USHINDI WAKO NI LEO KATIKA BWANA YESU.

Na Mtumishi Peter Mabula.

BWANA YESU atukuzwe ndugu yangu.
''Kwa sababu hiyo nawaambia, Yo yote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.-Marko 11:24''

=Haijalishi kuna bahari ya shamu mbele yako.Kwa jina la YESU KRISTO unavuka salama, BWANA YESU anaenda kukushindia.
BWANA YESU akuvushe salama katika hiyo bahari unayotegemea kuvuka. Bahari ya masomo BWANA akuvushe salama, Bahari ya uchumba BWANA akuvushe sala, Bahari ya ndoa JEHOVAH MUNGU akuvushe salama, Bahari ya majaribu akuvushe salama. na kila aina ya bahari ya shamu unayoipitia, MUNGU BABA akuvushe salama. Omba kisha shukuru.
Zaburi 136:1,13-15 ''Mshukuruni BWANA kwa kuwa ni mwema; Kwa maana fadhili zake ni za milele. eye aliyeigawa Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akawavusha Israeli katikati yake; Kwa maana fadhili zake ni za milele. Akamwangusha Farao na jeshi lake katika Bahari ya Shamu; Kwa maana fadhili zake ni za milele. ''


=Haijalishi Yeriko yako imegoma kubomoka, Mwite BWANA YESU leo ili aibomoe, kwa jina la YESU KRISTO yeriko ya magonjwa inakwenda kubomoka, yeriko ya utasa inakwenda kubomoka, yeriko ya kukataliwa inakwenda kubomoka kwa jina la YESU KRISTO, Kila aina ya yriko katika maisha yako ikabomoke kwa jina la YESU KRISTO, Omba leo na BWANA YESU anaenda kukubomolea Yeriko yako na utakaa salama.
BWANA hajaanza leo kuangusha kuta za Yeriko.
Yoshua 6:20 '' Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji. ''



=Haijalishi Goliathi amesimama na uchawi wake ili kukudhuru, lakini kwa maombi yako ya leo Goliath anaenda kuangamia na uchawi wake wote alioupanga kwa ajili yako unaenda kumwangamiza yeye kwa jina la YESU KRISTO. Kama kuna mchawi amegeuka goliathi wa kukutesa na kutesa familia yako, leo goliathi huyo anaenda kukutana na nyundo ya BWANA kupitia maombi yako na uchawi wake leo unaenda kuwa si kitu tena. Kila aina ya goliathi katika maisha yako mponde kwa jina la YESU KRISTO aliye hai milele. BWANA hajaanza leo kuwapiga akina goliathi, ona hapa.
1 Samweli 17:45-50 '' Ndipo Daudi akamwambia yule Mfilisti, Wewe unanijia mimi na upanga, na fumo, na mkuki, bali mimi ninakujia wewe kwa jina la BWANA wa majeshi, MUNGU wa majeshi ya Israeli uliowatukana.Siku hii ya leo BWANA atakuua mkononi mwangu, nami nitakupiga, na kukuondolea kichwa chako, nami leo nitawapa ndege wa angani na wanyama wa nchi mizoga ya majeshi ya Wafilisti, ili kwamba dunia nzima wajue ya kuwa yuko MUNGU katika Israeli.Nao jamii ya watu wote pia wajue ya kwamba BWANA haokoi kwa upanga wala kwa mkuki; maana vita ni vya BWANA, naye atawatia ninyi mikononi mwetu.Ikawa, hapo Mfilisti alipojiinua, akaenda akamkaribia Daudi, ndipo Daudi naye akapiga mbio, akalikimbilia jeshi ili akutane na yule Mfilisti. Daudi akatia mkono wake mfukoni, akatwaa humo jiwe moja, akalitupa kwa kombeo lake, akampiga Mfilisti katika kipaji cha uso; jiwe hilo likamwingilia kipajini, akaanguka chini kifudifudi. Hivyo Daudi akamshinda yule Mfilisti kwa kombeo na jiwe, akampiga Mfilisti, akamwua; walakini Daudi hakuwa na upanga mkononi mwake. ''

=Haijalishi Farao anatisha mbele yako na unaona ni ngumu sana kuondoka katika uteka wa farao, lakini kwa jina la YESU KRISTO farao na farasi zake zote na wapanda farasi wake wote wanaenda kuangamia kwa jina la YESU KRISTO. Farao na jeshi lake wanaenda kupondwa kwa jina la YESU KRISTO aliye hai milele.
Leo mpinge farao wako ambaye ni mizimu, majini, shetani, na kila mpango wa kuzimu juu ya maisha yako. Mwite BWANA amwangamize farao anayekuonea. kwa jila la YESU KRISTO farao na jeshi lake lote wanaenda kuangamia kwa jina la YESU KRISTO.
BWANA hajaanza leo kuwaua akina farao wanaotesa watu wake.
Kutoka 15:2-6 '' BWANA ni nguvu zangu, na wimbo wangu; Naye amekuwa wokovu wangu. Yeye ni MUNGU wangu, nami nitamsifu; Ni MUNGU wa baba yangu, nami nitamtukuza. BWANA ni mtu wa vita, BWANA ndilo jina lake. Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini, Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu.Vilindi vimewafunikiza, Walizama vilindini kama jiwe.BWANA, mkono wako wa kuume umepata fahari ya uwezo, BWANA, mkono wako wa kuume wawaseta-seta adui. ''

