NI LAZIMA UITAMBUE SIKU YA TOFAUTI.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
Karibu sana tujifunze Neno zuri la MUNGU.
Ni lazima uitambue siku ya tofauti.
Kila jambo lina wakati waakati wake chini ya mbingu.

Mhubiri 3:1 '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. ''

-Kwa sababu kila jambo lina wakati wake, hata siku ya kupokea kwako ina wakati wake, hata siku ya kupona kwako ina wakati wake, hata siku ya kufanikiwa kwako ina wakati wake, wakati wa kutubu nao kuna wakati wake maana kuna wengine walitarajia kutubu wakati furahi lakini wakati huo ukawa sio wakati wao maana wanakuta wameshaondoka duniani. Ni muhimu kuitambua siku ya tofauti ili uhusike na jambo jema wakati huo wa siku yako ya tofauti.
Ni lazima uitambue siku ya kufanikiwa kwako.

Bartimayo kipofu yeye aliiona siku yake ya kuondoka katika upofu wake maana licha ya wanadamu kumwambia asimsumbue YESU lakini yeye aliona nafasi hiyo akiitumia vizuri ndio kupona kwake kunafika na kweli akapona.

Luka 18:35-43 ''  Ikawa alipokaribia Yeriko, mtu mmoja kipofu alikuwa ameketi kando ya njia, akiomba sadaka; na alipowasikia makutano wakipita, aliuliza, Kuna nini? Wakamwambia, YESU wa Nazareti anapita. Akapiga kelele, akisema, YESU, Mwana wa Daudi, unirehemu. Basi wale waliotangulia wakamkemea ili anyamaze; lakini yeye alizidi sana kupaza sauti, Ee Mwana wa Daudi, unirehemu. YESU akasimama, akaamuru aletwe kwake; na alipomkaribia, alimwuliza, Wataka nikufanyie nini? Akasema, BWANA, nipate kuona. YESU akamwambia, Upewe kuona; imani yako imekuponya. Mara hiyo akapata kuona, akamfuata, huku akimtukuza MUNGU. Na watu wote walipoona hayo walimsifu MUNGU.'' 
-Siku ya tofauti kwa Bartimayo ilipofika aliitumia vizuri sana na kupona.
Ndugu yangu, wakati wa kupona kwako umefika kabisa ila tatizo tu wewe hujautambua wakati, hujaitambua siku ya tofauti. Kuwa watu waliwahi kusumbuliwa na uchawi na mizimu, walizunguka kwa kila matapeli ambao ni waganga wa kienyeji lakini hawakupona, walipogundua siku ya tofauti walikimbilia maombezi na kupona.
-Ndugu yangu kama ulikuwa hutambui tambua leo kwamba; Kuna mikutano ya injili hutokea maeneo yako kwa ajili tu ya wewe kupokea uzima, uponyaji,afya na baraka ambazo ulizitafuta kwa siku nyingi, unaposhindwa kuitambua siku hiyo ya kipekee kwako utabaki na ugonjwa wako. piga picha Bartimayo angesikia BWANA YESU anapita lakini akasema kupiga kelele ni kujiabisha ngoja labda atapita siku nyingine. ndugu hiyo siku nyingine inaweza ikawa ni baada ya mwaka mzima, ndio maana aliitumia vizuri siku ya tofauti na kupona.

-Kuna wadada siku zote wanalia ili kupata waume sahihi kutoka kwa MUNGU. Lakini kutokuijua kwao siku ya tofauti kumepelekea wabaki walivyo.
Rebeka aliitumia vizuri siku ya tofauti ndio maana akampata mme mwema Isaka. Sio lazima siku yako ya tofauti ya kupokea mchumba ujipendekeze kwa huyo mchumba bali timiza ucha MUNGU wako katika kuwasaidia na kuwahudumia wengine inaweza kuleta baraka yako.  Rebeka aliitimua vizuri siku ya tofauti na akapokea baraka yake ya mme (Mwazo 24:1-67)
Katika Hiyo Mwanzo 24 kuanzia mstari wa 12-21 Biblia inasema  


''Naye akasema, Ee BWANA, MUNGU wa bwana wangu Ibrahimu, nakuomba mambo yangu uyajalie yawe heri leo, ukamfadhili bwana wangu Ibrahimu. Tazama! Nimesimama karibu na kisima cha maji, na binti za watu wa mjini wanatoka kuteka maji, basi na iwe hivi; yule msichana nitakayemwambia, Tua mtungi wako, nakuomba, ninywe; naye akasema, Unywe, nami nitawanywesha na ngamia zako pia; basi huyu na awe ndiye uliyemchagulia mtumishi wako Isaka; na kwa hayo nitajua ya kuwa umemfadhili bwana wangu. Ikawa, kabla hajaisha kunena, tazama, Rebeka anatokea, binti wa Bethueli mwana wa Milka, mkewe Nahori, ndugu wa Ibrahimu, naye ana mtungi begani pake. Naye yule msichana alikuwa mzuri sana uso wake, bikira, wala mwanamume hajamjua bado; akashuka kisimani, akajaza mtungi wake, akapanda. Ndipo yule mtumishi akapiga mbio kwenda kumlaki, akasema, Tafadhali unipe maji kidogo katika mtungi wako ninywe. Naye akasema, Unywe, bwana wangu, akafanya haraka, akatua mtungi wake mkononi mwake, akamnywesha. Hata alipokwisha kumnywesha akasema, Na ngamia zako nitawatekea, hata watakapokwisha kunywa.
  Akafanya haraka, akamwaga maji ya mtungi wake katika birika, akapiga mbio kisimani ateke, akawatekea ngamia zake wote.
Basi yule mtu akamkazia macho, akanyamaza, ili ajue kwamba BWANA ameifanikisha safari yake ama sivyo.'' 


