MALI IDUMUYO

Na  Askofu Dk Josephat Gwajima.

1. Mali na Ucha Mungu.
“Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu. Kisha walizaliwa kwake wana saba, na binti watatu. Mali yake nayo yalikuwa ni kondoo elfu saba, na ngamia elfu tatu, na jozi za ng'ombe mia tano, na punda wake mia tano, na watu wa nyumbani wengi sana; basi hivi mtu huyo alikuwa ni mkuu sana kuliko watu wote wa upande wa mashariki. AYUBU 1:1 –
Mungu akitaka kumtumia mtu anaangalia mahali anapokaa, hali yake ya rohoni na anafahamu maisha ya mtu huyo jinsi anavyo ishi na anayahukumu maisha yake. Pia ametaja familia yake na mali zake.
Utajiri wa mtu unahusiana na mali anayo miliki. Ayubu alikuwa anamiliki kondoo elfu tatu ambao alikuwa anawatumia kutoa manyoya kwaajili ya kutengeza nguo na ingekuwa ni leo hii angekuwa na kiwanda cha kutengeneza nguo,alikuwa na ngamia elfu tatu ambao walikuwa wanatumika kubebea mizigo ingekuwa leo ana “semitrailer” elfu tatu kwaajili ya kusafirisha mizigo na ameokoka anampenda Mungu, alikuwa na jozi ya ngonbe miatano (jozi moja sawa na ngombe wawili au watatu) Ingekuwa leo ana matrekta mia tano ya kulimia, pia alikuwa na Punda mia tano wa kusafiria ambapo ingekuwa leo ni kama magari ya kifahari ya kusafiria sababu zamani mtu kumiliki punda lilikuwa ni jambo la kifahari sana. Zamani mtu alikuwa anaonyeshwa kuwa ni tajiri kwa jinsi hii.

“Naye Yabesi alikuwa mwenye heshima kuliko nduguze; na mamaye akamwita jina lake Yabesi, akisema, Ni kwa sababu nalimzaa kwa huzuni. Huyo Yabesi akamlingana Mungu wa Israeli, akisema, Lau kwamba ungenibarikia kweli kweli, na kunizidishia hozi yangu, na mkono wako ungekuwa pamoja nami, nawe ungenilinda na uovu, ili usiwe kwa huzuni yangu! Naye Mungu akamjalia hayo aliyoyaomba. 1 MAMBO YA NYAKATI 4:9-12
“Na jamaa za waandishi waliokaa Yabesi; Watirathi, na Washimeathi, na Wasukathi. Hao ndio Wakeni, waliotoka kwake Hamathi, babaye mbari ya Rekabu.” 1 MAMBO YA NYAKATI 2:55
Yabesi alikuwa mcha Mungu na alibarikiwa na Mungu mpaka utajiri wake ukafanya mji uitwe kwa jina lake.
Kuwa maskini na kutokujua kwamba unatakiwa unitoke kwenye hali hiyo ni kosa kubwa sana. Shetani anaogopa sana watu wa Mungu wakiwa wana fedha. Watu wengi wamepofushwa kwa elimu walizopewa kwamba hawatakiwi kuwa na mali na ikitokea watu wa Mungu wana mali basi hao sio wacha Mungu.
“Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea; ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu. 2 WAKORINTHO 4:3-4
Akili ni idara ya maamuzi iliyopo ndani ya nia ambayo ndiyo inaamua uwe tajiri au usiwe tajiri, uwe na makampuni au usiwe na makampuni, na hizi fikra ambazo dunia imewapa watu kwamba watu wanao mwabudu Mungu hawatakiwi kumiliki mali na kuwa matajiri sio za Bwana tunatakiwa tuondoke ndani ya elimu ya umasikini na tuwe na elimu ya Mungu yenye kutupa nguvu za kuwa matajiri kwa Jina na Yesu.
“Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele.” 1 YOHANA 5:18~20
“nami nitakupa hazina za gizani, na mali zilizofichwa za mahali pa siri, upate kujua ya kuwa mimi ni Bwana, nikuitaye kwa jina lako, naam, Mungu wa Israeli.” ISAYA 45:3
"Dunia iko chini ya yule mwovu ambaye ni ibilisi, ndio maana Yesu alipokuwa duniani alisema yeye sio wa ulimwengu huu na sisi sio wa ulimwengu huu. Sisi ni watu wa mbinguni na tupo hapa duniani kwa kazi maalum ambayo tutaifanya kwa miaka 70 hadi 80 na baadaye tutarudi mbinguni. Biblia inasema Mungu akimbariki mtu atampa mtu miaka 70/80 na unaweza kuiona ni mingi sana lakini ni midogo. Kwa mfano mtu anatakiwa alale masaa 8 kwa siku, ukipiga hesabu kwa wiki unalala masaa 56 na kwa mwaka unalala masaa 1912, ukigawanya usiku una lala miezi mine tu kwa mwaka mmoja achana na unavyo lala mchana, ukiishi kwa miaka themanini unapata miezi 323 ukigawanya kwa miaka unalala miaka 30 mpaka 40 na ndani ya miaka ile kuna miaka ya kusoma mfano kwa wale wanaomaliza chuo kikuu miaka 23 wanabakiza miaka 17 na wale wanaotaka kusoma digrii mpaka phD wanajikuta wanabakiza mpaka miaka 10 ya kuishi macho. Shetani anawapofusha watu fikra kwamba waone wana muda mwingi wa kuishi hapa duniani."
“Nimesulibiwa pamoja na Kristo; lakini ni hai; wala si mimi tena, bali Kristo yu hai ndani yangu; na uhai nilio nao sasa katika mwili, ninao katika imani ya Mwana wa Mungu, ambaye alinipenda, akajitoa nafsi yake kwa ajili yangu.” WAGALATIA 2:20
Unapomiliki utajiri mwingi wakristo wenzako ndio wakwanza kukuita wewe ndio freemason, shetani amefanikiwa kuwajaza akili kwamba unatakiwa uteseke kama Yesu lakini Yesu aliteseka ili sisi tusiteseke tena na alifanyika kuwa maskini ili sisi tuwe matajiri.
“Sasa hukumu ya ulimwengu huu ipo; sasa mkuu wa ulimwengu huu atatupwa nje.” YOHANA 12:31
“Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu.” YOHANA 14:30
Yesu anamtaja shetani ni mkuu wa ulimwengu huu na hana kitu kwake.
“kwa habari ya hukumu, kwa sababu yule mkuu wa ulimwengu huu amekwisha kuhukumiwa.” YOHANA 16:11

Yesu sikumoja alikuwa kwenye mkutano wa Injili pamoja na wanafunzi wake. Wanafunzi wake wakamwambia Yesu awaachie watu wakajitafutie chakula lakini Yesu akawaambia wapeni ninyi chakula, akawaambia wapeleke kile kidogo walicho nacho na Yesu akakibariki na wakala maelfu ya watu mpaka wakasaza. Haijalishi una kiasi gani ili ufanikiwe kilekile kidogo ulicho nacho ndicho kitakacho ongezeka na kudumu.
MAANDIKO MATATU AMBAYO WATU WAMEYATENGENEZA ILI KUWAFANYA WATU WABAKI KUWA MASKINI
“Kwa maana ni vyepesi ngamia kupita katika tundu la sindano kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” LUKA 18:25

Yesu alikuwa anatembea kijana mmoja akamwendea na kumuuliza “nifanyeje ili niingie mbinguni” na Yesu akamwambia ifuate torati usiibe, usiuwe, usizini, usiseme uongo. Yule kijana akasema yote nimeshayafanya ndipo Yesu akamwambia kagawe mali yake kwa watu wasiokuwa na mali na Yule kijana akakataa sababu aliwaibia sana watu mali na akakataa kuwasaidia wengine hapo ndipo andiko hilo linasema mtu kama huyo hawezi kuingia mbinguni na sio kutokumiliki mali na kuwa tajiri. Watu wanasema kama umeokoka na unakuwa tajiri huwezi kuingia mbinguni kitu ambacho sio kweli.
ANDIKO LA PILI
“Akasema, Palikuwa na mtu mmoja, tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya zambarau na kitani safi, na kula sikuzote kwa anasa. Na maskini mmoja, jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka katika meza ya yule tajiri; hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule maskini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani kwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi, kule kuzimu aliyainua macho yake, alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahimu kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. LUKA 16:19~25
Sio umasikini uliompeleka lazaro mbinguni na sio utajiri uliompeleka tajiri kuzimu bali tajiri pamoja na utajiri wake hakumsaidia lazaro na hakumwamini Bwana ndiomaana akaenda kuzimu na Lazaro alikuwa maskini ana vidonda lakini alimwamini Bwana . Sisi ni matajiri tunamcha Bwana na tutaenda Mbinguni kwa jina la Yesu.
ANDIKO LA TATU.
“Hakuna mtu awezaye kutumikia mabwana wawili; kwa maana atamchukia huyu, na kumpenda huyu; ama atashikamana na huyu, na kumdharau huyu. Hamwezi kumtumikia Mungu na mali. MATHAYO 6:24
Andiko halijasema huwezi kuwa na mali bali limesema huwezi kumtumikia Mungu na mali. Kwenye Biblia ya ‘king james’ andiko limesema huwezi kumtumikia Mungu Jehova na mungu mammon (mungu wa fedha) sio kuwa tajiri na kumtumikia Mungu.
“Nanyi mtamtumikia Bwana, Mungu wenu, naye atakibarikia chakula chako, na maji yako; nami nitakuondolea ugonjwa kati yako. Hapatakuwa na mwenye kuharibu mimba, wala aliye tasa, katika nchi yako; na hesabu ya siku zako nitaitimiza.” KUTOKA 23:25~27
Mungu hawezi kumletea mtu fedha bali ukitaka kupata mali unaweka mitego, mfano Isaka aliweka mitego na Mungu akambariki sana, lazima uwe na kitu cha kufanya ili Mungu akubariki kupitia kitu hicho.
“Hata siku ya sabato tukatoka nje ya lango, tukaenda kando ya mto, ambapo tukadhani ya kuwa pana mahali pa kusali; tukaketi, tukasema na wanawake waliokutana pale. Mwanamke mmoja, jina lake Lidia, mwenye kuuza rangi ya zambarau, mwenyeji wa Thiatira, mcha Mungu, akatusikiliza, ambaye moyo wake ulifunguliwa na Bwana, ayatunze maneno yaliyonenwa na Paulo. Hata alipokwisha kubatizwa, yeye na nyumba yake, akatusihi, akisema, Kama mmeniona kuwa mwaminifu kwa Bwana, ingieni nyumbani mwangu mkakae. Akatushurutisha Ikawa tulipokuwa tukienda mahali pale pa kusali, kijakazi mmoja aliyekuwa na pepo wa uaguzi akatukuta, aliyewapatia bwana zake faida nyingi kwa kuagua. MATENDO YA MITUME 16:13~20
Huu ni mji wa Ugiriki na Paulo alifika hapo akiwa hana mahali pa kukaa japokuwa ulikuwa mji wenye utajiri sana. Paulo alikosa mahali pa kukaa sababu mzunguko wa fedha za mji uilikuwa kwenye mikono ya kishetani lakini alikutana na mwanamke aitwaye lidia ambaye aliokoka na wakaanza kumtafuta Bwana, Kawaida Utajiri wa kudumu unaanza kwa kumtafuta Bwana.
Kwenye miji kuna fedha inayotokana na shetani na watu wengi wenye fedha mijini wanalo tumaini lao na ukilipiga hilo tumaini faida zao zinaanguka na kwisha. Kuna mali inayotokana na mashetani na mizimu lakini haidumu ni ya muda tu.
Yale maegemeo ya kichawi kwenye mji yanayowanufaisha watu wa mji ukiyapiga unamiliki fedha za mahali hapo na kuzifanya zizunguke mikononi mwa Mungu.
Ukiri:
“Kwa jina la Yesu ninakataa umasikini wa kila aina kwa jina la Yesu”
“Na Petro, akimkazia macho, pamoja na Yohana, akasema, Tutazame sisi. Akawaangalia, akitaraji kupata kitu kwao. Lakini Petro akasema, Mimi sina fedha, wala dhahabu, lakini nilicho nacho ndicho nikupacho. Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, simama uende. Akamshika mkono wa kuume, akamwinua, mara nyayo zake na vifundo vya miguu yake vikatiwa nguvu. Akaondoka upesi akasimama, akaanza kwenda; akaingia ndani ya hekalu pamoja nao, akienda, akirukaruka, na kumsifu Mungu. MATENDO YA MITUME 3:4~8

“Petro na Yohana walikuwa na miujiza lakini hawana fedha, kinacho leta fedha ni tofauti na kinacho leta miujiza Petro na Yohana wangekuwa na fedha wangemwambia mtu Yule fedha tunayo na uponyaji tunao simama chukua fedha hii ukaanze biashara lakini walimwambia hawana fedha bali walicho nacho ni uponyaji tu wakamwambia simama na utembee uende zako.”
Ukiri:
Kwa mamlaka ya jina la Yesu kristo ninamiliki mali iliyopo kwenye mzunguko wa kichawi kwa jina la Yesu, ninamiliki utajiri kwa jina la Yesu, namiliki maarifa ya kupata utajiri kwa jina la Yesu, ninawafyeka matajiri wa mji wanaomiliki fedha kwa uchawi kwa jina la Yesu ninateka mzunguko wa fedha wa kichawi naumiliki kwa jina la Yesu, mashetani yote yanayomiliki utajiri ninayafyeka kwa mamlaka ya jina la Yesu, watu wote wanaomiliki fedha kwa namna ya kichawi ninawafilisi utajiri kwa jina la Yesu, mimi ni tajiri namiliki utajiri kwa jina la Yesu namiliki utajiri udumuo kwa jina la Yesu kristo AMEN.

Comments