MUNGU HUVIPA HESHIMA ZAIDI VIUNGO VILIVYOPUNGUKIWA.



Mch.Gasper Madumla.
Na Mchungaji Gasper Madumla.

Bwana Yesu asifiwe…
MUNGU huvieshimisha zaidi vile ”viungo” vilivyopungukiwa. Neno ”viungo” napenda nilipe jina la ” vyombo” Ninaposema ” vyombo ” sina maana ya vyombo kama sahani,au masufuria ya kulia chakula nyumbani,bali nina maana ya mtu. Sisi machoni pa BWANA ni vyombo vyake kwa utukufu wa jina lake.
Wengine wamefanyika vyombo vya sifa,wengine vyombo vya injili N.K.Vyombo vyote vinathamani mbele za Bwana maana tunatumika tofauti tofauti kwa kufaidiana.
Sasa,wapo watu wenye kuona ubaya wa uwepo wa vyombo vingine na kuviona vyombo hivyo havina thamani  kumbe mbele za Mungu Baba kila chombo kina thamani yake kulingana na kazi yake aliyoitiwa. Leo nataka nikupe story ya chombo kimoja kilichokuwa kikidhalaulika lakini kumbe ndio chombo kizuri. Chombo chenyewe ndio hiki;
Kulikuwa na mdada mmoja alikuwa akidhalaulika kwa sababu ya maneno na vitendo vyake,tena alipewa jina ” fresh ” likiwa na maana kwamba ” chizi fulani hivi ” maana ndivyo watu walivyokuwa wakiimuita lakini watu waliokuwa wakimdhalau hawakujua kuwa MUNGU huvipa heshima viungo vile vilivyopungukiwa ( 1 Wakorintho 12:24).
Yaani waweza kumuona mtu ukamuhesabia mapungufu yake lakini mtu huyo anathamani kubwa mbele za Mungu.
Mdada huyu alikuwa ameokoka ingawa alidhalaulika katika jamii yake. Siku moja wakati akiwa katika harakati zake akajikuta akimuambia baba mmoja hivi, ”…Naomba unioe wewe…” yule mbaba akamuambia mbona mimi nina mke tayari,kwani hauoni pete?
Mdada akamjibu ” kwani pete kitu gani bhana! We sema kama unahitaji kunioa au lah…” yule mbaba alikuwa ni mtu wa makamu fulani hivi,na kwa sababu walikuwa wote kwenye banda la kuangalia mpira kama ilivyokuwa desturi yao kila siku za mechi,basi yule mbaba akamjibu ”…Basi,mimi ntakuoa wewe uwe mke wa pili,njoo nyumbani nikutambulishe kwa mke wangu…”
Alimjibu hivyo ili amlidhishe tu,na wala haikutoka moyoni maana alijua kwamba haiwezekani yeye kuoa mke mwingine katika ukristo,na si unajua tena watu wa namna hiyo wanapokuwa wakitizama mpira huwa wana masihara sana,na utani mwingi. (Katika wokovu hatutakiwi kuwa na mizaha mizaha,wala kutukana Zab.1:1-3)
Sasa,siku moja jamaa akiwa nyumbani kwake akijiandaa kutoka gafra anamuona yule dada ambaye wanamuita fresh,tena ameokoka huyu,akiwa anakuja kwa mbaliii. Sasa jamaa ikabidi amwambie mke wake kwamba ”… yule ajaye ni mdada anayetaka nimuoe tena,sasa  anakuja lakini huyu kweli ni chizi jamani,sasa ndio ulokole gani waliokuwa nao hawa ndugu…” aliyasema hayo kwa sababu ya mshangao mkubwa.
Baada ya mdada kuingia ndani wakaongea na kuchekaa,wakimsanifu yule mdada,maana hawakuamini kwamba mlokole kaja aolewe na mtu mwenye mke!!wakacheka hao.
Mwishoe yule mke wa jamaa akataka kujua ni wapi yule mdada anaabudu ili aone uchizi wao. Yule mdada akamwambia mahali anapoabudu,basi mke wa jamaa akamwambia ”… Haya,tumekusikia lakini ntakuja huko unapoabudu,asante…”
Siku moja,yule mke wa jamaa akafunga safari ili aje ashuhudie mahali anapoabudu yule mdada. Alipofika kanisani hapo,nakuambia huwezi kuamini sababu siku hiyo ndio ilikuwa ni siku ya kuokoka kwake maana alikutana na Yesu katika ibada iliyokuwa ikiendelea,akaokoka siku hiyo hiyo.
Na kuanza kulia,alishangaa njia za Mungu zilivyo za ajabu,na kilichomshangaza zaidi ni kwamba mambo yake yote yaliyokuwa yamefungwa yakafunguliwa,kumbe siku hiyo ndio ilikuwa ni siku yake . Aliyekuwa akiishi katika mateso ya nguvu za giza maana hakuwai kuamini wokovu.
Ila alipofika tu,katika kanisa la yule mdada anapoabudia ndipo mahali alipokutana na Yesu. Hata baadaye wazo la kuoana likapotea kabisaa,badala yake yule mke wa jamaa akaokoka na kuona raha ipatikanayo kwa Yesu.
Umeona MUNGU anavyoweza kuvitumia vyombo vionekanavyo dhaifu kwa kuvipa heshima. Sababu chanzo cha wokovu  wa yule mke kilianzia mbali kama mzaha vile,tena kwa kupitia mtu anayedhalaulika kabisa!!
We unafikiri ni nani aliyekuwa akijua kwamba mke wa jamaa ataokoka kwa njia ya namna hiyo? Sababu mtu huyu mke alikwisha hubiriwa sana lakini alikuwa akikataa na kupinga wokovu,kumbe MUNGU akamtafuta kupitia kisa cha kushangaza na hatimaye sasa ni mlokole mzuri tu.
Mdada huyu aliyeonekana chizi ndie aliyemleta mtu kwa Yesu tena wale wenye kumuona chizi hawakumleta hata mtu mmoja kwa Yesu. Sasa ngoja nikuulize ndugu;
Yupi mwenye thamani mbele za Mungu,Je ni wale watu wenye dharau wasiomleta mtu yeyote kwa Yesu Kristo,Au ni huyu mdada aliyeonekana chizi lakini kamleta mtu mmoja kwa Yesu Kristo?
Hutakiwi kuwadhalau watu,na kuwaona ni machizi. Mungu huwapenda watu wote haswa hao ambao wewe unawadharau.
 Njia za Mungu hazichunguziki,akiamua kumtafuta mtu njia yoyote inaweza kutumika. Upendo wa Mungu ni mkuu sana kwetu.
Kwa huduma ya maombi na maombezi,usisite kunipigia simu yangu hii 0655111149.
Mchungaji Gasper Madumla.
Beroya bible fellowship church ( Kimara-Dar,Tanzania )
UBARIKIWE.

Comments