MTU HUKUAJE KIROHO?

Na Mtumishi Peter Mabula
BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Kuna Ndugu Aliniuliza Anatamani Kukua Kiroho, Je Afanyeje Ili Akue Kiroho?. Yawezekana na wewe unaswali kama hilo hilo na unatamani kujua.
Naomba Niliseme Hili Kwa Kila Ndugu Anayetaka Kukua Kiroho. 

1 Petro2:2 ''Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;''
-Jambo la kwanza nataka tujue kwamba kukua kiroho kunakotakiwa ni kuukulia wokovu. Kudumu katika wokovu huku ukijifunza Neno la MUNGU sahihi ambalo Biblia inaliitwa Maziwa ya akili yasiyoghoshiwa. 
Huwezi kukua kiroho kama huambatani na Neno la MUNGU.  Kama hulihitaji Neno la MUNGU huwezi kukua kiroho maana kama huna muda wa kujifunza Neno la MUNGU na kulielewa basi lazima tu utakuwa unajifunza mambo ya dunia au mambo ya shetani ambayo siku zote yako kukuweka mbali na MUNGU. 
MUNGU anapatikana katika Neno lake hivyo Neno kama maziwa ya akili unatakiwa uyanywe kila siku ili kupata afya njema ya kiroho na afya njema ya kiroho ndio itakayokuwa sababu kuu ya wewe kukua kiroho.

Waebrania 5:12 ''Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya MUNGU; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu.'' 
-Kila mtu ili akue kiroho anahitaji kufundishwa Neno la MUNGU, Sasa kama wewe unalikwepa neno la MUNGU utakuaje kiroho?
Chakula kigumu ni Neno la MUNGU ambalo waliokuwa kiroho wanalipokea maana ambaye ni mchanga kiroho kuna masomo ya Neno la MUNGU akifundishwa anaweza hata kuacha wokovu kumbe ni kwa sababu tu ya uchanga wake wa kiroho na kutokuizingatia Biblia.
 
 Mtu anayeenda kimwili hawezi kukua kiroho.

1 Kor 2:14 '' Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya ROHO wa MUNGU; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni. '' 
-Ili ukue kiroho lazima uende kiroho na sio kimwili.

 UTAJUAJE KAMA UMEKUA KIROHO?

1.   Kukua Kiroho Hakutokei Kienyeji Bali Hutokea Baada Ya Kukusudia Au Kuweka Makusudio. 
-Kukua Kiroho Huja Kutokana Na Taarifa, Lazima Ujue Taarifa Yako Kwamba Unakuwa Kiroho Au Hukui, Taarifa Hiyo Utaijua Moja Kwa Moja Kutokea Ndani Ya Moyo Wako Pale Utakapofanya Jambo Litakalojulisha Kwamba Umekua Kiroho, Pia Unaweza Kuipata Taarifa Yako Ya Kukua Kiroho Kutoka Kwa Mchungaji Wako. Mchungaji anaweza kabisa kujua kwamba katika waumini wake ni nani na nani wanakua kiroho, ni nani na nani wanakufa kiroho, ni nani na nani wanadumaa kiroho.
Kama Taarifa Yako Ni Mbaya Tengeneza Na Jisahihishe
Filemoni 1:4-7 '' Namshukuru MUNGU wangu sikuzote, nikikukumbuka katika maombi yangu; nikisikia habari za upendo wako na imani uliyo nayo kwa BWANA YESU na kwa watakatifu wote;  ili kwamba ushirika wa imani yako ufanye kazi yake, katika ujuzi wa kila kitu chema kilicho kwetu, katika KRISTO. Maana nalikuwa na furaha nyingi na faraja kwa sababu ya upendo wako, kwa kuwa mioyo ya watakatifu imeburudishwa nawe, ndugu yangu. '' 
-Filemoni hapa hata kama alikuwa hajijui kama yuko vizuri kiroho baada ya kusikia maelezo ya Mtume Paulo kwake lazima angejua kabisa kwamba amekuwa kiroho. taarifa ya Filemoni ilikuwa kwamba anaendelea vyema sana katika imani ya KRISTO YESU, Huko ndiko kukua kiroho. Kanisa zima likuwa limejua kwambaFilemoni ni mzima kiroho ndio maana hata habari zake zikaenea kwamba ana upendo na tena anaenenda vizuri katika imani ya BWAN YESU.

