UFUNGUO WA KUJIBIWA MAOMBI YOTE

Na Askofu Mkuu Zakaria Kakobe.

SIKU YA KUICHAMBUA BIBLIA
SOMO:  UFUNGUO WA KUJIBIWA MAOMBI YOTE
W
iki iliyopita, tulianza SURA YA 15 ya Kitabu cha YOHANA katika Biblia zetu.  Leo, tunaendelea kujifunza sura hii, na tutatafakari YOHANA 15:9-17.  Ingawa kichwa cha somo letu la leo, ni “UFUNGUO WA KUJIBIWA MAOMBI YOTE“, hata hivyo kuna mengi zaidi ya kujifunza katika mistari hii.  Tutayagawa mafundisho yote tunayoyapata katika mistari hii, katika vipengele kumi:-
(1)      KAMA VILE BABA ALIVYONIPENDA MIMI (MST. 9);
(2)      UPENDO WA YESU KWETU (MST. 9,13);
(3)      JINSI YA KUKAA KATIKA PENDO LA YESU (MST. 10);
(4)      MAKUSUDI YA MAFUNDISHO YA YESU (MST. 11);
(5)      MPENDANE KAMA NILIVYOWAPENDA NINYI (MST. 12,17);
(6)      NINYI MMEKUWA RAFIKI ZANGU (MST. 14-15);
(7)      YOTE NILIYOYASIKIA KWA BABA NIMEWAARIFU (MST. 15);
(8)      NI MIMI NILIYEWACHAGUA NINYI (MST. 16);
(9)      SABABU YA KUCHAGULIWA NINYI (MST. 16)
(10)       UFUNGUO WA KUJIBIWA MAOMBI YOTE (MST. 16)

(1)            KAMA VILE BABA ALIVYONIPENDA MIMI (MST. 9)
Maneno haya, “Kama vile Baba alivyonipenda mimi“, ni maneno aliyoyasema Yesu, muda mfupi tu kabla ya kusalitiwa na Yuda, na hatimaye kupigwa mijeledi, kutemewa mate, n.k., na baadaye kusulibishwa.  Yesu aliyasema haya huku akijua saa yake imefika ya kutendwa haya.  Katika hali ya kukabiliwa na mateso makali, kukanwa na Petro, na kuachwa na wanafunzi wake wote, na hatimaye kufa, bado alikiri, “kupendwa na Baba“.  Kukiri upendo wa Mungu wakati wote, katika mazingira yoyote yale, ndiyo ilikuwa siri ya ushindi mkubwa wa Yesu duniani.  Wengi wetu hatuko kama Yesu.  Tunapokabiliwa na magumu, dhiki, mateso, kuachwa na ndugu au wapenzi wetu n.k.; katika mazingira hayo, huwa hatuukiri upendo wa Mungu kwetu.  Huwa tunaona Mungu hatupendi, hatujali wala hashughuliki nasi.  Huwa tunawaza, “Kama kweli Mungu ananipenda, mbona haya yamenipata?“.  Haitupasi kuwa hivi.  Watu waliotumiwa sana na Mungu, walikuwa watu wale alioukiri Upendo wa Mungu kwao, katika kukabiliwa na magumu ya kila aina.  Hiki ndicho hasa kipimo cha kumpenda Mungu.  “Akupendaye wakati wa dhiki, ndiye rafiki“, ni usemi maarufu wa Kiswahili.  Mtume Paulo, yeye naye alikuwa mtu aliyeukiri upendo wa Mungu kwake, katika mazingira yoyote magumu (WARUMI 8:35-39).  Paulo Mtume alihesabiwa kama takataka za dunia na kupata mateso mengi, lakini hata wakati mmoja, hakuwa na mashaka juu ya wito wake au kupendwa kwake na Mungu, na anatufundisha kujipatia sifa njema katika hali zozote ngumu (1 WAKORINTHO 4:11-13; 2 WAKORINTHO 11:23-28; 1 WAKORINTHO 1:1; 2 WAKORINTHO 1:1; WAEFESO 1:1; 2 WAKORINTHO 6:4-5).  Bwana atupe neema kumfuata Mtume Paulo kama alivyomfuata Yesu Kristo, ili tupate mafanikio makubwa.

(2)            UPENDO WA YESU KWETU (MST. 9,13)
Yesu Kristo, anatuhakikishia upendo wake kwetu, tena na tena.  Hatuna budi kukaa katika pendo lake tukitafakari upendo wake mwingi kwetu wakati wote.  Ni upendo mkuu, kwa mtu kuutoa uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.  Hata hivyo, ni rahisi kwa mtu kufa kwa ajili ya mtu mwema, lakini ni vigumu kwa mtu yeyote kufa kwa ajili ya mtu mwovu.  Yesu alikuwa na upendo wa kipekee sana, pale alipokufa kwa ajili yetu wenye dhambi, waovu (WARUMI 5:7-8).  Bwana atupe neema ya kukaa katika pendo lake kwa gharama yoyote.  Kupuuza pendo hili ni kukosa shukrani.

