SABABU ZA KUUGUA

Na Askofu mkuu Zakaria Kakobe, FGBF
B
wana ametupa neema tena siku hii ya leo, kuendelea kujifunza Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tutatafakari kwa makini YOHANA 8:48-59, na YOHANA 9:1-5.  Kichwa cha somo letu la leo, “SABABU ZA KUUGUA“, ni moja tu kati ya vipengele vingi vya somo letu.  Tutaligawa somo letu la leo katika vipengele saba:-

(1)KUVUNJIWA HESHIMA KWA MTUMISHI WA MUNGU (8:48-50);
(2)JINSI YA KUKWEPA MAUTI YA MILELE (8:51);
(3)YESU, MKUU KULIKO IBRAHIMU NA MANABII (8:52-58);
(4)KUJIFICHA KWA YESU (8:59);
(5)MTU KIPOFU TANGU KUZALIWA (9:1-3);
(6)SABABU ZA KUUGUA (9:3);
(7)KUZIFANYA KAZI ZA MUNGU MAADAMU NI MCHANA (9:4-5).

(1)       KUVUNJIWA HESHIMA KWA MTUMISHI WA MUNGU (8:48-50)
Bwana wetu Yesu Kristo, hapa walimwita MSAMARIA, tena ANA PEPO.  Wasamaria walikuwa ni maadui wakubwa wa Wayahudi na walikuwa hawachangamani kabisa (YOHANA 4:9).  Wasamaria walihesabiwa kuwa ni WAASI (HOSEA 13:16), na Msamaria yeyote alipoonekana hekaluni Yerusalemu, walimpiga kwa “kipigo cha waasi“, na kumtoa nje ya hekalu.  Wasamaria walikuwa washirikina sana na uchawi ulikuwa jadi yao (MATENDO 8:9-11).  Hivyo basi, Mafarisayo na Waandishi, walipomwita Yesu, Msamaria; walikuwa na maana kwamba yeye ni adui wa taifa lao na dini yao, tena ni mchawi anayestahili kupigwa “kipigo cha waasi“, na kutolewa kati yao! Ilikuwa heri mtu alipoitwa MGALILAYA ambalo lilikuwa jina la kuwabeza watu walio dhaifu, wanyonge, wasio na kitu!  (YOHANA 7:52; MARKO 14:70; LUKA 23:6).  Mpaka leo, Wayahudi wanawaita Wakristo “CUTHAEI“, kwa kuwabeza.  Jina “CUTHAEI“, lina maana ya WASAMARIA!  Yesu hakuitwa tu Msamaria bali pia walimwita “ana pepo“ kwa maana kwamba ni mwendawazimu, na hivyo hakuna haja ya kuyasikiliza maneno yake (YOHANA 10:20).  Mafarisayo hawa, pia walisema Yesu anatoa pepo kwa nguvu za mkuu wa pepo yaani shetani, hivyo walimwona ni Mtumishi wa Shetani na siyo Mtumishi wa Mungu! (MATHAYO 9:32-34).  Ni muhimu kwetu kujifunza kwamba shetani atatumia watu wa namna zote hata Mafarisayo na Waandishi, yaani viongozi wa dini kuvunja heshima ya Watumishi wa Mungu wanaoihubiri kweli, ili watu wasiwasikilize.  Paulo Mtume, aliitwa ana wazimu alipoisema kweli, (MATENDO 26:24-25).  Hata manabii wa zamani pia waliitwa wana wazimu (2 WAFALME 9:1-11).  Kanisa la Kwanza, kwa sababu lilihubiri kweli, LILINENWA VIBAYA KILA MAHALI (MATENDO 28:22).  Hatupaswi kuona ajabu, Mtumwa si mkubwa kuliko Bwana wake.  Yaliyompata Yesu, yatawapata Watumwa wake waaminifu leo (YOHANA 15:20-21).  Tukidumu katika kweli lazima dhehebu letu litanenwa vibaya kila mahali, hizi ni kazi za kwaida za shetani nyakati zote!  Yesu alisema, “Mimi sina pepo, lakini mimi namheshimu Baba yangu, na ninyi mwanivunjia heshima yangu“.  Hapa hakujibu lolote juu ya yeye kuitwa Msamaria maana yeye ni MSAMARIA MWEMA!  Pamoja na Yesu kuvunjiwa heshima hivyo, hakuitafuta heshima hiyo kwa nguvu  kati yao!  Heshima au utukufu wa kuutafuta mwenyewe, si utukufu (YOHANA 8:54; MITHALI 25:27).  Yesu alimwachia Baba kutafuta utukufu wa kumpa, kati yao, na kuwahukumu yeye mwenyewe.  Tunapovunjiwa heshima, tusijisumbue kuitafuta heshima hiyo kwa watu, kwa nguvu zetu.  Tumwachie Mungu wetu kazihiyo, yeye huifanya vizuri sana kwa wakati wake, tunapodumu kuwa waaminifu kuitenda kazi yake.  Vivyo hivyo ni muhimu kutambua kwamba wale wote wanaowaita Manabii wa Mungu kwamba ni wapumbavu, wana wazimu, wana pepo n.k; watapatilizwa au kuhukumiwa kwa maovu yao hayo (HOSEA 9:7).
(2)            JINSI YA KUKWEPA MAUTI YA MILELE (8:51)
Jinsi pekee ya kukwepa mauti ya milele, ni KULISHIKA NENO la Mungu.  Kulishika Neno ni tofauti na kulisikia.  Kulishika Neno maana yake KULITENDA NENO (YAKOBO 1:22).  Mtu anayelitenda neno la Mungu, hataopna mauti milele.  Maana yake nini maneno haya?  Je, mtu akiokoka na kudumu kulitenda Neno la Mungu, hatakufa kabisa?  Jibu ni kwamba, watu waliookoka, WANAKUFA kama watu wengine (WARUMI 8:36; 2 WAKORINTHO 4:11; 2 WAFALME 13:14; 2 TIMOTHEO 4:6).  Kinachosemwa hapa na Yesu, ni kwamba mtu anayelitenda Neno hataona MAUTI YA MILELE au MAUTI YA PILI yaani hatatupwa katika ziwa la moto (UFUNUO 20:6; 21:8).  Kufa kwa mtu anayelitenda Neno ni kupita katika mlango wa uzima na kwenda kukaa pamoja na Bwana Yesu (2 WAKORINTHO 5:6,8).

(3)            YESU, MKUU KULIKO IBRAHIMU NA MANABII (8:52-58)
Ibrahimu alikufa, manabii wote walikufa, na makaburi yao yako hata leo.  Yesu aliye mkuu kuliko hao, Yeye alikufa na kufufuka siku ya tatu kama alivyosema.  Kaburi lake, liko wazi hivi leo (MATENDO 2:29-36; LUKA 24:3).  Yesu Kristo alikuwako tangu zamani za kale, tangu milele, kabla ya Ibrahimu, kabla ya vitu vyote (MIKA 5:2; WAKOLOSAI 1:17).  YESU NI MUNGU (1 YOHANA 5:20; TITO 2:13), hivyo hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wala mwisho wa siku zake (WAEBRANIA 7:3).  Yesu hakuanza kuwapo alipozaliwa na Mariamu.  Katika MST. 54, Yesu anasema “Anitukuzaye ni Baba yangu ambaye ninyi mwanena kuwa ni Mungu wenu“.  Watu hawa WALINENA TU kuwa ni Mungu wao, lakini ukweli hawakumjua Mungu (1 YOHANA 2:3-5).

(4)            KUJIFICHA KWA YESU (8:59)
“Wakaokota mawe ili wamtupie“.  Waliokota mawe haya ili wamtupie, kwa sababu alionekana kwao kwamba ANAKUFURU, kwa kusema kabla Ibrahimu hajakuwako, yeye alikuwako, na kwamba Ibrahimu alishangilia kuiona siku ya kuwako Yesu duniani.  Kwa kuwaza hivyo, waliichukua sheria ya MAMBO YA WALAWI 24:16 mikononi mwao.  Yesu alijificha, akatoka hekaluni.  Hapa tunajifunza juambo la msingi.  Hatupaswi kuwaacha watu watuonee wakati tuna uwezo wa kujificha au kukimbia, kwa visingizio vya kukubali kuteswa kwa ajili ya Kristo.  Uzima wetu ni wa thamani sana kwa ajili ya Injili.  Mume ambaye hajaokoka anapotupiga na kutaka kutuua, hatuna budi kujificha na kutoka nje!

(5)            MTU KIPOFU TANGU KUZALIWA (9:1-3)
Baada ya Yesu kuvunjiwa heshima kiasi hicho, hakuacha kutenda kazi ya Mungu au kubadili msimamo wake!  Aliendelea kuitenda kazi ya Mungu kwa msimamo wake uleule!  Hii ndiyo siri ya kutumiwa sana na Mungu!  Vilevile wanafunzi wake hawakumwacha na kuona aibu kuambatana na Mchungaji wao, aliyenenwa vibaya na kuitwa ANA PEPO!  Ssisi nasi tunapaswa kufuata mfano wa wanafunzi hawa.  Kamwe tusione aibu kuambatana popote na Mchungaji anayesemwa vibaya kila mahali, na kuambiwa ana pepo au yeye ni pepo, wakati tuna hakika kwamba anafundisha kweli.  Hapa Yesu anakutana na mtu kipofu tangu kuzaliwa na kutufundisha kwamba sisi sote  ni vipofu tangu kuzaliwa kwetu kutokana na dhambi zetu.  Kipofu hutembea gizani na kuanguka shimoni pasipo kupenda.  Ndivyo alivyo mwenye dhambi yeyote.  Mtu akikataa kwamba yeye siyo kipofu hawezi kusamehewa dhambvi zake (YOHANA 9:39-41; ZABURI 51:5; WARUMI 3:23; 1 YOHANA 1:8-10).

(6)            SABABU ZA KUUGUA (9:3)
Wako watu wengine waliookoka ambao wakiona wake zao, waume zao au wapendwa wengine wanaugua, huwaambia kwamba wanaugua kwa sababu wametenda dhambi.  Huku ni kuitia jeraha dhamiri iliyo dhaifu na kumtenda dhambi Kristo (1 WAKORINTHO 8:11-12).  Hatupaswi kuhukumu hivyo.  Ziko sababu nyingi zinazoweza kumfanya mtu awe mgonjwa:-
  1. Dhambi (ZABURI 38:3-4; YEREMIA 30:12-14; YOHANA 5:14);
  2. Ili Mungu ajipatie utukufu kwa kumponya kwa muujiza (YOHANA 11:1-4);
  3. Ili kazi za Mungu zidhihirishwe ndani ya mtu huyo (YOHANA 9:3);
  4. Kutokana na KUONEWA na Ibilisi (MATENDO 10:38);
  5. Kumpa Ibilisi nafasi kwa kushindwa kumpinga na kumkemea (WAEFESO 4:27; YAKOBO 4:7);
  6. Upungufu wa Imani (MATHAYO 17:18-20; MARKO 6:5-6).
Ikiwa hatujatenda dhambi yoyote, hatupaswi kudanganywa na Ibilisi kwamba ugonjwa uliotupata umetupata sababu ya dhambi.  Zakaria na Elisabeti walikuwa tasa, lakini walikuwa wenye haki mbele za Mungu bila lawama yoyote (LUKA 1:5-7).  Tukimruhusu Shetani atudanganye hivyo, mioyo yetu hutuhukumu bure na kutukosesha ujasiri kwa Mungu, na hivyo maombi yetu huwa hayapati majibu (1 YOHANA 3:21-22).

(7)            KUZIFANYA KAZI ZA MUNGU MAADAMU NI MCHANA (9:4-5)
Giza linakuja, na wakati wa kulala utafika.  Kama baba zetu walivyolala, sisi nasi tutalala au kwa maneno mengine, tutakufa.  Siku ya kufa hatuijui.  Tufanye kazi ya Mungu kana kwamba KESHO HAIKO.  Hii ndiyo siri ya kufanikiwa.

…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!


Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe  tembelea.     
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe
SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Comments