2.  Kukua Kiroho Huja Kutokana Na Uzoefu Wa Kulizingatia Neno La MUNGU. Kama Hujifunzi Neno La MUNGU Je Utakuaje Kiroho?. 
Wakolosai 3:16-17 ''Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la BWANA YESU, mkimshukuru MUNGU BABA kwa yeye.'' 
-Ili ukue kiroho ni lazima Neno la KRISTO likae kwa wingi ndani yako. Kama unalikimbia neno la KRISTO utakuaje sasa kiroho?
-Ili ukue kiroho lazima uwe karibu na BWANA kwa kujifunza neno lake, kuomba na kushirikiana na washirika wengine katika kazi ya MUNGU.


3.  Kukua Pia Huja Baada Ya Wewe Kuwa Na Uhuru Rohoni. Uhuru Huo Huja Baada Ya Kumjua MUNGU Na Kuwa Mwombaji Pia Uhuru Huo Huja Baada Ya Wewe Kukubali Kuenenda Na Kuongozwa Na ROHO MTAKATIFU. 
Ndugu, Ni Heri Kukua Kiroho Kuliko Kudumaa Kiroho. Ni Heri Kupanda Viwango Vya Kukua Kuliko Kushuka Chini.

Yohana 8:36 '' Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli. '' 
-YESU akikuweka huru hakika utakuwa huru kweli kweli.
Katika YESU kukuweka huru kukupa ROHO MATAKTIFU ili uenende kama MUNGU atakavyo.

Isaya 55:6-7 '' Mtafuteni BWANA, maadamu anapatikana, Mwiteni, maadamu yu karibu; Mtu mbaya na aache njia yake, Na mtu asiye haki aache mawazo yake; Na amrudie BWANA, Naye atamrehemu; Na arejee kwa MUNGU wetu, Naye atamsamehe kabisa.   '' 

 Kuna vitu vinavyoweza kukusababishia usikue kiroho hata kama una juhudi ya kutaka kukua kiroho. dhambi ndio kikwazo namba moja cha kukuzuia kukua kiroho.

Kuna Kujifunza Kutokana Na Makosa Na Pia Kuna Kujifunza Kutokana Na Mafanikio. Kama Hukui Kiroho Basi Angalia Makosa Yaliyo Chanzo Cha Kutokukua Kwako kiroho, Yaache Makosa Hayo. Pia Kama Hukui Kiroho Na Unatamani Kukua Kiroho Basi Jifunze Kwa Waliofanikiwa Kiroho.


Webrania 13:7-9 ''Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la MUNGU; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao. YESU KRISTO  ni yeye yule, jana na leo na hata milele. Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.   ''

 Ukiwachunguza Waliokua Kiroho Utagundua Watu Hao Ni;
 -Waombaji.
-Hulitendea Kazi Neno La MUNGU.
-Wanaenenda Kwa ROHO MTAKATIFU.
-Wana Juhudi Katika Kutenda Mema.
-Ni Watoaji.
-Hawafuati Anasa Za Dunia.
-Sio Wasikiaji Tu Wa Neno La MUNGU Bali Hulifanya Neno Walilifundishwa Kuwa Sehemu Ya Maisha Yao.

Waige Hao Na Utafanikiwa Kukua Sana Kiroho. 
Ubarikiwe Na Endelea Zaidi Kujifunza Neno La MUNGU Na Kulitii Hakika Utakua Sana Kiroho. 
Yakobo 1:22-25 ''Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo. Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake. '' 
-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''

Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments