KWANINI TUNAJARIBIWA


Mch.Abiud Misholi akifundisha neno la Mungu madhabahuni EAGT City Center.

Isaya 40:3-5.
‘Sikiliza, ni sauti ya mtu aliaye, Itengezeni nyikani njia kuu kwa Mungu wetu . Kila bonde litainuliwa na kila mlima na kilima kitashushwa , palipopotoka patakuwa pamenyoka, na palipoparuza patasawazishwa na utukufu wa  BWANA  utafunuliwa na wote wenye mwili watauona pamoja kwa kuwa kinywa cha BWANA kimenena haya’.

1.TUNAJARIBIWA KWASABABU YA KIBURI
Dhambi zote mama yake ni kiburi ambapo kiburi hicho chaweza kuwa ni kiburi cha elimu, pesa, mali au majivuno tu. Watu wengi hushindwa kufika makanisani wakisingizia kuwa wana majaribu ambayo yanawasumbua katika maisha yao na husahau kuwa Mungu anawataka watu ili awashushe mizigo yao.
Alitolea mfano kuwa watu wengine hufikiri kulemewa na baadhi ya dhambi kama uzinzi ni kuwa na mizigo  kumbe ni kuendekeza tamaa za mwili.
Nje ya dhambi wengine hajidanganya kuwa hawamuhitaji Mungu na hii hutokana na kuwa na mahitaji yao yote ya kimwili kwa  wakati huo au kuwa na mali nyingi pasipo matatizo. Kumbe wanajidanganya kwani Mungu huweza kuondosha mali hizo kwa dakika chache tu wakabaki hawana kitu hivyo ni nzuri kuacha kiburi na kumuheshimu Mungu katika kila hali.

2. TUNAJARIBIWA KWASABABU YA UCHUNGU
Waefeso 4:31,
‘Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya’.
Uchungu pia ni njia moja wapo ya kufanya watu wajaribiwe. Mfano ; Katika moja ya sehemu zangu  nilizokuwa nikifanya huduma nilikutana na dada mmoja ambaye alikuwa na ujauzito wa miezi kumi na miwili ambapo alikuwa hapati uchungu wa kujifungua. Dada huyo alinifuata na kuniomba nimuombee ili apate uchungu na azae lakini Roho wa Mungu alimuonesha kuwa kuna tatizo katika familia yake.
Ndipo nilipomwambia aende kumwita mama yake mzazi ambapo baada ya mama huyo kufika aliniambia kuwa  binti yake huyo alimtukana  matusi mazito na ndipo nilipomwambia yule binti  amuombe maama yake msamaha na baada ya kufanya hivyo ghafla alipata uchungu na kukimbizwa hospitali na alifanikiwa kujifungua mtoto wa kiume.
Wakati mwingine unaweza kuwa na uchungu juu ya ndugu, jamaa na marafiki kutokana na mateso mbalimbali ambayo wamekutendea lakini unapaswa kutoa uchungu huo ili kuuachilia moyo kwa BWANA  ndipo utakapompa nafasi ya kukubariki. Lakini hali hiyo hutokana na kuweka mambo mengi ya kuumiza moyoni hivyo kufanya kushindwa kuachilia na kusamehe.
Mara nyingi wanawake wamekuwa ni watu wa kuhifadhi mambo katika mioyo yao na wakati mwingine kuyafanya mambo kuwa makubwa hata kama ni madogo.

3. TUNAJARIBIWA ILI TUJIFUNZE KUMTEGEMEA MUNGU KWA ASILIMIA MIA MOJA
Unajua wakati mwingine Mungu hutujaribu ili tujifunze kumtegemea, nakumbuka waakti mke wangu ni mjamzito na alipofikisha muda wa kujifungua sikuwa na pesa hata kidogo katika akiba yangu, hivyo ilipofika wakati anaumwa uchungu nikuwa na kiasi cha shilingi mia na hamsini (150) katika akiba yangu , pesa ambayo nisingeweza kumhudumia kwa kitu chochote. Ndipo nilipoamua kumzalisha mwenyewe japo kuwa sikuwa na ujuzi wowote wa ukunga.