-Yaani huyu Eliazeri ni kama waliambiana na Rebeka maana Rebeka aliitumia vizuri siku ya tofauti hata akaolewa na Isaka na ndivyo ilivyokuwa.
-Ndugu yangu, ni vizuri sana kuitumia siku ya tofauti ili upokee baraka yako.
Kwaya fulani ndogo siku moja waliitumia siku yao ya tofauti vizuri na kupokea kila mmoja baraka aliyoitaka.
Ilikuwa hivi; Kuna mama mmoja kutoka Mkoani mbeya alikuja kumuuguza mme wake hapa Dar es salaam na akawa anasali kanisa la kiroho ambalo vijana hao wanakwaya walikuwa wakisali. baada ya kama mwezi mmoja yule mme wake na yule mama akafariki. Yule mama alikuwa anahitaji sana msaada ili kusafirisha mwili wa mmewe mpenzi. kwaya ile walijitolea kuimba katika msiba ambao ulikuwa unafanyika kwa ndugu za yule mama kabla ya kusafirishwa kwenda mbeya, wale wanakwaya wakawa wanaimba msibani kwa juhudi na kuwafariji wafiwa, kisha  walipoona uchumi hauko vizuri kwa yule mama  walitoa pesa zao kwa ajili ya kusafirisha msiba kisha na wao wote wakasafiri kwenda mbeya msibani. baada ya mazishi yule mama aliwaita wale wanakwaya akawashukuru sana na kisha akawauliza ''Mnataka MUNGU awatendee nini? Niambieni kila mmoja analotaka atendewe na BWANA''. Wale wanakwaya kila mmoja akataja hitaji lake kwamba anahitaji kuajiriwa serikalini. wakawa na hitaji moja. Yule mama akawaambia ''Kila mmoja ndani ya mwaka huu ataajiriwa na kupata kazi nzuri aipendao''. Wale wanakwaya wakarudi nyumbani Dar es salaam. Ndugu zangu hata miezi 7 haikupita kila kijana katika wale wanakwaya akaajiriwa serikalini, hawakuwa na Elimu kubwa  hata kidogo lakini kwa Neno la yule maana wote wameajiriwa Serikalini na ni wafanya kazi wa serikali sio ajira ya muda bali ajili ya kudumu.
Waliitumia vuzuri siku yao ya tofauti.
 -Siku ya tofauti ni muhimu sana kuitumia ndugu yangu.
Mama Mshunemu aliitumia siku ya tofauti vizuri Enzi za Nabii Elisha na akabarikiwa kupata mtoto kwa muujiza katika ndoa yake ambayo kwa miaka mingi hakuwa amepata moto, tangu afunge ndoa hakuwa amepata mtoto.
Ndugu itumie vizuri siku yako ya tofauti kwa kwenda kwa YESU ili upokee.
2 Wafalme 4:5-17 '' Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula. ule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa MUNGU. Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo. Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala. Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake. Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe. Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee. Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni. Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa MUNGU, usiniambie mimi mjakazi wako uongo. Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia. ''
-Ndugu yangu, je wewe unateswa na nini?
-Je umesubiri nini kumkimbilia BWANA YESU ili akushindie?
Inawezekana kabisa umelisikia Neno la MUNGU sana na kila siku ila kuna siku Neno la MUNGU litakuja au lilikua kwa ajili yako tu ili upokee baraka yako.
-Kila mara umeona mikutano ya injili au semina mbalimbali na umedharau lakini wakati mwingine siku yako ya tofauti ilikuwa imefika na ndoa yako ingepona, ugonjwa wako ungeondoka. ungekaa salama tofauti na Mwanzo.
Ndugu siku ya tofauti itumie vizuri.
Lakini pia naomba utambue kwamba Hata siku ya kufa ni siku ya tofauti, inawezekana kabisa usiijue siku yako ya kufa lakini kujiandaa kwa ajili ya siku hiyo ni muhimu sana maana  unaweza kwenda mbinguni kama utaitii kweli ya MUNGU yaani KRISTO YESU.
Mhubiri 3:1-2a '' Kwa kila jambo kuna majira yake, Na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu. Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; '' 
-Siku ya tofauti ni mihimu sana kwako kuitumia.
-Watu walio wengi hawaitambui siku ya tofauti ndio maana siku zote wanabaki katika hali ile ile ya kwanza  bila mabadiliko.
-Wewe naamini utaitambua siku ya tofauti na utaitumia vizuri sana.

-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu
KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.
''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''
Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments