MAMBO MATATU(3) YANAYOAMBATANA NA TOBA YAKO YA KWELI.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU la uzima.
Leo nazungumzia toba.
BWANA YESU alikuja kwa ajili ya wanadamu watubu na kurudi katika miliki ya MUNGU kwa ajili ya uzima wa milele.
 Luka 5:32 ''  Sikuja kuwaita wenye haki, bali wenye dhambi, wapate kutubu. ''
 -Kutubu ni kugeuka kutoka kwenye dhambi na kuingia kwenye utakatifu. 
-Kutubu ni kuomba msamaha kwa MUNGU na baada ya kuomba msamaha unaacha dhambi zote ikiwemo na ile  iliyosababisha ukaomba msamaha.
-Kutubu ni mabadiliko katika mtazamo, kutoka mtazamo mbaya na kuingia katika mtazamo mzuri.
-Kutubu ni kutafuta kumpendeza MUNGU.
-Kutubu ni kujitenga na dhambi zote huku ukiambatana na KRISTO YESU.
-Kutubu ni muhimu sana.
Luka 15:7 '' Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu. ''
Mimi Peter Nilipookoka jambo la kwanza nilianza kuharibu vitu vyangu ambayo havimpendezi MUNGU, Ufahamu wangu kumbe kabla ya kuokoka haukujua mambo mambo mazuri. nilikusanya CD zangu zote na kukuta sina hata CD au DVD moja ya nyimbo za injili wala mahubiri, DVD zangu zote zilikuwa ni miziki tu ya kidunia na filamu tena filamu mbaya mbaya, nilizichukua na kuanza kuvunja, rafiki yangu mmoja aliniona na kunishangaa na kuniambia nimpe yeye lakini nilikataa na kuzivunja zote na kuna vitabu vya mambo mabaya nilivichoma moto. Video zote za ngono na picha kwenye simu yangu nilifuta maana nilidhamilia haswaaaaa kumpendeza MUNGU. 
Toba ya kweli ndugu zangu huambatana na mabadiliko yatakayodumu siku zote za maisha yako.

2 Petro 3:9 '' BWANA hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba.''

MAMBO 3 YANAYOAMBATANA NA TOBA YA KWELI.

       1.   TOBA YA KWELI HUAMBATANA NA KUBADILIKA NIA..

Warumi 12:2 ''  Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya MUNGU yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. '' 
-Baada ya kutubu dhambi lazima ubadilishe nia yako kutoka nia ya dhambi na kuingia katika nia ya utakatifu. kuna mtu kila siku hufanya uzinzi na kila siku hutubu, hiyo sio toba ya kweli maana nia yake haijabadilika. Nia ikibadilika hutaruhusu tena dhambi ambazo zilikutesa kabla hujatubu. kama nia yako imekuwa nia safi hakika huwezi hata kukaa katika bar ambayo kila siku ulikuwa unashinda pale kabla hujatubu kwa BWANA YESU. Kama nia yako isipobadilika hakika kila siku utakuwa unajikwaa katika lilelile unalolitubia na hapo unakuwa hujatubu toba ambayo inampendeza MUNGU. 

Mathayo 15:19 ''Kwa maana moyoni hutoka mawazo mabaya, uuaji, uzinzi, uasherati; wivi, ushuhuda wa uongo, na matukano; ''
-Ukibadilika nia kutoka nia  kuwaza uzinzi na uasherati hakika utafanikiwa kuingia katika toba ya kweli. kama mabaya hayo bado yako moyoni mwako hakika utajikuta tu unayatenda tena maana bado wewe ni mtumwa wa dhambi hizo.
-Ukitubia dhambi fulani hakikisha unabadilika nia ya kufuata dhambi hiyo tena.

Waebrania 8:10b '' Nitawapa sheria zangu katika nia zao, Na katika mioyo yao nitaziandika; Nami nitakuwa MUNGU kwao, Nao watakuwa watu wangu. '' 

-Katika nia yako MUNGU huweka sheria yake yaani huweka kila jambo ambalo unatakiwa uliendee au uliishi baada ya hapo. Sheria hiyo MUNGU huitoa kupitia watumishi wake na neno lake Biblia takatifu . baada ya kutubu unatakiwa usitende dhambi tena hiyo ndio sheria ya MUNGU kwako.