4. TUNAJARIBIWA KWASABABU YA UASI.
Roho ya kurudi nyuma ni moja kati ya vitu vinavyofanya mtu shindwe kusimama katika wokovu na wakati mwingine Mungu hutujaribu ili kutuondoa katika hali hiyo. Mungu huruhusu matatizo mbalimbali katika maisha yetu ili tumgeukie yeye. Kwa kawaida Mungu hutengeneza mtu anayempenda kwa gharama yoyote, huruhusu matatizo na misukosuko ili kumfanya asimuache.
Pia wapo watu ambao wapo makanisani kwasababu wana uhitaji wa mambo fulani hivyo pindi wanapopata mahitaji hayo humuacha Mungu kwa urahisi sana.Mfano ; Yupo binti mmoja Morogogoro alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa wa HIV, nilimuombea akapona akapata na mchumba lakini cha ajabu baada ya kupata mchumba alirudia tabia yake ileile.
Hivyo wakati mwingine wachungaji tunawaombea watu ambao tayari wana majibu ya shida zao au wanaelewa chanzo cha matatizo yao na wanakuwa wagumu katika kurekebisha.

5. TUNAJARIBIWA KWASABABU YA UBINAFSI
Wakati mwingine roho ya kijipenda wenyewe pasipo kuwajali wengine hufanya Mungu aruhusu majaribu ili kuturekebisha.
Wafilipi 2:3-4,
‘Msitende neno lolote kwa kishindana, wala kwa majivuno,bali kwa unyenyekevu, kial mtu na amhesabu mwenzie kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine’.
Mfano; Kuna dada mmoja alikuwa mtumishi mzuri tu kanisani lakini alikuwa na roho ya ubinafsi, alikuwa anavuna mahindi mengi sana lakini hakuwa kumbuka watu hata kidogo. Kutokana na hali hiyo Mungu aliruhusu jaribu ambapo wakati yeye yupo ibadani, nyumbani kwake walivamia majambazi ambapo walikusanya kila kitu katika nyumba yake yote hiyo ilikuwa ni katika kuhakikisha anamrekebisha tabia yake’.
Unapaswa kufurahia mafanikio ya watu wengine ndipo Mungu atakapo shughulika na maisha yako pia wivu huchangia kwa kiasi kikubwa kuharibu maisha ya kiroho.

6.TUNAJARIBIWA ILI TUWE NA HURUMA
‘Ambaye hakulala na njaa hawezi kujua ni sehemu gani chakula kipo’.Hivyo usipopitia matatizo huwezi kujua ni kwa namna gani unaweza kuwafariji wanaopitia matatizo.
2wakoritho1:3-5,
‘Na ahimidiwe Mungu bab wa BWANA wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja, atufarijie katika dhiki zetu zote ili nasi tunapate kuwafariji wale walio katika dhiki ya namna zote, kwa faraja hizo tunazofarijiwa na Mungu. Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo’.
Bila matatizo hatuwezi kuoneana huruma.

7.TUNAJARIBIWA ILI TUTHIBITISHE IMANI YETU.
Wakati mwingine watu hupita katika wakati mgumu ili kuweza kupimwa imani zao kwa Mungu.
Mfano; Wakati naanzisha huduma yangu kijijini nilikuwa na waumini wanne tu yaani mimi na mke wangu, na mzee wa kanisa na na mke wake, jambo la kusikitisha ilikuwa ni katika kipindi cha sadaka ambapo wote tulikuwa hatuna kitu basi ilikuwa kama mchezo wa kuigiza.
Wakati wa kuinuliwa ukifika umefika bwana, nakumbuka mara ya kwanza kupanda ndege nilikuwa naenda nchini  Kenya sasa wakati nimepata tiketi kwanza niliinusa....nikakuta harufu ya ndege, sasa nikapanda na wakati inaanza kupaa.... wakati huo nikiwa kimya naomba Mungu na kumwambia BABA NAIWEKA MIKONONI MWAKO ROHO YANGU huku nawaza cheupe wangu simuoni tena, kwakweli hali ilikuwa inatisha lakini nikakumbuka kuwa nilimuomba Mungu siku moja nipande ndege, hapohapo nikapata nguvu mpya.
Baada ya mahubiri hayo mtumishi wa Mungu Abiud kwa kushirikiana na Mch. Katunzi walifanya maombezi kwa watu mbalimbali ambapo wengi waliripuka mapepo na wagonjwa wengine kuanguka wakiwa hawajitambui.

Pamoja na maombezi hayo wapo watu wengine waliompokea BWANA YESU kuwa mwokozi wa maisha yao kwa kuongozwa sala ya toba.
Watumishi wa Mungu Mch. Katunzi na Abiud pia walifanya maombezi kwa wanawake waliokuwa na matatizo ya kutoshika mimba kwa muda mrefu sanjari na wale waliokuwa na uvimbe wa tumbo ambapo zaidi ya wanawake 30 walitoka kuombewa na wakipokea uponyaji wao.


Comments