=Haijalishi washami ni hodari kiasi gani na umekata tumaini kwamba huwezi kupigana nao lakini mbele yako mteule muombaji leo washami na jeshi lao wanaenda kupondwa kwa jina la YESU KRISTO, wanaenda kuangamia na kukimbia baada ya BWANA kuwasikilizisha mshindo mkuu utakaotokana na maombi yako leo kwa JEHOVAH BWANA.
2 Wafalme 7:5-7 ''Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.Kwa maana BWANA alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao. ''
Inawezekana waamaleki ni wengi na unaona huwezi kuwashinda , lakini napenda kukuambia omba tena omba leo kwa jina la YESU KRISTO BWANA anaenda kuwapiga waamaleki na anaenda kuufuta ukombusho wa amaleki kwa jina la YESU KRISTO. Kama mizimu na majini wamegeuka waamaleki kwako basi mwite BWANA YESU kwa maombi ili aufute ukumbusho wa waamaleki wako wote.
Kutoka 17:13-16 '' Yoshua akawaangamiza Amaleki na watu wake kwa ukali wa upanga. BWANA akamwambia Musa, Andika habari hii katika kitabu iwe ukumbusho, kisha ihubiri masikioni mwa Yoshua; ya kuwa nitaufuta ukumbusho wa Amaleki kabisa, usiwe tena chini ya mbingu. Musa akajenga madhabahu, akaiita jina lake YEHOVA-NISI; akasema, BWANA ameapa; Bwana atakuwa na vita na Amaleki kizazi baada ya kizazi. ''
-Hakika kwa jina la YESU KRISTO uko ushindi na uzima.
Ndugu omba na hakikisha unakuwa mtu wa maombi maana maombi ni maisha, maombi ndio mkono mrefu zaidi wa kupokea msaada kutoka kwa MUNGU.

''Na lo lote tuombalo, twalipokea kwake, kwa kuwa twazishika amri zake, na kuyatenda yapendezayo machoni pake. - 1 Yohana 3:22''
-Ndugu,Naamini umejifunza na utachukua hatua njema ya kumpokea BWANA YESU kama hujaokoka ili awe BWANA na MWOKOZI wako tangu leo na utaanza kuishi maisha matakatifu

KAMA UNATAKA KUTUBU RUDIA MANENO HAYA KISHA TAFUTA KANISA LA KIROHO UKAJIUNGE NA KUANZA KUISHI MAISHA MATAKATIFU.

''BABA katika jina la YESU KRISTO Niko mbele zako mimi mwenye dhambi, lakini leo nimetambua kosa langu na naomba unisamehe dhambi zangu zote, nisamehe dhambi ninazozikumbuka na pia zile ambazo sizikumbuki. futa jina langu katika kitabu cha hukumu na uliandike jina langu katika kitabu cha uzima. Neno lako katika Warumi sura ya 10 Mstari wa 9 na wa 10 Neno lako linasema ''Kwa sababu, ukimkiri YESU kwa kinywa chako ya kuwa ni BWANA, na kuamini moyoni mwako ya kuwa MUNGU alimfufua katika wafu, utaokoka. Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu '' . BWANA YESU mimi nimekuamini leo na hivyo naamini sasa napokea wokovu wako na hakika nimeokoka. Kuanzia leo Naufunga ukurasa wa dhambi na ninaufungua ukurasa wa matendo mema na matakatifu. BWANA nipe ROHO wako Mtakatifu ili aniwezeshe kushinda dhambi na anasa zote za dunia. Kuanzia leo mimi nimeokoka na ni mtoto wa MUNGU mwenye haki zote. ninafuta laana zote na kila roho ya shetani inayonifuatilia naiharibu kwa jina la YESU KRISTO kama neno la MUNGU linavyosema katika Yeremia sura ya kwanza mstari wa 10. BWANA YESU nakushukuru sana kwa kuniokoa. Yote haya kwa imani nimepokea na niko tayari sasa kwa ROHO MTAKATIFU kunitumia. Katika jina la YESU KRISTO nimeomba na kupokea Amen.''

Kama umetubu toba ya kweli hakika wewe kuanzia sasa ni mshindi na ni shujaa. Kwa sasa naishia hapo, MUNGU akitupa nafasi tutajifunza tena siku nyingine. ulishindwa kumpokea BWANA YESU nafasi yako bado ipo na muda wa kumpokea ni leo wala sio kesho, amua leo na atakuandika jina lako katika kitabu cha uzima na utaanza kuukulia wokovu kwa mafundisho kanisani. MUNGU ana makusudi kabisa na wewe, hataki upotelee motoni anataka uende uzimani aliko KRISTO BWANA.
MUNGU akubariki sana .
Ni mimi ndugu yako Peter M Mabula
+255714252292
mabula1986@gmail.com
MUNGU akubariki sana uliyesoma somo hili.

Comments