       2.   TOBA YA KWELI HUAMBATANA NA KUBADILIKA MTAZAMO.

 Yohana 15:4 '' Kaeni ndani yangu, nami ndani yenu. Kama vile tawi lisivyoweza kuzaa peke yake, lisipokaa ndani ya mzabibu; kadhalika nanyi, msipokaa ndani yangu.''.
-BWANA YESU hapo anaposema kwamba tukae ndani yake maana yake tusiondoke ndani yake kimtazamo na kimatendo.
-Huwezi kusema umetubu halafu mtazamo wako ukabaki kwamba hakuna haja ya kwenda kanisani wala kujifunza Neno la MUNGU. Ndugu ukifanya hivyo hutafika popote utajikwaa tu na kuirudia dhambi ambayo ilikufanya utubu. toba ya kweli ni pamoja na kubadilika mtazamo kutoka mitazamo mibaya na kuingia katika mtazamo mzuri ambao ni kukaa ndani ya YESU.

Kukaa ndani ya YESU ni;

-Kukaa katika Fundisho lake.
-Kukaa katika Wokovu wake.
-Kukaa katika Neno la MUNGU na maombi.
-Kukaa katika mapenzi yake.
-Kukaa katika utakatifu.
-Kukaa katika upenndo wa wake.
-Kukaa katika Imani pasipo kuondoka wala kuhama.

1 Kor 15:33-34 '' Msidanganyike; Mazungumzo mabaya huharibu tabia njema. Tumieni akili kama ipasavyo, wala msitende dhambi; kwa maana wengine hawamjui Mungu. Ninanena hayo niwafedheheshe.'' 

-Kama bado mtazamo wako uko katika kujumuika na marafiki zako watenda dhambi katika eneo lile lile lililokuwa linasababisha kutenda dhambi basi utajikuta tu unaanguka tena na tena katika dhambi.
-Kama mtazamo wako ni kwamba  unatubu kisha unajitenga na kanisa hakika  hutafika popote bali utaanguka tu dhambini.
Toba halisi ni pamoja na kubadilika mtazamo. kuna watu mtazamo wao ni kwamba kwenda disko kujirusha na kucheza ni jambo jema wakati mtazamo huo ni wa shetani maana ukiwa katika maeneo hayo utajikuta una ''onja ila usilewe'' kumbe ni usanii tu wa shetani. disko utajikuta unatamani watu wasiokuhusu maana upo katika uwepo wa shetani. Mtazamo kama huo lazima ubadilike ndipo toba yako itakaa maana adui hatapeleka mashitaki yeyote kuhusu wewe.

     3.     TOBA YA KWELI HUAMBATANA NA KUFANYA MABADILIKO KATIKA JINSI YA KUISHI.

2 Thesalonike 1:9-10 ''  Kwa kuwa wao wenyewe wanatangaza habari zetu, jinsi kulivyokuwa kuingia kwetu kwenu; na jinsi mlivyomgeukia MUNGU mkaziacha sanamu, ili kumtumikia MUNGU aliye hai, wa kweli; na kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye alimfufua katika wafu, naye ni YESU, mwenye kutuokoa na ghadhabu itakayokuja. ''.

-Huu ni mfano wa yule aliyebadilika baada ya toba na kuacha na maisha ya kuabudu sana au kusujudia. Kama alikuwa na sanamu nyumbani mwake ambayo kila siku alikuwa anaibussu na kuisujudia baada ya toba ya kweli anachoma moto sanamu hizo, hayo ndio matokeo halisi ya toba ya kweli.
-Kama ulikuwa mganga wa kienyenyi baada ya toba unabadilika na kuchoma moto zana zote za uganga na kuanza kuishi maisha mapya matakatifu mbele za MUNGU BABA, Hiyo ndio toba ya kweli.
-Kama ulikuwa unaroga watu au kuwatapeli, baada ya kumpokea YESU na kutubu unaamua kuharibu zana zote za uchawi ulizokuwa nazo, hayo ndio matokeo ya toba ya kweli.
-Haiwezekani mfano kijana mzinzi anaamua kumpokea YESU na kutubu kisha kuacha uzinzi lakini nyumbani kwake ana pakti 3 za kondomu na kila siku huvaa moja  kwa kijifurahisha na pia ana kitabu cha picha za x na katika laptop yake amejaza filamu za ngono. mtu wa hivyo kama anajishughulisha na vitu hivyo vitamnajisi tu na kujikuta akirudi tena dhambi.

Mathayo 3:8 '' Basi zaeni matunda yapasayo toba;''

-Ndugu, ni matunda gani au ni mambo gani yanazaliwa baada ya wewe kutubu? je unazaliwa utakatifu wa kudumu au utakatifu wa muda tu?
Ndugu nakushauri zaa matunda/matendo mazuri baada ya kutubu.

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKITI.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.

Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa.
Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA. MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments