UFANYEJE KATIKA HALI NGUMU YA UCHUMI?


Matatizo ya ugumu wa uchumi katika dunia hii siyo mapya. Tangu baada ya mwanadamu kuanguka katika dhambi – amekuwa mara kwa mara akisumbuliwa na matatizo ya uchumi. Ukisoma habari za Isaka na za Yakobo utaona jinsi hali hii ilivyojitokeza.
Lakini biblia inaeleza wazi kuwa siku hizi ni za mwisho. Katika siku hizi za mwisho, biblia pia inasema wazi kabisa kuwa dunia itapita kwenye vipindi vigumu vya uchumi
Kwa Mfano: Katika Mathayo 24:7 na Ufunuo wa Yohana 6:3-6 tunaona ya kuwa katika siku hizi za mwisho kutatokea njaa – au upungufu wa chakula. Sababu ya kuja kwa njaa hiyo ni vita vitakavyokuwa vinatokea katika nchi mbalimbali. Ni wazi kabisa kuwa palipo na vita au palipo na ugomvi, panakuwa na matatizo ya ulimaji mashamba na usafiri wa kuleta chakula toka sehemu zingine. Matokeo ni hilo eneo au nchi kukosa chakula, haya mambo yaliyotabiriwa kutokea siku hizi za mwisho wa dunia.
Ukisoma katika kitabu cha Ufunuo wa Yohana sura za 17 na 18 utaona ya kuwa hali ngumu ya kibiashara imetabiriwa kutokea katika siku hizi za mwisho. Kuuza au kununua kutafanyika kwa vibali. Watu watapenda fedha sana kuliko kumpenda Mungu. Kutakuwa na uhusiano mkubwa sana kati ya utajiri na biashara na uasherati. Wafanyabiashara wa siku hizi za mwisho watakuwa na sehemu kubwa katika utawala wa miji au vijiji wanavyokaa – hata wakati mwingine katika maongozi ya nchi au mataifa mbalimbali.
Matokeo ya hali namna hii inawafanya watu watafute njia au mbinu za kuweza kuishi katika vipindi vya namna hiyo. Lakini ni wazi kuwa si mbinu zote au njia zote ambazo wanadamu wanazitumia katika kuishi wakati wa hali ngumu ya uchumi zinampendeza Mungu.
Kunapotokea hali ngumu ya uchumi, tabia za watu zinabadilika. Mara kwa mara mambo yafuatayo hutokea;Kubana matumizi Kununua vitu kwa wingi na kuvirundika Uchoyo – kupunguza tabia ya utoaji na ukarimu Watu huacha kumtumikia Mungu na badala yake mtu huitumikia mali Rushwa, wizi na dhuluma huwa ni vitu vya kawaida Miradi ya kila namna huibuka kuanzia kwa watoto hadi watu wazima.
Jambo linalowafanya watu wawe na tabia hizi, ni lile la kutaka kutafuta namna ya kuishi katika kipindi kigumu cha uchumi.
Je!mkristo afanye nini ili aishi katika kipindi hiki kigumu cha uchumi bila kufanya mambo yatakayomkosea Mungu?
Wakristo wengine wamefika mahali pa kuhalalisha miradi ya kuwapatia fedha ambayo ni kinyume na ushuhuda wa kikristo – Je! hii ni sawa?Wengine wamefika hata mahali pa kufunga nira na wasioamini (wasio wakristo) KWA JINSI ISIYO SAWASAWA (yaani isiyokubalika) na neno la Mungu ili waweze kupata fedha kutokana na mradi wanaofanya pamoja. IKO "jinsi iliyo sawasawa" na utaifahamu ikiwa utakuwa mtendaji wa neno la Mungu.
Mungu akipenda kesho tutaendelea na jinsi ya kutenda sawasawa na mapenzi ya Mungu unapopitia ktk kipindi kigumu cha uchumi

Comments