NILIISHI NA MUME MCHAWI KWA MIAKA 25 BILA KUMTAMBUA KUWA NI MCHAWI

mkataba na shetani ni mbaya sana.

BWANA YESU ASIFIWE.
Nawasalimu katika jina la YESU, ndugu zangu wote mliokoka na ambao hamjaokoka natoa ushuhuda huu kwenu ili ukusaidie wewe unayesoma ushuhuda huu au ndugu yako au mpendwa yeyote unayamjua.
Mimi kwa sasa hivi ni mama nimeolewa nina watoto, nimeokoka nampenda YESU ndie BWANA na MWOKOZI wa maisha yangu.
USHUHUDA wangu una ujumbe ndani yake kuwa  ukisha mpata YESU usije ukathubutu kumwacha YESU kwa njia yoyote ile, utajiona mjanja kwa muda, kumbe umekalia kuti kavu wakati wowote linakatika unaanguka, pia maisha yako yanaharibika kabisa, ukimrudia YESU kama ulimwacha gharama za kurudia hali yako ya mwanzo kwako binafsi ni kubwa sana, kwa kuwa unakuwa umeharibu maisha yako, YESU anakuwa kisha kusamehe lakini mpaka wewe ujione tena umefiti nyumbani mwa BWANA ni gharama.
Historia yangu ni kwamba, mimi niliokoka nikiwa na miaka kati ya kumi na sita au saba nilikuwa Form III, niliokolewa, nikabatizwa maji mengi na kujazwa ROHO MTAKATIFU.
Nilipomaliza shule na kwenda chuoni hapo ndipo tatizo lilianza, nilianza kuona kuwa maisha ya ulokole ni ushamba nikajiingiza katika maisha yote ya kidunia ambayo unayaona au kuyasikia wanayoishi wasichana wasiokoka wanaojiita wa kileo/kisasa, niliishi maisha mabaya sana nilikuwa na rafiki wa kiume ambaye tulikuwa kama wachumba lakini hatukuoana.
Baada ya kumaliza chuo, nilipata kazi, maisha yangu yakawa yale yale ya kutompendeza MUNGU nilianza kunywa pombe, kwenda miziki na kuwa na ma boyfriend. Nilipokuwa nakutana na wapendwa niliokuwa naabudu nao zamani, nilikuwa nawakwepa au nikikutana nao uso kwa uso sipendi wanisalimie BWANA ASIFIWE.  Mbaya zaidi siku moja  katika kituo cha basi pale Posta Mpya nilikutana na Mchungaji wangu wa Kanisa nilipokuwa nikiabudu kabla ya kuacha wokovu, nilijikausha hata sikumsalimia sijui aliniona au la, lakini nilijipa matumaini kuwa hakuniona.
Katika maisha yangu nilikuwa najiona mzuri sana na shepu nzuri, nilikuwa nachagua sana wachumba, na wengine walikuwa wakiniomba uchumba nilikuwa nawakataa au nawadanganya kuwa nina mchumba wakati nilikuwa sijaamua kuwa na mchumba ila nilikuwa nawadanganya ili wasiendelee kunisumbua, ili niwe huru kufanya mambo yangu ya kijinga ambayo yameniletea majuto mpaka leo hii.
Kweli wahenga walisema ndege mjanja hunaswa na tundu bovu.  Katika hangaika zangu alitokea mwanaume mmoja akasema anataka kunioa, akawa ananifuata kazini, baadae akanihamishia kwake tukaanza kuishi pamoja bila ndoa, ambayo ilikuja kufungwa baadae.
Baada ya kuolewa nilikuwa nahisi vitu fulani toka kwa huyo mwanaume ambavyo sio vya kawaida, pia na maneno aliyokuwa akijifanya wakati mwingine kunisemesha/kuniuliza, nilikuja gundua baada ya kumrudia YESU,  alitaka agundue kama najua chochote kuhusu uchawi, lakini kwa vile nilikuwa nimefungwa nilikuwa sielewi/sigundui kitu, wakati mwingine angeanzisha stori za kishirikina kuona kama najua kitu, lakini nilikuwa sijui kitu,   pia alikuwa hataki niwe na marafiki au tutembelewe na marafiki au ndugu, nisiende popote bila yeye kujua, pia alikuwa hataki watu wa kwao wawe karibu na mimi au wanizoee, ili kuhakikikisha nakuwa peke yangu alinifanyia madawa nikawa mtu wa kukataliwa, kuchukiwa, kutokubalika, kutokuwa na kibali kwa watu ili mradi nisije nikapata mtu wa kuniambia siri zake, ambapo kabla ya kuolewa nilikuwa na marafiki wengi na nilipendwa na watu. Ndugu yangu mshike YESU naandika utaona kama rahisi nilipitia maisha magumu sana kuyaeleza ukayaelewa.
Wazazi wangu walikuwa hawajaokoka lakini hawakuwa watu wa kwenda kwa waganga wala sikuwai kuwaona wakitupeleka kwa waganga, nilikuja kugundua yeye na familia yake ni washrikina na  wanakwenda kwa waganga sana, ila nilifikiri ni kwenda kwa waganga tu kumbe!  mbaya zaidi na mimi akaanza kunipeleka kwa waganga, tukawa tunakwenda na watoto tunachanjwa, tunapewa madawa mengi ya kunywa, kuoga, kupaka n.k., mpaka na mimi nikazoea nikaanza kutafuta waganga na kwenda mwenyewe, nilikuwa nikipeleka  hela nyingi kwa waganga, na vitu kama kuku, mchele, vyombo, nguo, n.k., wakati mwingine nilikuwa nikiamuka nakuta nimechanjwa nilipokuwa nikimwambia ananiambia twende kwa mganga tunalogwa na watu.
Kipindi chote naishi nae nilikuwa mara kwa mara naota natembea nikiwa uchi, mara naota        nakula vitu usingizini, mara natolewa damu na sindano, kukabwa usingizini hasa siku za Jumamosi na Jumapili saa za alfajili ilikuwa sehemu ya maisha yangu nilikuwa najikuta nakabwa nikiwa nimelala. Mbaya zaidi alinitupia jini mahaba lliikuwa linanitumia siku hizo Jumamosi na Jumapili alfajiri nilikuwa sielewi ni nini, siku moja aliniambia kuwa alikwenda kwa mganga akamwambia nina jina mahaba, mimi sikujali kwa vile nilikuwa nimefungwa niliona kawaida nilinyamaza tu (sikuwa na akili zangu kamili ningeshtuka).
Katika maisha hayo mimi nilijiona sawa tu kumbe! nilikuwa najidanganya, nilikuwa na magari na majumba, nilijiona niko salama lakini kumbe! nilikuwa nimekalia kuti bovu wakati wowote lingekatika labda leo hii nisingekuwepo na kuandika ushuhuda huu kwani baada ya kumrudia YESU niligundua walikuwa wanapanga kuniua muda mrefu baada ya kuona sielekei kuingizwa kwenye uchawi (sijajua wangenifanya msukule au wangenila  jamani nikikumbuka ni huzuni sana).
Miaka yote ishirini na mitano (25) niliishi na mwanaume huyo sikujua kama ni mchawi tena mkubwa tu, baadae alianza kuharibu uchumi wangu, alikuwa anafanya dawa ili kazi nifukuzwe, (karibu ningefukuzwa), kila nilichofanya hakikifanikiwa maisha yetu yalikuwa ni ugomvi usiokwisha, kupigana, kutoelewana ilikuwa ni sehemu ya maisha yetu, tukaanza kuishi kiuhasama mpaka na familia yake yote wakawa wananionyesha uhasama wa wazi wazi.
Nilipoona uchumi wangu unaanza kupukutika ndipo kama mtoto mpotevu nilitafakari moyoni mwangu kuwa JIBU la yote ili kunasuka katika hali ile  na maisha niliyokuwa naishi,  ni  YESU, nikakumbuka wakati nikiwa na huyu YESU sikuishi kwa mateso, nilikuwa na amani na furaha sikukosa kitu nilimkimbia eti niishi kistaarabu ulokole niliona ushamba, nilikumbuka YESU katika Biblia alitoa mfano wa mwana mpotevu, aliporudi kwa baba yake baba yake  alipomuona kwa mbali alimkimbilia akamkumbatia hakujari kuwa mwanae amevaa madaso na kunuka mavi ya nguruwe aliokuwa akiwalisha, nikajiona mimi nanuka zaidi ya yule pia nilijiona madaso niliyovaa ni zaidi yake  nikakumbuka YESU ni mwenye REHEMA mwingi wa HURUMA.
Nilitafuta Kanisa lingine (kwenda nilikokuwa nikiabudu zamani niliona aibu), nilitubu dhambi zangu zote, YESU ni mwaminifu alinisamehe akaniosha dhambi zangu zote zilizokuwa nyekundu sana (maana nilifanya maovu mengi sana kwa kujua na kutojua) zikawa nyeupe kama theruji.
Baada ya kuokoka na kumrudia BWANA YESU, ndipo nilianza kugundua kuwa huyu mwanamume alikuwa mchawi mkubwa sana, yeye na mama yake na ndugu zake wengine nikafumbuliwa macho zaidi kwa msaada wa ROHO MTAKATIFU  kuwa, watoto alikuwa amekwisha wafanyia madawa mengi sana na mimi alikuwa amenifanyia madawa mengi sana, nikaanza kufunga sana na kuomba sana, mikesha uwa sikosi,  mwanzoni nilikuwa nikifunga nasikia harufu mbaya sana toka tumboni na kichwa kilikuwa kinauma, nilikuwa nikienda mkesha tumbo linauma sana, siku moja saa za alfajili wakati natoka mkesha nilitapika sana lakini nilikuwa natapika mate tu mengi, tangu siku hiyo tatizo la tumbo lilikwisha na kuumwa kichwa.  Jini mahaba likawa linaendelea kunitesa nikagundua alikuwa analitumia kuingilia wanawake usiku, mbaya zaidi alikuwa akiwaingilia kinyume na maumbile wakina dada na wakina mama bila YESU shetani anatumia mwili wako kukufanya atakavyo si unakuwa mtumwa wake, ukiokoka YESU anakuweka huru tena huru kweli kweli.
Niligundua alikuwa amenitumia chuma ulete na maroho ya uharibifu ili mali zangu zipukutike.  Kwa kweli uchawi ni mbaya sana alikuwa amefanya mambo mengi sana, pia mtaani kwetu  alikuwa anachukua sura yangu na za watoto anakwenda kufanyia uchawi, mtaani kwetu kumbe! nilikuwa mimi najulikana ndie mchawi watu wakawa wananiogopa wangine wakawa hawanisalimi siku izi ndipo wananisalimia na kuchangamuka zamani mtu akiniona kwa mbali anakatiza njia tusikutane wala mie nilikuwa sijui kinachoendelea, (nikikumbuka nalia sana nilikuwa naitwa mchawi bila kujua hiyo yote shauri ya ndoa ambayo iligeuka ndoano, kuna baba mmoja mtaani kwetu, siku moja aliniambia tulifikiri umeacha uchawi baada ya kuokoka nikamwambia mimi sikuwa mchawi. (kumbuka sura yangu ilikuwa inatumiwa na yule mwanaume kurogea yaani nikikumbuka nasikitika)
Kwa kweli nawaambia ndugu zangu nilifikiri nimepata kumbe nimepatikana ndio maana neno la MUNGU linasema tusichangamane na mataifa, tusifungiwe nira na wasio amini, hata wana wa Israel MUNGU aliwaonya sana wasichangamane watafundishwa kuabudu miungu na kupitisha watoto wao kwenye moto.
Mwenzenu yote yamenitokea kwenye ndoa nilifundishwa kwenda kwa waganga, sikumtegemea MUNGU, nilipigwa chale, wanangu tuliwapeleka kwa waganga walichanjwa.
Mimi nisingeacha wokovu yaani ningekaa miguuni kwa YESU kama Martha (soma Biblia) hayo yote yasingenipata,  mpaka leo hii bado naendele kufunguliwa baadhi ya vifungo lakini kwa kufunga na kuomba maana mwili wangu ulikuwa uisha tumikishwa sana bila mimi kujua na chale zinakwenda zinapotea kidogo kidogo maana nazichukia sana. Gharama nyingine ninayoipata nikiona wapendwa wazamani niliokuwa nao najikakamua kipendwa lakini ndani ya moyo wangu nakuwa naona aibu kuwa sijui wananionaje, ila nawafurahia tu.
Yule mwamume alipojua nimemgundua kuwa ni mchawi alinikimbia kumbuka miaka yote alivyonitesa, alivyokuwa akinilisha madawa bila kujua alivyokuwa anakuchukua damu zangu kwa ajili ya makafara yake  na alivyokuwa akitumikisha mwili wangu na sura yangu kwenye uchawi, naona aliona aibu mambo yake yote kuwa hadharani.
Nataka kuwaonya wenzangu na wewe unayesoma Ushuhuda huu mwambie na mwingine usimwache YESU, misri ni taabu tupu, tena ukiokoka na kurudi nyuma shetani anakutesa kweli kweli naona yule mwanaume alikuwa ametumwa animalize kabisa nisipate nafasi ya kutubu lakini YESU alinihurumia ni ‘NEEMA YA PEKEE’ NILIYOPATA KWA KWELI NAMSHUKURU SANA YESU KUNIPENDA UPEO.
Kwa sasa nikiona wenzangu niliokuwa nao waliomshika YESU tangu usichana/ ujana wao, walipata ndoa nzuri za wake/waume wazuri chaguo la MUNGU, ndoa zao ziko imara zina upendo, wanaelewana na wako juu sana kiroho.
Namalizia kwa kusema wasichana/wavulana usimwache YESU omba kabla ya kuoa/kuolewa mwenzenu nilimwacha YESU nikaolewa kwa kutumia akili zangu niliishia kuolewa na mme mchawi nilikaa nae miaka ishirini na mitano (25) bila kumjua, maisha yangu yote yalikuwa ya mateso nikawa mateka (japo mwanzoni nilifikiri nimepata nikajiona mjanja) mpaka YESU Aliponiweka huru KWA NEEMA YAKE.  NAWAOMBA NDUGU ZANGU KATIKA BWANA MZIDI KUNIOMBEA KATIKA JINA LA YESU VIFUNGO VYOTE NILIVYOKUWA NIMEFUNGWA VIKATIKE NA MADAWA YOTE NILIYO KUWA NIME CHANJWA NA KUYWESHA YAISHE NA VITU VYANGU WALIVYOCHUKUA VISIWE NA MAWASILIANO NA MIMI MAANA BADO WANANIFUATILIA SANA MUNGU AWABARIKI SANA. YESU NI MAMBO YOTE. AMEN.
Kutoka kwa Blogger- Jina la Mhusika sijaliweka kwa sababu maalum. siku akipenda mhusika nitaweka jina na picha yake halisi maana yupo hapa hapa Tanzania.

Comments