(3)            JINSI YA KUKAA KATIKA PENDO LA YESU (MST. 10)
Pamoja na Yesu kutupenda upeo, hata hivyo, anatuonya kwamba pendo lake litadumu kwetu pale tutakapozishika amri zake.  Yeye mwenyewe anatufundisha siri ya Yeye kukaa katika pendo la Baba yake wakti wote.  Alihakikisha anazishika amri zake wakati wote (YOHANA 8:29).  Watu wengi wanakosa pendo linalodumu kwao kwa sababu ya kuchagua amri za kushika na kuona kwamba nyingine zimepitwa na wakati.  Visingizio vya kuwa huru na kutokufungwa na sheria, vinavyowafanya watu wengi kuacha kuzishika amri za Yesu Kristo, na kukosa pendo la Yesu linalodumu kwao.  Bwana ampe neema kila mmoja wetu kuzishika amri za Yesu Kristo kwa gharama yoyote.

(4)            MAKUSUDI YA MAFUNDISHO YA YESU (MST. 11)
Maneno yote aliyotuambia Yesu, yana lengo la kutupa furaha iliyotimizwa hapa duniani, na zaidi sana milele na milele.  Kwa kutokuelewa, watu wengine wanafikiri kwamba amri za yesu, zina lengo la kutufanya wenye huzuni na kuwa mbali na kila namna ya furaha.  Furaha iliyotimizwa, inapatikana katika kuzingatia maneno ya Yesu, na siyo vinginevyo.  Furaha nyingine zote ni za muda tu na siyo furaha halisi.

(5)            MPENDANE KAMA NILIVYOPENDA NINYI (MST. 12,17)
Mafundisho ya Yesu katika siku zake za mwishomwisho katika huduma yake, alikazia sana kupendana sisi kwa sisi.  Muda mfupi uliopita tulijifunza katika YOHANA 13:34, jambo hilihili.  Neno lolote ambalo Yesu analitilia uzito namna hii na kulisisitiza hivi ni neno la msingi sana katika imani yetu ya Ukristo.  Hatuna budi kupendana kwa gharama yoyote.  Hatupaswi kuchoka kuchukuliana mizigo katika Makanisa ya Nyumbani, Seksheni na Zoni, na kuona michango imezidi kwa waliofiwa, na kuipuuza.  Bwana atupe neema hata ya kuutoa uhai wetu (siyo michango tu), kwa ajili ya ndugu katika Kristo (1 YOHANA 3:16).

(6)            NINYI MMEKUWA RAFIKI ZANGU (MST. 14-15)
Daudi na Sulemani, kila mmoja wao alikuwa na mtu MMOJA TU, aliyemwita RAFIKI, katika wengi waliokuwa karibu nao katika majumba yao ya kifalme (1 SAMWELI 15:37, 1 WAFALME 4:5).  Yesu, ni zaidi ya Daudi na Sulemani, upendo wake kwetu ni zaidi ya nabii yeyote (MATHAYO 12:42).  Yesu anawaita watu wote wanaoyatenda anayowaamuru, RAFIKI zake.  Sisi ni RAFIKI ZAKE!  Mtu yeyote hutumiwa uwezo wake wote kumfurahisha rafiki yake na kumpa mahitaji aliyo nayo.  Rafiki zetu wengine, wana mipaka!  Rafiki yetu Yesu, anavyote.  Furaha yake ni kutupa mahitaji yetu!  Hatuna budi kuamini!  Kuna jambo jingine la kujifunza hapa.  Ingawa Yesu alisema hawaiti tena wanafunzi wake watumwa, bali rafiki, akawapandisha juu, hata hivyo wanafunzi hao waliendelea kujiita watumwa (2 PETRO 1:1; YAKOBO 1:1).  Hata Yesu akitupandisha juu na kututumia kwa namna tofauti sana, hatuna budi kuchukua nafasi za chini kana kwamba hatujapandishwa popote.  Bwana atupe neema kuwa hivi wakati wote.

(7)            YOTE NILIYOYASIKIA KWA BABA NIMEWAARIFU (MST. 15)
Yesu Kristo, anatoa kielelezo kwa Mhubiri au Mwalimu wa Neno la Mungu.  Yesu Kristo, kama Mhubiri na Mwalimu wa Neno la Mungu, alifundisha yote aliyoyasikia kwa Baba.  Kwa msingi huo huo, ni wajibu wa kila Mhubiri na Mwalimu wa Neno la Mungu, kufundisha yote aliyotuamuru Yesu, bila kusaza kitu (MATHAYO 28:19-20). Hatupaswi kutafuta kupendwa na Viongozi wa dini au watu wa namna yoyote, kwa kuacha kuwaarifu watu KUSUDI LOTE LA MUNGU.  Tukitaka kuzitenda kazi alizozifanya Yesu na kumwona Roho Mtakatifu akitenda kazi pamoja nasi katika huduma zetu, hatuna budi kumshawishi Mungu kwa kuzingatia jambo hili, bila kujali watu kuondoka katika makanisa yetu.  Mtume Paulo alizingatia jambo  hili hata kama wengi walimwepuka kutokana na kweli yote aliyofundisha.  Hii ndiyo siri ya kutumiwa sana na Mungu (MATENDO 20:18-20, 26-27; 2 TIMOTHEO 1:15; WAGALATIA 1:10; 4:16-17).

