata neema mbele zangu, nami nakujua jina lako. ]…. Mungu anatujua kwa majina yetu.  Je,  uliwahi kumuona mfalme bila vazi la kifalme? Hata wewe, saa yako imefika ya kuvalishwa vazi la kuheshimika, Vazi la Baraka. Ninachokijua mimi ni kuwa ninalo vazi la kunitoa  katika maisha ya shida, na ya kuonewa,  nay a kuvuta bangi na kuingia katika maisha mapya katika Jina la Yesu Kristo wa Nazareti.
Kama mtu hujaokoka huwezi kulivaa hili vazi la neema ya Bwana. Kuokoka kwa kumpokea Yesu Krsito maishani mwako kuwa Bwana na Mwokozi  wako ni hatua ya kwanza ili kuweza kupokea kibali cha Bwana na kuwashinda adui zako wote.

UKIRI
Ewe vazi la kushindwa, leo ninakukataa kwa Jina la Yesu.  Ninakataa vazi la kichawi,  vazi walilonipa wazazi, vazi litokalo kuzimu nalikataa kwa Damu ya Mwanakondoo. Vazi la kunifanya nionewe,  mavazi ya urithi na ya uganga wa kienyeji nayakataa kwa Jina la Yesu. Leo nayakataa mavazi niliyovishwa ili niwe malkia wa kuzimu, nakataa mavazi yenu kwa Damu ya  Mwanakondoo. Nakataa vazi  la umaskini, vazi  la magonjwa nililovishwa kwa Jina la Yesu.  Vazi la bibi nalipiga. Nazivua nguo  za rohoni walizonivisha wachawi nyakati za usiku, nayakataa mavazi yao yote kwa Jina la Yesu. Ninakataa mavazi ya wafu. Nalivua vazi lenu. Vazi la kukataliwa nalivua kwa Jina la Yesu. Vazi la ukoo la kushindwa nalivua kwa Damu ya  Mwanakondoo. Achia maisha yangu ewe vazi  la kuzimu kwa Jina la Yesu.
 
Nalikataaa vazi lolote nililovishwa kwenye msiba nililopewa wakati wa msiba. Leo nalikataa kwa Jina la Yesu.kila vazi linalohusiana na wafu,  leo  nalivua kwa Jina la Yesu.  
 
Nalivaa vazi la neema ya Bwana,  nalivaa vazi la hashima, vazi la upendeleo, vazi la kuonekana, vazi la kupata kazi, vazi la utajiri, vazi la kusifiwa na kuinuliwa katika Jina la Yesu. Amen
 

Comments