(8)             NI MIMI NILIYEWACHAGUA NINYI (MST. 16)
Mtu hajichagui mwenyewe na kujifanya Mtume, Nabii, Mwinjilisiti, Mchungaji au Mwalimu.  Tukijichagua wenyewe, hatuwezi kuona amtokeo yanayokusudiwa.  Hatuna budi kuchaguliwa (WAEFESO 4:11).  Mtu akichaguliwa na Mungu katika huduma yoyote kati ya hizi, Mungu atakuwa pamoja naye kutenda kazi.  Tukiwa tumechaguliwa, hatupaswi kuogopa maneno ya wanadumu kinyume chtu.  Tumwogope Mungu tu (MATHAYO 10:27-28).  Tukipata kibali kwa Mungu, Mungu huyohuyo hatimaye atatupa kibali kwa wanadamu kama Mtume Paulo.
(9)            SABABU YA KUCHAGULIWA (MST. 16)
Sababu ya kuchaguliwa katika utumishi wa Mungu ni ili tuzae matunda na matunda hayo yapate kukaa.  Hatuna budi kuipima kazi yetu ya kuhubiri Injili, kutokana na wale wanaookoka wanaoendelea katika wokovu na siyo wale tu wanaokata shauri!  Hatukuchaguliwa ili kuwafanya watu wakate tu shauri bali kuwa fanya wadumu katika wokovu!

(10)                   UFUNGUO WA KUJIBIWA MAOMBI YOTE (MST. 16)
Pamoja na vifaa vya kisasa tulivyo navyo leo, Televisheni, Radio, Eropleni, Simu, Mitambo ya Kupiga Chapa, Vipaza Sauti, Setlaiti n.k.;  Wahubiri wengi wa injili duniani hawana uwezo wa mungu ndani yao kama wale wa Kanisa la Kwanza.  Maombi yao hayana nguvu!  Ni kwa nini?  Ufunguo wa kujijiwa maombi, ni kuhakikisha matunda ya Injili yanakaa!  Tukiwaambia watu waokoke na kubaki katika madhehebu yao yaliyojaa sanamu, tunakuwa tunaukosa ufunguo huu.  Matunda haya yatadumu namna gani katika kusanyiko lililojaa giza?  Tugeuke na kuuchukua ufunguo huu ili dunia hii ipinduliwe kizazi hiki.
…………………………………………………………………………………………………………………………………..
Ni sifa ipi ya kutuwezesha kuingia mbinguni?  Ni utakatifu (WAEBRANIA 12:14).  Ndani yake hakitaingia kamwe chochote kilicho kinyonge (UFUNUO WA YOHANA 21:27).  Kinyonge ni kipi?  Ni yule anayetenda dhambi.  Huyu ni mtu asiyefaa, ni mnyonge!  Je, wewe ni mtakatifu?  Jibu ni la!  Maisha yako yamejaa dhambi, pamoja na kusema una dini; hivyo wewe pia ni mnyonge, hufai kuingia mbinguni. Ukitubu leo dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na kuifuata njia ya Yesu Kristo, ndipo utakapopata rehema ya kuingia mbinguni (MITHALI 28:13;  YOHANA 14:6).  Je, uko tayari kutubu sasa ili upate rehema hii?  Najua uko tayari.  Basi fuatisha sala hii ya toba kwa dhati kutoka moyoni;  Mungu Baba asante kwa ujumbe huu.  Hakika mimi ni mnyonge, mwenye dhambi.  Sistahili kuingia mbinguni. Natubu dhambi zangu zote kwa kumaanisha kuziacha.  Kuanzia leo nataka niifuate njia ya Yesu Kristo.  Bwana Yesu niwezeshe.  Asante kwa kunisikia katika Jina la Yesu.  Amen.  Mpendwa msomaji umekubaliwa kuingia mbinguni.  Ili uzidi kudumu katika utakatifu mpaka siku ya kuiaga dunia hii, hakikisha unahudhuria mafundisho katika Kanisa linalohubiri wokovu.  MUNGU AKUBARIKI !!!
. . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . . 
Zipo Baraka nyingi kwa yeyote atakaye “share “ ujumbe huu katika Facebook , Twitter n.k, kwa ndugu, jamaaa na marifiki ili nao wapate nafasi ya kusoma ujumbe huu na kubarikiwa kama wewe ulivyo barikiwa. Kwasababu hii share ujumbe huu kwa kubonyeza neno“ share” lililopo chini ya “somo” hili, kwa kufanya hivyo ujumbe huu utafika kwa watu wengi. Hakika, Baraka za Mungu zitakuwa nawe..

Kwa Neno la Uzima kutoka kwa  Askofu Zachary Kakobe  Fungua      
Tovuti       : www.bishopzacharykakobe.org
Facebook : www.facebook.com/bishopkakobeministries
Youtube   : www.youtube.com/user/bishopkakobe

Comments